2019
Kuzungumzia Ponografia: Linda, Shughulikia, & Ponya
Oktoba 2019


Kuzungumzia Ponografia: Linda, Shughulikia, & Ponya

Kutoka kwenye ujumbe wa hutoba ya msingi ililotolewa kwenye mkutano wa Muungano Dhidi ya Ponografia wa Utah mnamo 2018 katika Jiji la Salt Lake, Utah.

Matumizi haya matatu ya upendo yanaweza kuwasaidia watoto wetu katika hatari za ponografia wanazoweza kukutana nazo.

Picha
mother and daughter hugging

Picha kutoka Getty Images, imetumika kwa malengo ya kielelezo, imeandaliwa kwa mtindo

Ninafahamu kwa maumivu makali juu ya athari ya ponografia kwa hata wale walio wadogo kabisa katika jamii yetu—watoto wetu. Maadili potovu ya kiwango cha juu, ponografia yanaweza kusababisha aibu, usaliti, uharibifu wa hisia, upotevu wa kujizuia, uraibu uliokithiri, na utekaji wote wa muda, mawazo, na nguvu. Kuna hitaji kubwa kwetu sote—wazazi, familia, walimu, viongozi—kuona hasa, thamani, na kuwalinda watoto na vijana wetu.

Upendo ni kati ya zawadi kubwa za Mungu. Kumpenda Mungu na kumpenda jirani ni amri kuu mbili tulizopewa kutoka kwa Yesu Kristo Mwenyewe. Upendo, ninaamini, pia ni silaha kuu katika kupigana dhidi ya ponografia.

Hakika, kama msemo maarufu unavyosema, “ponografia huua upendo,” lakini acha pia tukumbuke kwamba upendo huua ponografia. Hiyo haina maana kwamba upendo wetu kwa mtu unaweza kubadili uraibu wao au hata tabia zao. Bali upendo unaweza kutupatia msukumo—jinsi tunavyojiandaa, jinsi tunavyojibu, jinsi tunavyosikiliza—hususan kwa watoto wetu. Ikiwa tunakwenda kuwa na tumaini lolote la kufuta maadili haya potovu kutoka ulimwenguni, upendo lazima uwe mbele na msingi wa juhudi zetu zote.

Ninapenda kupendekeza matumizi matatu ya upendo ambayo ninatumai tutayafokasia, kuyakumbatia, na kuyafanya kuwa sheria. Matumizi haya matatu yameunganishwa kwenye awamu tatu za hatari ya ponografia watoto wetu wanaweza kukutana nazo.

Kwanza, tunasema “nakupenda” kwa kuwalinda kweli. Pili, tunasema “bado nakupenda” kwa jinsi tunavyoshughulikia mfichuo wao kwenye ponografia, iwe kwa kukusudia au la. Na tatu, tunasema “daima nitakupenda” kwa kutoa msaada wa upendo kwa ajili yao pale wanapofanyia kazi uponyaji ikiwa wapepata uzoefu wa matumizi yaliyokithiri au uraibu. Katika kila awamu, upendo ni muhimu.

1. Ulinzi: “Nakupenda”

Pata taswira akilini ya mtoto unayempenda. Wakati unapomwambia mtoto huyu, “Nakupenda,” hiyo ina maana gani? Kwenye kiini chake, ina maana kwamba tunatoa ulinzi ili kwamba tuweze kuwasaidia wale tunaowapenda kuwa bora na kukabili changamoto za maisha. Sehemu ya ulinzi ni kutengeneza mahusiano imara, yenye uaminifu, na yenye muendelezo. Aina hizi za mahusiano husaidia kuwaleta watoto wetu karibu. Wakati tunapojenga mahusiano ya uaminifu na kuwalinda watoto wetu na wajukuu zetu—au mtoto yeyote—tunawapa sehemu salama ya kugeukia. Ulinzi huu huwasaidia kuelewa wao ni akina nani na huwasaidia kufahamu uhusiano wao na Mungu. Kuhisi kuthaminiwa na kupendwa huwasaidia watoto kutazama na kutegemea ulinzi wa Baba wa Mbinguni anayetoa maelekezo kwa ajili ya furaha yao.

Nina wasiwasi kwamba wazazi wengi bado wanaweza wasitambue jinsi ponografia ilivyo hatari au wanaweza kudhani ni tatizo la mvulana wa jirani. Uhalisia ni kwamba tatizo hili linawaathiri wavulana na wasichana wetu, na hatulizungumzii vya kutosha.

Miaka mingi iliyopita, mimi na mume wangu tulisikia hadithi yenye maana ambayo tumeirudia mara nyingi kwa watoto wetu. Hadithi inahusu nyoka wa zamani mwenye mkia wa kuchacharika ambaye alimuomba mvulana mpita njia kumpeleka kwenye kilele cha mlima ili aone mawio ya mwisho ya jua kabla nyoka hajafa. Mvulana alisita, lakini nyoka aliahidi kutomuuma kama gharama ya kumbeba. Baada ya makubaliano hayo, mvulana kwa ukarimu alimpeleka nyoka kwenye kilele cha mlima ambapo walitazama mawio ya jua pamoja.

Baada ya kumrudisha nyoka chini ya bonde, mvulana aliandaa chakula kwa ajili yake na kitanda kwa ajili ya usiku. Asubuhi, nyoka aliuliza, “Tafadhali, kijana mdogo, unaweza kunirudisha nyumbani kwangu? Ni muda wangu sasa kuondoka katika ulimwengu huu, na ningependa kurudi nyumbani.” Mvulana alihisi amekuwa salama na nyoka alitimiza neno lake, hivyo aliamua angemrudisha nyoka nyumbani kama alivyoomba.

Kwa uangalifu alimwinua nyoka, akamweka karibu na kifua chake, na kumrudisha jangwani nyumbani kwake ili afe. Kabla tu hajamweka nyoka chini, nyoka aligeuka na kumuuma kifuani. Mvulana alilia na kumtupa nyoka chini. “Bwana Nyoka, kwa nini umefanya hivyo? Sasa nitakufa hakika!” Nyoka alimtazama na kumweleza kwa tabasamu: “Ulijua mimi ni nani uliponibeba.”

Katika ulimwengu wa leo, ninawaona wazazi wengi wakimpa mtoto wao nyoka. Ninazungumzia simu janja. Hatuwezi kuweka simu za mkononi zenye intaneti kwenye mikono ya watoto wetu wadogo ambao si wakubwa vya kutosha kuwa waliofundishwa vya kutosha, bado hawana uwezo muhimu wa kupambanua mambo na kufanya-uamuzi, na ambao hawana udhibiti wa wazazi na nyenzo zingine ili kusaidia kuwalinda. Jason S. Carroll, profesa wa maisha ya familia wa Chuo Kikuu cha Brigham Young, alisema, “Tunawalinda watoto wetu mpaka wakati ambapo wanaweza kujilinda wenyewe.” Shina la ubongo, ambalo linahifadhi viini vya burudani vya ubongo, vinajengeka kwanza. Ni mpaka baadaye ndipo uwezo wa kupambanua na kufanya-maamuzi kwenye upande wa mbele wa tabaka la nje la ubongo hujengeka kikamilifu. “Hivyo watoto wana pedeli ya gesi isiyo na breki kamili.”1

Kila simu inapaswa kuwa na ulinzi, hata za vijana. Huu ni ushauri mzuri pia kwa watu wazima. Hakuna aliyekingwa na muumo wa nyoka mwenye sumu. Baadhi ya wazazi wanatumia simu za kurusha kwa kidole kama mbadala kwa watoto wao ili kupunguza matumizi yabaki kwenye kupiga na kutuma arafa.

Zaidi ya simu janja kuna vyombo vingine vingi ambavyo vinaweza kufikia vyombo vya habari visivyotakiwa kupitia intaneti. Utafiti wa karibuni ulionesha kwamba asilimia 79 ya matumizi yasiyotakiwa ya ponografia yanafanyika nyumbani.2 Watoto wanaweza kujikuta kwenye ponografia kwa kutumia tablets, simu janja, michezo ya kuliwaza, DVD za kubebeka, na TV janja, kati ya vingine vingi. Ninazifahamu familia ambazo zimetengeneza eneo moja, lenye foleni-kubwa nyumbani kwao ambapo vifaa vya kielektroniki vinatumika. Familia hizi zinaliita “chumba cha vyombo vya habari,” na vifaa vyao vyote vimewekwa wazi, kwenye mwanga. Kamwe hakuna mtu yeyote anayekuwa peke yake chumbani kwenye kifaa cha vyombo vya habari.

Familia zingine zimechagua sheria kama hakuna simu kwenye vyumba vya kulala au maliwatoni. Baadhi husema tu, “kamwe usiwe peke yako na simu.” Bado wengine taratibu huongeza matumizi kwenye apps ambazo watoto wao wanaweza kutumia pamoja na maunzi laini ambayo huruhusu simu ya mtoto kusanidiwa na wazazi. Kwa njia hii wanafundisha kwamba uaminifu unapatikana na kwamba usalama wa simu ni muhimu.

Vyovyote mahitaji yalivyo kwa familia zetu, acha tumfundishe kila mwanafamilia kutumia teknolojia kwa busara na katika njia chanya tokea mwanzo—ili kujenga mzingatio wa kimaadili. Acha tuwape elimu watoto katika njia za kujenga ili watumie teknolojia kwa ajili ya wema. Tunaweza kuwafundisha kutathmini kwa kujiuliza wenyewe, “Je, kutumia hii kutatimiza malengo mema?” Chaguzi zetu katika jinsi tunavyozifundisha familia zetu sasa kutaathiri vizazi vijavyo.

Kama wazazi, natumaini tutafikiria umuhimu wa mahusiano yetu na watoto wetu na juhudi maalumu tunazofanya ili kuwalinda. Tunapoimarisha mahusiano haya ya kupendeza, watoto wataelewa vyema kwa nini Mungu anaonya dhidi ya uovu wa ponografia, watatambua jinsi ya kuiepuka, na watakuwa wamejiandaa ikiwa watakutana nayo.

Picha
father talking with his son

Picha kutoka Getty Images, imetumika kwa malengo ya kielelezo, imeandaliwa kwa mtindo

2. Kushughulikia: “Bado Nakupenda”

Kujenga mazungumzo ya kukaribisha, ya wazi, na yenye kualika ambayo yanahimiza watoto kushiriki mawazo yao, uzoefu, na maswali pamoja na wazazi wao si rahisi. Tunaweza kuwaalika watoto wa umri wote kuja mbele ikiwa au wakati wanapojenga hatua yoyote ya tatizo la ponografia—kuanzia matumizi ya mapema, yasiyo ya kukusudia ya mara chache, mpaka matumizi makubwa, na chini mpaka kwenye matumizi yaliyokithiri. Majadiliano ya mapema ni mazuri, na watoto watakuja mbele wakiwa tayari zaidi wakati wanapojua wanapendwa na hakuna wanachosema au kufanya kinaweza kubadili upendo huo.

Mara chache sana, hata hivyo, mtoto anakuja mbele kwa kujitolea. Mara nyingi inatokea wakati mzazi mchunguzi anapomjaribu mtoto kwa, “Kuna tatizo?” au “Huonekani kuwa kawaida.” Kadiri mtoto anavyohisi upendo, ndivyo inavyokuwa rahisi kwake kufunguka.

Hakikisho hili la upendo linajengwa katika akili zao kutokana na uzoefu mdogo ambao huchukua nafasi tena na tena. Matatizo madogo madogo yaliyozungumziwa katika njia ya upendo yanajenga msingi wa majibu mazuri ili kwamba wakati matatizo makubwa yanapokuja, mawasiliano yanakuwa bado wazi. Cha muhimu zaidi, watoto wanajua kwamba mwitikio wako utakuwa, “Bado nakupenda. Siachi kukupenda kwa sababu jambo fulani limetokea. Daima ninakupenda.”

Kwa sababu fulani, hatuzungumzi sana na vijana pamoja na watoto kuhusu moja ya hamu kubwa na majaribu makubwa watakayokabiliana nayo. Kutotaka kwetu kunawaweka kwenye kufundishwa na intaneti, watoto wengine au vijana wabalehe, au hata vyombo maarufu vya habari. Baadhi yetu tunaweza kusita hata kutumia neno ponografia karibu na watoto katika juhudi ya kulinda usafi wao. Linaonekana la aibu sana. Pengine wazazi wetu hawakuwahi kuzungumza nasi wazi hivyo. Vipi ikiwa mazungumzo yetu yanachochea udadisi? Vipi ikiwa wanataka kujua zaidi? Ni kwa jinsi gani tunatarajia watoto wetu kuzungumza nasi kuhusu ponografia ikiwa hatujawahi kamwe kuzungumza nao kuhusu hilo?

Wazazi, tunapaswa kuanzisha mazungumzo na kutosubiri watoto waje kwetu. Ninapenda pendekezo la kuwa na mazungumzo ya kawaida, ya mara kwa mara, ya kufariji badala ya tukio la mara-moja. Faida za mazungumzo yenye kujali ni kwamba wazazi na viongozi wa kuaminika ni wataalamu, siyo Google; mazungumzo yanaweza kutokea katika mazingira salama; na mazungumzo huongeza uaminifu wa mtoto. Tunataka watoto wahisi kuandaliwa na kuwezeshwa, siyo kuogopa. Tunataka kuzungumza nao na siyo kuwazungumzia.

Kama wazazi na walimu, hatuwezi kuwasaidia watoto ikiwa sisi wenyewe hatuna elimu. Kufundisha nini na kwa nini ni muhimu. Tunaweza kujifunza sisi wenyewe na kuwasaidia watoto kuelewa kwa nini ponografia ni mbaya, kwa nini ni hatari sana, kwa nini hatutaki iwaumize, na nini cha kufanya ikiwa watakutana nayo.

Je, tunawapa watoto wetu kwa nini ya kutosheleza katika njia zinazoendana na umri wao? Ikiwa sababu pekee tunayowapa ya kuepuka ponografia ni “Ni mbaya,” hiyo inaweza kuishia kuwa sababu isiyofaa. Badala yake, lazima tuwasilishe kwa nini nyingi kadiri tuwezavyo ili kujenga maadili ya muhimu ambayo yanaleta msukumo kwa vijana wetu.

Kuna sababu tele za kuepuka ponografia, lakini hizi ni motisha chache tu kutoka shirika la Fight the New Drug ambazo zinaweza kuwavutia vijana wetu:

  • Ponografia inaweza kubadilisha na kutandaza nyaya upya kwenye ubongo wako, na utafiti unaonesha kwamba inaweza hata kufanya ubongo wako kuwa mdogo na usioshiriki kikamilifu.

  • Ponografia inaweza kuwa uraibu.

  • Ponografia itaharibu kujiamini kwako.

  • Ponografia inaweza kukuacha mpweke.

  • Ponografia inaweza kuwaumiza wale unaowapenda.

  • Ponografia inaweza kuharibu kujamiiana kwenye siha.

  • Ponografia imeungana na vurugu.

  • Ponografia husababisha watu hatimaye kutokuwa waaminifu.

  • Ponografia itakunyang’anya muda wako na nguvu zako.

  • Ponografia husababisha msongo wa mawazo, wasiwasi na aibu.

Ningependa kuongeza kuwa ponografia ni kunyume na amri za Mungu. Hizi pamoja na sababu zingine nyingi, tunajenga kesi dhidi ya ponografia, lakini elimu bila utekelezaji hupelekea kukata tamaa. Lazima tuweke mipaka inayofaa, na yenye kusaidia, ukomo na matarajio. Kuwasaidia watoto kujenga uwazaji wao wenyewe wa kimantiki wa ndani kwa kutaka kukaa mbali na ponografia ni muhimu. Ikiwa mtoto hawezi kujiamulia mwenyewe wapi pa kusimama kwenye suala hili, anaweza kuwa sehemu ya takwimu za sasa za kushangaza.

3. Uponyaji: “Daima Nitakupenda”

Wakati watoto wanapokutana na ponografia na kunaswa nayo, wanahangaika kuonyesha hisia, kurudia hali ya mwanzo, na kupona. Msaada wa dhati, wa kweli, endelevu, imara, na wenye uvumilivu unahitajika pale watoto wanapochukua majukumu kwa ajili ya uponyaji wao na kusonga mbele. Hakuna anayeweza kutoa aina hii ya usaidizi kama mzazi anavyoweza kutoa. Baada ya kuwa tumefundisha ukweli kwa makini na kibinafsi, baada ya kuwa tumejenga uaminifu na kuhimiza mazungumzo, watoto wanahitaji kujua kwamba licha ya makosa na chaguzi zao, hakikisho letu litakuwa, “Daima nitakupenda hata iweje.”

Ninakumbuka tukio rahisi lililotokea katika familia yetu miaka iliyopita. Mimi na mume wangu tulikuwa mbali na nyumbani, na kijana wetu mkubwa alikuwa akiwaangalia watoto wengine. Tulipokea simu kutoka kwa jirani aliyekuwa na wasiwasi akitutahadharisha kwamba gari la zima moto lilikuwa nyumbani kwetu. Tuliharakisha nyumbani na kukuta kwamba mwana wetu wa miaka 10 alikuwa akicheza kwenye ua wa nyuma karibu na shamba la hekari-sita la nyasi ndefu, zilizokauka. Alijaribu kuona ikiwa angeweza kuwasha moto kwa cheche.

Na alifanya hivyo! Muda tuliofika, moto mdogo ulikuwa umezimwa na idara ya moto, na wazima moto walikuwa wamempa elimu mwana wetu, na majirani walianza kutawanyika. Mwana wetu alishikwa na aibu, woga, machozi, na alijua hakika alikuwa matatizoni.

Sote tuliingia ndani. Mwana wetu alikuwa na woga kwamba, japokuwa hali ilikuwa mbaya, yote tuliyoweza kufanya ilikuwa ni kuweka mikono yetu kumzunguka mvulana huyu mzuri na kumhakikishia upendo wetu na faraja kwamba hakuumia.

Wakati watoto wanapokutana na ponografia na hasa wanaponaswa kwenye utando wake, watakuwa na aibu, woga, na machozi pia. Ni vigumu kuchukua kitu ambacho kimekuwa gizani na kukiweka kwenye nuru. Inaleta hisia za aibu na kuhitaji msaada. Wanaweza kushindwa na kupata changamoto njiani pale wanaporudia hali ya mwanzo na kupona. Uhitaji wao wa upendo endelevu ni muhimu. Hata hivyo, wazazi wanahitaji kufahamu kwamba upendo wao daima utasaidia lakini siyo tu kitu kinachohitajika.

Katika kupona, utahitaji kugeuza upendo huo ulionao kwa mtoto wako kwenye kutafuta nyenzo sahihi za kusaidia. Upendo wako ni msingi wa kile kinachopaswa kutokea, lakini ikiwa mtu unayempenda amenaswa, yawezekana ukahitaji kutafuta wataalamu wanaoweza kumsaidia mpendwa wako na kukusaidia pia. 

Pale wewe na mpendwa wako mnapotafuta uponyaji, ninatumaini kwamba mtapata nguvu katika Yule ambaye ana nguvu za kuponya majeraha yote, kuwaunganisha watu pamoja, na kujenga mahusiano kupita uwezo wetu wa sasa wa kufikiria. Mwokozi wetu, Mponyaji muungwana, ana nguvu ya kuokoa. Tunaweza kuwa wazazi wa watoto wetu na kuwaelekeza Kwake, lakini Yeye pekee anaweza kuwa Mwokozi wao. Na kitu cha kupendeza ni kwamba Yeye anawapenda watoto wetu hata kikamilifu zaidi ya tunavyowapenda—bila kujali chochote.

Picha
Jesus with children

Maelezo ya kina kutoka Let the Little Children Come unto Me, by Carl Heinrich Bloch

Muhtasari

  1. Jason S. Carroll, katika Lisa Ann Thomson, “Mbinu Nane za Kuwasaidia Watoto Kukataa Ponografia,” Liahona, Aug. 2017, 19.

  2. “Ukweli kuhusu Tishio Mtandaoni,” Parents Television Council Watchdog (blog), June 21, 2017, w2.parentstv.org/blog.