2018
Baraka Katika Mwandiko wa Mama Yangu
Oktoba 2018


Baraka Katika Mwandiko wa Mama Yangu

Douglas Hedger

Nevada, Marekani

Picha
Preach My Gospel and mothers photo

Kielelezo na Dilleen Marsh

Jioni moja nilikuwa nikitafakari ni ujumbe gani ningetoa katika mkutano mkuu ujao wa kata. Nimekuwa nikisoma maandiko kwa wiki nzima, na ingawa nilikuwa nimepokea maelekezo na umaizi mkuu, lakini bado sikuwa na mwelekeo dhahiri wa nini Bwana alinitaka mimi, kama rais wa kigingi, kushiriki na waumini wa kata.

Katika sala ya dhati, niliomba mwongozo kutoka kwa Roho ili kuongoza mawazo yangu. Kisha nikafungua maandiko na kuanza kusoma tena. Mawazo yangu ghafla yakageukia kwenye malengo ya kata ambayo mimi na askofu tulikuwa tumeyajadili hivi karibuni. Moja kati ya malengo hayo ilikuwa ni kutumia Hubiri Injili Yangu katika kushiriki injili na marafiki na majirani.

Nilihisi kuvutiwa kujumuisha Hubiri Injili Yangu katika kujifunza kwangu binafsi jioni ile. Nilitoa nakala na kuifungua pasipo kufungua ukurasa maalum. Katika ukurasa ule, nilikuta marejeo ya maandiko mawili yakiwa yameandikwa kwa mkono—1 Nefi 8:8–11 na 1 Nefi 11:21–22. Wakati nikiyaangalia kwa ukaribu, niligundua marejeo yale yaliandikwa kwa mwandiko wa mama yangu. Mama yangu mpendwa alifariki miaka kadhaa iliyopita, miezi miwili baada ya adhimisho la kuzaliwa kwake la miaka 80. Alikuwa ni mfano wa ushupavu na kutokuwa mbinafsi, ambaye mara zote aliona mazuri kwa watu. Na alipenda maandiko.

Nilifungua maandiko katika mistari ile kuona nini kilimsukuma kuiandika. Wakati nikiisoma, mawazo yangu ghafla yalifunguka kwa ujumbe ambao ningeutoa. Ulikuwa ni ujumbe rahisi kwamba waumini wa Kanisa ambao wameonja utamu wa tunda la injili wakati mwingine wanaweza kusahau kwamba wengine wengi wanalitafuta tunda kama hilo. Tunatakiwa tuwafikie na tuwaambie wapi wanaweza kulipata.

Nilimfikiria mama yangu mpendwa wakati nikiangalia sehemu iliyobaki ya Hubiri Injili Yangu. Hakukuwa na jina, wala muhtasari wowote, au chochote cha kuashiria kwamba kitabu kilikuwa chake. Nilikaa nikishangaa wakati nikitafakari mfululizo wa misukumo ya kiroho iliyopelekea kufikia wakati huu. Roho alinithibitishia kwamba nilikuwa nimeongozwa kwenye mawazo yangu, kama nilivyokuwa nimeomba kwa ajili ya hilo. Mama yangu alijua kiasi kidogo tu, hata hivyo miaka mingi iliyopita aliandika marejo yale, kwamba Bwana angeyatumia kuwa jibu la sala ya unyenyekevu ya mwana wake.