Mkutano Mkuu
Angalia Barabarani
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


Angalia Barabarani

Kufokasi kwenye vitu ambavyo ni muhimu sana—hasa vitu vile “vilivyo barabarani,” vitu vile vya milele—ni muhimu katika kusonga katika maisha haya.

Nilipofikisha umri wa miaka 15, nilipokea kibali cha mwanafunzi, ambacho kiliniruhusu kuendesha gari ikiwa mmoja wa wazazi wangu atakuwa pamoja nami. Wakati baba yangu aliponiuliza kama ningependa kwenda kuendesha gari, nilifurahi sana.

Yeye aliendesha maili chache hadi nje ya mji hata kwenye barabara ndefu, iliyonyooka, yenye njia mbili ambayo watu wachache waliitumia—wacha nisema, labda mahali pekee ambapo yeye angehisi salama. Akasimamisha gari kando ya barabara, na tukabadilishana viti. Alinipatia mafunzo kiasi na kisha akaniambia, “Pole pole ingia barabarani na uendeshe mpaka nitakapokuambia simama.”

Nilifuata maagizo barabara. Lakini baada ya kama sekunde 60, alisema, “Mwanagu. Simamisha gari. Unanifanya nihisi kichefuchefu. Unayumba yumba kote barabarani.” Aliuliza, “Unaangalia nini?

Kwa kuudhika, nikasema, “Ninaangalia barabarani.”

Kisha akasema hivi: “Ninayaangalia macho yako, na wewe unaangalia tu kile kilicho hasa mbele ya boneti ya gari. Kama ukiangalia tu moja kwa moja kile kilicho mbele yako, kamwe hautaweza kuendesha gari kwa unyoofu.” Kisha akasisitiza, “Angalia Barabarani. Hiyo itakuwezesha kuendesha gari kwa unyoofu.”

Kama mwenye umri wa miaka 15, nilidhani kwamba hilo lilikuwa funzo zuri la kuendesha gari. Tangu wakati huo nimetambua kwamba hilo lilikuwa funzo kuu la maisha pia. Kufokasi kwenye vitu ambavyo ni muhimu sana—hasa vitu vile “vilivyo barabarani,” vitu vile vya milele—ni muhimu katika kusonga katika maisha haya.

Wakati mmoja katika maisha ya Mwokozi, Yeye alitamani kuwa peke yake, kwa hiyo “alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba.”1 Aliwatuma wanafunzi Wake mbali kwa maelekezo ya kuvuka bahari. Katika kiza cha usiku, mashua iliyowabeba wanafunzi ikakutana na dhoruba kali. Yesu alienda kuwaokoa lakini kwa njia isiyo ya kawaida. Maelezo ya maandiko yanasema, “Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari.”2 Wanafunzi walipomwona,wakaanza kuwa na hofu, kwani walidhania kitu kilichokuwa kinawajia kilikuwa ni pepo au kivuli. Yesu, alipoona kufadhaika kwao na akataka kuwatuliza akili zao na mioyo yao, alinena nao, “Jipeni moyo ni mimi; msiogope.”3

Petro hakufarijika tu bali pia alipata hamasa. Akiwa daima mwenye ujasiri na haraka Petro alimwambia Yesu, “Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.”4 Yesu akajibu kwa mwaliko unaofahamika na wa milele: “Njoo.”5

Petro, hakika akisisimka kwa matazamio haya, akashuka chomboni si ndani ya maji bali juu ya maji. Huku akifokasi kwa Mwokozi, angeweza kufanya yasiyowezekana, hata kutembea juu ya maji. Mwanzoni, Petro hakutishwa na dhoruba. Lakini “upepo mkali”6 mwishowe ulimvuruga, na akapoteza fokasi. Woga ukarejea. Hatimaye, imani yake ikafifia, na akaanza kuzama. “Akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.”7 Mwokozi, ambaye daima yu tayari kuokoa, alimfikia na kumwinua mpaka kwenye usalama.

Kuna masomo mengi ya kujifunza kutokana na tukio hili la kimuujiza, lakini nitataja matatu.

Fokasi juu ya Kristo

Somo la kwanza: Fokasi juu ya Yesu Kristo. Wakati Petro alipofokasi macho yake juu ya Yesu, aliweza kutembea juu ya maji. Dhoruba, mawimbi, na upepo visingemzuia yeye alimradi aliweka fokasi yake juu ya Mwokozi.

Kuelewa dhumuni letu la juu hutusaidia kuamua kile ambacho juu yake fokasi yetu inapaswa kuwa. Hatuwezi kucheza mchezo wenye mafanikio bila kujua lengo, wala hatuwezi kuishi maisha yenye maana bila kujua dhumuni lake. Mojawapo ya baraka kuu za injili ya urejesho ya Yesu Kristo ni kwamba hujibu, miongoni mwa vitu vingine, swali “Ni lipi dhumuni la maisha?” “Dhumuni letu katika maisha haya ni kuwa na furaha na kujiandaa kurudi kwenye uwepo wa Mungu.”8 Kukumbuka kwamba tuko hapa duniani kijiandaa kurudi kuishi pamoja na Mungu hutusaidia kufokasi kwenye vitu ambavyo vitatuongoza kwa Kristo.

Kufokasi juu ya Kristo huhitaji nidhamu, hasa kuhusu tabia ndogo ndogo na rahisi za kiroho ambazo hutusaidia kuwa wafuasi bora. Hakuna ufuasi pasipo nidhamu.

Fokasi yetu kwa Kristo inakuwa wazi zaidi tunapoangalia barabarani ambapo tunataka kuwa na ni kina nani sisi tunataka kuwa na kisha kutenga muda kila siku kufanya yale mambo ambayo yatatusaidia kufika huko. Kufokasi juu ya Kristo kunaweza kurahisisha maamuzi yetu na kutoa mwongozo wa jinsi tunavyoweza kutumia vyema muda wetu na rasilimali zetu.

Ingawa kuna vitu vingi vinavyostahili fokasi yetu, tunajifunza kutoka kwenye mfano wa Petro umuhimu wa daima kumweka Kristo katika kiini cha fokasi yetu. Ni kupitia Kristo pekee ambapo tunaweza kurudi kuishi na Mungu. Tunategemea neema ya Kristo tunapojitahidi kuwa kama Yeye na kutafuta msamaha Wake na nguvu za kuimarisha pale tunaposhindwa.

Jihadhari na Vitu Vinavyovuruga Umakini

Somo la pili: jihadhari na vitu vinavyovuruga umakini. Wakati Petro alipogeuza fokasi yake kutoka kwa Yesu na kuiweka kwenye upepo na mawimbi yaliyokuwa yakichapa miguu yake, alianza kuzama.

Kuna vitu vingi “mbele ya boneti” ambavyo vinaweza kuvuruga umakini wetu kutoka kwenye kufokasi juu ya Kristo na vitu vya milele ambavyo vipo “barabarani.” Ibilisi ni mvurugaji mkuu. Tunajifunza kutoka kwenye ndoto ya Lehi kwamba sauti kutoka katika jumba kubwa na pana zinatafuta kutuvutia kwenye vitu ambavyo vitatuchepua kutoka kwenye njia ya kujiandaa kurudi kuishi na Mungu.9

Lakini kuna vitu vingine vya kuvuruga umakini ambavyo si vya kawaida sana ambavyo vinaweza kuwa hatari. Kama msemo unavyosema, “Kitu muhimu pekee kinachohitajika ili uovu ushinde ni kwa watu wema kutofanya chochote.” Adui anaonekana kukusudia kuwafanya watu wema kutofanya chochote, au angalau kupoteza muda wao kwenye vitu ambavyo vitavuruga umakini wao kutoka kwenye madhumuni yao na malengo yao ya juu. Kwa mfano, baadhi ya mambo ambayo ni mbadala mzuri kwa kiasi yanaweza kuwa vivuruga mawazo visivyo na afya pasipo nidhamu. Adui anajua kwamba vivuruga mawazo si lazima viwe vibaya au visivyo na maadili ili viweze kufaa.

Tunaweza Kuokolewa

Somo la tatu: tunaweza kuokolewa. Wakati Petro alipoanza kuzama, alipiga yowe, “Bwana niokoe. Na mara moja Yesu akanyoosha mkono Wake, na akamshika.”10 Tunapojikuta tukizama, wakati tunakabiliana na mateso, au wakati tunapojikwaa, sisi pia tunaweza kuokolewa na Yeye.

Katikati ya mateso au majaribu, unaweza kuwa kama mimi na kutumaini kwamba uokozi utakuja haraka. Lakini kumbuka kwamba Mwokozi aliwasaidia Mitume katika wakati wa zamu ya nne usiku—baada ya kuwa wametumia masaa mengi ya usiku wakitaabika kwenye upepo.11 Tunaweza kuomba kwamba kama msaada hautakuja haraka, angalau utakuja katika zamu ya pili au hata ya tatu ya usiku wa mateso yetu. Inapobidi tusubiri, tuwe na uhakika kwamba Mwokozi daima anatazama, akihakikisha kwamba hatutahitaji kuvumilia zaidi ya vile tunavyoweza.12 Kwa wale wanosubiria katika zamu ya nne ya usiku, labda bado wako katikati ya kuteseka, msipoteze tumaini. Uokozi daima huja kwa waaminifu, iwe ni wakati wa maisha ya duniani au katika milele.

Wakati mwingine kuzama kwetu huja kwa sababu ya makosa yetu na uvunjaji wa sheria. Kama utajikuta ukizama kwa sababu hizo, fanya uchaguzi wa furaha wa kutubu.13 Ninaamini kwamba hakuna kinachompa Mwokozi furaha zaidi kuliko wale wanaogeuka, au wanaorudi, Kwake.14 Maandiko yamejaa hadithi za watu ambao mwanzo walikuwa wameanguka na kuwa na madoa lakini walitubu na kuwa imara katika imani ya Kristo. Ninadhani hadithi hizo zipo katika maandiko kutukumbusha kwamba upendo wa Mwokozi kwetu na uwezo Wake wa kutukomboa havina mwisho. Sio tu Mwokozi hupata shangwe tunapotubu, bali sisi pia tunapokea shangwe kuu.

Hitimisho

Ninawaalika muwe na kusudi kuhusu “kuangalia barabarani” na kuongeza fokasi yenu kwenye vitu vile ambavyo vina maana hasa. Na tumweke Kristo katika kiini cha fokasi yetu. Katikati ya vivuruga umakini vyote, vitu vilivyo “mbele ya boneti,” na vimbunga vinavyotuzunguka, ninashuhudia kwamba Yesu ni Mwokozi wetu na Mkombozi wetu na Muokoaji wetu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.