Maandiko Matakatifu
4 Nefi 1


Nefi wa Nne

Kitabu cha Nefi
Ambaye ni Mwana wa Nefi—Mmojawapo wa Wanafunzi wa Yesu Kristo

Historia ya watu wa Nefi, kulingana na maandishi yake.

Mlango wa 1

Wanefi na Walamani wote wanaongoka kwa Bwana—Vitu vyao vyote vinatumiwa kwa usawa, wanafanya miujiza, na wanafanikiwa nchini—Baada ya miaka mia mbili, migawanyiko, uovu, makanisa ya uwongo, na udhalimu vinatokea—Baada ya miaka mia tatu, wote Wanefi na Walamani wanakuwa waovu—Amaroni anaficha maandishi matakatifu. Karibia mwaka 35–321 B.K.

1 Na ikawa kwamba mwaka wa thelathini na nne ulipita, na pia mwaka wa thelathini na tano, na tazama wanafunzi wa Yesu walikuwa wameanzisha kanisa la Kristo katika eneo lote karibu. Na kadiri wengi walivyokuja kwao, na kutubu dhambi zao kwa ukweli, walibatizwa kwa jina la Yesu; na pia walipokea Roho Mtakatifu.

2 Na ikawa katika mwaka wa thelathini na sita, watu wote walimgeukia Bwana, nchini kote, wote Wanefi na Walamani, na hapakuweko na mabishano na ugomvi miongoni mwao, na kila mtu alimtendea mwingine haki.

3 Na vitu vyao vyote vilitumiwa kwa usawa miongoni mwao; kwa hivyo hakukuwa na tajiri na masikini, wafungwa na walio huru, lakini wote walifanywa huru, na washiriki wa karama ya mbinguni.

4 Na ikawa kwamba mwaka wa thelathini na saba ulipita pia, na bado kukaendelea kuwa na amani katika nchi.

5 Na kulikuwa na kazi kubwa na ya ajabu iliyofanywa na wanafunzi wa Yesu, mpaka kwamba waliponya wagonjwa, na kufufua wafu, na kusababisha vilema kutembea, na vipofu kupokea uwezo wa kuona, na viziwi kusikia; na walifanya kila aina ya miujiza miongoni mwa watoto wa watu; na hawakufanyia miujiza isipokuwa katika jina la Yesu.

6 Na hivyo ndivyo mwaka wa thelathini na nane ulivyopita, na pia wa thelathini na tisa, na wa arubaini na moja, na wa arubaini na mbili, ndiyo, hata miaka arubaini na tisa ilipita, na pia wa hamsini na moja, na wa hamsini na mbili; ndiyo, na hata miaka hamsini na tisa ilipita.

7 Na Bwana aliwafanikisha sana katika nchi; ndiyo, mpaka kwamba walijenga miji tena ambako miji ilichomwa.

8 Ndiyo, hata huo mji mkubwa Zarahemla, walisababisha kujengwa tena.

9 Lakini kulikuwa na miji mingi ambayo ilikuwa imezama, na maji kuja mahali pao; kwa hivyo, hii miji haingefanywa upya.

10 Na sasa, tazama, ikawa kwamba watu wa Nefi walipata nguvu, na wakaongezeka kwa haraka sana, na wakawa weupe sana na watu wa kupendeza.

11 Na walioa, na kuolewa, na walibarikiwa kulingana na wingi wa ahadi ambazo Bwana alikuwa amefanya kwao.

12 Na hawakutembea tena kulingana na vitendo na sheria ya Musa; lakini walitembea kulingana na amri ambazo walipokea kutoka kwa Bwana wao na Mungu wao, wakiendelea katika kufunga na sala, na kwa kukutana pamoja siku zote kuomba na kusikia neno la Bwana.

13 Na ikawa kwamba hakukuwepo na ubishi miongoni mwa watu wote, katika ile nchi yote; lakini kulikuwa na miujiza mikuu iliyofanywa na wanafunzi wa Yesu.

14 Na ikawa kwamba mwaka wa sabini na moja ulipita, na pia mwaka wa sabini na mbili, ndiyo, na kwa kifupi, mpaka mwaka wa sabini na tisa ulipopita; ndiyo, hata miaka mia moja ilikuwa imepita, na wanafunzi wa Yesu, ambao aliwachagua, wote walikuwa wameenda peponi kwa Mungu, isipokuwa wale watatu ambao wataendelea kuishi; na kulikuwa na wanafunzi wengine ambao walisimikwa mahali pao; na pia wengi wa kizazi hicho walikuwa wamekufa.

15 Na ikawa kwamba hakukuwa na ubishi katika nchi, kwa sababu ya mapenzi ya Mungu ambayo yaliishi katika mioyo ya watu.

16 Na hakukuwa na wivu, wala ubishi, wala misukosuko, wala ukahaba, wala uwongo, wala mauaji, wala uzinifu wa aina yoyote; na kwa kweli hakujakuwa na watu ambao wangekuwa na furaha zaidi miongoni mwa watu wote ambao waliumbwa na mkono wa Mungu.

17 Hakukuwa na wanyangʼanyi, wala wauaji, wala hakukuwa na Walamani, wala aina yoyote ya vikundi; lakini walikuwa kitu kimoja, watoto wa Kristo, na warithi wa ufalme wa Mungu.

18 Na jinsi gani walibarikiwa! Kwani Bwana aliwabariki kwa matendo yao yote; ndiyo, hata walibarikiwa na kufanikiwa mpaka miaka mia moja na kumi ikapita; na kizazi cha kwanza kutoka Kristo kilikuwa kimepita, na hakukuwa na ubishi katika nchi yote.

19 Na ikawa kwamba Nefi, yule ambaye aliandika maandishi haya ya mwisho, (na aliyaandika kwenye mabamba ya Nefi) alikufa, na mwana wake Amosi aliandika badala yake; na aliyaandika kwenye mabamba ya Nefi pia.

20 Na aliandika kwa miaka themanini na minne, na kulikuwa bado na amani nchini, isipokuwa sehemu ndogo ya watu ambao walikuwa wameasi kutoka kanisa na kujiita Walamani; kwa hivyo kulianza kuwa tena na Walamani katika nchi.

21 Na ikawa kwamba Amosi alifariki pia, (na ilikuwa miaka mia moja tisini nne kutoka kuja kwa Kristo) na mwana wake Amosi aliandika maandishi badala yake; na yeye pia aliandika kwenye mabamba ya Nefi; na ikaandikwa pia kwenye kitabu cha Nefi, ambacho ni kitabu hiki.

22 Na ikawa kwamba miaka mia mbili ilikuwa imepita; na kizazi cha pili chote kilikuwa kimepita isipokuwa wachache.

23 Na sasa mimi, Mormoni, ningetaka kwamba mjue kwamba watu walikuwa wameongezeka, mpaka kwamba walitapakaa kote usoni mwa nchi, na kwamba walikuwa wametajirika sana, kwa sababu ya kufanikiwa kwao katika Kristo.

24 Na sasa, katika mwaka huu wa mia mbili na moja kulianza kuwa miongoni mwao wale ambao waliinuliwa katika kiburi, kwa kuvaa nguo za thamani, na kila aina ya lulu nzuri, na vitu vizuri vya dunia.

25 Na tangu wakati ule na kuendelea, walikuwa na mali yao na utajiri wao, na vitu vyao havikuwa sawa miongoni mwao.

26 Na walianza kujigawanya kwenye vyeo; na wakaanza kujenga makanisa yao kwa kujipatia faida, na wakaanza kukataa kanisa la kweli la Kristo.

27 Na ikawa kwamba wakati miaka mia mbili na kumi ilipokuwa imepita kulikuwa na makanisa mengi katika nchi; ndiyo, kulikuwa na makanisa mengi ambayo yalidai kumjua Kristo, na bado yalikataa sehemu kubwa ya injili yake, mpaka kwamba yalikubali aina yote ya uovu, na yalitoa kila kilicho kitakatifu kwa yule ambaye alikuwa amekataliwa kwa sababu ya kutostahili.

28 Na hili kanisa liliongezeka sana kwa sababu ya uovu, na kwa sababu ya nguvu ya Shetani ambaye alishikilia mioyo yao.

29 Na tena, kulikuwa na kanisa lingine ambalo lilimkana Kristo; na walidhulumu kanisa la kweli la Kristo, kwa sababu ya uvumilivu wao na kuamini kwao katika Kristo; na waliwadharau kwa sababu ya miujiza mingi ambayo walifanya miongoni mwao.

30 Kwa hivyo walionyesha uwezo na mamlaka juu ya wanafunzi wa Yesu ambao walibaki nao, na waliwatupa gerezani; lakini kwa uwezo wa neno la Mungu, ambao ulikuwa ndani yao, magereza yalipasuka katikati, na wakaenda mbele wakifanya miujiza mikuu miongoni mwao.

31 Walakini, na ijapokuwa hii miujiza yote, watu walishupaza mioyo yao, na walitaka kuwaua, hata kama vile Wayahudi wa Yerusalemu walitafuta kumuua Yesu, kulingana na neno lake.

32 Na waliwatupa kwenye majiko ya moto, na wakatoka nje bila majeraha.

33 Na waliwatupa pia kwenye mapango ya wanyama wa mwitu, na walicheza na wale wanyama wa mwitu hata kama vile mtoto na mwanakondoo; na walitoka kutoka miongoni mwao, bila kupata majeraha.

34 Walakini, watu walishupaza mioyo yao, kwani waliongozwa na makuhani wengi na manabii wa uwongo kuanzisha makanisa mengi, na kufanya aina yote ya uovu. Na waliwapiga watu wa Yesu; lakini watu wa Yesu hawakulipiza kisasi. Na hivyo walififia katika kutoamini na uovu, kutoka mwaka mmoja hadi mwingine, hata hadi miaka mia mbili na thelathini ikapita.

35 Na sasa ikawa katika mwaka huu, ndiyo, katika mwaka wa mia mbili na thelathini na moja, kulikuwa na mgawanyiko mkubwa miongoni mwa watu.

36 Na ikawa kwamba katika mwaka huu kulitokea watu ambao waliitwa Wanefi, na walikuwa waumini wa kweli wa Kristo; na miongoni mwao kulikuwa na wale ambao waliitwa na Walamani—Wayakobo, na Wayusufu, na Wazoramu;

37 Kwa hivyo waumini wa kweli katika Kristo, na waabudu wa kweli wa Kristo, (miongoni mwao ambao walikuwa wale wanafunzi watatu wa Yesu ambao watakaa) waliitwa Wanefi, na Wayakobo, na Wayusufu, na Wazoramu.

38 Na ikawa kwamba wale ambao walikataa injili waliitwa Walamani, na Walemueli, na Waishmaeli; na hawakufifia kwa kutoamini, lakini waliasi makusudi dhidi ya injili ya Kristo; na waliwafundisha watoto wao kwamba wasiamini, hata vile babu zao, kutoka mwanzoni, walivyofifia.

39 Na ilikuwa kwa sababu ya uovu na machukizo ya babu zao, hata kama vile ilivyokuwa mwanzoni. Na walifundishwa kuchukia watoto wa Mungu, hata vile Walamani walifundishwa kuwachukia watoto wa Nefi kutoka mwanzo.

40 Na ikawa kwamba miaka mia mbili na arubaini na nne ilikuwa imekwisha, na hivyo ndivyo yalikuwa mambo ya watu. Na sehemu kubwa ya watu waovu ilipata nguvu, na walikuwa wengi sana kuliko watu wa Mungu.

41 Na bado waliendelea na kujenga makanisa yao, na kuyapamba na aina yote ya vitu vya thamani. Na hivyo miaka mia mbili na hamsini ilikwisha, na pia miaka mia mbili na sitini.

42 Na ikawa kwamba sehemu ya watu waovu walianza tena kuanzisha viapo vya siri na makundi maovu ya siri ya Gadiantoni.

43 Na pia watu ambao waliitwa watu wa Nefi walianza kujisifu katika mioyo yao, kwa sababu ya utajiri wao mwingi, na kuwa bure kama ndugu zao, Walamani.

44 Na kutoka wakati huu wanafunzi walianza kuhuzunika kwa sababu ya dhambi za dunia.

45 Na ikawa kwamba wakati miaka mia tatu ilipokwisha, watu wote wa Nefi na Walamani walikuwa wamepata kuwa waovu sana mmoja akiwa kama mwingine.

46 Na ikawa kwamba wanyangʼanyi wa Gadiantoni walitawanyika kote usoni mwa nchi; na hakukuwa wowote waliokuwa wa haki isipokuwa wanafunzi wa Yesu. Na waliweka dhahabu na fedha kwa wingi, na walifanya biashara na aina yote ya bidhaa.

47 Na ikawa kwamba baada ya miaka mia tatu na tano kupita, (na watu walibaki bado kwenye uovu) Amosi alifariki; na kaka yake, Amaroni, aliandika maandishi badala yake.

48 Na ikawa kwamba baada ya miaka mia tatu na ishirini kupita, Amaroni, akilazimishwa na Roho Mtakatifu, alificha maandishi yote matakatifu—ndiyo, hata maandishi yote matakatifu yaliyotolewa kutoka kizazi hadi kizazi, ambayo yalikuwa matakatifu—hata mpaka mwaka wa mia tatu na ishirini tangu kuja kwa Kristo.

49 Na aliyaficha kwa Bwana, kwamba yangekuja tena kwa baki la nyumba ya Yakobo, kulingana na unabii na ahadi za Bwana. Na huo ndiyo mwisho wa maandishi ya Amaroni.