2019
Baraka za Mtazamo wa Injili
Oktoba 2019


Baraka za Mtazamowa Injili

Kutoka kwenye hotuba ya ibada, “Mtazamo wa Injili,” Iliyotolewa katika Chuo Kikuu cha Brigham Young–Hawaii mnamo Septemba 19, 2017.

Mtazamo wa injili utakupa ubayana mkubwa kuhusiana na jinsi unavyofikiria kuhusu vipaumbele vyako vya maisha, kutatua matatizo, na kukabiliana na majaribu binafsi.

Picha
woman adjusting her eyeglasses

Picha kutoka Getty Images

Ni baraka kuu iliyoje kuwa muumuni wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho katika kipindi cha maongozi ya Mungu wakati ambapo urejesho wa funguo za ufalme na utimilifu wa unabii unaturuhusu kushuhudia moja kwa moja “injili ikienea hata miisho ya dunia, kama vile jiwe lililochongwa mlimani bila kazi ya mikono litabiringika, hadi litaijaza dunia yote” (Mafundisho na Maagano 65:2).

Unabii huu uliotolewa na Danieli wa Agano la Kale na baadaye kurudiwa katika kipindi hiki cha maongozi ya Mungu, unaonekana kuwa katikati ya utimilifu wake wakati tunaposhuhudia vigingi 3,300 vilivyoundwa katika Kanisa leo. Katika miaka 50 iliyopita, uumini katika Kanisa umeongezeka kutoka milioni 2.1 hadi zaidi ya milioni 16.1

Cha kupendeza kwangu kama ulivyo ukuaji huu mkubwa na badiliko ni ukweli kwamba kanuni na utamaduni wa injili havibadiliki, ikiwa ni pamoja na mtindo wa uongozi wa kiungu uliofunuliwa kwa ajili ya Kanisa la Yesu Kristo. Mtindo huu huruhusu uanzishwaji wa vigingi, vilivyokusudiwa kuwa “ngome, na makimbilio wakati wa tufani, na ghadhabu wakati itakapomiminwa pasipo kuchanganywa juu ya dunia yote” (Mafundisho na Maagano 115:6).

Akina kaka na akina dada, Bwana ni mkarimu kwa baraka Anazotupatia. Kuelewa kwamba baraka ni matendo ya utiifu wetu wa amri na kwamba kutii amri ni onyesho la upendo wetu kwa Bwana ni kanuni za thamani kujifunza. Kanuni za injili kama hizi hutoa mtazamo muhimu kwetu.

Hii huongoza kwenye mawazo mawili ambayo ningependa kusisitiza. Niligundua kwamba Rais Dallin H. Oaks, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza, aliwahi kushiriki mawazo haya mawili na vijana wadogo waseja mnamo 2015.

Dumisha Mtazamo wa Injili

Rais Oaks amesema kwamba “mtazamo humaanisha kuona kweli zote katika mahusiano yenye maana, mtazamo wa jumla.”2 Hapa ni baadhi ya mambo unayoelewa wakati unapoona kutokea kwenye mtazamo wa injili:

Fikiria nini hutokea ikiwa mtazamo wako wa injili unakuwa lenzi unayotazamia katika kila kipengele cha maisha yako. Mtazamo wa injili utakupa ubayana mkubwa kuhusiana na jinsi unavyofikiria kuhusu vipaumbele vyako vya maisha, kutatua matatizo, na kukabiliana na majaribu binafsi. Hii inaweza hakika kuathiri mtazamo wako kwa ujumla kwa maisha yako yote na maamuzi mbalimbali utakayofanya njiani.

Kwa mtazamo huu wa nje, tunajua kwamba Bwana anatamani kwamba tupokee sakramenti kila wiki na kwamba tusome maandiko na kusali Kwake kila siku. Kwa kuongezea, tunajua kwamba Shetani atatujaribu ili tusimfuate Mwokozi wetu au kusikiliza misukumo ya upole ya Roho Mtakatifu. Kisha tunaweza kujua zaidi kwamba mjaribu anajitahidi kuchukua uhuru wa kujiamulia na uwezo wa kuhimili juhudi zake kupitia uraibu, ikiwa ni pamoja na madawa ya kulevya na ponografia.

Kinyume chake, lenzi ya injili hutupatia uoni angavu wa umuhimu wa kuanzisha familia—kuchagua ndoa na kuwalea watoto katika haki. Mtazamo huu pia hufungua macho yetu kuona kwamba mjaribu angependa kuangamiza kitengo chote cha familia na kukanganya majukumu ya jinsia, hivyo kuongoza kwenye upungufu wa thamani ambao jamii inaweka kwenye kuunda na kujenga familia.

Dumisha Usawa wa Kiroho

Picha
balanced seesaw

Rais Oaks alisema: “Wakati vijana wakubwa wanapokuwa na mtazamo—mtazamo wa jumla—ni muhimu kwao kudumisha usawa wa kiroho katika maisha yao. Ili kufanya hivi, lazima mjiondoe kutoka kwenye baadhi ya vivutio vya ulimwengu na pia kufanya mambo muhimu ili kusogea karibu na Mwokozi.”3

Kwa upande mmoja, mna misukumo mingi na vipaumbele vya maisha vya aina zote na ukubwa wote, vyote vikihitaji umakini, fokasi, na mwelekeo. Orodha kwa kila mmoja wenu inaweza kuwa tofauti kulingana na hali zenu binafsi, lakini ndani yake hakika mtapata elimu, ajira, ndoa, na vyote kuwa vizuri kihisia na kimwili. Ndiyo, changamoto yenu ni kuwekea usawa majukumu haya muhimu ya maisha dhidi ya mambo yenu ya kiroho.

Rais Oaks pia ameshauri kwamba mnapaswa kuwa makini wakati “mnapopanga muda wenu ili kwamba msijishindishe njaa kiroho wakati ambapo shughuli zenu za msingi ziko kwenye mambo mengine. Kanuni hii inaelezea kwa nini ni muhimu hasa kwa vijana wakubwa … kufuata ushauri wa kuhudhuria mikutano ya Kanisa, kutumikia Kanisani na kusoma maandiko kila siku, kuwa na sala ya kupiga magoti ya familia, na kutumikia katika miito ya Kanisa.4

Katikati ya mahitaji yenu binafsi na tofauti, kuwekea usawa utafutaji na changamoto pamoja na mambo ya kiroho, mtakuja kugundua kwamba usawa unawezekana. Bwana hawahitaji mfanye jambo ambalo hamwezi kufanikisha. Nilimsikia Rais Thomas S. Monson (1927–2018) mara kadhaa akishauri kwamba “yule ambaye Bwana humwita, Bwana humstahilisha.”5 Ninadhani hili hasa ni kweli kwa waumini wa Kanisa.

Ya kutisha kama kuweka usawa huu kunavyoweza kuonekana, ninaahidi kwamba moja ya baraka kubwa ya kuwepo kwenu katika maisha haya itakuwa uwezo wenu wa kupata usawa kati ya mambo yenu ya kiroho na majukumu mengine muhimu ya maisha. Hii inaweza kutokea katika njia ambayo itawaruhusu si tu kudumisha mambo yenu ya kiroho na majukumu muhimu ya maisha kama hali ilivyo lakini pia kukua na kuendelea kwenye maeneo haya yote muhimu.

Sababu kuu ya hili kuwezekana ni kwamba Bwana yupo kwenye egemeo la wenzo. Yeye ni kitovu hasa cha mvutano cha usawa. Na Yeye ana mvuto wa kiungu kwako binafsi kama mmoja wa watoto Wake. Lakini matokeo haya hutoka kwenye fokasi na juhudi yako inayofaa ya kutafuta usawa.

Kutoka kwenye ugunduzi wangu na uzoefu binafsi, inaonekana kwamba tuna tabia kote katika maisha kuegemea zaidi upande mmoja au mwingine. Kubaki kwenye usawa katika maisha yetu kunahitaji juhudi na kujali kwetu kuliko endelevu. Kwa uchangamfu chagua kubaki imara.

Cha kuvutia, inaweza kuwa pande zote. Kunaweza kuwa na nyakati ambapo unajikuta unahitaji kujali ili kuwa na fokasi bayana kwenye kazi yako ya shule au ya kuajiriwa, pamoja na “shughuli za Kanisa zifanywe ndani ya muda wa shughuli za Kanisa.”6 Hata hivyo, kumbuka kumweka Bwana kama egemeo lako la wenzo ili uweze kupata usawa wako wa kiroho unaofaa.

Bwana atakusaidia

Tunapotunza mtazamo wa injili, inakuwa rahisi kuelewa ukweli wa msingi kwamba Bwana atatusaidia. Kanuni ya msingi ya injili ni kwamba sisi ni watoto wa Wazazi wa Mbinguni wenye upendo. Ni asili Yao kutusaidia sisi katika kila njia ili turudi nyumbani kwetu mbinguni.

Ningependa kushiriki mfano wa jinsi gani Bwana anaweza kuwasaidia. Mmoja wa viongozi wangu wa vijana, Thad Carlson, alishiriki nami miaka mingi iliyopita. Thad, ambaye amefariki hivi karibuni, alikuwa na matokeo makubwa kwangu wakati nilipokuwa nakua. Alizaliwa wakati wa Mporomoko Mkuu wa uchumi, akiwa wa tisa kati ya watoto 14. Familia yake ilipata kipato kwa kulima na kufuga ng’ombe. Ulikuwa ni wakati mgumu kifedha, na mali yao kubwa ilikuwa kundi la ng’ombe.

Katika ujana wa Thad, moja ya majukumu yake ilikuwa ni kutunza na, ilipohitajika, kuchunga ng’ombe ili kuhakikisha kwamba walipata malisho mazuri—kazi nzito kwa mvulana mdogo. Aliweza kufanya hili kwa msaada wa farasi mdogo mjanja ambaye alijua barabara nini cha kufanya kwa maelekezo kidogo. Farasi alipewa jina la Smoky Mzee. Lakini Smoky Mzee alikuwa na shida moja: hakutaka kukamatwa. Popote wakati mtu alipomsogelea, angekimbia, akijua kwamba angepewa kazi.

Picha
cowboy on a horse

Siku moja, baada ya Smoky Mzee kukamatwa, kufungwa ugwe, na kuwekewa tandiko, kijana Thad alimwendesha kuelekea mahali ng’ombe walipokuwa wakilisha. Ardhi ilikuwa kavu, na malisho hali kadhalika, lakini Thad aligundua kwamba nyasi nje ya malisho kandokando ya vyuma vya reli zilikuwa ndefu na za kijani. Hivyo alifikiri angewaongoza ng’ombe nje ya uzio wa malisho na kuwaacha wafurahie malisho mazuri kandokando ya vyuma vya reli.

Kwa msaada wa Smoky Mzee, Thad aliongoza ng’ombe nje ya malisho, ambapo walianza kwenda mbele na nyuma kandokando ya vyuma vya reli walika nyasi nzuri, za kijani. Ng’ombe walioridhika walionekana kujisimamia wenyewe, hivyo Thad alishuka kutoka kwenye farasi wake na kuketi juu ya kamba za ugwe, akifurahia mazingira yaliyomzunguka, akicheza na kujifurahisha mwenyewe. Akitafuta kujichunga mwenyewe kwenye nyasi za kijani, hata hivyo, Smoky Mzee hatimaye alienda zake, kamba zake zikiteleza nje kutoka chini ya Thad.

Wakati huu wa kupendeza na wa amani ulifikia kishindo na kusimama ghafla wakati Thad ghafla aliposikia kelele nyingi kutoka mbali. Ilikuwa ni king’ora cha kichwa cha garimoshi iliyokuwa ikija kwa kasi kwenye vyuma vile vya reli ambapo kundi la ng’ombe wake walikuwa wametapakaa kizembe mbele yake! Aligundua kwamba madhara yangeweza kuwa ya kutisha kwa kundi la mifugo na pia kwa familia yake kama asingefanya uamuzi wa haraka kurudisha ng’ombe kwenye malisho na mbali na garimoshi iliyokuwa inakuja. Alihisi kwamba asingeweza kujisamehe kwa kutotimiza majukumu yake aliyoaminiwa kwayo.

Thad kwa haraka aliruka na kusimama na kukimbia ili kushika kamba za Smoky Mzee. Smoky Mzee alimwona Thad akija na haraka aliruka mbali naye, kwa kutotaka kukamatwa. Bila pumzi na kwa kukata tamaa, pamoja na taswira za ng’ombe waliokufa na janga la familia vikipita akilini mwake, Thad alijua alipaswa kutenda kwa haraka.

Baadaye aliandika kile kilichotokea: “Mwalimu wangu wa Msingi alikuwa ametufundisha jinsi ya kusali na kuimarisha mafunzo niliyojifunza kutoka kwa mama yangu. Bila kuwa na njia nyingine, nilipiga magoti na kuanza kusali kwa ajili ya msaada wa kuwaondoa ng’ombe kutoka kwenye vyuma.”

Thad hakusikia sauti, lakini wazo dhahiri lilimuijia: “Umegundua jinsi ng’ombe wanavyoweza kutembea kando ya Smoky Mzee na hakimbii. Hivyo … sasa kwa kuwa umepiga magoti, pia weka mikono yako kwenye kazi. Fanya kama vile wewe ni ng’ombe na tambaa kuekekea kwa Smoky Mzee.”

That alisema: “nilifanya hivyo. hakukimbia. Nilishika kamba zake, kumuongoza kwenye uzio, nikaruka mgongoni kwake, na tulikimbia kama upepo kuwarudisha ng’ombe kwenye malisho. Smoky Mzee alikuwa mzuri sana kwenye kupindapinda na kugeuka.”

Baadaye, wakati Thad alipokuwa shule ya upili, ilieleweka kwake kikamilifu kwamba alikuwa amepokea jibu dhahiri kwa sala yake katika wakati hasa wa uhitaji. Alisema, “Malaika walimhudumia Smoky Mzee kupita uwezo wangu, na familia yetu ilikuwa imeepushwa na janga.” Baadaye alisema: “Huu ulikuwa wa kwanza kati ya misukumo mingi ambayo [ilipaswa] kuja kwangu. ‘Na chochote mtakachomwomba Baba katika jina langu, ambacho ni haki, mkiamini kwamba mtapata, tazama, kitapewa kwenu’ (3 Nefi 18:20).”7

Sote tuna ng’ombe wa kuwaondoa kutoka kwenye vyuma vya reli kabla ya garimoshi kufika. Magumu yetu huja kwa maumbo mengi na ukubwa tofauti. Baadhi ni hatari kama hali ya hatari ya Thad, yakiwa na madhara ya kutishia maisha au kutishia nafsi zetu au za wapendwa wetu.

Hali zingine tunazokumbana nazo zinaweza zisiwe na madhara ya hatari kama hayo lakini hata hivyo huelemea akili na mioyo yetu. Kitu kimoja ni hakika—kila mmoja wetu atapata dhiki na mateso katika maisha yetu kwa sababu ni sehemu ya uzoefu wetu wa maisha ya duniani. Lakini kumbuka, Bwana atatusaidia!

Ninayapenda maneno haya yanayopatikana kwenye Kitabu cha Mormoni: “Tunaona kwamba Mungu ni mwangalifu kwa kila watu, nchi yoyote ambayo wangekuwa ndani; ndio, huhesabu watu wake, na ana huruma za kutosha kwa ulimwengu wote” (Alma 26:37).

Hiyo humaanisha kila mmoja wetu. Ni faraja kuu iliyoje kujua kwamba Bwana atatusaidia.

Imani, Tumaini na Mtazamo wa Injili

Kwa ufupisho, ninawahimiza kukumbuka kudumisha mtazamo wa injili. Tazama ulimwengu unaokuzunguka kupitia lenzi ya injili ya Yesu Kristo.

Dumisha usawa wa kiroho. Sote tunapata changamoto na fursa katika majukumu yetu mbalimbali ya maisha, na yanahudumiwa ipasavyo wakati tunapoyawekea usawa na imani yetu katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake.

Mwisho, kuwa na imani na tumaini kwamba Bwana atakusaidia. Ufahamu huu ndio unaokusaidia kwa ujasiri kupambana na changamoto ambazo ni sehemu isiyoepukika ya misheni yako ya maisha ya duniani.

Muhtasari

  1. Ona “Ripoti ya Takwimu, 2018,” Liahona, Mei 2019, 112.

  2. Dallin H. Oaks, mkutano wa mafunzo wa vijana wakubwa waseja, Feb. 8, 2015, Jiji la Salt Lake, Utah.

  3. Dallin H. Oaks, mkutano wa mafunzo wa vijana wakubwa waseja, Feb. 8, 2015.

  4. Dallin H. Oaks, mkutano wa mafunzo wa vijana wakubwa waseja, Feb. 8, 2015.

  5. Thomas S. Monson, “Wajibu wa Miito,” Ensign, Mei 1996, 44.

  6. Dallin H. Oaks, mkutano wa mafunzo wa vijana wakubwa waseja, Feb. 8, 2015.

  7. Thad Carlson, barua binafsi.