2018
Mzee Ulisses Soares: Mtu Asiye na Hila.
Oktoba 2018


Mzee Ulisses Soares: Mtu Asiye na Hila

Picha
Elder and Sister Soares

Katika siku za mwanzo za huduma Yake, wakati Yesu alipokuwa akiteua Mitume Wake, Alimuona Nathanaeli Akimjia. Mara moja aliweza kutambua uzuri wa Nathanaeli, akatamka, “Tazama, Mwisraeli kweli kweli, ambaye hamna hila ndani yake!”1

Yesu alijua kwamba Nathanaeli alikuwa mtu wa usafi wa moyo, mwaminifu katika nia zake, na asiye na unafiki au udanganyifu. Bwana aliipenda tabia hii ya uadilifu mtakatifu, na Alimwita Nathanaeli kuwa Mtume.2

Ulisses Soares ni kama Nathanaeli wa kale, na Bwana amemuita yeye pia.

“Nuru ya Wazazi Wangu”

Ulisses, wa mwisho kati ya kaka wanne, alizaliwa huko São Paulo, Brazil, mnamo Oktoba 2, 1958. Alitokea kwenye mwanzo mnyenyekevu, lakini wazazi wake, Apparecido and Mercedes Carecho Soares, walikuwa wakiheshimika, wachapa kazi ambao kwa dhati walisikiliza wamisionari. Walijiunga na Kanisa mnamo 1965 wakati Ulisses alikuwa na umri wa miaka sita.

“Sikuweza kumuona kaka Apparecido akikosa mkutano,” anasema Osiris Cabral, ambaye alitumikia kama rais wa kigingi wakati Ulisses akiwa kijana mdogo. “Mercedes pia alikuwa mwaminifu sana. Ulisses alirithi kujitolea kwa wazazi wake.”

Picha
young Elder Soares and parents wedding portrait

Ulisses Soares “alikulia Kanisani akifuata nuru” ya wazazi wake, Apparecido and Mercedes Soares (kushoto). Ulisses alimwamini Bwana licha ya upinzani, alijifunza akiwa mvulana kushikilia kwa nguvu kwa Mwokozi na injili Yake.

Moyo mzuri kiuhalisia wa Ulisses ulichanua wakati akijifunza njia za Bwana. “Nilikulia Kanisani nikifuata nuru ya wazazi,” Mzee Soares anasema. Wakati akifuata nuru ile, ushuhuda wake ulikuwa imara zaidi licha ya upinzani.

“Nilikuwa muumini pekee wa Kanisa shuleni kwangu, na wavulana wengine kila mara walikuwa wakijaribu kunivuta chini na kunishinikiza kufanya vitu ambavyo vilikuwa si sahihi,” anasema. “Nilitakiwa kujifunza kujikinga mimi mwenyewe katika changamoto hizi, lakini mara zote niliamini katika Bwana kwa moyo wangu wote kunisaidia kufanikiwa. Nilijifunza kama kijana mdogo kwamba ikiwa utafanya sehemu yako, Bwana atafanya Yake. Lakini unahitajika kushikilia kwa nguvu mkono Wake na injili Yake.

Wakati Ulisses alipokuwa na miaka 15, askofu wake alimuomba kufundisha darasa la Shule ya Jumapili la vijana. Somo moja alilofundisha lilijikita kwenye kupata ushuhuda wa injili. Ulisses alikuwa amesoma Kitabu cha Mormoni, mara zote alihisi kuwa Kanisa ni la kweli, na kuamini katika Mwokozi Yesu Kristo.

Wakati akiandaa somo lake, alitaka kushuhudia kwa dhati kwenye darasa lake juu ya ukweli wa injili. “Nilisoma na kusali kwa dhati,” Mzee Soares anakumbuka. “Baada ya kupiga magoti, ndipo hisia nzuri ilikuja moyoni mwangu, sauti ndogo ambayo ilithibitisha kwangu kwamba nilikuwa katika njia sahihi. Ilikuwa yenye nguvu sana kiasi kwamba sikuweza kusema kwamba sikujua.”

Wakati Ulisses amekua, alijifunza kwamba kama angefanya zaidi ya kile ambacho kilitegemewa au kuombwa, Bwana kwa ukarimu angembariki. Mojawapo ya somo kama hilo ilikuja wakati akijiandaa kwa ajili ya misheni. Wakati wa usahili na Ulisses, askofu wake alisisitiza umuhimu wa kutii amri na kuishi kwa kustahiki. Pia alisisitiza maandalizi ya kifedha.

Leo hii, wamisionari wote kutoka Brazil wanachangia katika gharama zao za umisionari, pamoja na familia nyingi zingine zikichangia gharama. Wakati Ulisses akikaribia umri wa umisionari, alinuia kwamba angepata fedha zote zinazohitajika kwa ajili ya misheni yake. Akichukulia manufaa ya maadili ya ufanyaji kazi kwa bidii aliyojifunza akifanya kazi kwenye biashara ndogo ya baba yake na kuwa na uwezo wa kuchapa kwa haraka, Ulisses alipata kazi ya siku akiisaidia kampuni kuandaa orodha ya malipo ya mishahara.

Baada ya kufaulu mtihani mgumu sana wa kuingilia, alianza kusoma uhasibu jioni katika shule ya upili ya ufundi. Kila mwezi, baada ya kulipa zaka, angehifadhi fedha kwa ajili ya misheni yake. Baada ya mwaka, alihamishiwa kwenye kitengo cha uhasibu kwenye kampuni.

“Hivyo ndivyo nilivyohifadhi fedha kulipia misheni yangu,” Mzee Soares anasema. “Na kila mwezi kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuondoka, ningenunua kitu fulani nilichohitaji—shati, suruali, soksi, tai na begi.” Pia alihitaji, na akapokea, upendo wa nguvu na msaada kutoka kwa wazazi wake na viongozi wa eneo lake.

Ulisses aliitwa kutumikia misheni ya Brazil Rio de Janeiro. Alitumikia sehemu yake ya kwanza misheni chini ya Rais Helio da Rocha Camargo, ambaye baadae alikuwa Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka wa kwanza kuitwa kutoka Brazil. Ulisses alianza misheni yake mnamo mapema 1978. Hekalu la kwanza katika Amerika ya Kusini liliwekwa wakfu baadae mwaka huo huko São Paulo na Rais Spencer W. Kimball (1895–1985).

Picha
Elder Soares as a young missionary

Mnamo Januari 1980, Ulisses na mwenza wake wa misheni, ambaye pia hakuwa amepokea endaumenti yake, walipanda basi huko Rio de Janeiro kwa saa nane kwenda Hekaluni São Paulo Brazili. Wazazi wa Ulisses na ndugu zake walikutana naye huko, na familia ya Soares ilifunganishwa hekaluni kwa muda wa maisha ya hapa duniani na kwa milele yote. Ulisses kamwe hajasahau saa hizo tano pamoja katika hekalu la São Paulo. Baaade siku hiyo, yeye na mwenza wake wa misheni walirudi katika eneo la misheni.

Kumweka Mungu Kwanza

Ulisses alifurahia misheni yenye mafanikio, ambayo yaliimarisha zaidi ushuhuda wake. Aliporudi nyumbani, alipata kazi na kuanza kusomea uhasibu na uchumi katika chuo kikuu kilicho kwenye eneo lake.

Alikuwa amerudi nyumbani takribani miezi saba wakati alipokutana na “Dada Morgado” kwenye dansi ya vigingi mbalimbali. Ulisses alikuwa ametumikia kama kiongozi wake wa kanda kwa muda, na wawili hao walitumia jioni wakijikumbusha na kushiriki matukio ya misheni. Wiki tatu baadae, walianza kuwa kwenye miadi.

Rosana Fernandes Morgado alikuwa na miaka nane wakati dada yake mkubwa, Margareth, alipoanza kumpeleka kanisani. Hatimaye, wachunguzi wadogo wawili waaminifu walipokea ruhusa ya kubatizwa toka kwa baba yao, lakini kila mmoja alitakiwa kusubiri mpaka afikishe miaka 17. Rosana alihudhuria kanisani kwa miaka tisa kabla ya kupokea ruhusa ya kubatizwa.

Ulisses aliishi huko kaskazini mwa São Paulo, na Rosana aliishi na wazazi wake sehemu ya kusini mwa jiji. Kusafiri kupita jiji lililosambaa kulichukua saa mbili hadi tatu kwa basi na njia za chini ya ardhi. Kwa bahati nzuri, Margareth na mume wake, Claudio, waliishi karibu na nyumbani kwa wazazi wake.

Wakati Ulisses alipokuja siku za mwisho wa wiki kwenda kwenye miadi na Rosana, ilikuwa vigumu kwake kurudi nyumbani hasa wakati wa usiku,” Mzee Claudio R. M. Costa Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka wa Sabini anakumbuka, juu ya shemeji yake mtarajiwa. Hivyo, yeye na Margareth walimwalika Ulisses usiku kukaa nyumbani kwao baada ya miadi. “Tulimchukulia kama mmoja wetu kwa muda,” Mzee Costa anaongeza.

‘Angelala kwenye kochi kwenye sebule yetu,” anasema Dada Costa. “Tulikuwa ndio tumeoana karibuni, hivyo hatukuwa na mablanketi ya ziada. Lakini angejifunika na pazia la zamani tulilokuwanalo. Alikuwa na furaha kwa sababu angeweza kumuona Rosana tena siku inayofuata. Alikuwa ni mzuri kwa dada yangu, na wazazi wangu walimpenda sana.”

Ulisses na Rosana walioana katika Hekalu la São Paulo Brazil mnamo Oktoba 30, 1982.

Picha
Elder and Sister Soares

Kama utakaa na Mzee na Dada Soares kwa dakika chache, upendo wao, uzuri wao, na heshima baina ya kila mmoja wao haraka huwa dhahiri. Kwa Mzee Soares, Rosana “amekuwa mfano wa wema, upendo, na kujitolea kikamilifu kwa Bwana kwa ajili yangu na familia yangu.”3 Kwa Dada Soares, Ulisses ni “zawadi kutoka mbinguni.”

Dada Soares anaongeza: “Mara zote amekuwa mwajibikaji sana na mtakatifu, amekuwa mara zote akiitunza familia yetu, na mara zote amenitendea vizuri sana. Katika miito yake yote Kanisani, amefanya kila awezalo. Huenda na kufanya. Mara zote huweka vitu vya Mungu kwanza katika maisha yake. Ninampenda sana kwa sababu najua kama anaweka vitu vya Mungu kwanza, pia ataniweka mimi kwanza.”

Kuhusu mke wake, Mzee Soares anasema: “Yeye ni shujaa wa kweli na mwenye kutia msukumo katika familia yetu. Ana upendo, ni mkarimu na mvumilivu na kila mtu. Anaiunganisha familia yetu, na huona mazuri kwa kila mtu. Amechangia kwa kiasi kikubwa kwenye kile ambacho kimetokea katika maisha yangu. Kuhusu wito wangu kwenye Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, kwa utani nilimwambia, ‘nina kulaumu kwa hili kwa sababu umeikuza sana nguvu ya injili katika maisha yangu.’”

Moyo wa Kina

Gustavo, mtoto mkubwa wa akina Soares, anakumbuka usiku ambapo, kama mvulana, hakuwatii wazazi wake na kutoroka kwenda kuangalia maadhimisho ya mwaka katika eneo lao huko São Paulo yajulikanayo kama Festa Junina.

“Nilikuwa katikati ya umati mkubwa nikiwa na wakati mzuri wakati niliposikia mtangazaji akiniita mbele,” anasema. “Hapo ndipo nilimuona baba yangu.”

Wazazi wake walikuwa na wasiswasi mkubwa, lakini badala ya kumkaripia Gustavo, Ulisses alimkumbatia kwa nguvu.

“Tulikuwa na maongezi ya kina kuhusu kutoroka kwangu, lakini wazazi wangu walinichukulia kwa heshima,” Gustavo anakumbuka. “Nilihisi kulindwa, na nilijua kwamba walikuwa kweli wakinipenda.

Ulisses amejitoa kwa ajili ya familia yake. Bila kujali kazi zake nyingi na ratiba ya safari kwa miaka mingi, aliweza kuweka muda kujenga mahusiano na watoto wake.

Picha
Soares family photo

Wakati Mzee Soares alipokubaliwa kwenye Akidi ya Mitume Kumi na Wawili mnamo Machi 31, 2018, labda hakuna yeyote ambaye alishangazwa zaidi ya Gustavo na dada zake wawili, Lethicia Caravello na Nathalia Soares Avila. Lakini kama upendo, juhudi ya kazi, huruma, na unyenyekevu vinamstahilisha mtu kwa ajili ya utume, walisema, wanaweza kuelewa kwa nini Bwana alimuita baba yao.

“Wakati Yesu alipowaita Mitume Wake, Hakuwachagua mafarisayo waliokuwa na elimu kubwa sana, aliwachagua wavuvi,” Lethicia anasema. “Mama yangu na baba yangu wako hivyo. Wanamwamini Bwana kabisa, na huwatumia wao kutimiza kazi Yake kwa sababu Anajua hawana ubinafsi, wako tayari kufanya kazi kwa bidii, na ni wanyenyekevu vya kutosha kukubali masahihisho.”

“Moyo wa kina” wa baba yao utamsaidia wakati akiendelea mbele kama mmoja wa mashahidi maalum wa Bwana, anaongeza Nathalia. “Ana moyo kwa ajili ya hilo,” anasema. “Anahisi ushawishi wa mbinguni, na humpenda kila mtu na hutaka kufanya kilicho chema.”

“Kila kitu Kitafanikiwa”

Wakati Mzee Soares akitumikia kama rais wa misheni ya Porto Ureno tangu 2000 mpaka 2003, alijulikana sana kwa kutumia kirai cha kireno “Tudo vai dar certo”—kila kitu kitafanikiwa.

“Alitufundisha,” Anakumbuka Ty Bennett, mmoja kati ya wamisionari wake. “Anaishi maisha yake kwa imani na mtazamo chanya kwamba ikiwa tutafanya kile ambacho Bwana anataka tufanye, kila kitu kitafanikiwa.”

Pia aliwafundisha wamisionari wake kutotumia maneno vigumu au haiwezekani, anasema Richard Shields, mmisionari wake mwingine. “Tulirejea vitu kama ‘changamoto.’ Ushauri huo ulisaidia kuchonga maisha yangu, wakati nimeangalia vitu kama ‘changamoto’ ambazo tutazishinda kuliko kama ‘vigumu’ au ‘haiwezekani.’”

Imani kama hiyo na mtazamo chanya havijaja kutoka kwenye maisha ya raha. Mzee na Dada Soares wanajua vizuri masikitiko ya kutokuwa na kitu, uchovu wa siku ndefu za kazi na kujifunza, changamoto za afya iliyotetereka, na huzuni kubwa ya kuharibika kwa mimba, mtoto kufia tumboni, na kupoteza ndugu na wazazi.

Lakini kupitia safari ya kimaisha, wameweza kuweka imani yao katika maneno ya maandiko ayapendayo Mzee Soares: “Jinyenyekeze; na Bwana Mungu wako atakuongoza kwa mkono, na kukupa jibu la sala zako.”4

Changamoto ni sehemu ya ukuaji wetu,” Mzee Soares anasema. “Lakini wakati tunapokuwa wavumilivu katika masumbuko, wakati tunapojifunza kushinda changamoto za kimaisha, wakati tunapobakia waaminifu, Bwana hutupa heshima ya juu na hutubariki kwa baraka Alizoahidi.”

Na wakati tunaposhikilia fimbo ya chuma kwa nguvu, anaongeza, Bwana hatatuacha peke yetu.

“Kuwa na msimamo katika kushikilia kwa nguvu amri, kwenye injili, kwenye maandiko, na kwa Bwana Yesu Kristo hutusaidia sisi kushinda changamoto za kimaisha,” Mzee Soares anasema. ‘Wakati tukipiga magoti kusali, Atakuwa pamoja nasi na Atatuongoza. Atatutia msukumo wa wapi pa kwenda na nini cha kufanya. Wakati tukiwa watiifu na kunyenyekeza nafsi zetu, Bwana hujibu sala zetu.”

Mtume mwenye Kujitoa

Ulisses Soares ni mtu mwenye uwezo na maandalizi. Elimu yake, ikijumuisha shahada ya uzamili ya kusimamia biashara, vilimuandaa kufanya kazi kama mhasibu na mkaguzi wa hesabu kwenye makampuni ya kimataifa huko Brazili. Uzoefu huo ulimwandaa kufanya kazi kwenye kitengo cha fedha cha Kanisa, ambapo ilimuandaa katika umri wa miaka 31 kuwa mmoja kati ya wakurugenzi wa Kanisa wenye umri mdogo wa mambo ya muda. Maandalizi hayo yalimsaidia sana kama rais wa misheni na katika wito wake kama Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka wa Sabini mnamo Aprili 2, 2005.

Kabla ya kuitwa kwenye Urais wa Wale Sabini mnamo Januari 6, 2013, Mzee Soares alitumikia kama mshauri katika urais na baadae kama rais katika urais wa eneo la Brazil na kama mshauri katika Eneo la Afrika Kusini Mashariki. Pale, alihudumu kama mshauri wa Mzee Dale G. Renlund, ambaye wakati huo alikuwa ni Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka wa Sabini. Mzee Renlund, ambaye sasa ni mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, anakumbuka kwa shauku muda wao pamoja.

“Mzee Soares ni mchangamfu, mwenye kujitolea, mtume mwenye kujitolea wa Yesu Kristo,” anasema Mzee Renlund. “Simjui yeyote ambaye anahisi umakini zaidi kama alivyo katika kazi ya Bwana. Kama anaombwa kufanya kitu fulani, hufanya kwa uwezo wake wote.”

Picha
Elder Soares with Saints around the world

Iwe katika Watakatifu huko Peru (kushoto), Ghana (chini), au mataifa mengine ambapo alitumikia na kuhudumia, Mzee Soares ‘kiurahisi aliwapenda watu,” anasema Mzee Claudio R. M. Costa.

Anasema Mzee Soares haraka “aliwapenda” Watakatifu wa Afrika. Mojawapo kati ya majukumu yake ya kwanza katika eneo ilikuwa kusimamia mkutano wa kigingi huko Kananga, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. “Aliporudi, hakuweza kuacha kuongea kuhusu uzuri na kujitolea kwa watu aliokutana nao,” Mzee Renlund anasema.

Mzee L. Witney Clayton, aliyehudumu na Mzee Soares kwa miaka mitano na nusu katika Urais wa Wasabini, humuita Mzee Soares mjenga makubaliano. “Husikiliza na kupima mawazo yake. Huwa makini katika hali anavyojichukulia katika mikutano ili kwamba sauti zetu zitengeneze kiitikio, kuliko hali ya mashindano ya mtu mmoja kusikika.”

Mzee Soares ni mwenye staha kuhusu uwezo wake wa kuwasiliana kwa Kireno, Kiingereza, Kihispania, na Kifaransa. Lakini karama hiyo, ambayo huitaji umakini usiotetereka, ni baraka kwa Kanisa, anasema Mzee Clayton. Mzee Soares anaweza kuongea na watu wengi Kanisani katika lugha zao wenyewe.

Ulisses amekuwa kiongozi tangu alipokuwa mvulana,” anasema Mzee Claudio Costa juu ya shemeji yake. “Ana uelewa na uwezo sana, na huhisi uwajibikaji kwa kila mara kwa kufanya kila awezacho. Kiurahisi huwapenda wale wanaomzunguka. Ana moyo wa mwanafunzi wa kweli wa Mwokozi, na ana ushuhuda wa uhakika kwamba Yesu ndiye Kristo. Ninampenda na nina shukrani kumkubali kama Mtume wa Bwana.”

Na Mzee David A. Bednar, akiongea kwa niaba ya Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, anaongeza: “Mzee Soares ni msafi asiye na hila, na mwanafunzi asiye na hatia wa Bwana. Kupitia mwangaza wa mwonekano wake, tabasamu lake la dhati, na tabia yake yenye hisani, watu wasiohesabika pamoja na familia wamekuwa, wanakuwa na watakuwa na ushawishi mkubwa wa kumfuata Mwokozi na kuishi mwongozo wa injlili Yake.”

Picha
Elder Soares with grandchildren and wife

Picha pamoja na mkewe, Rosana, mbele ya Hekalu la Salt Lake, picha na Kristin Murphy, Deseret News

Katika kipindi chetu, Bwana alisema kuhusu Edward Patridge, “Moyo wake ni safi mbele zangu, kwani yeye ni kama Nathanaeli wa kale, hamna hila ndani yake.”5 Kuhusu Hyrum Smith, Bwana alisema “kwani Mimi, Bwana, ninampenda kwa sababu ya uadilifu wa moyo wake, na kwa sababu yeye hupenda yaliyo ya haki mbele zangu.”6

Kuhusu Ulisses Soares, Bwana angesema hivyo hivyo.