2018
Tabasamu la Kukubali
Oktoba 2018


Tabasamu la Kukubali

Franklin Romero

Manabí, Ecuador

Usiku mmoja kata yetu ilikuwa na shughuli ambayo tulitumia saa nyingi katika kuiandaa. Baada ya shughuli kijana mdogo mchunguzi aliniaga lakini baada ya dakika chache alirudi na kuuliza “Askofu lini nahitaji kurudi?” Nilimwambia Jumapili, na mvulana haraka akajibu, “Hapana, kwani hakuna shughuli nyingine?” Alikuwa amekuwa na wakati mzuri na vijana wa kata kwamba alitaka kurudi tena.

Pia nilizungumza na wanandoa ambao walikuwa wamehudhuria shughuli hii na kuwauliza walikuwa wamefikiria nini. Mume alijibu, “Tangu tulipofika hapa tumehisi amani na utulivu,” ambapo mke wake aliunga mkono kwa kutikisa kichwa. Nilishangazwa kwa hili kwa sababu mara ya kwanza walipofika, kulikuwa na watu wengi wakiongea na kupiga kelele. Lakini aliendelea na kuniangalia na kuuliza, “Huyo ni Roho Mtakatifu, sivyo?” Kwa mshangao ningeweza kusema tu ndiyo.

Kulikuwa na mengi ya kufanya kujiandaa na shughuli hii, kwa hiyo usiku ule wakati kila kitu kilipokwisha, kitu pekee nilichotaka kufanya ni kwenda nyumbani na kulala. Kwa sababu nilikuwa nimechoka, sikuweza kufikiria juu ya maongezi yangu na wachunguzi. Nilipofika nyumbani, nilisali na kwenda kulala, lakini sikuweza kusinzia; katika mawazo yangu nilivuta taswira ya Bwana akitabasamu. Lilikuwa ni tabasamu la kukubali. Kwa wakati huo nilianza kukumbuka vitu vizuri ambavyo vilikuwa vimetokea katika shughuli ile.

Nilielewa kwamba bidii na upendo wa waumini wa kata uliwezesha mioyo ya wachunguzi wale watatu kuguswa. Nilielewa kwamba tabasamu la kukubali lilikuwa ni kwa ajili ya tulichokuwa tukifanya. Sikuweza kujizuia kulia, na nilihisi kuwa na shukrani sana kwa zawadi ambayo Bwana alitupatia. Alikuwa ametupatia tabasamu la kukubali. Ninashuhudia kwamba maneno ya Bwana ni ya kweli; kwamba tunapoleta hata nafsi moja Kwake, shangwe yetu itakuwa kubwa katika Ufalme wa Baba (ona M&M 18:15).