Mlango wa 5
Nefi na Lehi wanajitoa wenyewe kuhubiri—Majina yao yanawakumbusha kuishi maisha mazuri kama babu zao—Kristo anakomboa wale ambao wanatubu—Nefi na Lehi wanapata waongofu wengi na wanafungwa gerezani, na moto unawazingira—Wingu la giza linawafunika watu mia tatu—Ardhi inatetemeka, na sauti inawaamrisha watu watubu—Nefi na Lehi wanaongea na malaika, na umati unazingirwa na moto. Karibia mwaka 30 K.K.
1 Na ikawa kwamba katika mwaka huo huo, tazama, Nefi alitoa kiti cha hukumu kwa mtu ambaye jina lake lilikuwa Sezoramu.
2 Kwani kwa vile sheria zao na serikali yao ilianzishwa kwa sauti ya watu, na waliochagua uovu walikuwa wengi sana kuliko wale waliochagua mema, kwa hivyo walikuwa wanajitayarisha kwa maangamizo, kwani sheria zilikuwa zimechafuliwa.
3 Ndiyo, na haya hayakuwa yote; walikuwa watu wa shingo ngumu, kiasi kwamba hawangetawaliwa na sheria wala haki, isipokuwa tu kwa uharibifu wao.
4 Na ikawa kwamba Nefi alikuwa amechoka kwa sababu ya uovu wao; na akaacha kiti cha hukumu, na akajichagua mwenyewe kuhubiri neno la Mungu siku zake zote zilizosalia, na kaka yake Lehi pia, siku zake zote zilizosalia;
5 Kwani walikumbuka maneno ambayo baba yao Helamani aliwazungumzia. Na haya ndiyo maneno aliyosema:
6 Tazama, wana wangu, ninataka kwamba mtii amri za Mungu; na ningetaka kwamba mwatangazie watu maneno haya. Tazama, nimewapatia majina ya wazazi wetu wa kwanza ambao walitoka nchi ya Yerusalemu; na nimefanya hivi ili mnapokumbuka majina yenu mtaweza kuwakumbuka; na mnapowakumbuka mngekumbuka kazi zao; na mkikumbuka kazi zao mngejua jinsi ilivyo semwa, na pia kuandikwa, kwamba walikuwa wema.
7 Kwa hivyo, wana wangu, ninataka kwamba mfanye yale ambayo ni mema, ili izungumzwe juu yenu, na pia iandikwe, hata vile ilivyozungumzwa na kuandikwa juu yao.
8 Na sasa wana wangu, tazama nina kitu kingine ambacho ningetamani mfanye, kutamani ambako ni, kwamba msifanye hivi vitu ili mjisifu, lakini kwamba mfanye hivi vitu kujiwekea wenyewe hazina mbinguni, ndiyo, ambayo ni ya milele, na ambayo haitafifia; ndiyo, ili mpate zawadi ya thamani ya uzima wa milele, ambayo tuna sababu ya kudhani imepewa kwa babu zetu.
9 Ee kumbukeni, kumbukeni, wana wangu, maneno ambayo mfalme Benjamini aliwazungumzia watu wake; ndiyo, kumbukeni kwamba hakuna njia nyingine wala gharama ambayo kwayo binadamu anaweza kuokolewa, isipokuwa kupitia kwa upatanisho wa damu ya Yesu Kristo, ambaye atakuja; ndiyo, kumbuka kwamba anakuja kuukomboa ulimwengu.
10 Na kumbuka pia maneno ambayo Amuleki alimzungumzia Zeezromu, katika mji wa Amoniha; kwani alimwambia kwamba Bwana lazima atakuja kuwakomboa watu wake, lakini kwamba hatakuja kuwakomboa katika dhambi zao, lakini kuwakomboa kutoka kwenye dhambi zao.
11 Na ana uwezo aliopewa kutoka kwa Baba kuwakomboa kutoka kwenye dhambi zao kwa sababu ya toba; kwa hivyo ametuma malaika wake kutangaza habari njema ya hali ya toba, ambayo inaleta uwezo wa Mkombozi, kuwezesha wokovu wa roho zao.
12 Na sasa, wana wangu, kumbukeni, kumbukeni kwamba ni juu ya mwamba wa Mkombozi wetu, ambaye ni Kristo, Mwana wa Mungu, kwamba lazima mjenge msingi wenu; kwamba ibilisi atakapotuma mbele pepo zake kali, ndiyo, mishale yake katika kimbunga, wakati mvua yake ya mawe na dhoruba kali itapiga juu yenu, haitakuwa na uwezo juu yenu kuwavuta chini kwenye shimo la taabu na msiba usioisha, kwa sababu ya mwamba ambao juu yake ninyi mmejengwa, ambao ni msingi imara, msingi ambao watu wote wakijenga hawataanguka.
13 Na ikawa kwamba haya ndiyo maneno ambayo Helamani aliwafundisha wanawe; ndiyo, aliwafundisha vitu vingi ambavyo havijaandikwa, na pia vitu vingi ambavyo vimeandikwa.
14 Na walikumbuka maneno yake; na kwa hivyo walienda mbele, wakitii amri za Mungu, kufundisha neno la Mungu miongoni mwa watu wote wa Nefi, kuanzia mji wa Neema;
15 Na baada ya hapo walienda hadi kwa mji wa Gidi; na kutoka mji wa Gidi hadi mji wa Muleki;
16 Na hata kutoka mji mmoja hadi mwingine, mpaka walipoenda mbele miongoni mwa watu wote wa Nefi ambao walikuwa katika nchi upande wa kusini; na kutoka hapo hadi kwenye nchi ya Zarahemla, miongoni mwa Walamani.
17 Na ikawa kwamba walihubiri kwa uwezo mwingi, mpaka kwamba waliwafadhaisha wengi wa wale waasi ambao walikuwa wameenda huko kutoka kwa Wanefi, mpaka kwamba walikuja mbele na kukiri dhambi zao na wakabatizwa ubatizo wa toba, na mara moja wakarudia Wanefi na kujaribu kurekebisha kwao mabaya ambayo wameyafanya.
18 Na ikawa kwamba Nefi na Lehi waliwahubiria Walamani kwa uwezo mkubwa na mamlaka, kwani walikuwa na uwezo na mamlaka waliyopewa ili waweze kusema, na pia walikuwa nayo yale ambayo wangesema walioneshwa—
19 Kwa hivyo waliweza kusema kwa mshangao mkubwa wa Walamani, kuweza kuwathibitishia, kwa matokeo kwamba kulikuwa Walamani elfu nane ambao walikuwa kwenye nchi ya Zarahemla na karibu na hapo walio batizwa ubatizo wa toba, na wamethibitishiwa juu ya uovu wa desturi za babu zao.
20 Na ikawa kwamba Nefi na Lehi walienda kutoka hapo mpaka kwenye nchi ya Nefi.
21 Na ikawa kwamba walikamatwa na jeshi la Walamani na kutupwa gerezani; ndiyo, hata hilo hilo gerezani ambamo Amoni na ndugu zake walitupwa na watumishi wa Limhi.
22 Na baada ya kutupwa gerezani kwa siku nyingi bila chakula, tazama, walienda gerezani ili wawakamate na kuwaua.
23 Na ikawa kwamba Nefi na Lehi walizungukwa na kile kilichoonekana kama moto, kiasi kwamba hawangeweza kuthubutu kuwagusa kwa mikono yao kwa kuogopa kwamba wangeungua Walakini, Nefi na Lehi hawakuungua; na walionekana kama wanasimama katikati ya moto na hawaungui.
24 Na walipoona kwamba wamezungukwa na nguzo za moto, na kwamba hazikuwachoma, mioyo yao ilipata ujasiri.
25 Kwani waliona kwamba Walamani hawakuthubutu kuwagusa; wala hawangethubutu kuwakaribia, lakini walisimama kama bubu kwa mshangao.
26 Na ikawa kwamba Nefi na Lehi walisimama mbele yao na kuanza kuwazungumzia, wakisema: Msiogope, kwani tazama, ni Mungu ambaye amewaonyesha hiki kitu cha ajabu, ambamo kwayo imeonyeshwa kwenu kwamba hamwezi kutuwekea mikono yenu kutuua.
27 Na tazama, wakati wanasema maneno haya, nchi ilitetemeka sana, na kuta za gereza zilitikisika kama vile zilikaribia kuanguka ardhini; lakini tazama, hazikuanguka. Na tazama, wale ambao walikuwa gerezani walikuwa Walamani na Wanefi ambao walikuwa waasi.
28 Na ikawa kwamba walifunikwa na wingu la giza, na woga wa kutisha mno uliwajia.
29 Na ikawa kwamba kulisikika sauti kama ilitokea juu ya wingu la giza, ikisema: Tubuni ninyi, tubuni ninyi, na msijaribu tena kuwaangamiza watumishi wangu ambao nimewatuma kwenu kutangaza habari njema.
30 Na ikawa wakati waliposikia sauti hii, na kuona kwamba haikuwa sauti ya radi, wala haikuwa sauti kubwa ya kuwachanganya, lakini tazama, ilikuwa sauti tulivu na kadiri, kama mnongʼono, na ilipenya hata kwenye roho—
31 Na ijapokuwa upole wa sauti, tazama ardhi ilitetemeka sana, na kuta za gereza zikatingishika tena, kama vile zilikuwa ziko karibu kuanguka ardhini; na tazama wingu la giza, ambalo lilikuwa limewafunika, halikuondoka—
32 Na tazama sauti ilikuja tena, ikisema: Tubuni ninyi, tubuni ninyi, kwani ufalme wa mbinguni uko karibu; na msijaribu tena kuwaangamiza watumishi wangu. Na ikawa kwamba nchi ilitetemeka tena, na kuta zilitikisika.
33 Na pia tena safari ya tatu sauti ilisikika, na kuzungumza kwao maneno ya ajabu ambayo hayawezi kuzungumzwa na binadamu; na kuta zikatingisika tena, na nchi ikatetemeka kama iko karibu kugawanyika katika sehemu mbili.
34 Na ikawa kwamba Walamani hawangeweza kukimbia kwa sababu ya wingu la giza ambalo liliwafunika; ndiyo, na pia hawangetembea kwa sababu ya woga ambao uliwajia.
35 Sasa kulikuwa mmoja miongoni mwao ambaye alikuwa Mnefi kwa kuzaliwa, ambaye wakati mmoja alikuwa mtu wa kanisa la Mungu lakini akaasi kutoka kwao.
36 Na ikawa kwamba aligeuka, na tazama, aliona kupitia kwenye wingu la giza na akaona nyuso za Nefi na Lehi; na tazama, zilingʼara sana, hata kama nyuso za malaika. Na akaona kwamba waliinua macho yao kuelekea mbinguni; na walikuwa kwa hali kama walikuwa wanaongea au kupaza sauti kwa kiumbe ambacho walimwangalia.
37 Na ikawa kwamba mtu huyu alipaza sauti kwa umati, kwamba wageuke na kuangalia. Na tazama, kulikuwa na uwezo uliotolewa kwao kwamba waligeuka na kutazama; na wakaona nyuso za Nefi na Lehi.
38 Na wakamwambia yule mtu: Tazama, hivi vitu vyote vinaamanisha nini, na ni nani ambaye hawa watu wanaongea naye?
39 Sasa jina la mtu huyu lilikuwa Aminadabu. Na Aminadabu aliwaambia: Wanaongea na malaika wa Mungu.
40 Na ikawa kwamba Walamani walimwambia: Tutafanya nini, ili hili wingu la giza liweze kuondolewa kwamba lisitufunike?
41 Na Aminadabu akawaambia: Lazima mtubu, na mlilie ile sauti, hata mpaka mtakapopata imani katika Kristo, ambaye mlifundishwa kumhusu na Alma, na Amuleki, na Zeezromu; na wakati mtakapofanya hivi, wingu la giza litatolewa kwa kutia kivuli kwenu.
42 Na ikawa kwamba wote walianza kulilia sauti ya yule ambaye alitetemesha nchi; ndiyo, walilia hata mpaka wingu la giza lilipoondoka.
43 Na ikawa kwamba wakati walipotupa macho yao karibu kuzunguka, na kuona kwamba wingu la giza limetoweka kutokana na kuwafunika, tazama, waliona kwamba wamezingirwa, ndiyo, kila nafsi, na nguzo ya moto.
44 Na Nefi na Lehi walikuwa katikati yao; ndiyo, walizingirwa; ndiyo, walionekana kama wako katikati ya ndimi za moto, lakini hazikuwadhuru, wala hazikuchoma kuta za gereza; na walijazwa na hiyo shangwe ambayo haiwezi kuzungumzwa na iliyojaa utukufu.
45 Na tazama, Roho Mtakatifu wa Mungu alishuka chini kutoka mbinguni, na kuingia kwenye mioyo yao, na walijazwa kama na moto, na walizungumza maneno ya ajabu.
46 Na ikawa kwamba kulisikika sauti kwao, ndiyo, sauti nzuri, kama mnongʼono, ikisema:
47 Amani, amani iwe kwenu, kwa sababu ya imani yenu kwa yule Mpendwa Wangu Sana, ambaye alikuwepo tangu msingi wa dunia.
48 Na sasa, wakati waliposikia hivi walitupa macho yao ili waone kule ile sauti ilikotokea; na tazama, waliona mbingu zikifunguka; na malaika wakaja chini kutoka mbinguni na kuwahudumia.
49 Na kulikuwa karibu watu mia tatu ambao waliona na kusikia hivi vitu; na waliambiwa waende na wasistajaabu, wala wasiwe na shaka.
50 Na ikawa kwamba walienda mbele, na kuhudumia watu, wakitangaza kote nchini mahali hapo vitu vyote ambavyo walisikia na kuona, mpaka kwamba sehemu kubwa ya Walamani ilisadikishwa juu yao, kwa sababu ya ushahidi mwingi ambao walikuwa wamepata.
51 Na kama wengi walivyothibitishwa waliweka chini silaha zao za vita na pia chuki yao na desturi za babu zao.
52 Na ikawa kwamba waliwapatia Wanefi nchi ya umiliki wao.