Mkutano Mkuu
Hifadhi Mabadiliko
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Hifadhi Mabadiliko

Kupitia Yesu Kristo, tunapewa nguvu ya kufanya mabadiliko ya kudumu. Tunapomgeukia Yeye kwa unyenyekevu, ataongeza uwezo wetu wa kubadilika.

Akina dada kwa kweli ni furaha kuwa pamoja nanyi.

Picha
Kulipia bidhaa sokoni

Fikiria mtu anakwenda sokoni kununua bidhaa. Kama akimlipa muuzaji zaidi ya gharama ya bidhaa hiyo, muuzaji atamrudishia chenji.

Picha
Kupokea chenji

Mfalme Benjamini aliwafundisha watu wake katika Amerika ya kale juu ya baraka nyingi tunazopokea kutoka kwa Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Aliumba mbingu, dunia na uzuri wote tunaoufurahia. 1 Kupitia Upatanisho Wake wenye upendo, Yeye anatoa njia kwa ajili yetu sisi kukombolewa kutokana na dhambi na kifo. 2 Tunapoonyesha shukrani zetu Kwake kwa kutii amri Zake kwa bidii, Yeye hutubariki kwa haraka, akituacha tuwe wadeni Wake daima.

Yeye hutupatia vingi, vingi zaidi ya thamani ya kile tunachoweza kumrudishia. Kwa hivyo, tunaweza kumpa nini Yeye, ambaye alilipa bei kubwa kwa ajili ya dhambi zetu? Tunaweza kumpa mabadiliko. Tunaweza kumpa mabadiliko yetu. Yanaweza kuwa mabadiliko ya mawazo, mabadiliko ya tabia, au mabadiliko katika mwelekeo tunaoelekea. Kama shukrani kwa ajili ya malipo yake yasiyokadirika kwa kila mmoja wetu, Bwana anatuomba kuwa na mabadiliko ya moyo. Mabadiliko Anayoyahitaji kutoka kwetu si kwa manufaa Yake, ila ya kwetu. Kwa hivyo, tofauti na mnunuzi sokoni ambaye angechukua chenji tuliyomrudishia, Bwana wetu mwenye rehema anatusishi tubaki na chenji.

Baada ya kusikia maneno yaliyozungumzwa na Mfalme Benjamini, watu wake walilia, wakitangaza kwamba mioyo yao ilikuwa imebadilika, wakisema, “Kwa sababu ya Roho wa Bwana Mwenyezi, ambaye ameleta mabadiliko makuu ndani yetu, … hatuna tamaa ya kutenda maovu tena, lakini kutenda mema daima.” 3 Maandiko hayasemi kwamba mara moja wakawa wakamilifu; badala yake, hamu yao ya kubadilika iliwalazimisha kuchukua hatua. Mabadiliko yao ya moyo yalimaanisha kumvua mwanamume au mwanamke wa tabia ya asili na kumsikiliza Roho kadiri walivyojitahidi kuwa zaidi kama Yesu Kristo.

Rais Henry B. Eyring anafundisha: “Uongofu wa kweli unategemea kutafuta kwa uhuru katika imani, kwa juhudi kubwa na maumivu kadhaa. Kisha ni Bwana anayeweza kutoa … muujiza wa utakaso na mabadiliko.” 4 Tukiunganisha juhudi zetu na uwezo wa Mwokozi wa kutubadilisha, tunapata kuwa viumbe wapya.

Nilipokuwa mdogo, nilijiona nikitembea kwenye njia ya mpando, iliyo wima kuelekea lengo langu la uzima wa milele. Kila wakati nilipofanya au kusema kitu kibaya, nilijihisi nikiteleza kurudi nyuma, na kuanza safari yangu upya. Ilikuwa kama kutua kwenye mraba mmoja kwenye mchezo wa watoto wa njia na ngazi ambazo zinakuteremsha kutoka juu kurudi mwanzo wa mchezo! Ilikuwa ya kukatisha tamaa! Lakini nilipoanza kuelewa mafundisho ya Kristo 5 na jinsi ya kuyatumia kila siku maishani mwangu, nikapata tumaini.

Picha
Mchakato wa mabadiliko unajumuisha uvumilivu

Yesu Kristo ametupatia mpangilio endelevu wa mabadiliko. Anatualika tuwe na imani Kwake, ambayo inatutia moyo kutubu—“imani na toba ambavyo huleta mabadiliko katika mioyo.” 6 Tunapotubu na kugeuza mioyo yetu kumuelekea Yeye, tunapata hamu kubwa ya kufanya na kuishi maagano matakatifu. Tunavumilia mpaka mwisho kwa kuendelea kutumia kanuni hizi kote katika maisha yetu na kumwalika Bwana ili atubadilishe. Kuvumilia hadi mwisho kunamaanisha kubadilika hadi mwisho. Sasa ninaelewa kuwa sianzi upya kwa kila jaribio lililoshindwa, lakini kwa kila jaribio, ninaendeleza mchakato wangu wa mabadiliko.

Kuna kifungu cha kutia moyo katika dhima ya Wasichana ambacho kinasema, “Ninathamini zawadi ya toba na kutafuta kuwa bora kila siku.” 7 Ninaomba kwamba tutathamini zawadi hii nzuri na kwamba tuwe na nia ya kutafuta mabadiliko. Wakati mwingine mabadiliko tunayohitaji kufanya yanahusishwa na dhambi nzito. Lakini mara nyingi, tunajitahidi kuboresha tabia zetu ili ziendane na sifa za Yesu Kristo. Chaguzi zetu za kila siku zinaweza kusaidia au kuzuia maendeleo yetu. Kidogo kidogo lakini kwa uimara, mabadiliko ya makusudi yatatusaidia kuwa bora. Usivunjike moyo. Mabadiliko ni mchakato wa maisha yote. Ninashukuru kwamba katika mapambano yetu ya kubadilika, Bwana hutuvumilia.

Kupitia Yesu Kristo, tunapewa nguvu ya kufanya mabadiliko ya kudumu. Tunapomgeukia Yeye kwa unyenyekevu, ataongeza uwezo wetu wa kubadilika.

Kwa kuongezea kwenye nguvu ya kubadilisha ya Upatanisho wa Mwokozi wetu, Roho Mtakatifu atatusaidia na kutuongoza tunapoweka juhudi zetu mbele. Anaweza hata kutusaidia kujua ni mabadiliko gani tunayohitaji kufanya. Tunaweza pia kupata msaada na kutiwa moyo kupitia baraka za ukuhani, sala, kufunga, na kuhudhuria hekaluni.

Vivyo hivyo, wanafamilia wanaoaminika, viongozi, na marafiki wanaweza kuwa msaada katika juhudi zetu za kubadilika. Nilipokuwa na umri wa miaka minane, mimi pamoja na kaka yangu mkubwa, Lee, tungetumia muda na rafiki zetu tukicheza kwenye matawi ya mti wa jirani. Tulipenda kuwa pamoja katika ushirika wa rafiki zetu kwenye kivuli cha mti huo. Siku moja, Lee alianguka kutoka kwenye mti na kuvunjika mkono. Kuvunjika mkono kulifanya iwe ngumu kwake kupanda mti peke yake. Lakini maisha ya mtini hayakuwa sawa bila yeye kuwapo. Kwa hivyo wengine wetu tulimsukuma kwa nyuma wakati wengine walimvuta mkono wake uliokuwa mzima, na bila juhudi nyingi, Lee alikuwa amerudi kwenye mti. Mkono wake ulikuwa bado umevunjika, lakini alikuwa nasi tena akifurahia urafiki wetu wakati akiendelea kupona.

Mara nyingi nimefikiria juu ya uzoefu wangu wa kucheza kwenye mti kama aina ya shughuli yetu katika injili ya Yesu Kristo. Katika kivuli cha matawi ya injili, tunafurahia baraka nyingi zihusianazo na maagano yetu. Wengine wanaweza kuwa wameanguka kutoka kwenye usalama wa maagano yao na wanahitaji msaada wetu kupanda tena kwenye usalama wa matawi ya injili. Inaweza kuwa ngumu kwao kurudi peke yao. Je, tunaweza kuvuta kidogo hapa na kuinua kidogo pale ili kuwasaidia kupona wakati wakifurahia urafiki wetu?

Kama una maumivu ya kuanguka, tafadhali ruhusu wengine wakusaidie kurudi kwenye maagano yako na baraka zinazotolewa na maagano hayo. Mwokozi anaweza kukusaidia kupona na kubadilika huku ukiwa umezungukwa na wale wanaokupenda.

Mara nyingi mimi hukimbilia kwa marafiki ambao sijawaona kwa miaka mingi. Wakati mwingine wanasema, “Hujabadilika kabisa!” Kila wakati ninaposikia hayo, mimi huguna kidogo, kwa sababu natumai nimebadilika katika miaka iliyopita. Natumai nimebadilika tangu jana! Natumai mimi ni mkarimu kidogo, mwenye kuhukumu kidogo, na mwenye huruma zaidi. Natumai ni mwepesi kuitikia mahitaji ya wengine, na natumai nina subira kidogo zaidi.

Ninapenda kupanda milima karibu na nyumbani kwangu. Mara nyingi, ninapata kijiwe ndani ya kiatu changu pale ninapotembea njiani. Hatimaye, mimi husimama na kutingisha kiatu changu. Lakini inanishangaza ni muda kiasi gani ninapanda kwa maumivu kabla ya kusimama na kuuondoa usumbufu huo.

Tunaposafiri katika njia ya agano, wakati mwingine mawe huingia kwenye viatu vyetu kwa njia ya mazoea mabaya, dhambi, au mitazamo mibaya. Kadiri tunavyoviondoa kwa kasi katika maisha yetu, ndivyo zaidi furaha yetu ya safari ya kimwili itakavyokuwa.

Kudumisha mabadiliko kunahitaji juhudi. Siwezi kufikiria kusimama njiani wakati wa safari ili tu kurudisha kwenye kiatu changu changarawe yenye kukasirisha na yenye uchungu ambayo nimeiondoa punde. Ni bora kwa kipepeo mzuri kuchagua kurudi kwenye kifukofuko chake kuliko kutaka kufanya hilo tena.

Ninashuhudia kwamba kwa sababu ya Yesu Kristo, tunaweza kubadilika. Tunaweza kurekebisha mazoea yetu, kubadilisha mawazo yetu, na kuboresha tabia zetu ili kuwa zaidi kama Yeye. Na kwa msaada Wake, tunaweza kuhifadhi mabadiliko. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.