Mkutano Mkuu
Fanya kwa Haki, Penda Rehema, na Tembea kwa Unyenyekevu pamoja na Mungu
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Fanya kwa Haki, Penda Rehema, na Tembea kwa Unyenyekevu pamoja na Mungu

Kutenda kwa haki inamaanisha kutenda kwa heshima na Mungu na watu wengine. Tunatenda kwa heshima na Mungu kwa kutembea kwa unyenyekevu pamoja Naye. Tunatenda kwa heshima na wengine kwa kupenda rehema.

Kama wafuasi wa Yesu Kristo, na kama Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunajitahidi—na tunahimizwa kujitahidi—kufanya vizuri zaidi na kuwa bora.1 Labda umejiuliza, kama nilivyojiuliza, “Je, Ninafanya vya kutosha?” “Nini kingine ninapaswa kufanya?” au “Ninawezaje, kama mtu mwenye makosa, kustahili ‘kukaa na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho’?”2

Mika nabii wa Agano la Kale aliuliza swali hivi: “Nimkaribie Bwana na kitu gani, na kuinama mbele za Mungu aliye juu?”3 Kwa tashtiti Mika alijiuliza ikiwa hata sadaka kubwa mno ingeweza kutosha kufidia dhambi, akisema, “Je! Bwana atapendezwa na elfu za kondoo waume, au na [elfu] kumi … za mito ya mafuta? je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa … dhambi ya roho yangu?”4

Jibu ni hapana. Matendo mema hayatoshi. Wokovu hauchumwi.5 Hata dhabihu kubwa zilizopendekezwa na Mika haziwezi kukomboa dhambi ndogo kabisa. Tukiachwa kutumia njia zetu wenyewe, matarajio ya kurudi kuishi mbele za Mungu hayapo.6

Bila baraka ambazo zinatoka kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, hatuwezi kamwe kufanya vya kutosha au kuwa vya kutosha sisi wenyewe. Habari njema, hata hivyo, ni kwamba kwa sababu ya na kwa kupitia kwa Yesu Kristo tunaweza kuwa vya kutosha.7 Watu wote watakombolewa kutokana na kifo cha kimwili kwa neema ya Mungu, kupitia kifo na Ufufuo wa Yesu Kristo.8 Na ikiwa tutageuza mioyo yetu kwa Mungu, wokovu kutokana na kifo cha kiroho unapatikana kwa wote “kupitia Upatanisho wa [Yesu] Kristo … kwa utiifu wa sheria na ibada za Injili.”9 Tunaweza kukombolewa kutoka kwenye dhambi ili kusimama tukiwa safi na bila doa mbele za Mungu. Kama vile Mika alivyoeleza, “[Mungu] amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako?”10

Mwongozo wa Mika juu ya kugeuza mioyo yetu kwa Mungu na kufuzu kwa ajili ya wokovu una vitu vitatu vinavyoshabihiana. Kutenda kwa haki inamaanisha kutenda kwa heshima na Mungu na watu wengine. Tunatenda kwa heshima na Mungu kwa kutembea kwa unyenyekevu pamoja Naye. Tunatenda kwa heshima na wengine kwa kupenda rehema. Kwa hivyo kutenda kwa haki ni matumizi halisi ya amri kuu ya kwanza na ya pili, “kumpenda Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili yako yote … [na] kumpenda jirani yako kama nafsi yako.”11

Kutenda kwa haki na kutembea kwa unyenyekevu na Mungu ni kuondoa mikono yetu kwa kukusudia kutoka kwenye uovu, kutembea katika amri Zake, na kutenda kwa uaminifu.12 Mtu mwenye haki huacha dhambi na humwelekea Mungu, hufanya maagano Naye, na ni mwaminifu kwa maagano hayo. Mtu mwenye haki huchagua kushika amri za Mungu, kutubu anapokosea, na kuendelea kujaribu.

Wakati Kristo aliyefufuka alipowatembelea Wanefi, Alielezea kwamba sheria ya Musa ilibadilishwa na sheria ya juu zaidi. Aliwaamuru “wasitoe … dhabihu na … sadaka za kuteketezwa” tena lakini watoe “moyo uliopondeka na roho iliyovunjika.” Pia aliahidi, “Na yeyote atakayekuja kwangu kwa moyo uliopondeka na roho iliyovunjika, na huyo nitambatiza kwa moto na Roho Mtakatifu.”13 Tunapopokea na kutumia zawadi ya Roho Mtakatifu baada ya ubatizo, tunaweza kufurahia ushirika wa muda wote wa Roho Mtakatifu na kufundishwa vitu vyote ambavyo tunapaswa kufanya,14 pamoja na jinsi ya kutembea kwa unyenyekevu na Mungu.

Dhabihu ya Yesu Kristo kwa ajili ya dhambi na wokovu kutoka kwenye kifo cha kiroho vinapatikana kwa wote ambao wana moyo uliopondeka na roho iliyovunjika.15 Moyo uliopondeka na roho iliyovunjika hutuchochea kutubu kila siku na kujaribu kuwa kama Baba yetu wa Mbinguni na Yesu Kristo. Tunapofanya hivyo, tunapokea nguvu ya utakaso wa Mwokozi, uponyaji, na nguvu ya kutuimarisha. Hatutendi tu kwa haki na kutembea kwa unyenyekevu na Mungu, pia tunajifunza kupenda rehema kama vile Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanavyofanya.

Mungu hufurahia katika rehema na hana husda kwenye kuitumia. Maneno ya Mika kwa Yehova, “Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, … aliye na huruma kwetu,” na “atatupa dhambi … zote katika vilindi vya bahari.”16 Kupenda rehema kama vile Mungu anavyopenda hakuwezi kutenganishwa na kutenda kwa haki kwa wengine na sio kuwatendea vibaya.

Umuhimu wa kutowatendea wengine vibaya unaangaziwa katika hadithi fupi kuhusu Hillel Mkubwa, msomi wa Kiyahudi aliyeishi karne ya kwanza kabla ya Kristo. Mmoja wa wanafunzi wa Hillel alikasirishwa na ugumu wa Torati—vitabu vitano vya Musa na amri zake 613 na maandishi ya kiyahudi yaliyohusiana nazo. Mwanafunzi huyo alitoa changamoto kwa Hillel kuelezea Torati kwa kutumia muda ambao Hillel angeweza kusimama kwa mguu mmoja. Huenda Hillel hakuwa na uwezo mkubwa wa kuhimili lakini alikubali changamoto hiyo. Alinukuu kutoka kwenye Mambo ya Walawi, akisema, “Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako.”17 Kisha Hillel alihitimisha: “Jambo la kuchukiza kwako, usimfanyie jirani yako. Hii ndio Torati yote; yaliyobakia ni ufafanuzi. Nenda na ukajifunze.”18

Daima kuwatendea wengine kwa heshima ni sehemu ya upendo wa rehema. Fikiria mazungumzo niliyoyasikia miongo kadhaa iliyopita katika idara ya dharura ya Hospitali ya Johns Hopkins huko Baltimore, Maryland, nchini Marekani. Mgonjwa, Bwana Jackson, alikuwa mwenye heshima, mtu mwema na aliyejulikana sana kwa wafanyakazi wa hospitali. Hapo awali alikuwa amelazwa mara kadhaa kwa matibabu ya magonjwa yanayohusiana na pombe. Katika tukio hili, Bwana Jackson alirudi hospitalini kwa dalili ambazo zingetambuliwa kama maambukizi ya kongosho yaliyosababishwa na unywaji pombe.

Kuelekea mwisho wa zamu yake, Daktari Cohen, daktari anayefanya kazi kwa bidii na anayependwa, alimtathmini Bwana Jackson na akaamua kuwa kulazwa hospitalini kulifaa. Dkt. Cohen alimpanga Dkt. Jones, daktari aliyekuwa akifuatia kwenye zamu, kumchukua Bwana Jackson na kusimamia matibabu yake.

Dkt. Jones alikuwa amehudhuria shule ya kifahari ya utabibu na alikuwa ndio ameanza masomo yake ya shahada ya pili. Mafunzo haya magumu yalikuwa mara nyingi yanaambatana na kukosa usingizi, kitu ambacho pengine kilichangia mwitikio hasi wa Dkt. Jones. Ikiwa ni kwa mara ya tano kuingia zamu ya usiku, Dkt. Jones alilalamika kwa sauti kubwa kwa Dkt Cohen. Alihisi kuwa sio haki kwamba atalazimika kutumia masaa mengi kumshughulikia Bwana Jackson kwa sababu shida yake, hata hivyo, ilikuwa ya kujitakia.

Jibu la msisitizo la Dkt. Cohen lilizungumzwa kama mnong’ono. Alisema, “Dkt. Jones, umekuwa daktari ili kuwajali watu na kufanya kazi ya kuwatibu. Haukuwa daktari wa kuwahukumu. Ikiwa hauelewi tofauti, huna haki ya kupata mafunzo katika taasisi hii.” Kufuatia rekebisho hili, Dkt Jones alimhudumia kwa bidii Bwana Jackson wakati wa kulazwa kwake.

Ni kitambo sasa tangu Bwana Jackson afariki. Wote Dkt Jones na Dkt Cohen wamekuwa na taaluma nzuri. Lakini katika wakati mgumu wa mafunzo yake, Dkt Jones alihitaji kukumbushwa kufanya kwa haki, kupenda rehema, na kumjali Bwana Jackson bila kuhukumu.19

Kwa miaka mingi, nimenufaika na ukumbusho huo. Kupenda rehema hakumaanishi kwamba tupende tu huruma ambayo Mungu ameitoa kwetu; tunafurahi kwamba Mungu huonyesha rehema hiyo hiyo kwa wengine. Na tunafuata mfano Wake. “Wote ni sawa kwa Mungu,”20 na sisi sote tunahitaji matibabu ya kiroho ili kusaidiwa na kuponywa. Bwana amesema, “Hamtatukuza mwili mmoja zaidi ya mwingine, au mtu asidhani kwamba yuko juu zaidi ya mwingine.”21

Yesu Kristo alionyesha mfano wa kile inachomaanisha kutenda kwa haki na kupenda rehema. Kwa uhuru alishirikiana na wenye dhambi, akiwatendea kwa uaminifu na kwa heshima. Alifundisha furaha ya kushika amri za Mungu na kutafuta kuinua badala ya kulaumu wale waliokuwa na changamoto. Aliwashutumu wale waliomlaumu kwa kuwahudumia watu ambao waliwaona hawastahili.22 Ubinafsi huo wa kujiona mwadilifu ulimkasirisha na bado unamkasirisha.23

Kuwa kama Kristo, mtu hufanya kwa haki, akifanya kwa heshima na Mungu na watu wengine. Mtu mwenye haki ni raia kwa maneno na vitendo na anatambua kuwa tofauti katika mtazamo au imani haizuii fadhila na urafiki wa kweli. Watu ambao hufanya kwa haki “hawatakuwa na nia ya kuumizana, bali kuishi kwa amani”24 mmoja kwa mwingine.

Kuwa kama Kristo, mtu hupenda rehema. Watu wanaopenda rehema hawahukumu; huonyesha huruma kwa wengine, haswa kwa wale ambao hawana bahati; wao ni wenye hisani, wema, na wenye heshima. Watu hawa humchukulia kila mtu kwa upendo na uelewa, bila kujali sifa kama rangi, jinsia, ushirika wa kidini, mwelekeo wa kijinsia, hali ya uchumi na jamii, na tofauti za kikabila, ukoo, au kitaifa. Upendo kama wa Kristo umechukua nafasi ya haya.

Kuwa kama Kristo, mtu humchagua Mungu,25 hutembea pamoja Naye kwa unyenyekevu, hutafuta kumpendeza, na huweka maagano Naye. Watu ambao hutembea kwa unyenyekevu na Mungu wanakumbuka kile Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wamewafanyia.

Je, mimi ninafanya vya Kutosha? Je, ninapaswa kufanya nini kingine? Hatua tunayochukua kujibu maswali haya ni ya msingi kwa furaha yetu katika maisha haya na katika umilele. Mwokozi hataki sisi tuuchukulie wokovu kama wa kawaida. Hata baada ya kufanya maagano matakatifu, kuna uwezekano kwamba tunaweza “kuanguka kutoka katika hali ya neema na kujitenga na Mungu aliye hai.” Kwa hivyo, tunapaswa “kuchukulia tahadhari na kusali daima” ili kuepuka kuangukia “ majaribuni.”26

Lakini wakati huo huo, Baba yetu wa Mbinguni na Yesu Kristo hawataki sisi tunyong’onyezwe na mashaka endelevu wakati wa safari yetu ya duniani, tukijiuliza ikiwa tumefanya vya kutosha ili kuokolewa na kuinuliwa. Kwa hakika hawataki tuteswe na makosa ambayo tumeyatubu, tukiyafikiria kama majeraha yasiyopona kamwe,27 au tuwe na wasiwasi mwingi kwamba tunaweza kujikwaa tena.

Tunaweza kutathmini maendeleo yetu wenyewe. Tunaweza kujua kwamba “mwendo wa maisha [ambao tunafuata], ni kulingana na mapenzi ya Mungu”28 tunapofanya kwa haki, kupenda rehema, na kutembea kwa unyenyekevu na Mungu wetu. Tunajumuisha sifa za Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo katika tabia zetu na tunapendana.

Unapofanya mambo haya, utafuata njia ya agano na kustahili “kukaa na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho.”29 Nafsi zenu zitajazwa na utukufu wa Mungu na nuru ya uzima wa milele.30 Utajazwa na furaha isiyo na kifani.31 Ninashuhudia kwamba Mungu yu hai na kwamba Yesu ni Kristo, Mwokozi na Mkombozi wetu, na Yeye kwa upendo na shangwe ametoa rehema Yake kwa wote. Je, hulipendi hili? Katika Jina la Yesu Kristo, amina.