Maandiko Matakatifu
2 Nefi 31


Mlango wa 31

Nefi anaeleza ni kwa nini Kristo alibatizwa—Wanadamu lazima wamfuate Kristo, wabatizwe, wampokee Roho Mtakatifu, na wavumilie hadi mwisho ili waokolewe—Toba na ubatizo ndiyo lango la kuingia katika njia ile nyembamba na iliyosonga—Uzima wa milele huja kwa wale wanaotii zile amri baada ya ubatizo. Karibia mwaka 559–545 K.K.

1 Na sasa mimi, Nefi, namaliza kuwatolea unabii, ndugu zangu wapendwa. Na siwezi kuandika isipokuwa tu vitu vichache, ambavyo najua kwa hakika lazima vitatimia; wala siwezi kuandika isipokuwa tu maneno machache ya kaka yangu Yakobo.

2 Kwa hivyo, vitu ambavyo nimeandika vimenitosha, ila tu maneno machache ambayo lazima niyazungumze kuhusu mafundisho ya Kristo; kwa hivyo, nitawazungumzia kwa uwazi, kulingana na unyofu wangu ninapotoa unabii.

3 Kwani nafsi yangu inafurahia unyoofu; kwani kwa namna hii ndivyo Bwana Mungu anavyotenda kazi miongoni mwa wanadamu. Kwani Bwana Mungu hutoa nuru kwa ufahamu; kwani huzungumza na wanadamu kulingana na lugha yao, kwa ufahamu wao.

4 Kwa hivyo, ningependa mkumbuke kwamba nimewahi kuwazungumzia kuhusu yule nabii ambaye Bwana alinionyesha, kwamba atambatiza Mwanakondoo wa Mungu, ambaye ataondoa dhambi za ulimwengu.

5 Na sasa, kama Mwanakondoo wa Mungu, akiwa mtakatifu, alihitaji kubatizwa kwa maji, ili kutimiza haki yote, Ee basi, jinsi gani tunahitaji zaidi sisi, tusio watakatifu, kubatizwa, ndiyo, hata kwa maji!

6 Na sasa, ningewauliza ninyi, ndugu zangu wapendwa, ni vipi Mwanakondoo wa Mungu alitimiza haki yote alipobatizwa kwa maji?

7 Je, hamjui kwamba alikuwa mtakatifu? Lakini ingawa alikuwa mtakatifu, anawaonyesha watoto wa watu kwamba, kulingana na mwili anajinyenyekeza mbele ya Baba, na kumshuhudia Baba kwamba yeye atakuwa mwaminifu kwake katika kutii amri zake.

8 Kwa hivyo, baada ya kubatizwa kwa maji Roho Mtakatifu alimshukia katika umbo la njiwa.

9 Na tena, inaonyesha watoto wa watu unyofu wa njia, na wembamba wa lango, ambalo wataliingilia, baada ya yeye kuwatolea mfano.

10 Na akawaambia watoto wa watu: Nifuateni mimi. Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, je, tunaweza kumfuata Yesu tusipokubali kushika amri za Baba?

11 Na Baba alisema: Tubuni, tubuni, na mbatizwe katika jina la Mwana wangu Mpendwa.

12 Na pia, sauti ya Mwana ilinijia, ikisema: Yule anayebatizwa katika jina langu, atapewa Roho Mtakatifu na Baba, kama mimi; kwa hivyo, nifuateni, na mfanye vitu ambavyo mmeniona nikifanya.

13 Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, najua kwamba kama mtamtii Mwana, kwa moyo wa lengo moja, bila unafiki na udanganyifu mbele yake Mungu, lakini kwa kusudi kamili, na kutubu dhambi zenu, mkishuhudia kwa Baba kwamba mnataka kujivika juu yenu jina la Kristo, kwa ubatizo—ndiyo, kwa kumfuata Bwana wenu na Mwokozi wenu chini majini, kulingana na neno lake, tazameni, ndipo mtapokea Roho Mtakatifu; ndiyo, kisha ubatizo wa moto na Roho Mtakatifu unakuja; na kisha mtaweza kuzungumza kwa lugha ya malaika, na kupiga kelele za sifa kwa yule Mtakatifu wa Israeli.

14 Lakini, tazama, ndugu zangu wapendwa, hivyo sauti ya Mwana ilinijia, ikisema: Baada ya kutubu dhambi zenu, na kushuhudia Baba kwamba mko tayari kutii amri zangu, kwa ubatizo wa maji, na kupokea ubatizo wa moto na wa Roho Mtakatifu, na kuzungumza kwa lugha mpya, ndiyo, hata lugha ya malaika, na baada ya haya mnikane, ingekuwa vyema kama hamkunifahamu.

15 Na nikasikia sauti kutoka kwa Baba, ikisema: Ndiyo, maneno ya Mpendwa wangu ni ya kweli na maaminifu. Yule atakayevumilia hadi mwisho, huyo ataokolewa.

16 Na sasa, ndugu zangu wapendwa, najua kwamba bila ya mwanadamu kuvumilia hadi mwisho, kwa kufuata mfano wa Mwana wa Mungu aliye hai, hawezi kuokolewa.

17 Kwa hivyo, fanyeni vitu ambavyo nimewaambia nimeona kwamba Bwana wenu na Mkombozi wenu atatenda; kwani, nimeonyeshwa haya kwa lengo hili, ili mjue ni kwa lango gani mtakaloingilia. Kwani lango ambalo mtaingilia ni toba na ubatizo kwa maji; na kisha unakuja msamaha wa dhambi zenu kwa moto kwa Roho Mtakatifu.

18 Na kisha mnaingia katika njia hii nyembamba iliyosonga ambayo inaelekea uzima wa milele; ndiyo, mmeingia kwa hilo lango; mmetenda kulingana na amri za Baba na Mwana; na mmempokea Roho Mtakatifu, ambaye anawashuhudia Baba na Mwana, katika kutimiza ahadi ambayo ametoa, kwamba mkiingia kwa njia mtapokea.

19 Na sasa, ndugu zangu wapendwa, baada yenu kuingia katika njia hii nyembamba na iliyosonga, nauliza je, yote yamekamilishwa? Tazama, nawaambia, Hapana; kwani hamjafika hapa ila tu kwa neno la Kristo na kwa imani isiyotingishika ndani yake, mkitegemea kabisa ustahili wa yule aliye mkuu kuokoa.

20 Kwa hivyo, lazima msonge mbele mkiwa na imani imara katika Kristo, mkiwa na mngʼaro mkamilifu wa tumaini, na upendo kwa Mungu na wanadamu wote. Kwa hivyo, kama mtasonga mbele, mkila na kusherekea neno la Kristo, na mvumilie hadi mwisho, tazama, hivyo ndivyo asemavyo Baba: Mtapokea uzima wa milele.

21 Na sasa, tazama, ndugu zangu wapendwa, hii ndiyo njia; na hakuna njia nyingine wala jina lililotolewa chini ya mbingu ambalo mwanadamu anaweza kuokolewa katika ufalme wa Mungu. Na sasa, tazama, hili ndilo fundisho la Kristo, na fundisho pekee na la kweli la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu, ambao ni Mungu mmoja, bila mwisho. Amina.