Mlango wa 6
Bwana ataifufua Israeli katika siku za mwisho—Ulimwengu utachomwa kwa moto—Lazima wanadamu wamfuate Kristo ili kuepuka ziwa la moto na kiberiti. Karibia mwaka 544–421 K.K.
1 Na sasa, tazameni, ndugu zangu, kama vile nilivyowaambia kwamba nitatoa unabii, tazama, huu ndiyo unabii wangu—kwamba vile vitu ambavyo huyu nabii Zeno alizungumza, kuhusu nyumba ya Israeli, ambapo aliwalinganisha na mzeituni, lazima vitimie.
2 Na siku ambayo atanyoosha mkono wake tena mara ya pili ili kuwaokoa watu wake, ni siku ile, ndiyo, hata mara ya mwisho, ambayo watumishi wa Bwana wataenda mbele kwa nguvu zake, kulisha na kupogoa shamba lake la mizabibu; na baada ya hayo mwisho utafika.
3 Na heri wale ambao wametumikia shamba lake la mizabibu kwa bidii; na jinsi gani watakavyolaaniwa wale ambao watatupwa mahala pao! Na ulimwengu utachomwa kwa moto.
4 Na jinsi gani alivyoturehemu sisi Mungu wetu, kwani anakumbuka nyumba ya Israeli, mizizi pamoja na matawi; na anawanyoshea mikono yake siku yote na ni watu wenye shingo ngumu na ubishi; lakini wale wote ambao hawatashupaza mioyo yao wataokolewa katika ufalme wa Mungu.
5 Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, ninawasihi kwa maneno ya kiasi kwamba mtubu, na mje kwa moyo wa lengo moja, na mjishikilie kwa Mungu kama vile anavyowashikilia. Na msishupaze mioyo yenu, wakati amewanyoshea mkono wake wa huruma mchana.
6 Ndiyo, leo, kama mtasikia sauti yake, msishupaze mioyo yenu; kwani, kwa nini mfe?
7 Kwani tazama, baada yenu kulishwa kwa neno jema la Mungu kwa siku yote, je, mtazaa matunda maovu, ili mkatwe na kutupwa motoni?
8 Tazameni, je, mtayakataa maneno haya? Je, mtayakataa maneno ya manabii; na je, mtayakataa maneno yote ambayo yamezungumzwa kuhusu Kristo, baada ya wengi sana kuzungumza kumhusu yeye; na kukana neno jema la Kristo, na nguvu ya Mungu, na kipawa cha Roho Mtakatifu, na kuzimisha Roho Mtakatifu, na kufanyia mzaha ule mpango mkuu wa ukombozi, ambao mmepangiwa ninyi?
9 Je, hamjui kwamba mkitenda vitu hivi, kwamba nguvu za ukombozi na ufufuo, ambazo ziko katika Kristo, zitawaleta kusimama katika kiti cha hukumu cha Mungu kwa aibu na hatia kuu?
10 Na kulingana na nguvu za haki, kwani haki haiwezi kuzuiwa, lazima mtupwe kwenye lile ziwa la moto na kiberiti, ambalo ndimi zake za moto hazizimiki, na ambalo moshi wake unapaa juu milele na milele, ambalo ziwa la moto na kiberiti ni mateso yasiyo na mwisho.
11 Ee basi, ndugu zangu wapendwa, tubuni ninyi, na muingie katika mlango uliosonga, na mwendelee katika njia ambayo ni nyembamba, hadi mtakapopokea uzima wa milele.
12 Ee muwe wenye hekima; niseme nini zaidi?
13 Mwishoni, nawaaga kwa heri, hadi nitakapokutana nanyi kwa furaha katika kiti cha enzi cha Mungu, kiti ambacho kinawatia walio waovu woga na hofu ya kutisha. Amina.