Mkutano Mkuu
Mwelekeo Mpya
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Mwelekeo Mpya

Ninakualika kugeuza moyo wako, akili, na nafsi kwa kiasi kikubwa kwa Baba yetu wa Mbinguni na Mwana Wake, Yesu Kristo.

Wapendwa akina kaka na akina dada, siku hizi mbili za mkutano zimekuwa tukufu! Ninakubaliana na Mzee Jeffery R. Holland. Kama alivyosema, jumbe, sala na muziki vyote vimevuviwa na Bwana. Ninashukuru kwa wote walioshiriki kwa njia yoyote ile.

Kote katika mkutano, nimepata taswira yenu mawazoni mwangu mkisikiliza mkutano. Nimemwomba Bwana anisaidie kuelewa kile mnachohisi, kinachowatatiza, au mnachojaribu kutatua. Nimejiuliza kile ninachoweza kusema ili kutamatisha mkutano huu ambacho kitawaaga kwa tumaini kuhusu wakati ujao ambacho ninajua Bwana anataka ninyi mhisi.

Tunaishi katika nyakati tukufu, zilizotabiriwa na manabii kwa karne nyingi. Hiki ni kipindi cha maongozi ya Mungu ambapo hakuna baraka ya kiroho itakayozuiliwa kwa wenye haki.1 Licha ya vurugu za ulimwengu,2 Bwana angependa sisi tutazame mbele kwenye siku zijazo “kwa matarajio yenye shangwe.”3 Acha tusizungushe magurudumu yetu kwenye kumbukumbu za jana. Ukusanyaji wa Israeli unasonga mbele. Bwana Yesu Kristo anaelekeza mambo ya Kanisa Lake, na Kanisa litafikia malengo yake matakatifu.

Changamoto kwenu na kwangu ni kuweka uhakika kwamba kila mmoja wetu atafikia uwezekano wake mtakatifu. Leo mara nyingi tunasikia kuhusu “mwelekeo mpya.” Ikiwa kweli unataka kukumbatia mwelekeo mpya, ninakualika kugeuza moyo wako, akili, na nafsi kwa kiasi kikubwa kwa Baba yetu wa Mbinguni na Mwana Wake, Yesu Kristo. Acha huo uwe mwelekeo wako mpya.

Kumbatia mwelekeo wako mpya kwa kutubu kila siku. Tafuta kuwa na ongezeko la usafi katika mawazo, maneno na matendo. Wahudumie wengine. Tunza mtazamo wa milele. Kuza wito wako. Na licha ya changamoto zako, wapendwa akina kaka na dada zangu, ishi kila siku ili kwamba uwe umejitayarisha zaidi kukutana na Muumba wako.4

Hiyo ndiyo sababu tuna mahekalu. Ibada na maagano ya Bwana vinatutayarisha kwa ajili ya uzima wa milele, baraka kuu kuliko zote za Mungu.5 Kama mnavyojua, maradhi ya COVID yalihitaji kufungwa kwa muda kwa mahekalu yetu. Kisha tulianza tena ufunguzi wa awamu zilizoratibiwa kwa umakini. Kwa awamu ya 2 sasa katika utendaji kwenye mahekalu mengi, maelfu ya wenza wameunganishwa na maelfu wamepokea endaumenti zao wenyewe kwa miezi michache tu iliyopita. Tunatazamia siku ambayo waumini wote wa Kanisa wenye kustahili wataweza tena kuwahudumia mababu zao na kuabudu ndani ya hekalu takatifu.

Sasa nina furaha kwa ajili ya ujenzi wa mahekalu mapya sita ambayo yatajengwa katika maeneo yafuatayo: Tarawa, Kiribati; Port Vila, Vanuatu; Lindon, Utah; Greater Guatemala City, Guatemala; São Paulo East, Brazil; na Santa Cruz, Bolivia.

Tunapojenga na kutunza mahekalu haya, tunaomba kwamba kila mmoja wenu atajijenga na kujitunza mwenyewe ili muweze kuwa wenye kustahili kuingia ndani ya hekalu takatifu.

Sasa, wapendwa akina kaka na akina dada, ninawabariki mjazwe na amani ya Bwana Yesu Kristo. Amani Yake inapita uelewa wote wa mwanadamu.6 Ninawabariki kwa ongezeko la hamu na uwezo wa kutii sheria za Mungu. Ninaahidi kwamba mnapofanya hivyo, mtapokea baraka nyingi, ikiwa ni pamoja na ujasiri mkubwa, ongezeko la ufunuo binafsi, utulivu mzuri katika nyumba zenu, na shangwe, hata katikati ya mashaka.

Na tusonge mbele pamoja ili kutimiza agizo letu takatifu—lile la kujitayarisha wenyewe na kuutayarisha ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Bwana. Ninaomba hivyo, kwa onyesho langu la upendo kwenu, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.