Mkutano Mkuu
Kumngojea Bwana
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Kumngojea Bwana

Imani humaanisha kumtegemea Mungu katika nyakati nzuri na mbaya, hata kama hiyo inajumuisha mateso fulani hadi tunapouona mkono Wake ukifunuliwa kwa niaba yetu.

Wapendwa kaka na dada zangu, sisi sote tunahamu—hakuna aizidiye yangu—ya kusikia hotuba ya kufunga kutoka kwa mpendwa nabii wetu, Rais Russell M. Nelson. Huu umekuwa mkutano wa kupendeza, lakini ni mara ya pili janga la COVID-19 linatulazimisha kuachana na utamaduni wetu wa kukusanyika katika kituo cha mikutano. Tumechoka sana na hili janga kiasi kwamba tunahisi kuvuta na kung’oa nywele zetu. Kiukweli, baadhi ya ndugu zangu tayari wameshachukua uamuzi huo. Tafadhali jueni kwamba tunaomba bila kukoma kwa ajili ya wale ambao wameathiriwa kwa njia yoyote ile hasa kwa yoyote aliyepoteza wapendwa wake. Kila mmoja anakubali kwamba hili limechukua muda mrefu, muda mrefu sana.

Je, ni kwa muda gani tutasubiri kupata msaada kutokana na ugumu ambao huja juu yetu? Je, vipi kuhusu kustahimili majaribu binafsi wakati tunaposubiri na kusubiri, na msaada kuonekana kuja pole pole sana? Kwa nini kucheleweshwa wakati mizigo inaonekana kuwa mizito kuliko tunavyoweza kuibeba?

Wakati tukijiuliza maswali kama haya, sisi tunaweza, kama tunajaribu, kusikiliza mwangwi wa kilio cha mwingine kutoka kwenye unyevunyevu unaotia kinyaa, chumba cha giza cha gereza wakati fulani wa majira ya baridi sana katika eneo lile.

“Ee Mungu, uko wapi?” tunasikia kutoka ndani ya kina cha Jela ya Liberty. “Na ni wapi lilipo hema lifichalo mahali pako pa kujificha? Ni kwa muda gani mkono wako utazuiliwa?”1 Ni kwa muda gani, Ee Bwana, ni kwa muda gani?

Hivyo, sisi sio wa kwanza wala hatutakuwa wa mwisho kuuliza maswali kama haya wakati huzuni zikitulemea au maumivu moyoni mwetu yakiendelea na kuendelea. Mimi sasa siongelei majanga au magereza bali juu ya ninyi, familia zenu, na majirani zenu ambao wanakabiliwa na idadi yoyote ya changamoto za namna hiyo. Ninaongelea matamanio ya wengi ambao wangetaka kuolewa na hawaolewi au wale ambao wameoa na wangetaka uhusiano wao ungekuwa wa kiselestia kidogo. Ninaongeleaa juu ya wale ambao wanashughulika na mwonekane usiotakiwa wa hali mbaya za kiafya—pengine hali moja isiyotibika—au wanaokabiliwa na mpambano wa maisha yote wa hitilafu ya kinasaba ambayo haina tiba. Ninaongelea juu ya mahangaiko yenye kuendelea ya changamoto za kimhemko na afya ya akili ambazo zinawalemea kiuzito nafsi za wengi wanaoteseka pamoja nao, na kwenye mioyo ya wale wanao wapenda na kuteseka pamoja nao. Ninaongelea juu ya wale masikini, ambao Mwokozi alituambia kamwe tusiwasahau, na ninaongelea juu yako wewe unayesubiria kurejea kwa mtoto, bila kujali umri, ambaye amechagua njia tofauti na ile uliyoomba yeye achukue.

Zaidi ya haya, ninatambua kwamba hata hii orodha ndefu ya mambo ambayo kwayo sisi binafsi tunasubiria haijaribu kuelezea wasiwasi wetu mpana wa kiuchumi, kisiasa na kijamii ambao unatukabili kwa pamoja. Baba yetu wa Mbinguni kwa uwazi anatutarajia sisi kushughulikia mambo haya yenye kuumiza umma vile vile ya kibinafsi, lakini kutakuwa na nyakati katika maisha yetu wakati ambapo hata jitihada zetu bora kabisa na za dhati, sala zetu za kusihi hazitazaa ushindi ambao tumeutamani, iwe hiyo ni kuhusu mambo mapana ya kidunia au yale madogo ya kibinafsi. Hivyo wakati tukifanya kazi na kusubiri kwa pamoja majibu kwa baadhi ya maombi yetu, ninawapeni ninyi ahadi yangu ya kitume kwamba zimesikika na zinajibiwa, ingawa pengine sio kwa wakati ule, au katika njia tunayotaka sisi. Lakini daima zinajibiwa katika wakati na katika njia ya mzazi mjua yote na mwenye huruma anavyopaswa kuyajibu. Wapendwa kaka zangu na dada zangu, tafadhali fahamuni kwamba Yeye ambaye kamwe halali wala kusinzia2 anajali furaha na hatima ya kuinuliwa kwa watoto Wake juu ya vitu vingine vyote ambavyo kiumbe mtakatifu atafanya. Yeye ni upendo safi, kiumbe aliyetukuka, na Baba Mwenye Huruma ndilo jina Lake.

“Kama hivyo ndivyo,” ungeweza kusema, “je, kwa nini upendo Wake na rehema Yake visingeigawa Bahari yetu binafsi ya Shamu na kuturuhusu sisi kutembea ili kuvuka matatizo yetu juu ya nchii kavu? Je, Yeye asingepaswa kuwatuma shakwe wa baharini wa karne ya 21 wakiruka kutoka mahali fulani ili wawameze wadudu wasumbufu walio kwetu wa karne ya 21?”

Jibu kwa swali kama hilo ni “Ndiyo, Mungu anaweza kutoa miujiza wakati huo huo, lakini punde au baadae tunajifunza kwamba nyakati na majira ya safari yetu duniani ni Yake na Yake yeye pekee kuongoza.” Huitawala kalenda binafsi ya kila mmoja wetu. Kila mtu dhaifu anayeponywa mara moja wakati akisubiria kuingia Birika la Bethzatha,3 mtu mwingine atatumia miaka 40 jangwani akisubiri kuingia katika nchi ya ahadi.4 Kwa kila Nefi na Lehi wakilindwa kiungu na mwale wa moto kuwazunguka kwa ajili ya imani yao,5 tunaye Abinadi aliyeungua kwenye kiginga cha moto uwakao kwa ajili ya imani yake.6 Na tunakumbuka kwamba Eliya yule yule ambaye papo kwa papo aliita moto kutoka mbinguni ili kutoa ushuhuda dhidi ya makuhani wa Baali7 ndiye huyo huyo Eliya ambaye aliyevumilia kipindi ambapo hapakuwa na mvua kwa miaka kadhaa na ambaye, kwa wakati, alilishwa tu kwa chakula kidogo mno ambacho kiliweza kubebwa na kucha za kunguru.8 Kwa makadirio yangu, hicho hakiwezi kuwa kitu chochote tunachoweza kuita “mlo wa kufurahia.”

Hoja ni? Hoja ni kwamba imani inamaanisha kumtegemea Mungu katika nyakati nzuri na mbaya, hata kama hiyo inajumuisha mateso fulani hadi tunapouona mkono Wake ukifunuliwa kwa niaba yetu.9 Hiyo inaweza kuwa vigumu katika ulimwengu wetu wa kileo wakati wengi wamekuja kuamini kwamba mema ya juu zaidi katika maisha ni kuepuka mateso yote, kwamba mtu yeyote hapaswi kuomboleza juu ya chochote.10 Lakini kuamini huko kamwe hakuwezi kutuongoza kwenye “kipimo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.”11

Pamoja na kuomba msamaha kwa Mzee Neal A. Maxwell kwa kuthubutu kurekebisha na kurefusha kitu fulani wakati mmoja alisema, mimi pia napendekeza kwamba “maisha ya mtu … hayawezi kuwa vyote yaliyojaa-imani na yasiyo na msongo wa mambo.” Haiwezekani tu “kuteleza kinyoofu hadi mwisho wa maisha yote,” tukisema kama vile tunapokunywa glasi nyingine ya maji ya limau yaliyotiwa sukari: “Bwana nipe mema teule yako yote, lakini uwe na uhakika hutanipa machungu, huzuni, wala maumivu, wala upinzani. Tafadhali usiache mtu yeyote asinipende au kunisaliti, na zaidi ya hayo, kamwe usiache nijisikie nimesahaulika na Wewe au wale niwapendao. Kwa kweli, Bwana, uwe mwangalifu kuniweka mimi mbali na matukio yote ambayo yalikufanya Wewe uwe mtukufu. Lakini wakati kuteleza kugumu kwa wengine kukimalizika, tafadhali acha mimi nije na kuishi na Wewe, ambapo nitaweza kujigamba kuhusu namna ya mfanano tulionao wakati nikielea kwa shangwe juu ya wingu langu la Ukristo usio na taabu.”12

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, Ukristo ni wenye kufariji, lakini mara nyingi sio usio na taabu. Njia iendayo kwenye utakatifu na furaha hapa na baada ya hapa ni ndefu na wakati mwingine ni yenye miamba. Inagharimu muda, inahitaji nguvu ya kung’ang’ania ili kuitembea. Lakini, bila shaka, thawabu yake kwa kufanya hivyo ni kubwa sana. Ukweli huu unafundishwa kwa uwazi zaidi na kwa msisitizo mkubwa katika mlango wa 32 wa Alma katika Kitabu cha Mormoni. Humo huyu kuhani mkuu anafundisha kwamba kama neno la Mungu limepandwa katika mioyo yetu kama mbegu tu, na kama tutaijali vya kutosha kuimwagilia maji, kungolea magugu, kuilisha, na kuihimiza, baadae itazaa matunda “ambayo ni ya thamani sana, … matamu kupita kiasi,” ulaji ambao unatuongoza kwenye hali ya kutokuwa na kiu tena na bila njaa.13

Masomo mengi yanafundishwa katika mlango huu maarufu, lakini kitovu cha yote ni usemi unaochukuliwa kuwa kweli bila uthibitisho wa hoja kwamba ile mbegu inahitaji kulishwa na lazima tusubiri ikomae, “tukitazamia kwa jicho la imani matunda yake.”14 Mavuno yetu, Alma anasema, yanakuja “hatua kwa hatua.”15 Kwa mshangao kidogo anahitimisha maelekezo yake mazuri kwa kurudia mara tatu wito wa bidii na subira katika kulisha neno la Mungu katika mioyo yetu, “kusubiri” kwa “uvumilivu mkubwa,” kama asemevyo, “kwa mti kukuletea matunda.”16

COVID na saratani, mashaka na hofu, matatizo ya kifedha na majaribu ya kifamilia. Ni lini mizigo hii itaondoshwa? Jibu ni “hatua kwa hatua.”17 Na ama kwamba itakuwa kipindi kifupi au kile kirefu daima sio juu yetu sisi kusema, lakini kwa neema ya Mungu baraka zitakuja kwa wale wanaoshikilia kwa nguvu kwenye injili ya Yesu Kristo. Jambo hili lilimalizwa katika bustani ya faragha na juu ya kilima cha umma huko Yerusalemu miaka mingi iliyopita.

Sasa tunapomsikiliza mpendwa nabii wetu akifunga mkutano huu, naomba tukumbuke kama Russell Nelson ambavyo ameonyesha maisha yake yote, kwamba wale “wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya [na] watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; … watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.”18 Ninaomba kwamba “hatua kwa hatua”—punde au baadae—baraka zile zije kwa kila mmoja wenu anayetafuta msaada kutokana na masikitiko yenu na uhuru kutokana na huzuni zenu. Ninatoa ushahidi wa upendo wa Mungu na wa Urejesho wa injili Yake tukufu, ambayo ndiyo jibu la kila jambo linalotukabili. Katika jina takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.