Mkutano Mkuu
Mioyo Iliyounganishwa katika Haki na Umoja
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Mioyo Iliyounganishwa katika Haki na Umoja

Katika kipindi hiki cha miaka 200 katika historia yetu ya Kanisa, acha tujiwekee msimamo wa kuishi kwa haki na kuwa na umoja kuliko hapo awali.

Haki na umoja ni vya maana sana. 1 Wakati watu wanapompenda Mungu kwa mioyo yao yote na kwa haki wakijitahidi kuwa kama Yeye, kunakuwa na ugomvi na malumbano machache katika jamii. Kunakuwa na umoja zaidi. Ninapenda maelezo ya kweli ambayo yanaonyesha hili.

Kama kijana asiye wa imani yetu, Jenerali Thomas L. Kane aliwasaidia na kuwatetea Watakatifu walipokuwa wakitakiwa kuondoka Nauvoo. Yeye alikuwa wakili wa Kanisa kwa miaka mingi. 2

Mwaka 1872, Generali Kane, mke wake mwenye vipaji, Elizabeth Wood Kane, na wana wao wawili walisafiri kutoka nyumbani kwao huko Pennsylvania kwenda Jijini Salt Lake. Waliandamana na Brigham Young na washirika wake katika safari ya kusini hadi St. George, Utah. Elizabeth alikaribia kufika Utah kwa mara ya kwanza huku akiwafikiria wanawake. Alishangazwa na baadhi ya vitu alivyojifunza. Kwa mfano, aligundua kuwa kazi yoyote ambayo kwayo mwanamke angeweza kupata pesa ilikuwa wazi kwao huko Utah. 3 Aligundua pia kuwa waumini wa Kanisa walikuwa wema na wenye uelewa kwa Waamerika wa Asili. 4

Wakati wa safari walifikia Fillmore nyumbani kwa Thomas R. na Matilda Robison King. 5

Elizabeth aliandika kwamba wakati Matilda akiwa anaandaa chakula kwa ajili ya Rais Young na kundi lake, Wahindi watano wa Amerika waliingia ndani. Ingawa hawakualikwa, ilikuwa wazi kuwa walitarajia kuungana na na kundi hilo. Dada King alizungumza nao “katika lahaja yao.” Walikaa chini na mablanketi yao wakiwa na furaha kwenye nyuso zao. Elizabeth alimwuliza mmoja wa watoto wa King, “Mama yako alisema nini kwa wanaume hao?”

Jibu la mtoto wa Matilda lilikuwa “Alisema, Hawa wageni walifika mwanzo, na nimewapikia chakula cha kuwatosha wao tu; lakini chakula chenu kiko kwenye moto kinapikwa, na nitawaita mara tu kitakapokuwa tayari.’”

Elizabeth aliuliza, “Je! Atafanya hivyo, au atawapa tu mabaki kwenye mlango wa jikoni?” 6

Mtoto wa Matilda alijibu, “Mama atawahudumia kama vile anavyokufanyia wewe, na kuwapa nafasi kwenye meza yake.”

Na hivyo ndivyo alivyofanya, na “walikula kwa usahihi kamili.” Elizabeth alielezea kwamba mhudumu huyu wa kike alipanda kwa asilimia 100 kwenye maoni yake. 7 Umoja huimarishwa wakati watu wanapotendewa kwa utu na heshima, hata ingawa wapo tofauti katika tabia za nje.

Kama viongozi, hatuko chini ya udanganyifu kwamba zamani mahusiano yote yalikuwa makamilifu, mwenendo wote ulikuwa kama wa Kristo, au maamuzi yote yalikuwa ya haki. Walakini, imani yetu inafundisha kwamba sisi sote ni watoto wa Baba yetu wa Mbinguni, na tunamwabudu Yeye na Mwanawe, Yesu Kristo, ambaye ni Mwokozi wetu. Tamaa yetu ni kwamba mioyo na akili zetu viunganishwe katika haki na umoja, na kwamba tuwe kitu kimoja pamoja Nao. 8

Haki ni neno pana, lenye mambo mengi lakini hakika linajumuisha kuishi amri za Mungu. 9 Inatustahilisha kwa ajili ya ibada takatifu ambazo zinaanzisha njia ya maagano na kutubariki kuwa na Roho mwenye kutoa mwelekeo kwenye maisha yetu. 10

Kuwa mwenye haki hakutegemei kila mmoja wetu kuwa na kila baraka katika maisha yetu kwa wakati huu. Yawezekana tusiwe na ndoa au kubarikiwa kupata watoto au kuwa na baraka zingine tunazotamani sasa. Lakini Bwana ameahidi kwamba wenye haki ambao ni waaminifu “wanaweza kuishi na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho.” 11

Umoja pia ni neno pana, lenye mambo mengi lakini kwa hakika ni mfano wa amri kuu ya kwanza na ya pili ya kumpenda Mungu na kuwapenda wenzetu. 12 Linaashiria watu wa Sayuni ambao mioyo na akili zao “vimeunganishwa pamoja katika umoja.” 13

Muktadha wa ujumbe wangu ni utofauti na masomo kutoka katika maandiko matakatifu.

Imekuwa miaka 200 tangu Baba na Mwanawe kuonekana kwa mara ya kwanza na kuanzisha Urejesho wa injili ya Yesu Kristo mwaka 1820. Maelezo katika 4 Nephi katika Kitabu cha Mormoni yanajumuisha kipindi kama hicho cha miaka 200 baada ya Mwokozi kuonekana na kuanzisha Kanisa Lake katika Amerika ya zamani.

Kumbukumbu ya kihistoria tunayoisoma katika 4 Nefi inaelezea watu ambapo hakukuwa na wivu, ubishi, misukosuko, uwongo, mauaji, au uzinifu wa aina yoyote. Kwa sababu ya haki hii, kumbukumbu inasema “kwa kweli hakujakuwa na watu ambao wangekuwa na furaha zaidi miongoni mwa watu wote ambao waliumbwa na mkono wa Mungu.” 14

Kwa kuheshimu umoja, 4 Nefi inasomeka, “Hakukuwa na ubishi katika nchi, kwa sababu ya mapenzi ya Mungu ambayo yaliishi katika mioyo ya watu.” 15

Kwa bahati mbaya, 4 Nefi kisha inaelezea mabadiliko makubwa ambayo yalianza katika “mwaka wa mia mbili na moja,” 16 wakati uovu na mgawanyiko vilipoharibu haki na umoja. Undani wa upotovu uliotokea wakati huo ulikuwa mbaya sana hata kwamba nabii mkuu Mormoni anamlilia mwanawe Moroni:

“Lakini Ee mwana wangu, inawezekanaje watu kama hawa, ambao hupendezwa sana na machukizo mengi—

“Tunawezaje kutumaini kwamba Mungu atajizuia kutoa hukumu yake dhidi yetu?” 17

Katika kipindi hiki cha maongozi ya Mungu, ingawa tunaishi katika wakati maalum, ulimwengu haujabarikiwa kuwa na haki na umoja vilivyoelezewa katika 4 Nefi. Ndiyo, tunaishi katika wakati wa mgawanyiko mkubwa sana. Walakini, mamilioni ambao wameipokea injili ya Yesu Kristo wameweka msimamo wao wenyewe kufanikisha vyote haki na umoja. Sote tunatambua kuwa tunaweza kufanya vizuri zaidi, na hiyo ndiyo changamoto yetu katika siku hii. Tunaweza kuwa nguvu ya kuinua na kubariki jamii kwa ujumla. Katika kipindi hiki cha miaka 200 katika historia yetu ya Kanisa, acha tujiwekee msimamo kama waumini wa Kanisa la Bwana wa kuishi kwa haki na kuwa na umoja kuliko hapo awali. Rais Russell M. Nelson ametuomba “kuonyesha ustaarabu mkubwa, maelewano na heshima baina ya watu wa rangi na kabila mbali mbali.” 18 Hii inamaanisha kupendana na kumpenda Mungu na kumkubali kila mtu kama kaka na dada na kuwa kweli watu wa Sayuni.

Pamoja na mafundisho yetu yote ya ujumuishi, tunaweza kuwa chemchemi ya umoja na kusherehekea utofauti. Umoja na utofauti sio kinyume. Tunaweza kufikia umoja zaidi tunapoendeleza mazingira ya ujumuishi na kuheshimu utofauti. Katika kipindi nilichotumikia katika urais wa Kigingi wa San Francisco California, tulikuwa na mikusanyiko iliyozungumza Kihispania-, Kitonga-, Kisamoa-, Kitagalog-, na Kimandarini. Kata zetu zinazozungumza Kiingereza ziliundwa na watu kutoka asili tofauti za rangi na tamaduni. Kulikuwa na upendo, haki, na umoja.

Kata na matawi katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho yanaamuliwa kwa jiografia au lugha, 19 si kwa rangi au tamaduni. Rangi haijabainishwa kwenye rekodi za uumini.

Mapema katika Kitabu cha Mormoni, takriban miaka 550 kabla ya kuzaliwa kwa Kristo, tunafundishwa amri ya msingi kuhusu uhusiano kati ya watoto wa Baba wa Mbinguni. Wote wanapaswa kutii amri za Bwana, na wote wamealikwa kushiriki wema wa Bwana; “na hamkatazi yeyote ambaye anayemjia, mweusi kwa mweupe, wafungwa na walio huru, wake kwa waume; na anawakumbuka kafiri; na wote ni sawa kwa Mungu, wote wawili, Myahudi na Myunani.” 20

Huduma na ujumbe wa Mwokozi vimetangaza kila wakati kuwa watu wa jamii na rangi zote ni watoto wa Mungu. Sisi sote ni kaka na dada. Katika mafundisho yetu tunaamini kwamba katika nchi mwenyeji wa Urejesho, Marekani, Katiba ya Marekani 21 na hati zinazohusiana, 22 zilizoandikwa na watu wasio wakamilifu, ziliongozwa na Mungu ili kuwabariki watu wote. Tunaposoma katika Mafundisho na Maagano, nyaraka hizi “zilianzishwa, na zinatakiwa kulindwa kwa ajili ya haki na ulinzi wa wote wenye mwili, kulingana na kanuni zilizo za haki na takatifu.” 23 Kanuni mbili kati ya hizi zilikuwa haki ya kujiamulia na uwajibikaji kwa dhambi za mtu mwenyewe. Bwana alitangaza:

“Kwa hiyo, siyo sahihi kwamba mtu yeyote awe mtumwa kwa mtu mwingine.

“Na kwa dhumuni hili nimeiweka Katiba ya nchi hii, kwa mikono ya watu wenye hekima ambao niliwainua hasa kwa dhumuni hili, na kuikomboa nchi kwa kumwaga damu.” 24

Ufunuo huu ulipokelewa mwaka 1833 wakati watakatifu katika Missouri walikuwa wanapata mateso makubwa. Kichwa cha habari kwenye Mafundisho na Maagano sehemu ya 101 kinasomeka kwa sehemu: “Makundi ya watu wenye fujo yaliwafukuza kutoka majumbani mwao katika Wilaya ya Jackson. … Vitisho vya mauaji dhidi ya [waumini] wa Kanisa vilikuwa vingi.” 25

Huu ulikuwa wakati wa mvutano kwa pande kadhaa. Watu wengi wa Missouri waliwachukulia Wamarekani wa Asili kuwa adui asiye na huruma na walitaka waondoshwe kwenye ardhi. Kwa kuongezea, wakaazi wengi wa Missouri walikuwa wamiliki wa watumwa na walihisi kutishwa na wale ambao walikuwa wanapinga utumwa.

Kinyume chake, mafundisho yetu yaliwaheshimu Wamarekani wa Asili na hamu yetu ilikuwa kuwafundisha injili ya Yesu Kristo. Kuhusiana na utumwa, maandiko yetu yalikuwa yameonyesha wazi kwamba hakuna mtu anayepaswa kuwa mtumwa wa mwingine. 26

Mwishowe, Watakatifu walifukuzwa kwa nguvu kutoka Missouri 27 na kisha kulazimika kuhamia Magharibi. 28 Watakatifu walifanikiwa na kupata amani inayoambatana na haki, umoja, na kuishi injili ya Yesu Kristo.

Ninafurahi katika Maombezi ya Mwokozi yaliyoandikwa katika Injili ya Yohana. Mwokozi alikiri kwamba Baba alikuwa amemtuma na kwamba Yeye, Mwokozi, alikuwa amemaliza kazi Aliyotumwa kuifanya. Aliomba kwa ajili ya wanafunzi Wake na kwa wale watakaomwamini Kristo: “Kwamba wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu.” 29 Umoja ndio kitu ambacho Kristo alikiombea kabla ya kusalitiwa Kwake na Kusulubiwa.

Katika mwaka wa kwanza baada ya Urejesho wa injili ya Yesu Kristo, uliorekodiwa katika sehemu ya 38 ya Mafundisho na Maagano, Bwana anazungumza juu ya vita na uovu na anatangaza, “Ninawaambia, muwe na umoja; na kama hamna umoja ninyi siyo wangu.” 30

Utamaduni wa Kanisa letu unatoka kwenye injili ya Yesu Kristo. Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi ni wa maana. 31 Kanisa la kwanza huko Roma liliundwa na Wayahudi na Wayunani. Wayahudi hawa wa mwanzo walikuwa na tamaduni za Kiyahudi na “walishinda ukombozi wao, na wakaanza kuongezeka na kustawi.” 32

Wayunani huko Roma walikuwa na utamaduni wenye nguvu ya ushawishi mkubwa wa Kihelenistiki, ambao Mtume Paulo aliuelewa vizuri kwa sababu ya uzoefu wake huko Athene na Korintho.

Paulo anaweka injili ya Yesu Kristo kwenye mtindo wenye mambo mengi. Anaandika mambo yanayofaa kuhusu utamaduni wa Kiyahudi na Kiyunani 33 ambayo yanapingana na injili ya kweli ya Yesu Kristo. Kimsingi anawaomba kila mmoja wao aachane na vizuizi vya kitamaduni kutoka kwenye imani na tamaduni zao ambavyo havilingani na injili ya Yesu Kristo. Paulo anawahimiza Wayahudi na Wayunani kushika amri, kupendana na anakiri kwamba haki huleta wokovu. 34

Utamaduni wa injili ya Yesu Kristo siyo utamaduni wa Kiyunani au utamaduni wa Kiyahudi. Hautambuliwi kwa rangi ya ngozi ya mtu au mahali anapoishi. Wakati tunafurahia katika utofauti wa tamaduni, tunapaswa kuacha nyuma mambo ya tamaduni hizo ambayo yanapingana na injili ya Yesu Kristo. Waumini wetu na waongofu wapya mara nyingi hutoka kwenye asili tofauti za rangi na tamaduni. Ikiwa tunapaswa kufuata ushauri wa Rais Nelson wa kukusanya Israeli iliyotawanyika, tutapata kuona sisi ni tofauti kama Wayahudi na Wayunani walivyokuwa katika wakati wa Paulo. Hata hivyo tunaweza kuwa na umoja katika upendo wetu wa, na imani katika Yesu Kristo. Waraka wa Paulo kwa Warumi unarasimisha kanuni kwamba tunafuata utamaduni na mafundisho ya injili ya Yesu Kristo. Ni mfano wa kuigwa kwetu hata leo. 35 Ibada za hekaluni zinatuunganisha kwa njia maalum na kuturuhusu tuwe kitu kimoja kwa kila njia ya milele.

Tunawaheshimu waumini wetu waanzilishi ulimwenguni kote si kwa sababu walikuwa wakamilifu lakini kwa sababu walishinda magumu, walitoa dhabihu, walitamani kuwa kama Kristo, na walikuwa wakijitahidi kujenga imani na kuwa kitu kimoja na Mwokozi. Umoja wao pamoja na Mwokozi uliwafanya wawe na umoja kwa kila mmoja. Kanuni hii ni ya kweli kwako na kwangu leo.

Wito wa ufafanuzi kwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni kujitahidi kuwa watu wa Sayuni ambao wana moyo mmoja na nia moja na wanaishi katika haki. 36

Ni maombi yangu kwamba tutakuwa wenye haki na umoja na kufokasi kikamilifu kwenye kumtumikia na kumwabudu Mwokozi wetu, Yesu Kristo, ambaye ninashuhudia juu yake. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Mafundisho na Maagano 38:27.

  2. Huduma ya Thomas Kane kwa niaba ya waumini imekuwa ikionyeshwa mara kwa mara kama “kitendo cha dhabihu isiyo na ubinafsi kwa kijana mwenye itikadi ambaye alishuhudia udhalimu uliofanywa kwa watu wachache wa dini walioteswa na watu wengi wenye ukatili na uadui” (introduction to Elizabeth Wood Kane, Twelve Mormon Homes Visited in Succession on a Journey through Utah to Arizona, ed. Everett L. Cooley [1974], viii).

  3. Ona Kane, Twelve Mormon Homes, 5.

  4. Ona Kane, Twelve Mormon Homes, 40.

  5. Ona Lowell C. (Ben) Bennion and Thomas R. Carter, “Touring Polygamous Utah with Elizabeth W. Kane, Winter 1872–1873,” BYU Studies, vol. 48, no. 4 (2009), 162.

  6. Inavyoonekana, Elizabeth alidhani Wamarekani wengi wakati huo wangewapa Wahindi wa Amerika mabaki tu na kuwatendea tofauti na wageni wao wengine.

  7. Ona Kane, Twelve Mormon Homes, 64–65. Inashangaza kuwa Wamarekani wengi wa Asili, ikiwa ni pamoja na machifu kadhaa, walikuwa waumini wa Kanisa. Ona pia John Alton Peterson, Utah’s Black Hawk War (1998) 61; Scott R. Christensen, Sagwitch: Shoshone Chieftain, Mormon Elder, 1822–1887 (1999), 190–95.

  8. Katika kipindi hiki cha maongozi ya Mungu “wenye haki watakusanywa kutoka miongoni mwa mataifa yote, nao watakuja Sayuni, wakiimba nyimbo za shangwe isiyo na mwisho.” (Mafundisho na Maagano 45:71).

  9. Ona Mafundisho na Maagano 105:3–5. Maandiko yameteua kuwajali masikini na wahitaji kama kipengele muhimu cha haki.

  10. Ona Alma 36:30; ona pia 1 Nefi 2:20; Mosia 1:7. Sehemu ya mwisho ya Alma 36:30 inasomeka, “kadiri utakavyoacha kutii amri za Mungu utatolewa kwenye uwepo wake. Sasa hii ni kulingana na neno lake.”

  11. Mosiah 2:41. Rais Lorenzo Snow (1814–1901) alifundisha: “Hakuna Mtakatifu wa Siku za Mwisho anayekufa akiwa ameishi maisha ya uaminifu ambaye atapoteza chochote kwa sababu ya kushindwa kufanya mambo fulani wakati ambapo fursa hazikuruhusu yeye kufanya hivyo. Kwa maneno mengine, ikiwa mvulana au msichana hana fursa ya kufunga ndoa, na wanaishi maisha ya uaminifu mpaka wakati wa kifo chao, watapata baraka zote, kuinuliwa na utukufu ambao mwanamume au mwanamke yeyote atapata ambaye alikuwa na fursa hii na akaiboresha. Hilo ni hakika na chanya” ( Teachings of Presidents of the Church: Lorenzo Snow [2012], 130). Ona pia Richard G. Scott, “The Joy of Living the Great Plan of Happiness,” Ensign, Nov. 1996, 75.

  12. Ona 1 Yohana 5:2.

  13. Mosia 18:21; ona pia Musa 7:18.

  14. 4 Nefi 1:16.

  15. 4 Nefi 1:15.

  16. 4 Nefi 1:24.

  17. Moroni 9:13–14.

  18. Russell M. Nelson, katika “First Presidency and NAACP Leaders Call for Greater Civility, Racial Harmony,” Mei 17, 2018, newsroom.ChurchofJesusChrist.org; ona pia “President Nelson at Worldwide Priesthood Celebration,” Juni 1, 2018, newsroom.ChurchofJesusChrist.org.

  19. Mafundisho na Maagano 90:11 inasema, “Kila mtu atasikia utimilifu wa injili … katika lugha yake mwenyewe.” Kadiri ipasavyo, mikusanyiko ya lugha kwa kawaida huidhinishwa.

  20. 2 Nefi 26:33.

  21. Ona Katiba ya Marekani.

  22. Tazama Azimio la Uhuru la Marekani, 1776; Katiba ya Marekani, Marekebisho I–X (Muswada wa Haki), National tovuti ya Makavazi ya Taifa, archives.gov/founding-docs.

  23. Mafundisho na Maagano 101:77; msisitizo umeongezewa.

  24. Mafundisho na Maagano 101:79–80.

  25. Mafundisho na Maagano 101, kichwa cha habari cha sehemu.

  26. Ona Watakatifu: Hadithi ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, vol. 1, The Standard of Truth, 1815–1846 (2018), 172–74; James B. Allen and Glen M. Leonard, The Story of the Latter-day Saints, 2nd ed. (1992), 93–94; Ronald W. Walker, “Seeking the ‘Remnant’: The Native American during the Joseph Smith Period,” Journal of Mormon History vol. 19, no. 1 (spring 1993), 14–16.

  27. Ona Watakatifu, 1:359–83; William G. Hartley, “The Saints’ Forced Exodus from Missouri,” in Richard Neitzel Holzapfel and Kent P. Jackson, eds., Joseph Smith: The Prophet and Seer (2010), 347–89; Alexander L. Baugh, “The Mormons Must Be Treated as Enemies,” in Susan Easton Black and Andrew C. Skinner, eds., Joseph: Exploring the Life and Ministry of the Prophet (2005), 284–95.

  28. Ona Watakatifu: Hadithi ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, vol. 2, No Unhallowed Hand, 1846–1893 (2020), 3–68; Richard E. Bennett, We’ll Find the Place: The Mormon Exodus, 1846–1848 (1997); William W. Slaughter and Michael Landon, Trail of Hope: The Story of the Mormon Trail (1997).

  29. Yohana 17:21.

  30. Mafundisho na Maagano 38:27.

  31. Waraka kwa Warumi ni maarifa katika kutangaza mafundisho. Warumi inajumuisha mtajo pekee wa Upatanisho katika Agano Jipya. Nilikuja kuthamini Waraka kwa Warumi kwa kuwaunganisha watu anuwai kupitia injili ya Yesu Kristo wakati nilipohudumu kama rais wa kigingi nikiwa na waumini kutoka jamii na tamaduni nyingi wakizungumza lugha tofauti.

  32. Frederic W. Farrar, The Life and Work of St. Paul (1898), 446.

  33. Ona Farrar, The Life and Work of St. Paul, 450.

  34. Ona Warumi 13.

  35. Ona Dallin H. Oaks, “The Gospel Culture,” Liahona, Mar. 2012, 22–25; ona pia Richard G. Scott, “Removing Barriers to Happiness,” Ensign, Mei 1998, 85–87.

  36. Ona Musa 7:18.