Mkutano Mkuu
Palikuwa na Chakula
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Palikuwa na Chakula

Tunapotafuta kujiandaa kimwili, tunaweza kukabiliana na majaribu ya maisha kwa kujiamini zaidi.

Kabla ya vizuizi vya kusafiri vilivyosababishwa na janga la ulimwengu la sasa, nilikuwa nikirejea nyumbani kutoka kwenye kazi ya kimataifa ambayo, kwa sababu ya masuala ya ratiba, ilitengeneza mapumziko ya Jumapili. Nilikuwa na wakati kabla ya ndege nyingine kuhudhuria mkutano wa sakramenti wa mahali hapo, ambapo pia niliweza kushiriki ujumbe mfupi. Kufuatia mkutano huo, shemasi mwenye shauku alinijia na kuniuliza ikiwa ninamfahamu Rais Nelson na ikiwa nimewahi kupata nafasi ya kusalimiana naye kwa mkono. Nilijibu kwamba nilikuwa namfahamu, na kwamba nilikuwa nimewahi kusalimiana naye kwa mkono na kwamba, kama mshiriki wa Uaskofu Simamizi nilikuwa na nafasi ya kukutana na Rais Nelson na washauri wake mara kadhaa kila wiki.

Shemasi mdogo kisha akaketi kwenye kiti, akarusha mikono yake juu hewani, na kusema kwa sauti kubwa, “Hii ni siku kuu zaidi katika maisha yangu!” Akina kaka na akina dada, siwezi kurusha mikono yangu hewani na kusema kwa sauti kubwa, lakini ninashukuru milele kwa nabii aliye hai na kwa mwongozo tunaopokea kutoka kwa manabii, waonaji, na wafunuzi, hususan nyakati hizi za changamoto.

Tangu mwanzo wa nyakati, Bwana ametoa mwongozo ili kuwasaidia watu Wake kujiandaa kiroho na kimwili dhidi ya majanga na majaribu ambayo Yeye anajua yatakuja kama sehemu ya uzoefu wa duniani. Majanga haya yanaweza kuwa ya binafsi au ya jumla kwa asili, lakini mwongozo wa Bwana utatoa ulinzi na msaada kwa kiwango ambacho tunatii na kutendea kazi ushauri Wake. Mfano mzuri unatolewa katika maelezo kutoka kitabu cha Mwanzo, ambapo tunajifunza juu ya Yusufu wa Misri na tafsiri yake yenye mwongozi wa kiungu ya ndoto ya Farao.

“Ndipo Yusufu akamwambia Farao, … Mungu amemfunuliwa Farao mambo atakayofanya hivi karibuni. …

“Tazama, inakuja miaka saba ya chakula kingi katika nchi yote ya Misri.

“Lakini baadaye itafuata miaka saba ya njaa; hata hiyo shibe isahaulike kabisa katika nchi ya Misri.” 1

Farao alimsikiliza Yusufu, akaitikia kile Mungu alichokuwa amemwonyesha katika ndoto na mara moja akaanza kujiandaa kwa kile kitakachokuja. Maandiko kisha yanasema:

“Ikawa katika miaka ile saba ya shibe, nchi ikazaa kwa wingi sana.

“Akakusanya chakula chote cha miaka ile saba. …

“Na Yusufu akakusanya nafaka kama mchanga wa pwani, … hata akaacha kuhesabu; maana ilikuwa haina hesabu.” 2

Mara tu miaka saba ya neema ilipopita, tunaambiwa kwamba “ikaanza kuja miaka ile saba ya njaa, kama vile Yusufu alivyosema: kukawa na njaa katika nchi zote, bali katika nchi yote ya Misri palikuwa na chakula.” 3

Leo tumebarikiwa kuongozwa na manabii ambao wanaelewa hitaji la sisi kujiandaa dhidi ya maafa “ambayo yanapaswa kuja” 4 na ambao pia wanatambua mapungufu au vizuizi ambavyo tunaweza kukutana navyo katika kujitahidi kufuata ushauri wao.

Kuna ufahamu ulio wazi kwamba athari za COVID-19, pamoja na majanga angamizi ya asili, hayawapendelei watu na yanavuka mipaka ya kikabila, kijamii, na kidini katika kila bara. Kazi zimepotea na mapato yamepungua wakati fursa za kufanya kazi zimeathiriwa na kufutwa kazi na uwezo wa kufanya kazi umeathiriwa na changamoto za kiafya na kisheria.

Kwa wote ambao wameathiriwa, tunaelezea uelewa na kujali hali yako, na pia imani thabiti kwamba siku nzuri ziko mbele. Mmebarikiwa kuwa na maaskofu na marais wa matawi ambao wanawatafuta washiriki wa mikusanyiko wenye mahitaji ya kimwili na ambao wana vifaa na rasilimali ambazo zinaweza kuwasaidia kuanzisha tena maisha yenu na kuwaweka kwenye njia ya kujitegemea pale mnapofanyia kazi kanuni za kujitayarisha.

Katika mazingira ya leo, pamoja na janga ambalo limeharibu uchumi wote na maisha ya watu binafsi, itakuwa kinyume na Mwokozi mwenye huruma kupuuza ukweli kwamba wengi wanahangaika na kuwataka waanze kujenga hifadhi ya chakula na akiba ya pesa kwa ajili ya baadaye. Hata hivyo, hiyo haina maana kwamba tunapaswa kupuuza kabisa kanuni za kujitayarisha—ni kwamba tu kanuni hizi zinapaswa zitumike “kwa hekima na mpango” 5 ili kwamba baadaye tuweze kusema, kama vile Yusufu alivyosema huko Misri, “palikuwa na chakula.” 6

Bwana hatarajii sisi kufanya zaidi ya tunavyoweza kufanya, lakini Anatarajia sisi kufanya yale tunayoweza kufanya, pale tunapoweza kuyafanya. Kama Rais Nelson alivyotukumbusha katika mkutano wetu mkuu uliopita, “Bwana anapenda juhudi.” 7

Picha
Kitabu cha kiada cha Fedha Binafsi katika lugha tofauti

Viongozi wa kanisa mara nyingi wamewahimiza Watakatifu wa Siku za Mwisho “kujitayarisha kwa ajili ya shida katika maisha kwa kuwa na akiba ya chakula cha muhimu na maji na pesa zingine kwenye akiba.” 8 Wakati huo huo, tunahimizwa “kuwa na hekima” na “sio kupita kiasi” 9 katika juhudi zetu za kuanzisha hifadhi ya chakula nyumbani na akiba ya fedha. Nyenzo yenye jina Fedha Binafsi kwa ajili ya Kujitegemea, iliyochapishwa mnamo 2017 na inayopatikana sasa kwenye tovuti ya Kanisa katika lugha 36, inaanza na ujumbe kutoka kwa Urais wa Kwanza, ambao unasema:

“Bwana ametangaza, ‘Na ni madhumuni yangu kuwa niwapatie mahitaji watakatifu wangu’ [Mafundisho na Maagano 104:15]. Ufunuo huu ni ahadi kutoka kwa Bwana kwamba atatoa baraka za kimwili na kufungua mlango wa kujitegemea. …

“… Kukubali na kuishi kanuni hizi kutakuwezesha kupokea baraka za kimwili zilizoahidiwa na Bwana.

“Tunakualika kwa bidii ujifunze na kuzifanyia kazi kanuni hizi na uzifundishe kwa washiriki wa familia yako. Unapofanya hivyo, maisha yako yatabarikiwa … [kwa sababu] wewe ni mtoto wa Baba wa Mbinguni. Anakupenda na kamwe hatakutelekeza. Anakujua na yuko tayari kukupa baraka za kiroho na za kimwili za kujitegemea.” 10

Nyenzo hii inajumuisha sura zilizotengwa rasmi ili kufundisha kutengeneza na kuishi ndani ya bajeti, kulinda familia yako dhidi ya shida, kusimamia shida ya kifedha, kuwekeza kwa ajili ya siku zijazo na mengine mengi na inapatikana kwa kila mtu kwenye tovuti ya Kanisa au kupitia viongozi wako wa mahali ulipo.

Wakati tukizingatia kanuni ya kujitayarisha, tunaweza kumtazama Yusufu huko Misri kwa ajili ya mwongozo wa kiungu. Kujua kitakachotokea hakungetosha kuwavusha kupita miaka ya “njaa” bila kiwango cha dhabihu wakati wa miaka ya mavuno mengi. Badala ya kula chote ambacho Farao angeweza kuzalisha, mipaka ilianzishwa na kufuatwa, kutoa chakula cha kutosha kwa mahitaji yao ya sasa, na pia ya baadaye. Haikutosha tu kujua kuwa nyakati za changamoto zingekuja. Walilazimika kuchukua hatua, na kwa sababu ya bidii yao, “palikuwa na chakula.” 11

Hii inatupeleka kwenye swali muhimu: “Kwa hivyo, nini basi?” Mahali pazuri pa kuanzia ni kuelewa kuwa vitu vyote ni vya kiroho kwa Bwana, “na hata kwa wakati wo wote” Yeye hajatupa sisi “sheria ambayo ni ya kimwili.” 12 Kila kitu, kisha, kinaelekeza kwa Yesu Kristo kama msingi ambao juu yake tunalazimika kujenga hata kujitayarisha kwetu kimwili.

Kuwa tuliojitayarisha kimwili na wenye kujitegemea inamaanisha “kuamini kwamba kupitia neema, au nguvu inayowezesha, ya Yesu Kristo na juhudi zetu wenyewe, tunaweza kujipatia mahitaji yote ya kiroho na ya kimwili ya maisha ambayo tunahitaji sisi wenyewe na familia zetu.” 13

Vipengele vya ziada vya msingi vya kiroho kwa ajili ya kujitayarisha kimwili ni pamoja na kutenda “kwa hekima na mpango,” 14 ambayo inamaanisha kujenga pole pole hifadhi ya chakula na akiba ya fedha, kwa muda, vilevile kukumbatia njia “ndogo na rahisi”, 15 ambazo ni dhihirisho la imani kwamba Bwana atakuza juhudi zetu ndogo lakini endelevu.

Tukiwa na msingi wa kiroho mahali pake, tunaweza kisha kufanikiwa kutumia elementi mbili muhimu za kujitayarisha kimwili—kusimamia fedha na hifadhi ya nyumbani.

Kanuni muhimu za kusimamia fedha zako zinajumuisha malipo ya zaka na matoleo, kuondoa na kuepuka madeni, kuandaa na kuishi ndani ya bajeti, na kujiwekea akiba kwa ajili ya siku zijazo.

Kanuni muhimu za uhifadhi wa nyumbani ni pamoja na uhifadhi wa chakula, uhifadhi wa maji, pamoja na mahitaji mengine kulingana na mahitaji ya mtu binafsi na ya familia, yote kwa sababu “ghala bora zaidi” 16 ni nyumbani, ambapo huwa “hifadhi inayopatikana zaidi wakati wa uhitaji.” 17

Tunapokumbatia kanuni za kiroho na kutafuta mwongozo wa kiungu kutoka kwa Bwana, tutaongozwa kujua mapenzi ya Bwana kwetu, binafsi na kama familia, na njia nzuri zaidi ya kutumia kanuni muhimu za kujitayarisha kimwili. Hatua muhimu zaidi ya zote ni kuanza.

Mzee David A. Bednar alifundisha kanuni hii wakati aliposema: “Kuchukua hatua ni zoezi la imani. … Imani ya kweli inalenga kwa, na katika Bwana Yesu Kristo na daima hutuongoza kwenye matendo.” 18

Akina kaka na akina dada, katika ulimwengu unaobadilika, lazima tujitayarishe kwa ajili ya yasiyotarajiwa. Hata pamoja na siku nzuri mbele yetu, tunajua kwamba vilele vya kimwili na mabonde ya vifo vitaendelea. Tunapotafuta kuwa waliojitayarisha kimwili, tunaweza kukabiliana na majaribu ya maisha kwa kujiamini zaidi, amani mioyoni mwetu, na kama Yusufu huko Misri, tutaweza kusema, hata wakati wa shida “palikuwa na chakula.” 19 Katika Jina la Yesu Kristo, amina.