Mkutano Mkuu
Utafutaji kwa Uaminifu Hupewa Tuzo
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


Utafutaji kwa Uaminifu Hupewa Tuzo

Nawaalikeni sote tuongeze imani yetu kwa Kristo daima, ambaye anaendelea kubadilisha maisha ya wale wote wanaomtafuta Yeye.

Kuanzia mwaka 1846, maelfu ya waanzilishi wanaume, wanawake na watoto walielekea magharibi hadi Sayuni. Imani yao kubwa ilichochea ujasiri wao usio na mipaka. Kwa wengine, safari hiyo haikumalizika kwani walifariki njiani. Wengine, wakikabiliwa na dhiki kubwa, walisonga mbele kwa imani.

Kwa sababu yao, vizazi vingi baadaye, familia yangu ilifurahia baraka za injili ya kweli ya Yesu Kristo.

Kama vile kijana mwingine, ambaye nitamtaja baadaye, nilikuwa na miaka 14 wakati nilipoanza kuhoji kuhusu dini na imani yangu. Nilihudhuria kanisa la dhehebu lingine karibu na nyumba yangu, lakini nilihisi hamu ya kutembelea makanisa mengi tofauti.

Alasiri moja, niliwaona vijana wawili wakiwa wamevalia suti nyeusi na mashati meupe wakiingia nyumbani kwa jirani yangu. Vijana hawa walionekana—maalumu.

Siku iliyofuata nilikutana na jirani yangu, Leonor Lopez, na kumuuliza juu ya wanaume hao wawili. Leonor alielezea kwamba walikuwa wamisionari wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Aliniambia kwa furaha kwamba familia yake ilibatizwa Kanisani mwaka mmoja uliopita. Akiwa ameona nia yangu, Leonor alinialika kukutana na wamisionari na kujifunza juu ya Kanisa.

Siku mbili baadaye, nilijiunga na familia ya Lopez kukutana na wamisionari. Walijitambulisha kama Mzee John Messerly kutoka Ogden, Utah, na Mzee Christopher Osorio kutoka Walnut Creek, California. Kamwe sitawasahau.

Picha
Wamisionari wakifundisha kwenye chakula cha jioni

Kwa kuwa nilikuwa na miaka 14 tu, Mzee Messerly alisisitiza twende mlango uliofuatia ambapo ni nyumbani ili mama yangu afahamu kile walichokuwa wakinifundisha. Pale, alielezea kwa ukarimu kwamba walikuja kushiriki ujumbe kuhusu Yesu Kristo na kumwomba mama ruhusa ya kunifundisha. Mama alikubali na hata alijiunga nasi wakati wakinifundisha.

Wamisionari kwanza walimwomba Leonor kutoa sala. Hili lilinigusa sana kwa sababu sala yake haikuwa marudio ya maneno ya kukariri lakini ilikuwa kutoka moyoni mwake. Nilihisi alikuwa hasa akiongea na Baba yake wa Mbinguni.

Wamisionari kisha walitufundisha kuhusu Yesu Kristo. Walionyesha picha Yake iliyonivutia kwa sababu ilikuwa picha ya Kristo aliyefufuka, aliye hai.

Picha
Mwokozi Yesu Kristo

Waliendelea, wakitufundisha jinsi Yesu alivyoanzisha Kanisa Lake katika nyakati za zamani, Yeye akiwa mkuu akifuatiwa na Mitume kumi na wawili. Walitufundisha juu ya Ukengeufu—jinsi ukweli na mamlaka ya Kristo yalivyochukuliwa kutoka duniani baada ya Mitume Wake kufa.

Walituambia kuhusu kijana mdogo wa miaka 14 aliyeitwa Joseph Smith ambaye, mwanzoni mwa miaka ya 1800, alitembelea makanisa tofauti tofauti akitafuta ukweli. Kadiri muda ulivyosonga, Joseph alikanganyikiwa zaidi. Baada ya kusoma katika Biblia kwamba tunaweza “kumwomba Mungu”1 kwa ajili ya hekima, Joseph, akifanya kwa imani, alikwenda kwenye msitu wa miti kuomba na kuuliza ni kanisa gani ambalo anapaswa kujiunga nalo.

Mmoja wa wamisionari alisoma maelezo ya Joseph juu ya kile kilichotokea wakati akiomba:

“Niliona nguzo ya mwanga juu ya kichwa changu, ambao ulikuwa ni mng’aro uliozidi mwangaza wa jua, ambao ulishuka taratibu hadi ukatua juu yangu.

“… Mwanga ulipotua juu yangu nikawaona Viumbe wawili, ambao mng’aro na utukufu wao wapita maelezo yote, wakiwa wamesimama juu yangu angani. Mmoja wao akaniambia, akiniita mimi kwa jina na kusema, huku akimwonyesha yule mwingine—Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!2

Wakati wa somo hilo, Roho alinithibitishia kweli kadhaa.

Kwanza, Mungu husikiliza sala zote za dhati za watoto Wake, na mbingu iko wazi kwa wote—sio kwa wachache tu.

Pili, Mungu Baba, Yesu Kristo, na Roho Mtakatifu ni viumbe watatu tofauti, walioungana katika kusudi lao la “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.”3

Tatu, tumeumbwa kwa mfano wa Mungu. Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye, Yesu Kristo, wana miili ya nyama na mifupa kama sisi, lakini yao imejaa utukufu na ni mikamilifu, na Roho Mtakatifu ana mwili wa kiroho.4

Nne, kupitia Joseph Smith, Yesu Kristo alirejesha injili Yake na Kanisa la kweli duniani. Mamlaka ya ukuhani yaliyotunukiwa kwa Mitume wa Kristo miaka 2,000 iliyopita ni ukuhani ule ule uliotunukiwa kwa Joseph Smith na Oliver Cowdery na Petro, Yakobo na Yohana.5

Mwishowe, tulijifunza kuhusu ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo: Kitabu cha Mormoni. Kikiwa kimeandikwa na manabii wa kale, kinasimulia juu ya watu walioishi Amerika kabla, wakati na baada ya kuzaliwa kwa Yesu. Kutoka kwenye kitabu hicho tunajifunza jinsi walivyomjua, kumpenda, na kumwabudu Kristo, aliyeonekana kwao kama Mwokozi aliyefufuka.

Niliguswa sana na Roho wakati nilipojifunza juu ya tangazo la Mwokozi kwao: “Tazama, mimi ni Yesu Kristo, ambaye manabii walishuhudia kwamba atakuja ulimwenguni.”6

Wamisionari walitupatia nakala yetu ya Kitabu cha Mormoni. Tulikisoma na kukubali mwaliko unaopatikana mwishoni mwa Kitabu cha Mormoni, unaosomeka:

“Na mtakapopokea vitu hivi, ningewashauri kwamba mngemwuliza Mungu, Baba wa Milele, katika jina la Kristo, ikiwa vitu hivi si vya kweli; na ikiwa mtauliza na moyo wa kweli, na kusudi halisi, mkiwa na imani katika Kristo, atawaonyesha ukweli wake kwenu, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

“Na kwa uwezo wa Roho Mtakatifu mtajua ukweli wa vitu vyote.”7

Imekuwa karibu miaka 45 tangu mimi na mama yangu tulipojua furaha na nguvu ya kuwa na imani katika Kristo. Ilikuwa ni kwa sababu ya imani yao kwa Kristo kwamba familia ya Lopez walishiriki pamoja nami imani yao mpya. Ilikuwa ni kwa sababu ya imani yao kwa Kristo kwamba wamisionari hawa wawili waliacha nyumba zao huko Marekani kunitafuta mimi na mama yangu. Ilikuwa ni imani ya marafiki hawa wote ambayo ilipanda mbegu ya haradali ya imani ndani yetu ambayo tangu hapo imekua kufikia mti mkubwa wa baraka za milele.

Katika miaka hii ya heri, tumejua, kama Rais Russell M. Nelson alivyotangaza: “Kila kitu kizuri maishani—kila baraka inayowezekana ya umuhimu wa milele—huanza na imani. Kuruhusu Mungu ashinde katika maisha yetu huanza na imani kwamba Yeye yuko tayari kutuongoza. Toba ya kweli huanza na imani kwamba Yesu Kristo ana uwezo wa kutusafisha, kutuponya na kutuimarisha.”8

Ninawaalikeni sote tuongeze imani yetu kwa Kristo daima, ambaye amebadilisha maisha yangu na ya mama yangu mpendwa na anayeendelea kuyabadili maisha ya wale wote wanaomtafuta Yeye. Ninajua kwamba Joseph Smith ni Nabii wa Urejesho, kwamba Rais Nelson ndiye nabii wetu leo, kwamba Yesu ndiye Kristo aliye hai na Mkombozi wetu, na kwamba Baba wa Mbinguni yu hai na anajibu maombi yote ya watoto Wake. Ninashuhudia juu ya kweli hizi katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.