Mkutano Mkuu
Nguvu ya Uponyaji ya Yesu Kristo
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Nguvu ya Uponyaji ya Yesu Kristo

Tunapokuja kwa Yesu Kristo kwa kuonyesha imani Kwake, kutubu, na kufanya na kutunza maagano, kuvunjika kwetu—licha ya kisababishi chake—kunaweza kuponywa.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, tumeshughulika na matukio mengi yasiyotegemewa. Upotevu wa maisha na mapato kutokana na janga lililoenea ulimwenguni kote kwa kweli vimeathiri jumuia na uchumi wa ulimwengu.

Matetemeko ya ardhi, moto, na mafuriko katika sehemu mbalimbali za ulimwengu, pamoja na maafa mengine yanayohusiana na hali ya hewa, yamewaacha watu wakihisi kukosa msaada, kukosa tumaini, na waliovunjika mioyo, wakijiuliza ikiwa maisha yao yatarejea kuwa sawa.

Acha niwaeleze hadithi binafsi kuhusu kuvunjika.

Wakati watoto wetu walipokuwa wadogo, waliamua kutaka kuchukuwa masomo ya piano. Mimi na mume wangu Rudy, tulitaka kuwapa watoto wetu fursa hii, lakini hatukuwa na piano. Hatukuweza kumudu kuwa na piano mpya, kwa hiyo Rudy alianza kutafuta iliyokwishatumika.

Mwaka ule kwa ajili ya Krismas, alitushangaza wote kwa piano, na kwa miaka yote, watoto wetu walijifunza kuipiga.

Picha
Piano ya zamani

Wakati vijana wetu walipokua na kuondoka nyumbani, piano ya zamani ilijawa na vumbi kwa hiyo tuliiuza. Miaka michache ilipita, na tulikuwa tumetunza kiasi cha fedha. Siku moja Rudy alisema, “Nafikiri ni muda sasa wa kupata piano mpya.”

Nilimwuuliza, “Kwa nini tupate piano mpya, wakati hakuna kati yetu anayeweza kuipiga?”

Alisema, “Oh, lakini tunaweza kupata piano ambayo inajicheza yenyewe! Kwa kutumia iPad, unaweza kuiprogramu piano kucheza zaidi ya nyimbo 4,000, ikiwa ni pamoja na nyimbo za kanisa, nyimbo za kwaya ya Tabernacle, Nyimbo zote za msingi, na nyingine nyingi zaidi.”

Rudy ana ushawishi mkubwa, nikisema kwa ufupi.

Picha
Piano mpya

Tulinunua piano mpya nzuri inayojicheza, na siku chache baadae, wanaume wawili, wenye nguvu waliileta nyumbani kwetu.

Niliwaonyesha wapi nilitaka ikae na niliwapa nafasi.

Picha
Kusogeza piano

Ilikuwa kubwa na nzito, na ili kuipitisha mlangoni, waliondoa miguu yake na kufanikiwa kuiweka piano kwa upande juu ya toroli ya mkono waliyokuja nayo.

Nyumba yetu ilikuwa kwenye mteremko kidogo, na kwa bahati mbaya mapema siku hiyo theluji ilianguka, na kuacha vitu vimelowa na matope mepesi. Unaweza kuona matokeo ya hili?

Wakati wanaume wakiisogeza piano juu ya mteremko mdogo, iliteleza, na nilisikia kishindo kikubwa. Piano ilikuwa imeanguka kutoka kwenye toroli na kugonga ardhi kwa nguvu sana kiasi kwamba iliacha mbonyeo mkubwa katika uwanja wetu wa nyasi.

Nilisema, “Oh, jamani. Mko Salama?”

Kwa shukrani wanaume wote wawili Walikuwa salama.

Macho yao yalikuwa wazi walipotazamana, kisha wakanitazama mimi na kusema, “Tunaomba radhi. Tutairudisha dukani na kumwambia meneja wetu awasiliane nawe.”

Punde meneja alikuwa akizungumza na Rudy kupanga kuletewa piano mpya. Rudy ni mpole na mwenye kusamehe, na alimwambia meneja ilikuwa SAWA kama wangerekebisha tu palipo haribika na kuirudisha piano ileile, lakini meneja alisisitiza wangeleta mpya.

Rudy alijibu, akisema, “Haitakuwa mbaya kiasi hicho. Itengeneze tu na irudishe.”

Meneja alisema, “Ubao umevunjika, na mara ubao unapovunjika, kamwe haiwezi kutoa sauti nzuri. Utapata piano mpya.”

Akina dada na akina kaka, je, sisi sote si kama piano hii, tumevunjika kidogo, tuna ufa, na tumeharibika, tukihisi kama kamwe hatutakuwa vizuri tena? Hata hivyo, tunapokuja kwa Yesu Kristo kwa kuonyesha imani Kwake, kutubu, na kufanya na kutunza maagano, kuvunjika kwetu—licha ya kisababishi chake—kunaweza kuponywa. Mchakato huu, ambao hualika nguvu ya Mwokozi ya uponyaji kwenye maisha yetu, hauturejeshi tu sisi kwenye kile tulichokuwa kabla bali hutufanya bora zaidi ya tulivyowahi kuwa. Ninajua kwamba kupitia mwokozi wetu, Yesu Kristo, sote tunaweza kurekebishwa, kufanywa wakamilifu, na kutimiza lengo letu, kama vile piano mpya-kabisa, inayotoa sauti ya kupendeza.

Rais Russell M. Nelson alifundisha: “Wakati mateso yenye uchungu yanapotujia, ni muda wa kuongeza imani yetu katika Mungu, kufanya kazi kwa bidii, na kuwatumikia wengine. Kisha Yeye atatuponya mioyo yetu iliyovunjika. Atatoa juu yetu amani binafsi na faraja. Karama hizo kubwa haziwezi kuharibiwa, hata kwa kifo.” 1

Yesu alisema:

“Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.

“Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi” (Mathayo 11:28–30).

Picha
Mwokozi wetu, Yesu Kristo

Ili kupona uvunjikaji kwa kuja Kwake, tunahitaji kuwa na imani katika Yesu Kristo. “Kuwa na imani katika Yesu Kristo inamaanisha kumtegemea Yeye kikamilifu—kuamini katika nguvu Yake isiyo na kikomo … na upendo Wake. Inajumuisha kuamini mafundisho Yake. Inamaanisha kuamini kwamba hata kama hatuelewi vitu vyote, Yeye anaelewa. Kwa sababu amepata uzoefu wa maumivu yetu yote, mateso, na udhaifu, Anajua jinsi ya kutusaidia kuinuka juu ya magumu yetu ya kila siku.” 2

Tunapokuja Kwake, “tunaweza kujazwa na furaha, amani, na faraja. Yote yale ambayo ni [magumu na yenye changamoto] kuhusu maisha yanaweza kufanywa sawa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.” 3 Yeye ametushauri, “Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope” (Mafundisho na Maagano 6:36)

Katika Kitabu cha Mormoni wakati Alma na watu wake walipokaribia kuzidiwa na mizigo waliyotwishwa, watu walisihi wapate msaada. Bwana hakuondoa mizigo yao; badala yake aliwaahidi:

“Na pia nitawapunguzia mizigo ambayo imewekwa mabegani mwenu, hata kwamba hamtaisikia kamwe migongoni mwenu, hata mkiwa utumwani; na nitafanya haya ili muwe mashahidi wangu hapo baadaye, na kwamba mjue kwa hakika kwamba mimi, Bwana Mungu, huwatembelea watu wangu katika mateso yao.

“Na sasa ikawa kwamba mizigo ambayo ilikuwa wamewekewa Alma na ndugu zake ilifanywa miepesi; ndio, Bwana aliwapa nguvu kwamba wabebe mizigo yao kwa urahisi, na walitii kwa furaha na subira kwa mapenzi yote ya Bwana” (Mosia 24:14–15).

Juu ya uwezo wa Mwokozi kuponya na kufanya miepesi mizigo, Mzee Tad R. Callister amefundisha:

“Moja ya baraka za Urejesho ni kwamba tunaweza kupokea nguvu ya usaidizi ya Mwokozi. Isaya alizungumzia mara kwa mara juu ya uponyaji wa Bwana, ushawishi tulivu. Alishuhudia kwamba Mwokozi alikuwa ‘ngome ya mhitaji katika dhiki yake, mahali pa kukimbilia wakati wa tufani, kivuli wakati wa hari’ (Isaya 25:4). Na kwa hao wenye huzuni, Isaya alitangaza kwamba Mwokozi alikuwa na nguvu za ‘kuwafariji wote waliao’ (Isaya 61:2), na ‘atafuta machozi katika nyuso zote’ (Isaya 25:8; ona pia Ufunuo 7:17); ‘kuhuisha roho ya unyenyekevu’ (Isaya 57:15); na ‘kuwaganga waliovunjika moyo’ (Isaya: 61:1; ona pia Luka 4:18; Zaburi 147:3). Uliofikia kote ulikuwa uwezo wake wa kusaidia kwamba angeweza kubadili ‘taji la maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito’ (Isaya 61:3).

“Oh, matumaini yaliyoje yanapaa katika ahadi hizo! … Roho wake anaponya; anatakasa; anafariji; anatoa maisha mapya kwenye mioyo isiyo na matumaini. Ana nguvu ya kubadilisha vyote ambavyo ni vibaya na viovu na visivyofaa katika maisha kuwa kitu fulani chenye mamlaka na fahari ya utukufu. Ana nguvu ya kubadili majivu ya kufa kuwa uzuri wa milele.” 4

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wetu mpendwa, Mkombozi, Mponyaji Mkuu, na rafiki mwaminifu. Kama tutamgeukia, atatuponya na kutufanya wazima tena. Ninashuhudia hili ni Kanisa Lake na anajitayarisha kurudi tena kwenye dunia hii kutawala kwa nguvu na utukufu. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Russell M. Nelson, “Yesu Kristo—Mponyaji Mkuu,” Liahona, Nov. 2005, 87.

  2. Imani katika Yesu Kristo,” Mada za Injili, topics.ChurchofJesusChrist.org

  3. Preach My Gospel: A Guide to Missionary Service,, toleo jipya (2018), 52, ChurchofJesusChrist.org.

  4. Tad R. Callister, Upatanisho Usio na Mwisho (2000), 206–7.