Rafiki
Usingizi Wakati wa Muda wa Maandiko
Januari 2024


“Usingizi Wakati wa Muda wa Maandiko,” Rafiki, Jan. 2024, 30–31.

Usingizi Wakati wa Muda wa Maandiko

Ingawa ilikuwa mapema sana, Elvira alijua kusoma maandiko kulikuwa na thamani.

Hadithi hii ilitokea huko Norway.

Elvira aliamshwa na sauti ya Baba. “Muda wa maandiko,” alisema.

Aliketi kitandani na kupikicha macho yake yenye usingizi. Nje bado kulikuwa na giza. Na kulikuwa na baridi! Elvira hakutaka kutoka kwenye kitanda chake chenye joto.

Mama alisema kusoma maandiko ndiyo njia ambayo wangeweza kumjua vyema Yesu. Lakini kusoma maandiko kila asubuhi ilikuwa vigumu!

Elvira alipanda ngazi taratibu na kuketi kando ya Sigrid, dada yake, kwenye kochi. Alikumbatia mto na kujikunyata ndani ya joto la blanketi lake la manyoya. Kaka zake walikuwa chumba kingine wakianza darasa lao la mtandaoni la seminari.

Simu ya baba iliita. Aliipokea na wanafamilia walionekana kwenye skrini. Mama mdogo Liv alikuwa amekwishavalia na tayari kwenda kazini. Binamu yao, Dorothea, alikuwa bado amevalia nguo za kulalia, kama vile Elvira.

Picha
alt text

Elvira aliwapungia mkono kupitia video na akapiga mwayo. Mara zote walifanya muda wa maandiko pamoja na Mama mdogo Liv na Dorothea. Waliishi upande mwingine wa Norway umbali wa masaa manne. Ilikuwa rahisi kwao wote kusoma maandiko pale walipokuwa na lengo la kupigiana simu kila asubuhi. Na Elvira alipenda kumwona binamu yake!

Dakika chache baadaye, Mama alijiunga pia. “Habari yenu wasichana,” alisema. Alikuwa na safari ya kikazi wiki hii, lakini bado alipiga simu kwa ajili ya muda wa familia wa kusoma maandiko.

Walisali. Kisha Elvira alifungua maandiko yake. Walikuwa wakisoma Kitabu cha Mormoni pamoja. Kila mmoja alichukua zamu kusoma mistari.

Elvira alisikiliza wakati wengine wakisoma, lakini ilikuwa vigumu kuacha kusinzia. Sigrid alikuwa amesinzia kwenye kochi. Elvira alimgusa kwa kidole. Lakini kisha jambo kwenye mstari likavuta umakini wake.

“Na nikaona fimbo ya chuma, na ilinyooka kando ya ukingo wa mto, mpaka kwenye mti niliposimama,” Dorthea alisoma.*

“Naijua hadithi hii!” Elvira alisema. “Ni ndoto ya Lehi.” Alikuwa ametazama video ya maandiko kuhusu ndoto hiyo. Kulikuwa na mti wa kupendeza wenye tunda jeupe na watu walishikilia fimbo ili iwasaidie waufikie mti.

Picha
alt text

“Je, mnakumbuka fimbo ni kama nini?” aliuliza mama.

“Maandiko?”

“Hiyo ni sawa!” Baba alisema. “Nefi anafundisha baadaye kwamba fimbo ni kama neno la Mungu. Ni kwa namna gani mnadhani tunaweza kushikilia fimbo kama vile watu katika ndoto ya Lehi?”

“Tunashikilia fimbo sasa hivi!” Elvira alinyanyua juu Kitabu chake cha Mormoni. “Kwa kuwa na muda wa maandiko.”

Mama alikubali kwa kichwa. “Tunaposoma maandiko, tunasonga karibu na Yesu Kristo. Kama vile watu walivyosonga karibu na mti wakati waliposhikilia fimbo.”

Wakati wakiendelea kusoma, Elvira alijifikiria akiwa ameshikilia fimbo na akitembea kuelekea mti wa kupendeza. Hakuhisi usingizi tena.

Punde uliwadia muda wa kuondoka. Mama mdogo Liv na Mama walihitaji kwenda kazini. Na Elvira, Sigrid na Dorothea walihitaji kujiandaa kwa ajili ya shule.

“Kwaheri kila mmoja!” Elvira aliwapungia familia yake kwenye skrini. “Nawapenda!”

Alipokuwa akikimbia kushuka ngazi ili ajiandae kwa ajili ya shule, Elvira alihisi vizuri moyoni. Na si kwa sababu ya blanketi lake la manyoya. Alijua hisia nzuri zilikuwa Roho Mtakatifu akimwambia Kitabu cha Mormoni kilikuwa cha kweli. Ilikuwa namna nzuri ya kuianza siku!

Picha
PDF ya hadithi

Vielelezo na Hector Borlasca