Maandiko Matakatifu
1 Nefi 11


Mlango wa 11

Nefi anaona Roho wa Bwana na anaonyeshwa kwa ono mti wa uzima—Anamuona mama wa Mwana wa Mungu na kufahamu kuhusu ufadhili wa Mungu—Anaona ubatizo, huduma, na kusulibiwa kwa Mwanakondoo wa Mungu—Pia anaona mwito na huduma ya Mitume Kumi na Wawili wa Mwanakondoo. Karibia mwaka 600–592 K.K.

1 Kwani ikawa baada ya kutamani kujua vitu ambavyo baba yangu aliona, na nikiamini kwamba Bwana anaweza kunijulisha haya kwangu, nikiwa nimekaa nikiwaza moyoni mwangu nilinyakuliwa na Roho wa Bwana, ndiyo, hadi kwenye mlima mrefu zaidi, ambao sijawahi kuona hapo awali kamwe, na ambao juu yake sijawahi kukanyagisha mguu wangu kamwe hapo awali.

2 Na Roho akaniambia: Tazama, ni nini unachotamani?

3 Na nilisema: Natamani kuona vitu ambavyo baba yangu aliona.

4 Na Roho akaniambia: Unaamini kwamba baba yako aliuona mti ambao ameuzungumzia?

5 Na nikasema: Ndiyo, wewe unajua kwamba ninaamini maneno yote ya baba yangu.

6 Na baada ya mimi kuzungumza maneno haya, Roho akapaza sauti, na kusema: Hosana kwa Bwana, Mungu aliye juu sana; kwani yeye ndiye Mungu juu ya ardhi yote, ndiyo, hata juu ya yote. Na umebarikiwa ewe, Nefi, kwa sababu unamwamini Mwana wa Mungu aliye juu sana; kwa hivyo, wewe utaona vitu ulivyotamani.

7 Na tazama utapewa kitu hiki kama ishara, kwamba baada ya kuona mti ambao ulizaa tunda ambalo baba yako alionja, wewe utaona pia mtu akiteremka kutoka mbinguni, na wewe utashuhudia; na baada ya kumwona wewe utashuhudia kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.

8 Na ikawa kwamba Roho akaniambia: Tazama! Na nikatazama na kuona mti; na ulikuwa kama ule mti ambao baba yangu aliuona; na urembo wake ulikuwa hauna kipimo, ndiyo, zaidi ya urembo wote; na weupe wake ulizidi weupe wa theluji ivumayo.

9 Na ikawa baada ya kuona huu mti, nikamwambia Roho: Nimeona kuwa umenionyesha mti ulioadimika zaidi ya yote.

10 Na akaniambia: Nini unachotamani?

11 Na nikamwambia: Kufahamu maana yake—kwani nilimzungumzia kama mwanadamu; kwani niliona kuwa alikuwa kwa mfano wa mwanadamu; walakini, nilijua kwamba ni Roho wa Bwana; na akanizungumzia kama mwanadamu anavyozungumzia na mwingine.

12 Na ikawa kwamba akaniambia: Tazama! Na nikatazama ili nimwone, na sikumwona; kwani alikuwa ameenda kutoka machoni mwangu.

13 Na ikawa kwamba nilitazama na nikaona mji mkuu wa Yerusalemu, na pia miji mingine. Na nikaona mji wa Nazareti; na katika mji wa Nazareti nikamwona bikira, na alikuwa mrembo na mweupe.

14 Na ikawa kwamba niliona mbingu zikifunguka; na malaika akateremka na kusimama mbele yangu; na akaniambia: nini unachokiona, Nefi?

15 Na nikamwambia: Ni bikira, ambaye ni mrembo na mtakatifu zaidi ya bikira wengine wote.

16 Na akaniambia: Je wajua ufadhili wa Mungu?

17 Na nikamwambia: Najua kwamba anawapenda watoto wake; walakini, sijui maana ya vitu vyote.

18 Na akaniambia: Tazama, bikira unayemwona ni mama wa Mwana wa Mungu, katika kimwili.

19 Na ikawa kwamba niliona alinyakuliwa na Roho; na baada ya kunyakuliwa na Roho kwa muda, malaika akanizungumizia, akisema: Tazama!

20 Na nikatazama na kumwona yule bikira tena, akimbeba mtoto mikononi mwake.

21 Na malaika akaniambia: Tazama Mwanakondoo wa Mungu, ndiyo, hata Mwana wa Baba wa Milele! Je, unajua maana ya ule mti ambao baba yako aliuona?

22 Na nikamjibu, nikasema: Ndiyo, ni upendo wa Mungu, ambao umejimimina mioyoni mwa watoto wa watu, kwa hivyo, ni wa kupendeza zaidi ya vitu vyote.

23 Na akanizungumzia, na kusema: Ndiyo, na inafurahisha moyo kwa shangwe.

24 Na baada ya kusema maneno haya, akaniambia: Tazama! Na nikatazama, na nikamwona Mwana wa Mungu akienda miongoni mwa watoto wa watu; na nikawaona wengi wakiinama mbele ya miguu yake na kumuabudu.

25 Na ikawa kwamba niliona ile fimbo ya chuma, ambayo baba yangu aliiona, ilikuwa neno la Mungu, na ilielekea hadi kwenye chemchemi ya maji ya uhai, au kwenye mti wa uzima; maji ambayo ni kielelezo cha upendo wa Mungu; na pia nikaona kwamba ule mti wa uzima ulikuwa pia kielelezo cha upendo wa Mungu.

26 Na malaika akaniambia tena: Angalia na uone ufadhili wa Mungu!

27 Na nikatazama na kuona Mkombozi wa ulimwengu, ambaye baba yangu alikuwa amenena kumhusu; na pia nikaona nabii atakayemtayarishia njia mbele yake. Na Mwanakondoo wa Mungu akamwendea na akabatizwa naye; na baada ya kubatizwa, nikaona mbingu zikifunguka, na Roho Mtakatifu akishuka kutoka mbinguni na kutua juu yake kwa mfano wa njiwa.

28 Na nikaona kwamba alienda na kuwahudumia watu, kwa uwezo na utukufu mkuu; na umati ukakusanyika kumsikiliza; na nikaona kwamba walimfukuza kutoka miongoni mwao.

29 Na pia nikaona wengine kumi na wawili wakimfuata. Na ikawa kwamba walichukuliwa na Roho kutoka machoni mwangu, na sikuwaona.

30 Na ikawa kwamba malaika akanizungumzia tena, akisema: Angalia! Na nikaangalia, na kuona mbingu zikifunguka tena, na nikaona malaika wakiwashukia watoto wa watu; na kuwahudumia.

31 Na akanizungumzia tena, akasema: Angalia! Na nikaangalia, na nikamwona Mwanakondoo wa Mungu akienda miongoni mwa watoto wa watu. Na nikaona umati wa watu waliokuwa wagonjwa, na ambao walikuwa wakiugua kutokana na aina zote za magonjwa, pamoja na ibilisi na pepo wachafu; na malaika akazungumza na kunionyesha hivi vitu vyote. Na wakaponywa kwa nguvu za Mwanakondoo wa Mungu; na ibilisi pamoja na pepo wachafu wakafukuzwa.

32 Na ikawa kwamba malaika akanizungumzia tena, akisema: Angalia! Na nikaangalia na nikamwona Mwanakondoo wa Mungu, kwamba alikamatwa na watu; ndiyo, Mwana wa Mungu asiye na mwisho alihukumiwa na ulimwengu; na niliona na kuyashuhudia.

33 Na mimi, Nefi, nikaona kwamba aliinuliwa juu ya msalaba na kuuawa kwa dhambi za ulimwengu.

34 Na baada ya yeye kusulubiwa nikaona umati wa dunia, ukiwa umekusanyika pamoja kupigana dhidi ya mitume wa Mwanakondoo; kwani hivi ndivyo wale kumi na wawili waliitwa na malaika wa Bwana.

35 Na umati wa dunia ulikusanyika pamoja; na nikaona kwamba walikuwa kwenye jengo kubwa na pana, kama jengo lile baba yangu aliloliona. Na malaika wa Bwana akanizungumzia tena, akisema: Tazama ulimwengu na hekima yake; ndiyo, tazama nyumba ya Israeli imekusanyika pamoja kupinga mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo.

36 Na ikawa kwamba niliona na ninashuhudia, kwamba lile jengo kuu na pana lilikuwa ni kiburi cha ulimwengu; na lilianguka, na muanguko wake ulikuwa mkuu zaidi. Na malaika wa Bwana akanizungumizia tena, akisema: Hivyo ndivyo mataifa yote, makabila yote, lugha zote, na watu wote, ambao wanawapinga wale mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo wataangamizwa.