Maandiko Matakatifu
Joseph Smith—Mathayo 1


Joseph Smith—Mathayo

Dondoo kutoka tafsiri ya Biblia kama ilivyofunuliwa kwa Joseph Smith Nabii mwaka 1831: Mathayo 23:39 na mlango wa 24.

Mlango wa 1

Yesu atabiri angamizo la Yerusalemu lililokaribu—Pia afundisha juu ya Ujio wa Pili wa Mwana wa Mtu, na angamizo la waovu.

1 Kwa maana ninawaambia, kwamba hamtaniona kamwe tangu sasa na kujua kwamba Mimi ndiye yule ambaye iliandikwa na manabii, hadi mtakaposema: Heri yeye ajaye kwa jina la Bwana, katika mawingu ya mbinguni, na malaika wote watakatifu pamoja naye. Ndipo wanafunzi wake wakaelewa kwamba atakuja tena duniani, baada ya kutukuzwa na kuvikwa taji mkono wa kuume wa Mungu.

2 Na Yesu akatoka nje, na akaondoka hekaluni; nao wanafunzi wake wakamjia, ili wapate kumsikiliza, wakisema: Bwana, tuonyeshe juu ya majengo ya hekalu, kama vile ulivyosema—Yatatupwa chini, na kubaki ukiwa.

3 Na Yesu akawaambia: Je, hamyaoni mambo haya yote, na wala hamyaelewi? Amini ninawaambia, halitasalia hapa, juu ya hekalu hili jiwe moja juu ya jiwe jingine ambalo halitabomolewa.

4 Na Yesu akawaacha, na akaenda juu ya Mlima wa Mizeituni. Na alipokaa juu ya Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wakamwendea kwa faragha, wakisema: Tuambie mambo haya uliyoyanena juu ya angamizo la hekalu, na Wayahudi yatakuwa lini? na nini ishara ya ujio wako, na juu ya mwisho wa ulimwengu, au angamizo la waovu, ambalo ndiyo mwisho wa ulimwengu?

5 Na Yesu akajibu, na kuwaambia: Angalieni mtu asiwadanganye;

6 Kwa sababu wengi watakuja katika jina langu, wakisema—Mimi ni Kristo—nao watawadanganya wengi;

7 Kisha watawatoa ili mteswe, na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote, kwa ajili ya jina langu;

8 Na kisha wengi watakoseshwa, na watasalitiana, na kuchukiana;

9 Na manabii wengi wa uongo watatokea, na watawadanganya wengi;

10 Na kwa sababu ya kuongezeka kwa maasi, upendo wa wengi utapoa;

11 Lakini yule atakayebaki kuwa thabiti pasipo kushindwa, huyo ataokolewa.

12 Basi, hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na Danieli nabii, juu ya angamizo la Yerusalemu, ndipo mtasimama katika mahali patakatifu; yeyote asomaye na afahamu.

13 Waacheni walio katika Uyahudi wakimbilie milimani;

14 Mwacheni aliye juu ya paa akimbie, na asirudi kuvichukua vitu vilivyomo ndani ya nyumba yake;

15 Mwacheni aliye kondeni asirudi nyuma kuzichukua nguo zake;

16 Na ole wao wale wenye watoto, na kwa wake wanyonyeshao siku hizo;

17 Kwa hiyo, mwombeni Bwana ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato;

18 Maana ndipo katika siku hizo, kutakuwapo taabu kubwa juu ya Wayahudi, na juu ya wakazi wa Yerusalemu, taabu ambayo mwanzoni haijapata kuletwa juu ya Israeli, ya Mungu, tangu mwanzo wa ufalme wao hadi sasa; hapana, wala kamwe haitaletwa tena juu ya Israeli.

19 Mambo yote yaliyowashukia ni mwanzo tu wa huzuni ambayo itakuja juu yao.

20 Na kama siku hizo zisingefupishwa, asingeokoka mwenye mwili yeyote; lakini kwa ajili ya wateule, kulingana na agano, siku hizo zitafupishwa.

21 Tazama, mambo haya nimekuambieni ninyi juu ya Wayahudi; na tena, baada ya taabu ya siku hizo ambazo zitakuja juu ya Yerusalemu kama mtu yeyote atakuambieni ninyi, Lo, Kristo yupo hapa, au pale, msimsadiki;

22 Kwa maana katika siku hizo watatokea Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu, ili mradi, kwamba, kama ikiwezekana, wapate kuwadanganya hata wale walio wateule, ambao ni wateule kulingana na agano.

23 Tazama, ninayasema mambo haya kwenu kwa ajili ya wateule; nanyi pia mtasikia juu ya vita, na minongʼono ya vita; angalieni kwamba msifadhaike, kwa maana yote niliyowaambia lazima yatatokea; lakini mwisho ungali bado.

24 Tazama, nimekwisha kuwaambieni mapema;

25 Hivyo basi, kama wakikuambieni: Tazama, yuko jangwani; msitoke: Tazama, yuko katika vyumba vya siri; msisadiki;

26 Kwa maana kama vile mwanga wa asubuhi ujavyo mashariki, na kuangaza hata magharibi, na kuifunika dunia yote, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.

27 Na sasa ninakuonyesheni mfano. Tazama, popote ulipo mzoga, hapo ndipo watakapokusanyika tai; hivyo ndivyo wateule wangu watakavyokusanyika kutoka pembe nne za dunia.

28 Nao watasikia juu ya vita, na minongʼono ya vita.

29 Tazama ninasema kwa ajili ya wateule wangu; kwa maana taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme; hapo patakuwa na njaa, na maradhi, na matetemeko ya ardhi, mahali mbali mbali.

30 Na tena, kwa sababu maovu yataongezeka, upendo wa watu utapoa; bali yule asiyeshindwa, huyo ataokolewa.

31 Na tena, Injili hii ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote, kwa ajili ya ushahidi kwa mataifa yote, na ndipo mwisho utakuja, au maangamizo ya waovu;

32 Na tena chukizo la uharibifu, lililonenwa na nabii Danieli, litatimizwa.

33 Na mara baada ya taabu ya siku zile, jua litatiwa giza, nao mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka kutoka mbinguni, na nguvu za mbingu zitatikisika.

34 Amini, ninawaambia, kizazi hiki, ambacho mambo haya yataonyeshwa, hakitapita hadi yote niliyowaambia yatimie.

35 Ingawa, siku zitakuja, kwamba mbingu na dunia zitapita; lakini maneno yangu hayatapita, bali yote yatatimia.

36 Na, kama nilivyosema mapema, baada ya taabu ya siku zile, na nguvu za mbingu zitatikisika, ndipo itaonekana ishara ya Mwana wa Mtu mbinguni, na kisha makabila yote ya dunia yataomboleza; nao watamwona Mwana wa Mtu anakuja katika mawingu ya mbingu, mwenye uwezo na utukufu mkuu;

37 Na yeyote mwenye kuyahifadhi katika hazina maneno yangu, hatadanganyika, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja, naye atawatuma malaika zake mbele zake kwa sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya pamoja mabaki ya wateule wake kutoka pepo hizo nne, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwingine.

38 Sasa jifunzeni kwa mfano wa mtini—Wakati matawi yake yakiwa bado machanga, na kuanza kutoa majani, mwatambua kwamba wakati wa joto u karibu;

39 Hivyo vile vile, wateule wangu, watakapoyaona mambo haya yote, watajua kwamba yu karibu, hata milangoni;

40 Walakini kuhusu siku ile, na saa ile, hakuna ajuaye; hapana, hata malaika wa Mungu walio mbinguni, ila Baba yangu pekee.

41 Lakini kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu, ndivyo pia kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu;

42 Kwani itakuwa kwao, kama ilivyokuwa katika siku zile zilizokuwa kabla ya gharika; kwa maana hadi siku ile ambayo Nuhu aliingia katika safina watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa;

43 Na wasitambue hadi gharika ikaja, na ikawachukua wote; ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.

44 Ndipo litakapotimia lile lililoandikwa, kwamba katika siku za mwisho, watu wawili watakuwako kondeni, mmoja atatwaliwa, na mwingine aachwa;

45 Wawili watakuwa wakisaga, mmoja atatwaliwa, na mwingine aachwa;

46 Na lile nimwaambialo mmoja, nalisema kwa watu wote; kesheni, basi, kwa maana hamjui ni saa ipi Bwana wenu atakuja.

47 Lakini fahamuni hili, kama mwenye nyumba angelijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, na wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa, bali angelijiweka tayari.

48 Kwa sababu hiyo nanyi pia jiwekeni tayari, kwa maana katika saa msiyodhani, Mwana wa Mtu yu aja.

49 Ni nani, basi, aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake alimweka mtawala juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa majira yake?

50 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake, ajapo, atamkuta akifanya hivyo; na amini ninawaambia, atamweka mtawala juu ya mali zake zote.

51 Lakini kama mtumishi yule mwovu atasema moyoni mwake: Bwana wangu anakawia kuja,

52 Na akaanza kuwapiga watumishi wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi,

53 Bwana wa mtumishi huyo atakuja katika siku asiyo itazamia, na katika saa asiyoijua,

54 Naye atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

55 Na hivyo ndivyo ujavyo mwisho wa waovu, kulingana na unabii wa Musa, akisema: Watakatiliwa mbali kutoka miongoni mwa watu; lakini mwisho wa dunia bado, lakini u karibu.