2019
Baraka ya Bonasi
Oktoba 2019


Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Baraka ya Bonasi

Roberto Atúncar Nieto

Lima, Peru

Picha
man holding bags of food

Kielelezo na Ale + Ale, Morgan Gaynin

Mimi na mke wangu, Carmen, tulipata mtoto wetu wa kwanza wakati nilipoitwa kuwa askofu wa kata yetu. Wakati huo, tulikuwa na hali mbaya kifedha. Ilinipa msongo wa mawazo kuwahudumia familia yangu na wakati huohuo kuwaangalia na kuwatunza waumini wa kata yangu.

Jumapili moja, nilimwona mama asiye na mume akiwa na watoto wake wanne katika mkutano wa sakramenti. Alikaa kwenye kiti cha mwisho kanisani na alijaribu kadiri alivyoweza kuwaweka kimya watoto wake. Nilijua alikuwa vilevile na hali mbaya kifedha, lakini hakuwahi kuomba usaidizi. Wiki zilipita, na kila Jumapili alikuja kanisani pamoja na watoto wake.

Siku moja, nilipokea hundi yangu ya malipo. Nikiwa nimebarikiwa kupokea bonasi, niliamua kutumia pesa ya ziada kununua vifaa kwa ajili ya ukarabati muhimu uliohitajika katika nyumba yangu. Lakini nilipokuwa nikielekea sokoni, dada huyu na watoto wake waliniijia akilini mwangu. Nilihisi nilipaswa kutumia pesa ya ziada kununua chakula kwa ajili yao. Nilimpigia Carmen na kumwambia kile nilichohisi nilihitaji kufanya. Alikubali.

Wakati nikifanya manunuzi, macho yangu yalitua kwenye biskuti. Niliwaza kwamba pengine watoto wangependa peremende. Nilijaza mifuko miwili kwa vyakula na kushika njia kuelekea kwenye nyumba ya dada huyu.

Niligonga mlango wa mbao uliochakaa mara kadhaa. Nilipokuwa karibu kuondoka, mlango hatimaye ulifunguliwa. “Askofu,” dada alisema, “nimeshangaa kukuona hapa.” Mara moja, watoto wake walikimbia nje kutoka nyuma yake.

“Nimewaletea chakula,” nilisema.

Mmoja wa mabinti zake aliona biskuti na kusema kwa sauti, “Biskuti!” Kaka zake na dada zake kwa furaha walikusanyika. Binti wa miaka saba alinikumbatia. “Asante, Askofu!” alisema.

Nilitazama ndani ya nyumba yao na kuona kwamba dada huyu alikuwa anafua ndani ya sufuria sakafuni. Familia haikuwa na meza na walilala kwenye magodoro juu ya sakafu. Nilitambua kwa kiasi gani walikuwa na uhitaji. Nilifanya mipango kuhakikisha wangepata meza na kwamba kila mmoja angepata kitanda.

Uzoefu huu ulinisaidia kutambua kwamba Bwana huwaongoza na kuwabariki watumishi Wake. Hatuhitaji wito maalumu ili kuwasaidia akina kaka na dada zetu. Tunahitaji tu kuwa kwenye tuni na Roho, kutambua nani anahitaji usaidizi wetu, na kuwa tayari kuwa vyombo katika mikono ya Bwana.