Maandiko Matakatifu
2 Nefi 12


Mlango wa 12

Isaya anaona hekalu la siku za mwisho, kusanyiko la Israeli, na hukumu ya milenia na amani—Walio na kiburi na waovu watashushwa chini katika Ujio Wake wa Pili—Linganisha Isaya 2. Karibia mwaka 559–545 K.K.

1 Neno ambalo Isaya, mwana wa Amozi, aliona kuhusu Yuda na Yerusalemu:

2 Na itakuwa kwamba katika siku za mwisho, wakati mlima wa nyumba ya Bwana utajengwa kileleni mwa milima, na utainuliwa juu ya vilima, na mataifa yote yataitiririkia.

3 Na watu wengi wataenda na kusema, Njooni ninyi, na hebu twende juu ya mlima wa Bwana, kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo; na atatufundisha njia zake, na tutatembea katika mapito yake; kwani kutoka Sayuni itatokea sheria, na neno la Bwana kutoka Yerusalemu.

4 Na atahukumu miongoni mwa mataifa, na kukemea watu wengi: na watafua panga zao kuwa majembe, na mikuki yao itakuwa visu vya kupogoa—taifa halitainua upanga kwa taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena.

5 Ee nyumba ya Yakobo, njooni na tutembee katika nuru ya Bwana; ndiyo, njooni, kwani nyote mmepotea, kila moja katika njia zake mbovu.

6 Kwa hivyo, Ee Bwana, wewe umewaacha watu wako, nyumba ya Yakobo, kwa sababu wamejaa na mila za mashariki, na wanatii wachawi kama Wafilisti, na wanajifurahisha na watoto wa wageni.

7 Nchi yao pia imejaa fedha na dhahabu, wala hakuna mwisho wa hazina zao; nchi yao pia imejaa farasi, wala hakuna mwisho wa magari yao makubwa.

8 Nchi yao pia imejaa sanamu; wanaabudu kazi ya mikono yao yenyewe, yale ambayo vidole vyao vyenyewe vimeunda.

9 Na mtu wa kawaida hainami chini, na yule mtu aliye jasiri hanyenyekei, kwa hivyo, usimsamehe.

10 Ee ninyi mlio waovu, ingieni kwenye mwamba, na mjifiche wenyewe kwenye mavumbi, kwani woga wa Bwana na utukufu wa nguvu zake utawachapa.

11 Na itakuwa kwamba kiburi cha mwanadamu kitanyenyekeshwa, na maringo ya wanadamu yatashushwa, na Bwana pekee ndiye atainuliwa katika siku ile.

12 Kwani siku ya Bwana wa Majeshi hivi punde itatukia kwa mataifa yote, ndiyo, katika kila mmoja; ndiyo, kwa wale walio na kiburi na maringo, na kwa kila mmoja aliyejiinua, na atashushwa chini.

13 Ndiyo, na siku ya Bwana itateremkia mierezi yote ya Lebanoni, kwani iko juu na kuinuliwa; na juu ya mialoni yote ya Bashani;

14 Na juu ya milima yote mirefu, na juu ya vilima vyote, na juu ya mataifa yote yaliyoinuliwa, na juu ya kila watu;

15 Na juu ya kila mnara mrefu, na juu ya kila ukuta uliozungushwa;

16 Na juu ya meli zote za bahari, na juu ya meli zote za Tarshishi, na juu ya picha zote nzuri.

17 Na kiburi cha mwanadamu kitashushwa, na maringo ya wanadamu kuteremshwa; na Bwana pekee ndiye atayeinuliwa katika siku ile.

18 Na ataangamiza sanamu kabisa.

19 Na zitaingia katika mashimo ya miamba, na mapango ya dunia, kwani woga wa Bwana utawafikia na utukufu wa fahari yake utawapiga, atakapoinuka kusukasuka ulimwengu vikali.

20 Katika siku ile mwanadamu atatupa sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, ambazo alijiundia mwenyewe kwa kuabudu, kwa fuko na kwa popo;

21 Kuingia katika mianya ya miamba, na vilele vya miamba iliyopasuka, kwani woga wa Bwana utawajia na fahari ya utukufu wake utawachapa, atakapoinuka kusukasuka ulimwengu vikali.

22 Achaneni ninyi na mwanadamu, ambaye pumzi yake iko katika pua zake; kwani ni katika nini yeye atawajibika?