2020
Beglind Guðnason—Árnessýsla, Iceland
Aprili 2020


Taswira za Imani

Berglind Guðnason

Árnessýsla, Iceland

Picha
sisters hugging

Berglind (kushoto) pamoja na dada yake Elín (kulia). Wakati Berglind alipokumbana na mfadhaiko mkubwa zaidi ambao amewahi kupitia, alihisi kwamba hangeweza kuendelea. Kwa kuzungumzia mapambano yake pamoja na familia na marafiki, amepata uponyaji wa kiroho na kihisia kupitia vifaa ambavyo Baba wa Mbinguni ametoa.

Mindy Selu, Mpiga Picha

Nimekuwa nikipambana na mfadhaiko tangu nilipokuwa na miaka 13. Wakati mmoja, hali ilikuwa mbaya kwamba nilijaribu kujitoa uhai. Sikuwa na matumaini wakati huo. Nilifikiria, “Sitawahi kuwa na furaha. Sitawahi kutimiza chochote.”

Kuna wakati nilifikiria kuacha Kanisa ilikuwa ndiyo suluhisho la shida zangu kwa sababu sikuwa na matumaini juu ya kitu chochote. Ni rahisi sana kufanya kinyume na matarijio ndani ya Iceland. Kanisa ni dogo sana hapa. Ilikuwa ni mimi tu na ndugu zangu katika madarasa yetu ya Kanisa wakati nikikua. Nilihisi mpweke na kwa muda fulani sikuwa napenda kwenda kanisani.

Watu wengi Iceland hupuuza dini. Watu huanza kunywa pombe wakiwa na umri mdogo. Nilipatikana katika hilo, na sikushiriki kikamilifu kwa muda fulani katika maisha yangu. Sifurahii hilo, lakini ni sehemu ya uzoefu wangu na nilijifunza kwa sababu yake. Nilisoma hotuba ya Mzee Jeffrey R. Holland na nikafurahia kile alichosema: “Ya kale yatufundishe na siyo ya kuyaishi. … Tunapokuwa tumejifunza kile tunachokihitaji … , kisha tunatazama mbele na kukumbuka kwamba imani mara zote imeelekeza kwenye siku za usoni.”1

Siku moja wakati nilipokuwa nikipitia wakati mgumu zaidi, nilisoma baraka yangu ya kipatriaki. Nilipokuwa nikiisoma, nilitambua kwamba niko na siku za usoni. Mungu ana mpango kwa ajili yangu, na Yeye kweli ananipenda. Kwenda Kanisani, kushiriki sakramenti, kusoma maandiko, na kusali kumeleta nuru kubwa na furaha tele maishani mwangu. Baada ya muda niligundua, “Hii kwa kweli inanisaidia.” Hapo ndipo nilipojua siku zote nilitaka injili maishani mwangu. Baada ya yote ambayo nimepitia, ninajua kwamba injili imeokoa maisha yangu, na nina furaha kubwa kwa sababu hiyo.

Kuzungumza kuhusu mfadhaiko wangu pamoja na familia na marafiki kumenisaidia sana. Pia ilileta usaidizi zaidi. Sikutaka kumeza vidonge au kwenda kwenye matibabu. Nilishinda nikijiambia, “Niko na Mungu.” Lakini Mungu anatoa vifaa vingine vingi, kama vile madawa na matibabu, kwa matumizi yetu ikiwa ni pamoja na vitu vya kiroho.

Wakati nilipokuwa nikianza kusoma maandiko yangu zaidi kila siku na kumkaribia Mungu kupitia sala, nilipokea baraka nyingi na ufunuo kwamba lengo langu ni kuwasaidia wengine. Ninahisi kwamba wengi wetu wanakabiliana na shida nyingi za kiakili na tunajaribu kuficha. Mfadhaiko na mapambano yangu vimenifundisha kwamba ni vyema kuzungumza na kuhusiana na wengine. Rafiki yangu hivi karibuni alinifichulia kuhusu kupambana kwake na mfadhaiko. Tulizungumza juu ya hilo na kwa kweli tulielewana.

Si siku zote tunatambua kile wengine wanachopambana nacho, lakini wakati mwingine mimi hutembea tu na kuwaangalia watu wengine na kutambua kwamba Mungu anamfahamu kila mmoja wetu. Anatupenda na anajua hasa kile ambacho kila mmoja wetu anapitia, Na tunaweza kusaidiana.

Kupitia mapambano yangu na mfadhaiko, nimejifunza kuuliza, “Ni nini naweza kujifunza kutoka kwenye jaribu hili?” badala ya “Ni kwa nini napitia jaribu hili?” Napenda Etheri 12:27, ambapo inasema kwamba vitu dhaifu vinaweza kuwa vyenye nguvu kama tutakuwa na imani katika Yesu Kristo. Hii daima inakuwa faraja kwangu.

Sisi wote tulichagua kuja hapa duniani. Tulijua tungeteseka kwa majaribu. Na kwa kweli hicho ndicho kile kinachofanya maisha kuwa mazuri Kwa sababu tunajua kuna mambo mema yatakayokuja. Tunajua kwamba kama tutamfuata Mwokozi kupitia kila kipindi kigumu, tunaweza kupata uzima wa milele na baraka hizi zote ambazo zinatusubiri sisi.

Hakika nimegundua jinsi ambavyo nimebadilika kupitia mfadhaiko wangu. Upatanisho wa Mwokozi ni wa kweli, moyo wangu umabadilika, na nimeimarika. Ninahisi kama mimi ni mtu tofauti na yule niliyekuwa wakati fulani. Watu hutambua na kusema, “Umebadilika.” Msichana mmoja kutoka shuleni alisema, “Naona tofauti na nuru ndani yako.” Ni ajabu kwa sababu yeye hata si muumini wa Kanisa, na hatukuwa tumezungumza sana hapo kabla.

Wakati nilipokuwa katika mfadhaiko wangu mbaya zaidi, watu wangeniambia, “Itakuwa sawa.” Ningechoka sana kusikia hivyo lakini, ajabu na inavyosikika, ni kweli.

Lakini unahitaji kutaka kupata nafuu. Nimejifunza kwamba huwezi kutarajia kupata nafuu kwa kutofanya lolote. Unahitaji kutaka kuwa na furaha na kuamini kwamba una uwezo na siku za usoni. Ni muhimu kukumbuka kwamba unapendwa na watu wengi, ikiwa ni pamoja na Baba yako wa Mbinguni. Wote wapo kukusaidia.

Sikuwahi kufikiria ningekuwa na furaha kama vile nilivyo sasa. Siku zingine bado napambana, lakini pamoja na vifaa ambavyo Baba wa Mbinguni amenipa mimi, naweza kufanikiwa. Sasa wakati nahisi nikiteleza katika mfadhaiko, ninajiambia ninapendwa, ninao watu wa kuzungumza nao, na mambo yatakuwa sawa.

Picha
Berglind sitting down

Kupambana na mfadhaiko kumemfanya Berglind apate ufahamu zaidi wa jinsi ambavyo tunaweza kusaidiana wakati tunapopitia changamoto. “Mungu anamjua kila mmoja wetu, Anatupenda, na Anajua hasa kile ambacho kila mmoja wetu anapitia. Na tunaweza kusaidiana.”

Picha
Berglind smiling

Berglind ameona mabadiliko ndani yake kupitia changamoto zake. “Upatanisho wa Mwokozi ni wa kweli,” anasema. “Moyo wangu umebadilishwa, na nimeimarika. Ninahisi kama mimi ni mtu tofauti na yule niliyekuwa wakati fulani.”

Picha
Berglind reading scriptures

“Wakati nilipokuwa nikianza kusoma maandiko yangu zaidi kila siku,” Berglind anasema, “nilipokea baraka nyingi na ufunuo kwamba lengo langu ni kuwasaidia wengine. Napenda Etheri 12:27, ambapo inasema kwamba vitu dhaifu vinaweza kuwa vyenye nguvu kama tutakuwa na imani katika Yesu Kristo. Hii daima inakuwa faraja kwangu.”

Muhtasari

  1. Jeffrey R. Holland, “‘Kumbuka Mke wa Lutu’: Imani Ni kwa ajili ya Siku za Usoni” (Ibada ya Brigham Young University, Jan. 13, 2009), speeches.byu.edu.