2018
Kufunzwa na Roho Mtakatifu.
Oktoba 2018


Kufunzwa na Roho Mtakatifu

Vijana hawa walijiandaa kufunzwa na Roho kabla ya mkutano mkuu. Hapa ni yale waliyojifunza kutoka kwenye mkutano mkuu uliopita na kile wanachofanya tofauti kutokana na hilo.

Maelekezo yenye msukumo wa kiungu

Picha
Madelyn

Picha kutoka Getty Images

Nilipata msukumo wa kiungu kutoka kwenye mkutano mkuu. Wakati nikisikiliza maelekezo kutoka kwa viongozi wetu kuwatumikia wengine, kumwamini Kristo, na kushikilia kwa nguvu fimbo ya chuma, nilihisi Roho Mtakatifu akinishuhudia kwamba injili hii ni ya kweli na kwamba tunaweza kupata uzima wa milele kwa kushika amri na kufuata neno la Mungu. Nimeweka malengo ya kuwa wa kutoa huduma zaidi katika jamii yangu na kuimarisha ushuhuda wangu kupitia sala na kujifunza maandiko kila siku. Ninajua kwamba mimi ni binti wa Baba wa Mbinguni. Anaishi na ananipenda mara zote na milele.

Madelyn B., miaka 16, Delaware, Marekani

Majibu ya maswali

Picha
Isaak

Kabla ya mkutano mkuu nilikuwa na maswali mawili: (1) Ninawezaje kuendelea kuwa na mtazamo mzuri na kuwasaidia marafiki zangu wakati wakifanya chaguzi mbaya? Na (2) Ninawezaje kushuhudia kuhusu Kanisa bila wao kunidhihaki? Wakati wa mkutano, Roho alinishuhudia kwamba siko peke yangu. Sasa najua kwamba kwa kusoma maandiko kwa moyo wangu wote, nitapokea majibu ya maswali yangu kuhusu marafiki zangu. Ninajua kwamba Baba yangu husikiliza sala zangu, na nitajitahidi kuwa bora zaidi kila siku.

Isaak R., miaka 13, Pichincha, Ecuador

Kujitayarisha Kujifunza

Picha
Ben

Ninamhisi Roho kwa nguvu sana katika mkutano mkuu. Tangu nimeanza kuandaa maswali na kujiandaa kiroho kwa ajili ya mkutano, imekuwa tofauti sana katika maisha yangu, na nimeweza kujifunza mengi zaidi kupitia kila hotuba. Ninashukuru sana kwa nabii na mitume, na ninajua kwamba wametumwa toka kwa Baba wa Mbinguni kutuelekeza na kutuongoza sisi katika maisha yetu!

Ben H., miaka 17, Kentucky, Marekani

Kualikwa Kukua

Picha
Vincente

Mkutano mkuu uliniimarisha kwa kuwa na nia ya kufuata njia ya injili ya Yesu Kristo. Ulinisaidia kujua na kuelewa kwamba hili ni Kanisa la kweli, ambalo hutuletea nuru na furaha. Nilihisi Roho akinialika kukua kila siku na kusoma Kitabu cha Mormoni kupata ushuhuda imara wa injili. Ninaamini kwamba Baba yangu wa Mbinguni alinitaka nisikilize hotuba hizi zenye msukumo wa kiungu.

Vicente A., miaka 16, Eneo la Metropolitan, Chile

Kutafuta Nuru

Picha
Olivia

Mwaka kabla ya mwaka jana ulikuwa wenye changamoto kwangu. Baba yangu alikuwa anasumbuliwa na saratani, na kulikuwa na shambulio la kigaidi katika jiji langu. Nilisumbuliwa na woga, nikitafakari jinsi gani ningeweza kupata amani wakati nikiwa na woga kwa ajili ya usalama wangu kimwili na kiroho. Kutoka kwenye mkutano mkuu nilijifunza kwamba tunaweza kupata amani kama tukiishi kwa kustahiki, tukijaza mioyo yetu kwa imani, na kuwa na mtazamo wa umilele. Nilipata msukumo wa kiungu wa kumgeukia Kristo katika nyakati ngumu badala ya kutegemea akili zangu mwenyewe. Ninajua kwamba ninaweza kushinda ushawishi wa giza kwa kutafuta mng’aro wa nuru ya Kristo.

Olivia H., miaka 17, Ubelgiji