Mkutano Mkuu
Je, Hapana Zeri katika Gileadi?
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


Je, Hapana Zeri katika Gileadi?

Nguvu ya uponyaji ya Mwokozi si tu uwezo Wake wa kuponya miili yetu, pengine hata muhumu zaidi, uwezo Wake wa kuponya mioyo yetu.

Muda mfupi baada ya misheni yangu, nikiwa mwanafunzi wa Chuo cha Brigham Young, nilipokea ujumbe wa simu kutoka kwa baba yangu. Aliniambia kwamba alikuwa amegundulika kuwa na saratani ya kongosho na kwamba, japokuwa uwezekano wake wa kunusurika ulikuwa mdogo, alikusudia kuponywa na kurejea kwenye shughuli zake za kawaida za maisha. Ujumbe ule wa simu ulikuwa wasaa wa huzuni kwangu. Baba yangu amekuwa askofu wangu, rafiki yangu na mshauri wangu. Wakati mimi, mama yangu na ndugu zangu tulipotafakari wakati ujao, ulionekana kuwa na kiza. Kaka yangu mdogo, Dave, alikuwa akitumikia misheni huko New York na alishiriki akiwa mbali katika matukio haya magumu ya familia.

Watoa tiba wa siku hizo walipendekeza upasuaji ili kujaribu na kupunguza kuenea kwa saratani. Familia yetu kwa dhati ilifunga na kuomba kwa ajili ya muujiza. Nilihisi kwamba tulikuwa na imani ya kutosha kwamba baba yangu angeponywa. Kabla tu ya upasuaji, mimi pamoja na kaka yangu mkubwa, Norm, tulimpa baba baraka. Kwa imani yote ambayo tungeweza kuleta pamoja, tuliomba kwamba angeweza kuponywa.

Upasuaji ulipangwa kuchukua masaa mengi, lakini baada ya muda mfupi tu, daktari alikuja kwenye chumba cha kusubiria kukutana na familia yetu. Alituambia kwamba walipoanza upasuaji, waliweza kuona kwamba saratani ilikuwa imesambaa kote katika mwili wa baba yangu. Kulingana na kile walichogundua, baba yangu alikuwa na muda mchache tu wa kuishi. Tulipatwa na hofu.

Baba yangu alipozinduka kutoka kwenye upasuaji, alikuwa na hamu ya kujua ikiwa upasuaji ulikuwa wenye mafanikio. Tulishiriki naye taarifa ya kuogofya.

Tuliendelea kufunga na kuomba kwa ajili ya muujiza. Wakati afya ya baba yangu ilipodhoofu kwa haraka, tulianza kuomba kwamba aweze kuondolewa maumivu. Hatimaye, pale hali yake ilipozidi kuwa mbaya, tulimwomba Bwana ampumzishe haraka. Miezi michache tu baada ya upasuaji, kama ilivyobashiriwa na daktari, baba yangu alifariki.

Upendo mwingi na kujali vilitolewa na waumini wa kata pamoja na marafiki kwa familia yetu. Tulikuwa na mazishi mazuri ambayo yalitoa heshima kwa maisha ya baba yangu. Hata hivyo, kadiri muda ulivyopita, na tulipitia maumivu ya kutokuwepo kwa baba yangu, nilianza kujiuliza kwa nini baba yangu hakuponywa. Nilijiuliza ikiwa imani yangu haikuwa imara vya kutosha. Kwa nini baadhi ya familia zinapokea muujiza lakini familia yetu haikupokea? Nilikuwa nimejifunza katika misheni yangu kugeukia maandiko kwa ajili ya majibu, hivyo nilianza kupekua maandiko.

Agano la Kale linafundisha juu ya kiungo chenye harufu nzuri au mafuta, yaliyotumika kuponya majeraha, yaliyotengenezwa kutokana na kichaka kilichostawi huko Gileadi. Katika nyakati za Agano la Kale, mafuta hayo yalikuja kujulikana kama “zeri ya Gileadi.”1 Nabii Yeremia aliomboleza juu ya majanga ambayo aliyaona miongoni mwa watu wake na kutazamia uponyaji. Yeremia aliuliza, “Je, Hapana zeri katika Gileadi? huko hakuna tabibu?”2 Kupitia fasihi, muziki na sanaa, Mwokozi Yesu Kristo mara nyingi amekuwa akifananishwa na Zeri ya Gileadi kwa sababu ya nguvu Yake kuu ya uponyaji. Kama vile Yeremia, nilikuwa nikijiuliza, “Je, Hapana zeri katika Gileadi kwa ajili ya familia ya Nielson?”

Katika Marko sura ya 2 ya Agano Jipya, tunamkuta Mwokozi akiwa Kapernaumu. Neno la nguvu ya uponyaji ya Mwokozi lilikuwa limeenea kote katika mji na watu wengi walisafiri kwenda Kapernaumu ili waponywe na Mwokozi. Kulikuwako wengi wamekusanyika kuzunguka mahali ambapo Mwokozi alikuwapo kwamba hapakuwa na nafasi ya kutosha kuwapokea wote. Wanaume wanne walimbeba mtu mgonjwa wa kupooza ili aponywe na Mwokozi. Hawakuweza kumkaribia kwa sababu ya makutano na hivyo walitoboa dari ya nyumba na kumshusha mgonjwa chini ili akutane na Mwokozi.

Niliposoma tukio hili, nilishangazwa na kile Mwokozi alichosema alipokutana na mwanamume huyu: “Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.”3 Niliwaza kwamba ikiwa ningekuwa mmoja wa wale wanaume wanne waliombeba mtu huyu, ningeweza kumwambia Mwokozi, “Sisi tulimleta hapa mahususi ili aponywe.” Nadhani Mwokozi angeweza kujibu, “Nimemponya.” Je, iliwezekana kwamba sikuwa nimeelewa kikamilifu—kwamba nguvu ya uponyaji ya Mwokozi haikuwa tu uwezo Wake wa kuponya miili yetu bali, pengine hata muhumu zaidi, uwezo Wake wa kuponya mioyo yetu na mioyo iliyovunjika ya familia yangu?

Mwokozi alifunza somo muhimu kupitia uzoefu huu wakati Yeye hatimaye alipomponya mtu huyu kimwili. Ilikuwa wazi kwangu kwamba ujumbe Wake kwangu ulikuwa kwamba Yeye angeweza kugusa macho ya wale waliokuwa vipofu na wangeweza kuona. Angeweza kugusa masikio ya wale waliokuwa viziwi na wangeweza kusikia. Angeweza kugusa miguu ya wale ambao hawakuweza kutembea na wangetembea. Anaweza kuponya macho yetu na masikio yetu na miguu yetu, lakini muhimu zaidi ya yote, Yeye anaweza kuponya mioyo yetu wakati anapotusafisha kutoka dhambi na kutuinua kupita majaribu magumu.

Wakati Mwokozi anapoonekana kwa watu katika Kitabu cha Mormoni baada ya ufufuko wake, Anazungumza tena juu ya nguvu Yake ya uponyaji. Wanefi wanasikia sauti Yake kutoka mbinguni ikisema, “je mtarudi kwangu sasa, na kutubu dhambi zenu, na kugeuka ili niwaponye?”4 Baadaye, Mwokozi anafundisha, “Kwani hamjui lakini watarudi na kutubu, na kuja kwangu kwa moyo wa lengo moja, na nitawaponya.”5 Mwokozi hakuwa akimaanisha uponyaji wa kimwili bali uponyaji wa kiroho wa nafsi zao.

Moroni analeta uelewa wa ziada pale anaposhiriki maneno ya baba yake, Mormoni. Baada ya kuzungumza juu ya miujiza, Mormoni anaeleza, “Na Kristo amesema: Ikiwa mtakuwa na imani ndani yangu mtakuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote ambacho ni cha kufaa kwangu.”6 Nilijifunza kwamba kusudio la imani yangu lazima liwe Yesu Kristo na kwamba nilihitaji kukubali kile kilichofaa Kwake wakati nilipoonesha imani Kwake. Ninaelewa sasa kwamba kufariki kwa baba yangu ilikuwa ni ya kufaa kwenye mpango wa Mungu. Sasa, wakati ninapoweka mikono yangu juu ya kichwa cha mwingine ili kumbariki, imani yangu ipo katika Yesu Kristo, na ninaelewa kwamba mtu anaweza na ataweza kuponywa kimwili, ikiwa jambo hilo linafaa katika Kristo.

Upatanisho wa Mwokozi, ambao unafanya upatikanaji wa vyote ukombozi na nguvu yake ya kuwezesha, ni baraka ya juu ambayo Yesu Kristo hutoa kwa wote. Tunapotubu kwa kusudi halisi la moyo, Mwokozi hutusafisha kutoka dhambini. Tunapoyakabidhi kwa furaha mapenzi yetu kwa Baba, hata katika nyakati ngumu, Mwokozi atainua mizigo yetu na kuifanya miepesi.7

Lakini hapa ni somo kubwa zaidi nililojifunza. Niliamini kimakosa kwamba nguvu ya uponyaji ya Mwokozi haikufanya kazi kwa familia yangu. Ninapotazama nyuma sasa kwa macho yaliyokomaa na uzoefu zaidi, ninaona kwamba nguvu ya Mwokozi ya uponyaji ilikuwa dhahiri katika maisha ya kila mwanafamilia yangu. Nilikuwa nimefokasi zaidi kwenye uponyaji wa kimwili kiasi kwamba nilishindwa kuona miujiza ambayo ilitokea. Bwana alimuimarisha na kumwinua mama yangu zaidi ya uwezo wake kupita jaribu hili gumu na mama aliongoza maisha marefu na yenye tija. Alikuwa na ushawishi chanya wa kuvutia kwa watoto na wajukuu zake. Bwana alitubariki mimi na ndugu zangu kwa upendo, umoja, imani na uthabiti ambavyo vilikuwa sehemu muhimu ya maisha yetu na vinaendelea leo.

Lakini vipi kuhusu baba yangu? Kama ilivyo kwa wote watakaotubu, yeye aliponywa kiroho pale alipotafuta na kupokea baraka zinazopatikana kwa sababu ya Upatanisho wa Mwokozi. Alipokea ondoleo la dhambi zake na sasa anangojea muujiza wa Ufufuo. Mtume Paulo alifundisha, “Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.”8 Unaona, nilikuwa namwambia Mwokozi, “Tulimleta baba yangu kwako ili aponywe,” na sasa ni dhahiri kwangu kwamba Mwokozi alimponya. Zeri ya Gileadi ilifanya kazi kwa familia ya Nielson—si katika njia ambayo tuliitegemea, bali katika njia yenye maana zaidi ambayo imebariki na inaendelea kubariki maisha yetu.

Katika Yohana sura ya 6 ya Agano Jipya, Mwokozi alifanya muujiza wa kuvutia sana. kwa samaki wachache na mikate michache, Mwokozi aliwalisha watu 5,000. Nimesoma tukio hili mara nyingi, lakini kuna kipengele cha uzoefu huo nilikikosa ambacho sasa kina maana kubwa kwangu. Baada ya Mwokozi kuwalisha watu 5,000, aliwaambia wanafunzi wake wakusanye vipande vilivyobakia, mabaki, ambayo yalijaza vikapu 12. Nimejiuliza kwa nini Mwokozi alichukua muda kufanya hivyo. Imekuwa wazi kwangu kwamba somo moja tunaloweza kujifunza kutokana na tukio hilo ni hili: Yeye angeweza kuwalisha watu 5,000 na kulikuwa na mabaki. “Na neema yangu inatosha watu wote.”9 Nguvu ya Mwokozi ya ukombozi na uponyaji inaweza kufunika dhambi yoyote, jeraha au jaribu—bila kujali ni kubwa kiasi gani au gumu kiasi gani—na kuna masalia. Neema yake yatosha.

Kwa ufahamu huo, tunaweza kusonga mbele kwa imani, tukijua kwamba nyakati ngumu zinapokuja—na hakika zitakuja—au dhambi inapozingira maisha yetu, Mwokozi anasimama na “uponyaji katika mbawa zake,”10 akitualika tuje Kwake.

Ninatoa ushahidi wangu juu ya Zeri ya Gileadi, Mwokozi Yesu Kristo, Mkombozi wetu na juu ya nguvu Yake kuu ya uponyaji. Ninatoa ushahidi wangu juu ya tamanio Lake la kukuponya wewe. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.