Mkutano Mkuu
Hitaji la Kanisa
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


Hitaji la Kanisa

Maandiko kwa uwazi yanafundisha chanzo na hitaji la kanisa lililoongozwa na Bwana wetu, Yesu Kristo, na kwa mamlaka Yake.

Miaka mingi iliyopita, Mzee Mark E. Petersen, mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alianza hotuba kwa mfano huu wa dhahania.

“Keneth na mkewe, Lucille, ni watu wema, waaminifu na waadilifu. Hawaendi kanisani, hata hivyo, na wanahisi wanaweza kuwa wema vya kutosha bila kanisa. Wanawafunza watoto wao uaminifu na utu wema na wanajiambia wao wenyewe kwamba hayo ndiyo Kanisa linaloweza kuwafanyia.

“Na, hata hivyo, wanasisitiza kwamba wanahitaji wikiendi zao kwa ajili ya burudani za familia … [na] kwenda kanisani kutaingilia ratiba zao.”1

Leo, ujumbe wangu unahusu watu kama hao wema na wenye fikra ya kidini ambao wameacha kuhudhuria au kushiriki katika makanisa yao.2 Ninaposema “makanisa,” ninajumuisha masinagogi, misikiti au mashirika mengine ya kidini. Tuna wasiwasi kwamba mahudhurio kwenye majengo haya yote yameshuka kwa kiasi kikubwa, nchi nzima.3 Ikiwa tutaacha kuyapa umuhimu makanisa yetu kwa sababu yoyote ile, tunahatarisha maisha yetu binafsi ya kiroho na idadi kubwa inayojitenga kutoka kwa Mungu inapunguza baraka Zake kwa nchi zetu.

Uhudhuriaji na ushiriki kikamilifu kanisani hutusaidia kuwa watu bora na ushawishi bora katika maisha ya wengine. Kanisani tunafunzwa jinsi ya kufanyia kazi kanuni za kidini. Tunajifunza kutoka kwa kila mmoja. Mfano wenye ushawishi una nguvu kubwa kuliko mahubiri. Tunaimarishwa kwa kujumuika na wengine wenye mawazo sawa na yetu. Katika kuhudhuria na kushiriki kanisani, mioyo yetu inakuwa, kama Biblia inavyosema, “imeunganishwa katika upendo.”4

I.

Maandiko ambayo Mungu amewapa Wakristo katika Biblia na katika ufunuo wa siku za leo kwa uwazi yanafundisha hitaji la kanisa. Yote yanaonesha kwamba Kristo alianzisha kanisa na akaona kwamba kanisa lingeendeleza kazi Yake baada Yake. Aliwaita Mitume Kumi na Wawili na kuwapatia mamlaka na funguo za kuliongoza. Biblia inafundishwa kwamba Kristo ni “kichwa cha kanisa”5 na kwamba maafisa wa kanisa waliwekwa “kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe.”6 Hakika Biblia iko wazi kwenye chanzo cha kanisa na hitaji la kanisa sasa.

Baadhi husema kwamba kuhudhuria mikutano ya kanisa hakuwasaidii. Baadhi husema, “Sikujifunza chochote leo” au “Hakuna aliyekuwa rafiki kwangu” au “Nilikwazwa.” Kutokuridhika binafsi hakupaswi kamwe kutuondoa kwenye injili ya Kristo, ambaye alitufunza kutumikia, na si kutumikiwa.7 Tukiwa na hili akilini, muumini mwingine alielezea fokasi ya uudhuriaji wake Kanisani:

“Miaka mingi iliyopita, nilibadili mtazamo wangu juu ya kwenda kanisani. Siendi tena kanisani kwa ajili yangu, bali kuwafikiria wengine. Mimi nahakikisha kuwa nimesalimia watu ambao huketi peke yao, nakaribisha wageni, … najitolea kwa jukumu fulani. …

“Kwa ufupi, ninaenda kanisani kila wiki kwa nia ya kushiriki kikamilifu, si kutoshiriki, na kuleta tofauti chanya kwenye maisha ya watu.”8

Picha
Makaribisho kanisani

Rais Spencer W. Kimball alifundishwa kwamba “Hatuendi kwenye mikutano ya Sabato ili kuburudishwa au kufundishwa tu. Tunakwenda kumwabudu Bwana. Ni jukumu la mtu binafsi. … Kama ibada ni mbaya kwako, ni wewe ndiye umeshindwa. Hakuna awezaye kuabudu kwa ajili yako; unapaswa kujifanyia mwenyewe kumngojea kwako Bwana.”9

Uhudhuriaji kanisani unaweza kuifungua mioyo yetu na kutakasa nafsi zetu.

Picha
Mkutano wa baraza la kata.

Kanisani hatuhudumu peke yetu au kwa uchaguzi wetu au manufaa yetu. Daima tunahudumu kama timu. Katika kuhudumu tunapata fursa muafaka za kuinuka juu ya ubinafsi wa umri wetu. Huduma inayoongozwa na Kanisa hutusaidia kushinda ubinafsi ambao unaweza kudumaza ukuaji wetu wa kiroho.

Kuna faida zingine muhimu za kutaja, hata kwa ufupi. Kanisani tunajumuika na watu wema ambao wanajitahidi kumtumikia Mungu. Hii inatukumbusha kwamba hatuko peke yetu katika shughuli zetu za kidini. Sote tunahitaji kujumuika na wengine na mijumuiko ya kanisa ni baadhi ya mijumuiko mizuri zaidi tunayoweza kuwa nayo, kwa ajili yetu na wenza wetu na watoto wetu. Bila mijumuiko hiyo, hususani kati ya watoto na wazazi waaminifu, utafiti unaonesha ongezeko la ugumu kwa wazazi kuwalea watoto katika imani yao.10

II.

Mpaka hapa, nimezungumza kuhusu makanisa kwa ujumla. Sasa ninazungumzia sababu maalumu za uumini, uhudhuriaji na ushiriki katika Kanisa la Mwokozi lililorejeshwa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Picha
Hekalu la Salt Lake

Sisi, hata hivyo, tunathibitisha kwamba maandiko, ya kale na ya siku za leo, kwa uwazi yanafundisha chanzo na hitaji la Kanisa lililoongozwa na Bwana wetu, Yesu Kristo, na kwa mamlaka Yake. Tunashuhudia pia kwamba Kanisa lililorejeshwa la Yesu Kristo limeanzishwa ili kufundisha utimilifu wa mafundisho Yake na kutenda kwa mamlaka Yake ya ukuhani kufanya ibada muhimu za kuingia ufalme wa Mungu.11 Waumini ambao huacha kuhudhuria Kanisani na kutegemea mambo yao binafsi ya kiroho hujitenga kutoka kwenye mambo haya muhimu ya injili: nguvu na baraka za ukuhani, utimilifu wa mafundisho yaliyorejeshwa na motisha na fursa za kufanyia kazi mafundisho hayo. Wanapoteza fursa yao ya kufuzu kuiendeleza familia yao milele.

Faida nyingine kubwa ya Kanisa lililorejeshwa ni kwamba linatusaidia kukua kiroho. Ukuaji humaanisha badiliko. Katika mtazamo wa kiroho hii humaanisha kutubu na kutafuta kuwa karibu zaidi na Bwana. Katika Kanisa lililorejeshwa tuna mafundisho, hatua na visaidizi vyenye mwongozo ambavyo hutusaidia katika kutubu. Lengo lake hata katika mabaraza ya uumini, si adhabu, kama yalivyo matokeo ya mahakama za makosa ya jinai. Mabaraza ya uumini ya Kanisa kwa upendo hutafuta kutusaidia tustahili neema ya msamaha iliyowezeshwa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.

Picha
Wamisionari wanandoa
Picha
Kutembea kuelekea hekaluni

Mambo binafsi ya kiroho kamwe hayawezi kutoa motisha na mpangilio kwa ajili ya huduma isiyo na ubinafsi inayotolewa na Kanisa lililorejeshwa. Mifano mikubwa ya hili ni wavulana na wasichana na wanandoa wazee ambao huweka kando shule yao au shughuli za kustaafu ili kukubali miito ya umisionari. Wanahudumu kama wamisionari kwa watu wasiowafahamu katika sehemu wasizozijua ambazo hawakuzichagua. Hilo ni kweli pia kwa waumini waaminifu ambao hushiriki katika huduma isiyo na ubinafsi tunayoiita “kazi ya hekalu.” Huduma kama hiyo isingewezekana bila Kanisa ambalo linaidhamini, linaipangilia na linaiongoza.

Imani ya kidini ya waumini wetu na huduma ya Kanisa vimewafunza jinsi ya kufanya kazi kwa juhudi za ushirikiano ili kunufaisha jumuiya kubwa. Uzoefu na maendeleo ya namna hiyo havitokei katika ubinafsi ambao umekithiri katika matendo ya jamii zetu za leo. Katika mpangilio wa kijiografia wa kata zetu, tunajumuika na kufanya kazi na watu ambao vinginevyo tusingewachagua, watu ambao hutufunza na kutujaribu.

Katika kuongezea kwenye kutusaidia kujifunza sifa za kiroho kama vile upendo, huruma, msamaha na uvumilivu, hii hutupatia fursa ya kujifunza jinsi ya kufanya kazi na watu wenye tamaduni na mapendeleo tofauti. Faida hii imewasaidia wengi wa waumini wetu na mashirika mengi yamebarikiwa kwa ushiriki wao. Watakatifu wa Siku za Mwisho ni mashuhuri kwa uwezo wao wa kuongoza na kuungana katika juhudi za ushirikiano. Utamaduni huo ulianza kwa waanzilishi wetu majasiri ambao waliitawala sehemu ya milima ya Magharibi na kuanzisha utamaduni wetu wenye thamani wa ushirikiano usio na ubinafsi kwa faida ya wote.

Picha
Mradi wa Mikono Saidizi

Juhudi nyingi za kibinadamu na za hisani zinahitaji kufanikishwa kwa kuleta pamoja na kusimamia rasilimali za mtu mmoja mmoja kwa kiwango kikubwa. Kanisa lililorejeshwa hufanya hili kwa juhudi zake kubwa za kibinadamu ulimwenguni kote. Hizi hujumuisha usambazaji wa vifaa vya elimu na madawa, kuwalisha wenye njaa, kuwatunza wakimbizi, kusaidia kuzuia matokeo ya uraibu na nyingine nyingi. Waumini wetu wa kanisa ni maarufu kwa miradi yao ya Mikono Saidizi katika majanga ya asili. Uumini Kanisani huturuhusu kuwa sehemu ya juhudi hizo kubwa. Waumini pia hulipa matoleo ya mfungo ili kuwasaidia masikini walio miongoni mwao.

Picha
Kushiriki sakramenti.

Katika kuongezea kwenye kuhisi amani na furaha kupitia wenza wa Roho, waumini wetu wanaohudhuria Kanisani hufurahia matunda ya kuishi injili, kama vile baraka za kuishi neno la hekima na ustawi wa kifedha na kiroho ulioahidiwa kwa kuishi sheria ya zaka. Tunayo pia baraka ya ushauri kutoka kwa viongozi waliopokea uvuvio.

Nzuri zaidi ya haya yote ni ibada za muhimu za ukuhani zilizo muhimu kwa ajili ya milele, ikijumuisha sakramenti tunayopokea kila siku ya Sabato. Ibada ya juu katika Kanisa lililorejeshwa ni agano lisilo na mwisho la ndoa, ambalo linafanya uwezekane mwendelezo wa mahusiano matukufu ya familia. Rais Russell M. Nelson alifundisha kanuni hii katika njia ya kukumbukwa. Alisema: “Hatuwezi kutamani njia yetu kwenye uwepo wa Mungu. Lazima tutii sheria ambazo juu yake [baraka hiyo] imetoka.”12

Moja ya sheria hizo ni kuabudu kanisani kila siku ya Sabato.13 Kuabudu kwetu na kutumia kwetu kanuni za milele hutuleta karibu zaidi na Mungu na kukuza uwezo wetu wa kupenda. Parley P. Pratt, mmoja wa Mitume wa mwanzo wa kipindi hiki, alieleza vile alivyohisi wakati Nabii Joseph Smith alipoelezea kanuni hizi: “Nilihisi kwamba Mungu hakika alikuwa Baba yangu wa mbinguni; kwamba Yesu alikuwa kaka yangu na kwamba mke wangu wa halali alikuwa asiyekufa, mwenza wa milele: mkarimu, malaika mhudumiaji, niliyepewa kama faraja na taji ya utukufu milele na milele. Kwa ufupi, ningeweza sasa kupenda kwa roho na kwa uelewa pia.”14

Katika kuhitimisha, ninawakumbusha wale wote ambao hatuamini kwamba mema yanaweza tu kupatikana kupitia kanisa. Mbali na kanisa, tunaona mamilioni ya watu wakiunga mkono na kufanya kazi nyingi njema. Kama watu binafsi, Watakatifu wa Siku za Mwisho wanashiriki kwenye nyingi za hizo. Tunaona kazi hizi kama dhihirisho la ukweli wa milele kwamba “Roho hutoa nuru kwa kila mtu ajaye katika ulimwengu.”15

Licha ya kazi njema ambazo zinaweza kufanywa bila kanisa, utimilifu wa mafundisho na ibada zake za kuokoa na kuinuliwa zinapatikana tu katika Kanisa lililorejeshwa. Kwa nyongeza, uhudhuriaji Kanisani hutupatia nguvu na ongezeko la imani ambalo huja kutokana na kujumuika na waaminio wengine na kuabudu pamoja na wale ambao wanajitahidi pia kubaki kwenye njia ya agano na kuwa wafuasi wazuri wa Kristo. Ninaomba kwamba sote tuweze kuwa imara katika uzoefu huu wa Kanisa wakati tunapotafuta uzima wa milele, zawadi ambayo ni kuu kuliko zawadi zote za Mungu, katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Mark E. Petersen, “Eternal Togetherness,” Ensign, Nov. 1974, 48.

  2. Ona D. Todd Christofferson, “Kwa Nini Kanisa,” Liahona, Nov. 2015, 108–11.

  3. Ona Jeffrey M. Jones, “U.S. Church Membership Falls Below Majority for First Time,” Gallup, Mar. 29, 2021, news.gallup.com/poll/341963/church-membership-falls-below-majority-first-time.aspx.

  4. Wakolosai 2:2.

  5. Ona Waefeso 5:23–24.

  6. Waefeso 4:12.

  7. Ona Yakobo 1:27.

  8. Mark Skousen to Dallin H. Oaks, Feb. 15, 2009.

  9. Teachings of Presidents of the Church: Spencer W. Kimball (2006), 173–74.

  10. Ona Elizabeth Weiss Ozotak, “Social and Cognitive Influences on the Development of Religious Beliefs and Commitment in Adolescence,” Journal for the Scientific Study of Religion, vol. 28, no. 4 (Dec. 1989), 448–63.

  11. Ona Yohana 3:5.

  12. Russell M. Nelson, “Now Is the Time to Prepare,” Liahona, Mei 2005, 18.

  13. Ona Mafundisho na Maagano 59:9.

  14. Autobiography of Parley P. Pratt,, ed. Parley P. Pratt Jr. (1938), 298.

  15. Mafundisho na Maagano 84:46; msisitizo umeongezwa, ona pia Mafundisho na Maagano 58:27–28.