Mkutano Mkuu
Kuimarisha Uongofu Wetu kwa Yesu Kristo
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


Kuimarisha Uongofu Wetu kwa Yesu Kristo

Maandiko na ufahamu wetu juu ya Mungu ni zawadi—zawadi ambazo mara nyingi tunachukulia kawaida. Acha tuthamini baraka hizi.

Asante sana, Mzee Nielson, kwa ujumbe wako mzuri. Tulihitaji kusikia hilo.

Kaka na dada zangu wapendwa, Rais Russell M. Nelson ametufundisha hivi karibuni: “Kufanya jambo lolote vizuri kunahitaji jitihada. Kuwa mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo nako kunahitaji jitihada. Kuongeza imani yako na kumwamini Yeye kunahitaji jitihada.” Miongoni mwa mapendekezo ambayo alitupatia ili kuongeza imani yetu kwa Yesu Kristo ni kwamba tuwe wanafunzi wanaojishughulisha, kwamba tujishughulishe na maandiko ili kuelewa vyema utume na huduma ya Kristo. (Ona “Kristo Amefufuka; Imani Kwake Itahamisha Milima,” Liahona, Mei 2021, 103.)

Tunajifunza katika Kitabu cha Mormoni kwamba maandiko yalikuwa sehemu muhimu ya familia ya Lehi—muhimu sana kiasi kwamba Nefi na kaka zake walirejea Yerusalemu kuchukua mabamba ya shaba (ona 1 Nefi 3–4).

Maandiko yanaweka wazi mapenzi ya Mungu kwetu, kama vile Liahona ilivyofanya kwa Nefi na baba yake. Baada ya kuvunja upinde wake, Nefi alihitaji kujua ni wapi anapaswa kwenda kupata chakula. Baba yake, Lehi, aliangalia Liahona na kuona vitu vilivyoandikwa. Nefi aliona kwamba mishale kwenye Liahona ilifanya kazi kulingana na imani, bidii na umakini iliyopewa. Aliona pia maandishi ambayo yalikuwa rahisi kusoma na ambayo yaliwapa ufahamu kuhusu njia za Bwana. Aligundua kuwa Bwana huleta vitu vikubwa kupitia njia ndogo. Alikuwa mtiifu bila kujali maagizo yaliyotolewa kwenye Liahona. Alikwenda juu ya mlima na akapata chakula kwa ajili ya familia yake, ambayo ilikuwa imeteseka sana kutokana na kukosa chakula. (Ona 1 Nefi 16:23–31.)

Inaonekana kwangu kwamba Nefi alikuwa mwanafunzi aliyejikita kwenye maandiko. Tunasoma kwamba Nefi alifurahishwa na maandiko, akiyatafakari moyoni mwake, na kuyaandika kwa ajili ya mafunzo na faida ya watoto wake (ona 2 Nephi 4:15–16).

Rais Russell M. Nelson alisema:

“Kama ‘tutasonga mbele, tukisherehekea neno la Kristo, na tuvumilie hadi mwisho, … [sisi] tutapokea uzima wa milele’ [2 Nefi 31:20].

“Kusherehekea inamaanisha zaidi ya kuonja. Kusherehekea inamaanisha kufurahia. Tunafurahia maandiko kwa kujifunza katika roho ya ugunduzi yenye furaha na utii aminifu. Wakati sisi tunaposherehekea maneno ya Kristo, yanaingia ‘katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama.’ [2 Wakorintho 3:3]. Yanakuwa sehemu muhimu ya asili yetu” (“Living by Scriptural Guidance,” Liahona, Jan. 2001, 21).

Je, Ni Baadhi ya Mambo Gani Ambayo Tungefanya Kama Nafsi Zetu Zinafurahia katika Maandiko?

Hamu yetu ya kuwa sehemu ya kusanyiko la Israeli katika pande zote mbili za pazia itaongezeka. Itakuwa kawaida na ya asili kwetu kualika familia na marafiki zetu kuwasikiliza wamisionari. Tutastahili, na tutakuwa na kibali hai cha hekalu ili kwenda hekaluni mara nyingi iwezekanavyo. Tutafanya kazi kupata, kuandaa na kuwasilisha majina ya babu zetu hekaluni. Tutakuwa waaminifu katika kutunza siku ya Sabato, kuhudhuria kanisani kila Jumapili ili kufanya upya maagano yetu na Bwana kadiri tunavyoshiriki kwa kustahili katika kuchukua sakramenti. Tutadhamiria kubaki kwenye njia ya agano, tukiishi kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. (ona Mafundisho na Maagano 84:44).

Inamaanisha Nini Kwako Kufurahia katika Mambo ya Bwana?

Kufurahia katika maandiko ni zaidi ya njaa na kiu ya maarifa. Nefi alipata furaha kubwa wakati wa maisha yake. Walakini, alikabiliwa pia na shida na huzuni (ona 2 Nephi 4:12–13). “Lakini,” alisema, “ninajua ninayemwamini” (2 Nephi 4:19). Tunapojifunza maandiko, tutaelewa vizuri mpango wa Mungu wa wokovu na kuinuliwa, na kutumaini ahadi ambazo Amezitoa kwetu katika maandiko, pamoja na ahadi na baraka za manabii wa sasa.

Picha
Daudi na Goliathi

Alasiri moja, mimi na mke wangu tulialikwa nyumbani kwa rafiki. Mtoto wao wa miaka saba, David, alikuwa hajawahi kusikia hadithi ya Biblia ya Daudi na Goliathi, na alitaka kuisikia. Nilipoanza kusimulia hadithi hiyo, aliguswa na jinsi Daudi, kwa imani yake na kwa jina la Mungu wa Israeli, alimjeruhi na kumuua Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akiwa hana upanga mkononi mwake.(ona 1 Samweli 17).

Akiniangalia kwa macho yake yenye weusi mwingi, aliniuliza kwa uthabiti, “Mungu ni nani?” Nilimuelezea kwamba Mungu ni Baba yetu wa Mbinguni na kwamba tunajifunza kumhusu Yeye katika maandiko.

Kisha akaniuliza, “Je, maandiko ni nini?” Nilimwambia kwamba maandiko ni neno la Mungu na kwamba ndani yake atapata hadithi nzuri ambazo zitamsaidia kumjua Mungu vizuri. Nilimwomba mama yake atumie Biblia aliyokuwa nayo nyumbani kwake na kwamba asimruhusu David alale bila kumsomea hadithi yote. Alifurahi alipoisikiliza hadithi hiyo. Maandiko na ufahamu wetu juu ya Mungu ni zawadi—zawadi ambazo mara nyingi tunachukulia kawaida. Acha tuthamini baraka hizi.

Wakati nikitumikia misheni nikiwa kijana, niligundua kwamba kufundisha kwetu kwa kutumia maandiko, maisha ya watu wengi yalibadilishwa. Niligundua nguvu ndani yao na jinsi maandiko yanavyoweza kubadilisha maisha yetu. Kila mtu ambaye tulimfundisha injili ya urejesho alikuwa mtu wa kipekee na mwenye mahitaji tofauti. Maandiko matakatifu—ndio, unabii ulioandikwa na manabii watakatifu—viliwaleta kwenye imani katika Bwana na toba na kubadilisha mioyo yao.

Maandiko yaliwajaza shangwe walipopokea msukumo, mwelekeo, faraja, nguvu na majibu ya mahitaji yao. Wengi wao waliamua kufanya mabadiliko katika maisha yao na kuanza kushika amri za Mungu.

Nefi anatuhimiza kufurahi katika maneno ya Kristo, kwa sababu maneno ya Kristo yatatuambia mambo yote tunayohitaji kufanya (ona 2 Nephi 32:3).

Picha
Kujifunza maandiko kama familia

Ninakualika uwe na mpango wa kudumu wa kusoma maandiko. Njoo, unifuate ni nyenzo kubwa tuliyonayo ya kufundisha na kujifunza injili, kuimarisha uongofu wetu kwa Yesu Kristo na kutusaidia kuwa kama Yeye. Tunapojifunza injili, sio tu tunatafuta habari mpya; bali, tunatafuta kuwa “kiumbe kipya”(2 Wakorintho 5:17).

Roho Mtakatifu anatuongoza kuelekea ukweli na anashuhudia kwetu ukweli (see Yohana 16:13). Yeye huangaza akili zetu na hufanya upya uelewa wetu na hugusa mioyo yetu kwa kupitia ufunuo wa Mungu, ambaye ni chanzo cha ukweli wote. Roho Mtakatifu hutakasa mioyo yetu. Yeye huchochea ndani yetu tamaa ya kuishi kulingana na ukweli na hutunong’onezea njia za kufanya hivyo. “Roho Mtakatifu … atawafundisha yote” (Yohana 14:26).

Nikiongea kuhusu maneno aliyomfunulia Nabii Joseph Smith, Mwokozi wetu alisema:

“Maneno haya si ya wanadamu wala mwanadamu, bali ni yangu; …

“Kwani ni sauti yangu ambayo huyasema kwenu; kwani yanatolewa kwa Roho yangu kwenu, …

“Kwa hiyo basi, ninyi mnaweza kushuhudia kwamba mmesikia sauti yangu na mnayajua maneno yangu” (Mafundisho na Maagano 18:34–36).

Tunapaswa kutafuta ushirika wa Roho Mtakatifu. Lengo hili linapaswa kutawala maamuzi yetu na kuongoza mawazo na matendo yetu. Lazima tutafute kila kitu kinachoalika ushawishi wa Roho na kukataa chochote ambacho ni kinyume na ushawishi huu.

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana mpendwa wa Baba wa Mbinguni. Ninampenda Mwokozi wangu. Ninashukuru kwa maandiko Yake na kwa manabii Wake walio hai. Rais Nelson ni nabii Wake. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.