Mlango wa 3
Wana wa Lehi warejea Yerusalemu kupata mabamba ya shaba nyeupe—Labani anakataa kuwapa mabamba—Nefi anawasihi na kuwatia moyo kaka zake—Labani anaiba mali yao na anajaribu kuwauwa—Lamani na Lemueli wanawapiga Nefi na Samu na wanashutumiwa na malaika. Karibia mwaka 600–592 K.K.
1 Na ikawa kwamba mimi, Nefi, nilirudi kwenye hema la baba yangu, baada ya kusema na Bwana.
2 Na ikawa kwamba akanisemesha, na kuniambia: Tazama nimeota ndoto, ambapo Bwana ameniamrisha kwamba wewe na kaka zako mtarejea Yerusalemu.
3 Kwani tazama, Labani anazo kumbukumbu za Wayahudi na pia nasaba ya babu zangu, na zimechorwa kwenye mabamba ya shaba nyeupe.
4 Kwa hivyo, Bwana ameniamrisha mimi kwamba wewe na kaka zako mwende nyumbani kwa Labani, mtafute hayo maandishi, na kuyaleta hapa nyikani.
5 Na sasa, tazama kaka zako wananungʼunika, wakisema kuwa ni kitu kigumu ninachokihitaji kutoka kwao; lakini, tazama mimi sijahitaji hilo kwao, lakini ni amri ya Bwana.
6 Kwa hivyo nenda, mwana wangu, nawe utapendeka kwa Bwana, kwa sababu wewe hujanungʼunika.
7 Na ikawa kwamba mimi, Nefi, nilimwambia baba yangu: Nitaenda na kutenda vitu ambavyo Bwana ameamuru, kwani ninajua kwamba Bwana hatoi amri kwa watoto wa watu, isipokua awatayarishie njia ya kutimiza kitu ambacho amewaamuru.
8 Na ikawa kwamba baada ya baba yangu kusikia maneno haya alifurahi sana, maana alijua kuwa nimebarikiwa na Bwana.
9 Na mimi, Nefi, na kaka zangu tukachukua safari nyikani, pamoja na mahema yetu, tukielekea nchi ya Yerusalemu.
10 Na ikawa kwamba tulipokuwa tumesafiri hadi nchi ya Yerusalemu, mimi na kaka zangu tulijadiliana.
11 Na tukapiga kura—ni nani kati yetu ataingia nyumbani mwa Labani. Na ikawa kwamba kura ikamwangukia Lamani; na Lamani akaenda nyumbani mwa Labani, na akaongea na yeye alipokuwa ameketi nyumbani mwake.
12 Na akamwomba Labani zile kumbukumbu ambazo zilikuwa zimechorwa kwenye mabamba ya shaba nyeupe, ambazo zilikuwa na nasaba ya baba yangu.
13 Na tazama, ikawa kwamba Labani alikasirika, na akamtoa nje; na asitake kumpatia yale maandishi. Kwa hivyo, akamwambia: Tazama wewe ni mnyangʼanyi, na nitakuua.
14 Lakini Lamani alitoroka kutoka kwake, na akatuelezea vitu ambavyo Labani alitufanyia. Na tulishikwa na huzuni nyingi, na kaka zangu walikuwa karibu kurudi nyikani kwa baba yangu.
15 Lakini tazama nikawaambia kwamba: Kadiri Bwana aishivyo, na tuishivyo sisi, hatutarudi kwa baba yetu nyikani mpaka tukamilishe kile kitu ambacho Bwana alituamrisha sisi.
16 Kwa hivyo, tuwe waaminifu katika kushika amri za Bwana; kwa hivyo tuteremke hadi kwa nchi ya urithi ya baba yetu, kwani tazama aliacha dhahabu na fedha, na kila aina ya utajiri. Na haya yote ametenda kwa sababu ya amri za Bwana.
17 Kwani alijua kwamba lazima Yerusalemu iangamizwe, kwa sababu ya uovu wa watu.
18 Kwani tazama, wamekataa maneno ya manabii. Kwa hivyo, kama baba yangu ataishi katika nchi baada ya kuamriwa atoroke nchi hiyo, tazama, pia yeye ataangamia. Kwa hivyo, inabidi lazima atoroke nchi hiyo.
19 Na tazama, ni hekima katika Mungu tupate kuchukua maandishi haya, ili tuweze kuhifadhia watoto wetu lugha ya baba zetu;
20 Na pia kwamba tuwahifadhie maneno yaliyonenwa kwa vinywa vya manabii watakatifu, ambayo walipewa na Roho na nguvu za Mungu, tangu mwanzo wa ulimwengu, hadi nyakati za sasa.
21 Na ikawa kwamba niliwashawishi kaka zangu kwa maneno haya, ili wawe waaminifu kwa kushika amri za Mungu.
22 Na ikawa kwamba tulishuka na kwenda katika nchi yetu ya urithi, na tukakusanya dhahabu yetu, na fedha yetu, na vitu vyetu vya thamani.
23 Na baada ya kukusanya hivi vitu pamoja, tukaenda tena nyumbani mwa Labani.
24 Na ikawa kwamba tulikutana na Labani, na tukataka atupatie zile kumbukumbu ambazo zilikuwa zimechorwa kwenye mabamba ya shaba nyeupe, kwa ajili hiyo nasi tungempatia dhahabu yetu, na fedha yetu, na vitu vyetu vyote vya thamani.
25 Na ikawa kwamba wakati Labani alipoona mali yetu, na kwamba ilikuwa nyingi sana, aliitamani, hadi kwamba akatufukuza nje, na akatuma watumishi wake watuue, ili kwamba aweze kupata mali yetu.
26 Na ikawa kwamba tuliwakimbia watumishi wa Labani, na ikatubidi kuacha mali yetu, na ikangukia mikononi mwa Labani.
27 Na ikawa kwamba tulitorokea nyikani, na watumishi wa Labani hawakutupata, na tukajificha kwenye pango la mwamba.
28 Na ikawa kwamba Lamani alinikasirikia mimi, na baba yangu pia; na pia Lemueli, kwani alisikiliza maneno ya Lamani. Kwa hivyo Lamani na Lemueli walituzungumzia kwa maneno mengi ya uchungu, sisi wadogo zao, na wakatupiga sisi hata kwa bakora.
29 Na ikawa kwamba walipokuwa wakitupiga kwa bakora, tazama malaika wa Bwana alikuja na akasimama mbele yao, na akawazungumzia, akisema: Kwa nini mnampiga mdogo wenu kwa bakora? Hamjui kuwa Bwana amemchagua yeye kuwa kiongozi wenu, na hii ni kwa sababu ya maovu yenu? Tazama mtarudi tena Yerusalemu, na Bwana atamkabidhi Labani mikononi mwenu.
30 Na baada ya malaika kutuzungumzia, akatoweka.
31 Na baada ya malaika kutoweka, Lamani na Lemueli wakaanza kunungʼunika tena, wakisema: Vipi itawezekana kwamba Bwana atamkabidhi Labani mikononi mwetu? Tazama, yeye ni mtu shujaa, na anaweza kuamuru watu hamsini; ndiyo, hata kuwaua watu hamsini; je, kwa nini asituue sisi?