Maandiko Matakatifu
1 Nefi 8


Mlango wa 8

Lehi anaona ono la mti wa uhai—Anakula matunda yake na kutamani jamii yake pia nao wale—Anaona fimbo ya chuma, na njia nyembamba imesonga, na ukungu wa giza ambao unafunika wanadamu—Saria, Nefi, na Samu wanakula matunda, lakini Lamani na Lemueli wanakataa. Karibia mwaka 600–592 K.K.

1 Na ikawa kwamba tulikuwa tumekusanya namna zote za mbegu za kila aina, pamoja na nafaka za kila aina, na pia mbegu za kila aina ya matunda.

2 Na ikawa kwamba wakati baba yangu alipoishi nyikani alituzungumzia, akisema: Tazama, nimeota ndoto; au kwa maneno mengine, nimeona ono.

3 Na tazama, kwa sababu ya kitu ambacho nilikuwa nimekiona, nina sababu ya kutoa shukrani kwa Bwana kwa sababu ya Nefi na pia ya Samu; nina sababu ya kuamini kwamba wao, na pia wengi wa uzao wao, watakombolewa.

4 Lakini tazama, Lamani na Lemueli, ninaogopa sana kwa sababu yenu; kwani tazama, nilidhania niliona ndotoni mwangu, nyika yenye giza na yenye kuhuzunisha.

5 Na ikawa kwamba niliona mtu, na alikuwa amevaa joho jeupe; na akaja na kusimama mbele yangu.

6 Na ikawa kwamba alinizungumzia, na aliniamuru nimfuate.

7 Na ikawa kwamba nilipokuwa namfuata nilijiona kwamba nilikuwa katika mahali penye giza na ukiwa wa jangwa.

8 Na baada ya kusafiri kwa masaa mengi gizani, nilianza kumwomba Bwana anihurumie, kulingana na wingi wa rehema na fadhili zake.

9 Na ikawa kwamba baada ya mimi kumwomba Bwana, niliona uwanja mkubwa na mpana.

10 Na ikawa kwamba niliona mti, ambao matunda yake yalitamanika kumfurahisha mwanadamu.

11 Na ikawa kwamba nilienda na nikala matunda yake; na nikagundua kwamba yalikuwa matamu, zaidi ya yote ambayo nilikuwa nimeonja. Ndiyo, na nikaona kwamba tunda lake lilikuwa leupe, kushinda weupe wote ambao nilikuwa nimeuona.

12 Na nilipokula tunda lile lilijaza nafsi yangu na shangwe tele; kwa hivyo, nikaanza kutaka jamii yangu na wao pia wale; kwani nilijua kwamba lilikuwa tunda la kupendeza zaidi ya yote.

13 Na nilipotazama hapa na pale, ili pia labda nione jamii yangu, niliona mto wa maji; na ulitiririka, karibu na mti ule ambao nilikuwa nikila matunda yake.

14 Na nikatazama nione ulitoka wapi; na nikaona chimbuko lake mbali kidogo; na kwenye chimbuko nikaona mama yenu Saria, na Samu, na Nefi; na walisimama wakawa kama hawajui wanapoenda.

15 Na ikawa kwamba niliwapungia mkono; na pia kwa sauti kubwa nikawaambia wanikaribie, na wale tunda, ambalo lilikuwa la kupendeza zaidi kuliko tunda lingine.

16 Na ikawa kwamba walinikaribia na kula tunda pia.

17 Na ikawa kwamba nilitaka pia Lamani na Lemueli waje na kula tunda; kwa hivyo, nikatazama kwenye chimbuko la mto, kwamba labda niwaone.

18 Na ikawa kwamba niliwaona, lakini hawakunijia na kula tunda.

19 Na nikaona fimbo ya chuma, na ilinyooka kando ya ukingo wa mto, mpaka kwenye mti niliposimama.

20 Na pia nikaona njia nyembamba imesonga, ambayo iliambatana na fimbo ya chuma, hata hadi ambapo nilipokuwa nimesimama kwenye mti; na pia ilielekea kwenye chimbuko la chemchemi, hadi kwenye uwanja mkubwa mpana, kama kwamba ni ulimwengu.

21 Na nikaona umati mkubwa wa watu usio na idadi, wengi wao ambao walikuwa wanasogea mbele, ili wapate kufikia njia ambayo ilielekea kwenye mti ambapo nilikuwa nimesimama.

22 Na ikawa kwamba walifika hapo mbele, na kuipata njia iliyoelekea kwenye mti.

23 Na ikawa kwamba kulitokea ukungu wa giza; ndiyo, hata ukungu mkubwa wa giza, hadi wale ambao walikuwa wametangulia njia walipotea njia, kwamba walizungukazunguka na kupotea.

24 Na ikawa kwamba niliona wengine wakisonga mbele, na wakafika mbele na wakashika mwisho wa fimbo ya chuma; na wakasonga mbele na kupenya ukungu wa giza, wakishikilia fimbo ya chuma, hadi wakafika na kula matunda ya mti.

25 Na baada ya kula matunda ya mti wakatupa macho yao hapa na pale wakawa kama wanaaibika.

26 Na pia nikatupa macho yangu hapa na pale, na nikaona, kwenye ngʼambo nyingine ya mto wa maji, jengo kubwa na pana; na lilikuwa ni kama linaelea hewani, juu zaidi ya ardhi.

27 Na lilikuwa limejaa watu, wazee kwa vijana, wanaume kwa wanawake; na mavazi yao yalikuwa mazuri kupita kiasi; na walikuwa na tabia ya kufanya mzaha na kuwaonyesha kwa vidole vyao wale ambao walikuwa wanakuja na kula matunda.

28 Na baada ya kuonja matunda waliaibika, kwa sababu ya wale waliokuwa wakiwadharau; na wakaingia katika njia zilizokataliwa na wakapotea.

29 Na sasa mimi, Nefi, sizungumzi maneno yote ya baba yangu.

30 Lakini, nikifupisha katika kuandika, tazama, aliona umati mwingine ukisonga mbele; na wakaja na kushika mwisho wa ile fimbo ya chuma; na wakasonga mbele, daima wameshikilia ile fimbo ya chuma, hadi wakafika na kuinama na kula matunda ya ule mti.

31 Na pia akaona umati mwingine ukipapasapapasa wakielekea kwa lile jengo kubwa na pana.

32 Na ikawa kwamba wengi walizama kwenye kilindi cha chemchemi; na wengi wakapotea asipate kuwaona, wakizururazurura katika njia ngeni.

33 Na umati ule ulioingia kwenye lile jengo geni ulikuwa mkubwa. Na baada ya kuingia kwenye lile jengo walitufanyia ishara za madharau kwa vidole vyao mimi na wale ambao walikuwa wakila matunda; lakini hatukuwasikiza.

34 Haya ndiyo maneno ya baba yangu: Kuwa wengi waliowasikiza, walianguka.

35 Na Lamani na Lemueli hawakula lile tunda, alisema baba yangu.

36 Na ikawa kwamba baada ya baba yangu kuzungumza maneno yote ya ndoto yake au ono, ambayo yalikuwa mengi, akatuambia sisi, kwa sababu ya vitu hivi vyote ambavyo alivyoona katika ono, aliwahofia kupita kiasi Lamani na Lemueli; ndiyo, alihofia wasije wakatupiliwa mbali kutoka kwenye uwepo wa Bwana.

37 Na aliwasihi kwa huruma zote za mzazi mwenye upendo, kwamba wasikilize maneno yake, na pengine Bwana angewarehemu, na asiwatupilie mbali; ndiyo, baba yangu aliwahubiria.

38 Na baada ya kuwahubiria, na pia kuwatolea unabii wa vitu vingi, aliwaamuru kuweka amri za Bwana; na akakoma kuwazungumzia.