Mkutano Mkuu
Kabiliana na Siku Zijazo kwa Imani
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Kabiliana na Siku Zijazo kwa Imani

Siku zijazo zitakuwa tukufu kwa wale ambao wamejitayarisha na ambao wanaendelea kujitayarisha kuwa vyombo mikononi mwa Bwana.

Hii imekuwa jioni isiyosahaulika. Dada zangu wapendwa, ni heshima kuwa pamoja nanyi. Mmekuwa kwenye mawazo yangu mara nyingi katika kipindi cha miezi hii michache iliyopita. Ninyi ni imara zaidi ya milioni nane. Hamna tu idadi bali nguvu za kiroho za kuubadilisha ulimwengu. Nimewatazama mkifanya hivyo wakati wa janga hili la ulimwengu.

Wengine wenu ghafla mlijikuta mkitafuta vifaa ambavyo vilikuwa vichache au kazi mpya. Wengi waliwafundisha watoto na kuwajulia hali majirani. Wengine waliwakaribisha wamisionari nyumbani mapema kuliko ilivyotarajiwa, wakati wengine mlibadilisha nyumba zenu kuwa Vituo vya Mafunzo ya Umisionari. Mmetumia teknolojia kuunganika na familia na marafiki, kuwahudumia wale ambao walihisi wametengwa, na kujifunza Njoo, Unifuate pamoja na wengine. Mmepata njia mpya za kuifanya Sabato kuwa ya furaha. Na mmetengeneza barakoa—mamilioni ya hizo!

Kwa huruma ya dhati na upendo, moyo wangu unawaendea wanawake wengi ulimwenguni kote ambao wapendwa wao wamekufa. Tunalia pamoja nanyi. Na tunawaombea. Tunawasifu na kuwaombea wote wanaofanya kazi bila kuchoka ili kulinda afya za wengine.

Ninyi wasichana pia mmekuwa wa kushangaza. Ingawa mitandao ya kijamii imejaa ubishani, wengi wenu mmepata njia za kuwatia moyo wengine na kushiriki nuru ya Mwokozi wetu.

Akina dada, nyote mmekuwa mashujaa kabisa! Ninastaajabia nguvu zenu na imani yenu. Mmeonyesha kuwa katika hali ngumu, mnaendelea kwa ujasiri. Ninawapenda, na nawahakikishia kwamba Bwana anawapenda na anaona kazi kubwa mnayoifanya. Asanteni! Kwa mara nyingine tena, mmethibitisha kuwa ninyi ni tumaini la Israeli!

Mnajumuisha matumaini ambayo Rais Gordon B. Hinckley alikuwa nayo kwenu alipotambulisha “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” miaka 25 iliyopita katika mkutano mkuu wa Septemba 1995 wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama. 1 Ni muhimu kwamba alichagua kutambulisha tangazo hili muhimu kwa akina dada wa Kanisa. Kwa kufanya hivyo, Rais Hinckley alisisitiza ushawishi usioweza kubadilishwa wa wanawake katika mpango wa Bwana.

Sasa, ningependa kujua nini mmejifunza mwaka huu. Je! umesogea karibu na Bwana, au unahisi uko mbali zaidi na Yeye? Na je, jinsi gani matukio ya sasa yamekufanya uhisi kuhusu siku zijazo?

Kwa kweli, Bwana amezungumzia siku yetu kwa maneno ya kutafakari. Alionya kuwa katika siku yetu “watu [wangevunjika] mioyo” 2 na kwamba hata wateule watakuwa katika hatari ya kudanganywa. 3 Alimwambia Nabii Joseph Smith kwamba “amani [ingeondolewa] kutoka duniani” 4 na majanga yangewapata wanadamu.

Walakini Bwana pia alitoa maono ya jinsi kipindi hiki kilivyo cha kushangaza. Alimpa msukumo Nabii Joseph Smith kutangaza kwamba “kazi … ya siku hizi za mwisho, ni yenye uzito na upana mkubwa. … Utukufu wake hauelezeki, na ukuu wake hauwezi kufikika.” 6

Sasa, ukuu hauwezi kuwa neno ambalo ungechagua kuelezea miezi hii michache iliyopita! Je! tunapaswa kushughulikia vipi unabii wenye huzuni na matamko matukufu juu ya siku zetu? Bwana alituambia jinsi ya kufanya hilo kwa hakikisho rahisi, lakini la kushangaza: “kama mmejitayarisha hamtaogopa.” 7

Ni ahadi iliyoje! Ni moja ambayo inaweza kubadilisha jinsi tunavyoona siku zetu zijazo. Hivi karibuni nilimsikia mwanamke mwenye ushuhuda mzito akikiri kwamba janga hilo, pamoja na tetemeko la ardhi katika Bonde la Salt Lake, vilikuwa vimemsaidia kugundua kuwa hakuwa amejitayarisha kama alivyodhani. Wakati nilipouliza ikiwa alikuwa akimaanisha akiba yake ya chakula au ushuhuda wake, alitabasamu na kusema, “Ndio!”

Ikiwa matayarisho ni ufunguo wetu wa kukabiliana na kipindi hiki cha maongozi ya Mungu na siku zetu zijazo kwa imani, tunawezaje kujitayarisha vyema?

Kwa miongo kadhaa, manabii wa Bwana wametuhimiza kuhifadhi chakula, maji, na akiba ya kifedha kwa ajili ya wakati wa uhitaji. Janga la sasa limeimarisha hekima ya ushauri huo. Ninawaomba kuchukua hatua kujitayarisha kimwili. Lakini nina wasiwasi zaidi juu ya matayarisho yenu ya kiroho na kihisia.

Katika hali hiyo, tunaweza kujifunza zaidi kutoka kwa Kapteni Moroni. Kama kamanda wa majeshi ya Wanefi, alikabiliwa na vikosi vya upinzani ambavyo vilikuwa na nguvu, wengi kwa idadi na wakatili. Kwa hivyo, Moroni aliwatayarisha watu wake kwa njia tatu muhimu.

Kwanza, aliwasaidia kutengeneza maeneo ambapo wangekuwa salama—“mahali pa ulinzi” alipaita hivyo. 8 Pili, alitayarisha “akili za watu kwa uaminifu kwa Bwana.” 9 Na tatu, kamwe hakuacha kuwatayarisha watu wake—kimwili au kiroho. 10 Acha tuzingatie kanuni hizi tatu.

Kanuni ya kwanza: tengeneza mahali pa ulinzi

Moroni aliimarisha kila mji wa Wanefi kwa matuta, ngome, na kuta. 11 Walamani walipokuja dhidi yao, “walishtushwa sana, kwa sababu ya hekima ya Wanefi katika kutayarisha mahali pao pa ulinzi. 12

Vivyo hivyo, wakati misukosuko inazidi kutuzunguka sisi, tunahitaji kutengeneza mahali ambapo sisi tupo salama, kimwili na kiroho. Wakati nyumba yako inapokuwa kimbilio binafsi la imani—ambapo Roho hukaa—nyumba yako inakuwa safu ya kwanza ya ulinzi.

Vivyo hivyo, vigingi vya Sayuni ni “kimbilio kutoka kwenye dhoruba” 13 kwa sababu vinaongozwa na wale ambao wana funguo za ukuhani na wanatumia mamlaka ya ukuhani. Unapoendelea kufuata ushauri wa wale ambao Bwana amewapa mamlaka kukuongoza, utahisi usalama zaidi.

Hekalu—nyumba ya Bwana—ni mahala pa usalama tofauti na pengine popote. Huko, ninyi akina dada mnajaliwa nguvu ya ukuhani kupitia maagano matakatifu ya ukuhani mnayofanya. 14 Huko, familia zenu zinaunganishwa milele. Hata mwaka huu, wakati ufikiaji wa mahekalu yetu umekuwa mdogo sana, endaumenti yako imekupa ufikiaji wa mara kwa mara wa nguvu za Mungu wakati ulipoheshimu maagano yako pamoja Naye.

Ikisemwa kwa urahisi, mahali pa ulinzi ni popote ambapo unaweza kuhisi uwepo wa Roho Mtakatifu na kuongozwa na Yeye. 15 Wakati Roho Mtakatifu yuko pamoja nawe, unaweza kufundisha ukweli, hata wakati ukweli unapopingana na maoni yaliyopo. Na unaweza kutafakari maswali ya dhati kuhusu injili katika mazingira ya ufunuo.

Ninawaalika, dada zangu wapendwa, kutengeneza nyumba ambayo ni mahali pa ulinzi. Na ninarudia upya mwaliko wangu kwenu wa kuongeza uelewa wenu wa nguvu ya ukuhani na wa maagano na baraka za hekalu. Kuwa na mahali pa ulinzi ambapo unaweza kujificha itakusaidia kukabiliana na siku zijazo kwa imani.

Kanuni namba mbili: Tayarisha akili yako kuwa mwaminifu kwa Mungu.

Tumefanya mradi mkubwa wa kuongeza maisha na uwezo wa Hekalu la Salt Lake.

Picha
Hekalu la Salt Lake kwenye ujenzi

Wengine walitilia shaka hitaji la kuchukua hatua hizo za kustaajabisha. Walakini, wakati Bonde la Salt Lake lilipopatwa na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 5.7 mapema mwaka huu, hekalu hili la heshima lilitikisika kiasi kwamba tarumbeta kwenye sanamu ya malaika Moroni ikaanguka! 16

Picha
Malaika Moroni pamoja na tarumbeta iliyoanguka

Kama vile msingi wa Hekalu la Salt Lake unavyotakiwa kuwa imara kuhimili majanga ya asili, misingi yetu ya kiroho lazima iwe imara. Kisha, wakati matetemeko ya kistiari yanapotikisa maisha yetu, tunaweza kusimama “thabiti na bila kutikisika” kwa sababu ya imani yetu. 17

Bwana alitufundisha jinsi ya kuongeza imani yetu kwa kutafuta “maarifa, hata kwa kujifunza na pia kwa imani.” 18 Tunaimarisha imani yetu katika Yesu Kristo tunapojitahidi kutii amri Zake na “daima kumkumbuka.” 19 Zaidi ya hayo, imani yetu huongezeka kila wakati tunapoonyesha imani yetu Kwake. Hiyo ndiyo maana ya kujifunza kwa imani.

Kwa mfano, kila wakati tunapokuwa na imani ya kutii sheria za Mungu—hata wakati maoni maarufu yanapotushusha—au kila wakati tunapopinga burudani au itikadi zinazosherehekea kuvunja maagano, tunatumia imani yetu, ambayo nayo huongeza imani yetu.

Zaidi ya hayo, ni vitu vichache vinajenga imani kuliko kuzama mara kwa mara katika Kitabu cha Mormoni. Hakuna kitabu kingine kinachoshuhudia juu ya Yesu Kristo kwa nguvu na uwazi kama hicho. Manabii wake, kama walivyoongozwa na Bwana, waliona siku yetu na wakachagua mafundisho na kweli ambazo zingetusaidia sisi zaidi. Kitabu cha Mormoni ni mwongozo wetu wa kuendelea kuishi katika siku za mwisho.

Kwa kweli, ulinzi wetu wa juu huja tunapojifunga nira kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo! Maisha bila Mungu ni maisha yaliyojawa na hofu. Maisha pamoja na Mungu ni maisha yaliyojawa na amani. Hii ni kwa sababu baraka za kiroho huja kwa waaminifu. Kupokea ufunuo binafsi ni mojawapo ya baraka hizo kuu.

Bwana ameahidi kwamba kama tutaomba, tunaweza kupokea “ufunuo juu ya ufunuo.” 20 Ninaahidi kwamba unapoongeza uwezo wako wa kupokea ufunuo, Bwana atakubariki kwa ongezeko la mwelekeo kwa ajili ya maisha yako na kwa karama nyingi za Roho.

Kanuni namba tatu: usiache kamwe kujitayarisha.

Hata wakati mambo yalipokwenda vizuri, Kapteni Moroni aliendelea kuwatayarisha watu wake. Hakuacha. Yeye hakuwahi kuridhika kamwe.

Mpinzani haachi kushambulia. Hivyo, hatuwezi kamwe kuacha kujitayarisha! Kadiri tunavyojitegemea—kimwili, kihisia, na kiroho—ndivyo tunavyojitayarisha zaidi kuzuia mashambulio ya Shetani yasiyokoma.

Akina dada wapendwa, ninyi ni hodari wa kujenga mahali pa ulinzi kwa ajili yenu na wale mnaowapenda. Zaidi, mna endaumenti takatifu inayowawezesha kujenga imani kwa wengine kwa njia za ushawishi. 21 Na ninyi kamwe hamkomi. Mmeonyesha hilo tena mwaka huu.

Tafadhali, endeleeni kusonga! Umakini wenu katika kulinda nyumba zenu na kupandikiza imani katika mioyo ya wapendwa wenu utaleta thawabu kwa vizazi vijavyo.

Dada zangu wapendwa, tuna mengi sana ya kuyatarajia! Bwana aliwaweka hapa sasa kwa sababu alijua mnao uwezo wa kupata suluhisho la ugumu wa sehemu ya mwisho ya siku hizi za mwisho. Alijua mngefahamu ukuu wa kazi Yake na kuwa na ari ya kusaidia kuitimiza.

Sisemi kwamba siku zijazo zitakuwa rahisi, lakini ninawaahidi kwamba siku zijazo zitakuwa tukufu kwa wale ambao wamejitayarisha na ambao wanaendelea kujitayarisha kuwa vyombo mikononi mwa Bwana.

Wapendwa dada zangu, si tu tuvumilie kipindi hiki cha sasa. Acha tukabiliane na siku zijazo kwa imani! Nyakati za misukosuko ni fursa kwetu kufanikiwa kiroho. Ni nyakati ambazo ushawishi wetu unaweza kupenya zaidi kuliko nyakati za utulivu.

Ninaahidi kwamba tunapotengeneza mahali petu pa ulinzi, kutayarisha akili zetu kuwa waaminifu kwa Mungu, na kamwe kutoacha kujitayarisha, Mungu atatubariki. Yeye “atatukomboa; ndio, mpaka kwamba [atazungumza] amani kwa roho zetu, na [atatupatia] imani kubwa, na … kutusababishia kwamba [tuwe] na matumaini kwake kwa ukombozi wetu.” 22

Unapojiandaa kukabiliana na siku zijazo kwa imani, ahadi hizi zitakuwa zako! Nashuhudia hayo, kwa onyesho langu la upendo kwa ajili yenu, na ujasiri wangu kwenu ninyi, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.