Mkutano Mkuu
Wapendeni Adui Zenu
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Wapendeni Adui Zenu

Kujua kwamba sisi sote ni watoto wa Mungu hutupatia ono la thamani ya wengine na uwezo wa kuinuka juu ya chuki.

Mafundisho ya Bwana ni ya milele na kwa ajili ya watoto wote wa Mungu. Katika ujumbe huu nitatoa baadhi ya mifano kutoka Marekani, lakini kanuni ninazofundisha zinatumika kila mahali.

Tunaishi katika kipindi cha hasira na chuki katika mahusiano ya kisiasa na sera. Tumehisi hilo majira haya ya joto ambapo baadhi wameonyesha zaidi ya upingaji wa amani na kujihusisha katika tabia za uharibifu. Tunahisi hilo katika baadhi ya kampeni za sasa kwa ajili ya ofisi za umma. Kwa bahati mbaya, baadhi ya haya yamejipenyeza hata kwenye kauli za kisiasa na marejeleo yasiyo ya ukarimu katika mikutano yetu ya Kanisa.

Katika serikali yenye demokrasia daima tutakuwa na tofauti juu ya wagombea waliopendekezwa pamoja na sera. Hata hivyo, kama wafuasi wa Kristo lazima tuachane na hasira na chuki ambazo kwazo chaguzi za kisiasa zinajadiliwa au kutolewa shutuma katika mazingira ya aina nyingi.

Picha
Mahubiri ya Mlimani

Haya ni moja ya mafundisho ya Mwokozi wetu, huenda yajulikanayo vema lakini yanayoonekana kufanyiwa kazi kwa nadra:

“Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na umchukie adui yako.

“Lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, watendeeni mema wanaowachukia, na waombeeni wanaowatumia kwa hila, na kuwatesa” (Mathayo 5:43–44). 1

Kwa vizazi vingi, Wayahudi walikuwa wamefunzwa kuwachukia adui zao, na walikuwa kwa wakati huo wakiteseka chini ya utawala na udhalimu wa umiliki wa Rumi. Na bado Yesu aliwafundisha, “wapendeni adui zenu” na watendeeni mema … wanaowachukia ninyi.”

Picha
Yesu akifundisha huko Amerika

Ni mafundisho ya kimapinduzi yaliyoje kwa ajili ya mahusiano binafsi na ya kisiasa! Lakini hilo ndilo bado Mwokozi wetu anaamuru. Katika Kitabu cha Mormoni tunasoma “Kwani amin, amin, nawaambia, yule ambaye ana roho ya ubishi siye wangu, lakini ni wa ibilisi, ambaye ni baba wa ubishi, na huchochea mioyo ya watu kubishana na hasira mmoja kwa mwingine” (3 Nefi 11:29).

Kuwapenda watesi na adui zetu si rahisi. “Wengi wetu bado hatujafikia hatua hiyo ya … upendo na msamaha,” Rais Hinckley alisema, akiongeza, “Inahitaji nidhamu binafsi huenda kubwa kuliko tuliyonayo.” 2 Lakini lazima iwe ya muhimu, kwani ni sehemu ya amri mbili kuu za Mwokozi za “kumpenda Bwana Mungu wako” na “kumpenda jirani yako kama nafsi yako” (Mathayo 22:37, 39). Na lazima iwezekane, kwani Yeye pia amefundisha, “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona” (Mathayo 7:7). 3

Tunawezaje kushika amri hizi takatifu katika ulimwengu ambapo sisi pia tupo chini ya sheria za mwanadamu? Kwa bahati nzuri, tuna mfano wa Mwokozi mwenyewe wa jinsi ya kuweka usawa wa sheria Zake za milele na utekelezaji wa sheria zilizowekwa na mwanadamu. Wakati wajaribu walipojaribu kumtega kwa swali kuhusu ikiwa Wayahudi wanapaswa kulipa kodi kwa Rumi, Yeye alionyesha picha ya Kaisari kwenye sarafu zao na kutangaza, “Vya Kaisari mpeni Kaisari, na vya Mungu mpeni Mungu” (Luka 20:25). 4

Picha
Mpeni Kaisari

Kwa hiyo, tunapaswa kufuata sheria za wanadamu (kumpa Kaisari) ili tuishi kwa amani chini ya mamlaka ya kiraia, na tunafuata sheria za Mungu ili kuelekea takdiri yetu ya milele. Lakini tunafanyaje hili—hasa tunajifunzaje kuwapenda watesi wetu na maadui zetu?

Fundisho la Mwokozi la “kushinda hasira” ni hatua nzuri ya kwanza. Ibilisi ni baba wa ubishi, na ni yeye anayewachochea wanadamu wabishane kwa hasira. Anachochea mahusiano ya uadui na chuki kati ya watu na ndani ya makundi. Rais Thomas S. Monson alifundisha kwamba hasira ni “nyenzo ya Shetani,” kwani “kuwa na hasira ni kukubali ushawishi wa Shetani. Hakuna anayeweza kutufanya tukasirike. Ni uchaguzi wetu.” 5 Hasira ni njia ya mgawanyiko na uadui. Tunasogea kwenye kuwapenda maadui zetu wakati tunapoepuka hasira na uhasama kwa wale ambao tunatofautiana nao. Inasaidia pia ikiwa tuko tayari hata kujifunza kutoka kwao.

Kati ya njia zingine za kukuza uwezo wa kuwapenda wengine ni mbinu rahisi iliyoelezewa katika maneno ya muziki wa zamani sana. Wakati tunapojaribu kuelewa na kujihusisha na watu wa tamaduni tofauti tofauti, lazima tujaribu kuwajua. Katika nyakati zisizohesabika, wasiwasi wa mtu asiyekuwa wa mahali husika au hata uhasama hutoa nafasi kwa ajili ya urafiki au hata upendo wakati uhusiano wa mtu na mtu unapozalisha uelewa na heshima ya pamoja. 6

Msaada mkubwa zaidi katika kujifunza kuwapenda watesi na maadui zetu ni kutafuta kuelewa nguvu ya upendo. Yafuatayo ni mafundisho matatu ya kinabii kati ya mengi kuhusu hili.

Nabii Joseph Smith alifundisha kwamba “ni msemo wa muda mrefu kwamba upendo huzaa upendo. Acha tusambaze upendo—tuonyeshe ukarimu wetu kwa wanadamu wote.” 7

Rais Howard W. Hunter alifundisha: “Ulimwengu ambamo tunaishi ungenufaika kwa kiasi kikubwa kama wanaume na wanawake kila mahali wangekuwa na upendo msafi wa Kristo, ambao ni ukarimu, unyenyekevu na upole. Hauna wivu au kiburi. … Hautafuti chochote kama malipo. … Hauna nafasi kwa unyanyapaa, chuki, au vurugu. … Unawahimiza watu tofauti kuishi pamoja katika upendo wa Kikristo licha ya imani za kidini, rangi, utaifa, hali ya kifedha, elimu, au utamaduni.” 8

Na Rais Russell M. Nelson ametualika “kupanua mduara wetu wa upendo ili kukumbatia familia yote ya mwanadamu.” 9

Sehemu muhimu ya kuwapenda adui zetu ni kumpa Kaisari kwa kutii sheria za nchi zetu mbalimbali. Japokuwa mafundisho ya Yesu yalikuwa ya kimapinduzi, Yeye hakufundisha mapinduzi au uvunjifu wa sheria. Alifunza njia nzuri zaidi. Ufunuo wa siku za leo hutoa funzo sawa na hilo:

“Na mtu yeyote asivunje sheria za nchi, kwani yule ambaye hushika sheria za Mungu hana haja ya kuvunja sheria za nchi.

“Kwa hiyo, mzitii mamlaka zilizopo” (Mafundisho na Maagano 58:21–22).

Na makala yetu ya imani, iliyoandikwa na Nabii Joseph Smith baada ya Watakatifu wa mwanzo kuteseka mateso makali kutoka kwa viongozi wa Missouri, inatangaza, “Tunaamini katika kuwa chini ya wafalme, marais, watawala, na waamuzi, katika kutii, kuheshimu, na kuzishika sheria” (Makala ya Imani 1:12).

Hii haina maana kwamba tunakubaliana na yote yanayofanywa na nguvu ya sheria. Ina maana kwamba tunatii sheria ya sasa na tunatumia njia za amani kuibadili. Pia ina maana kwamba tunakubali kwa amani matokeo ya uchaguzi. Hatutashiriki kwenye vurugu zilizotishiwa na wale ambao hawakuridhika na matokeo. 10 Katika jamii yenye demokrasia mara zote tuna fursa na wajibu wa kuendelea kwa amani mpaka uchaguzi ujao.

Fundisho la Mwokozi la kuwapenda adui zetu lipo kwenye uhalisia kwamba watu wote ni watoto wapendwa wa Mungu. Kanuni hiyo ya milele na baadhi ya kanuni za msingi za sheria zilijaribiwa katika upingaji wa hivi karibuni katika miji mingi ya Marekani.

Picha
Upingaji wa amani

Kwa upande mmoja, baadhi wameonekana kusahau kwamba Marekebisho ya Kwanza kwenye Katiba ya Marekani yanatoa hakikisho la “haki ya watu kukusanyika kwa amani na kuiomba Serikali kutenda haki juu ya malalamiko.” Hiyo ni njia iliyoruhusiwa ya kuinua uelewa wa umma na kufokasi kwenye udhalimu katika maudhui au utawala wa sheria. Na kumekuwa na udhalimu. Katika matendo ya hadharani na katika mitazamo binafsi, tumesikia ubaguzi wa rangi na malalamiko kama hayo. Katika insha binafsi yenye ushawishi, Mchungaji Theresa A. Dear wa the National Association for the Advancement of Colored People (NAACP) ametukumbusha kwamba “ubaguzi wa rangi husitawi kwenye chuki, ukandamizaji, upinzani wa kimyakimya, utofauti na ukimya.” 11 Kama raia na kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, lazima tufanye vizuri zaidi kusaidia kungo’a ubaguzi wa rangi.

Picha
Vurugu zilizo kinyume na sheria

Kwa upande mwingine, wachache wa washiriki na waungaji mkono wa upingaji huu na matendo yaliyo kinyume na sheria ambayo yamefuatia wanaonekana kusahau kwamba upingaji unaolindwa na Katiba ni upingaji katika njia ya amani. Wapingaji hawana haki ya kuharibu, kufuja, au kuiba kitu au kukandamiza nguvu halali za polisi wa serikali. Katiba na sheria havina mwaliko wa mapinduzi au vurugu. Sisi sote—polisi, wapingaji, waungaji mkono, na washangiliaji—tunapaswa kuelewa ukomo wa haki zetu na umuhimu wa wajibu wetu kubaki ndani ya mipaka ya sheria iliyopo. Abraham Lincoln alikuwa sahihi aliposema, “Hakuna madai ambayo yanaweza kurekebishwa kwa ghasia.” 12 Marekebisho ya madai kwa ghasia ni marekebisho kwa njia isiyo halali. Hiyo ni vurugu, hali ambayo haina serikali na polisi madhubuti, ambayo inakandamiza badala ya kulinda haki za raia.

Sababu moja ya upingaji wa hivi karibuni wa Marekani kuwa wa kushtusha kwa wengi ilikuwa ni kwamba uhasama na ukosefu wa haki uliohisiwa kati ya makundi ya tamaduni mbalimbali katika mataifa mengine haupaswi kuhisiwa Marekani. Nchi hii inapaswa kuwa bora katika kuondoa ubaguzi wa rangi si tu dhidi ya Wamarekani Weusi, ambao walionekana sana katika upingaji wa hivi karibuni, bali pia dhidi ya Walatino, Waasia, na makundi mengine. Historia ya taifa hili ya ubaguzi wa rangi si ya kufurahisha na tunapaswa kufanya vizuri zaidi.

Picha
Kisiwa cha Ellis
Picha
Wahamiaji

Marekani iligunduliwa na wahamiaji wa mataifa mbalimbali na tamaduni mbalimbali. Lengo lake la kuunganisha halikuwa kuanzisha dini fulani au kukuza tamaduni anuwai zozote au uaminifu wa kikabila wa nchi za kale. Kizazi kilichoigundua kilitafuta kuwa na umoja kwa katiba na sheria mpya. Hii haina maana kusema kwamba hati zetu za kuleta umoja au uelewa wa kipindi hicho wa maana zao vilikuwa na ukamilifu. Historia ya karne mbili za kwanza za Marekani zilionyesha hitaji la marekebisho mengi, kama vile haki za kupiga kura kwa wanawake na, hasa, usitishaji wa utumwa, ikiwemo sheria za kuhakikisha kwamba wale ambao walikuwa utumwani wangepata haki zote za uhuru.

Wanazuoni wawili kutoka Chuo Kikuu cha Yale hivi karibuni walitukumbusha:

“Licha ya mapungufu mengi, Marekani ina uwezo wa kipekee wa kuunganisha jamii mbalimbali na zilizogawanyika. …

“… Raia wake si lazima wachague kati ya utambulisho wa utaifa na tamaduni nyingi. Wamarekani wanaweza kuwa na vyote. Lakini muhimu ni uzalendo wa kikatiba. Tunapaswa kubaki wenye umoja kwenye, na kupitia Katiba, licha ya kutofautiana kiitikadi.” 13

Miaka mingi iliyopita, katibu muhtasi wa mambo ya nje wa Uingereza alitoa ushauri huu mkuu katika mdahalo ndani ya Bunge: “Hatuna marafiki wa milele na hatuna maadui wa kudumu. Matamanio yetu ni ya milele na ya kudumu, na matamanio haya ni wajibu wetu kuyatafuta.” 14

Hiyo ni sababu nzuri ya kidunia ya kutafuta matamanio ya “milele na ya kudumu” katika maswala ya siasa. Kwa kuongezea, mafundisho ya Kanisa la Bwana yanatufunza tamanio jingine la milele la kutuongoza: mafundisho ya Mwokozi wetu, ambaye alitoa msukumo kwenye Katiba ya Marekani na sheria za msingi za nchi zetu nyingi. Uaminifu kwenye sheria zilizowekwa badala ya “ushirika” wa muda mfupi ni njia nzuri ya kuwapenda watesi na adui zetu wakati tunapotafuta umoja hata katika utofauti.

Kujua kwamba sisi sote ni watoto wa Mungu hutupatia ono la kiungu la thamani ya wengine wote na nia na uwezo wa kuinuka juu ya chuki na ubaguzi wa rangi. Kama nilivyoishi kwa miaka mingi katika sehemu tofauti za taifa hili, Bwana amenifunza kwamba inawezekana kutii na kutafuta kuboresha sheria za taifa letu na pia kuwapenda watesi na adui zetu. Japo si rahisi, inawezekana kwa msaada wa Bwana wetu, Yesu Kristo. Yeye alitoa amri hii ya kupenda, na Anaahidi usaidizi Wake pale tunapotafuta kuitii. Ninashuhudia kwamba tunapendwa na tutasaidiwa na Baba yetu wa Mbinguni na Mwana wake, Yesu Kristo. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona pia Luka 6:27–28, 30.

  2. Gordon B. Hinckley, “The Healing Power of Christ,” Ensign, Nov. 1988, 59; ona pia Teachings of Gordon B. Hinckley (1997), 230.

  3. Ona pia Mafundisho na Maagano 6:5.

  4. Ona pia Mathayo 22:21; Marko 12:17.

  5. Thomas S. Monson, “School Thy Feelings, O My Brother,” Liahona, Nov. 2009, 68.

  6. Ona Becky and Bennett Borden, “Moving Closer: Loving as the Savior Did,” Ensign, Sept. 2020, 24–27.

  7. Joseph Smith, katika Historia ya Kanisa, 5:517. Vilevile, Martin Luther King Jr. (1929–68) alisema: “Kulipiza vurugu kwa vurugu huzidisha vurugu, huongeza giza nene kwenye usiku usio na nyota. Giza haliwezi kufukuza giza: ni nuru pekee inaweza kufanya hivyo. Chuki haiwezi kufukuza chuki: ni upendo pekee unaweza kufanya hivyo” (Where Do We Go from Here: Chaos or Community? [2010], 64–65).

  8. Mafundisho ya Marais wa Kanisa: Howard W. Hunter (2015), 263.

  9. Russell M. Nelson, “Blessed Are the Peacemakers,” Liahona, Nov. 2002, 41; ona pia Teachings of Russell M. Nelson (2018), 83.

  10. Ona “A House Divided,” The Economist, Sept. 5, 2020, 17–20.

  11. Theresa A. Dear, “America’s Tipping Point: 7 Ways to Dismantle Racism,” Deseret News, June 7, 2020, A1.

  12. Abraham Lincoln, hotuba kwenye ukumbi wa mikutano wa Wavulana wa Springfield, Illinois, Jan. 27, 1838, katika John Bartlett, Bartlett’s Familiar Quotations (2012), 444.

  13. Amy Chua and Jed Rubenfeld, “The Threat of Tribalism,” Atlantic, Oct. 2018, 81, theatlantic.com.

  14. Henry John Temple, Viscount Palmerston, remarks in the House of Commons, Mar. 1, 1848; katika Bartlett, Bartlett’s Familiar Quotations, 392; msisitizo umeongezwa.