Mkutano Mkuu
Yenye Kupendeza kwa Urahisi—Yenye Urahisi wa Kupendeza
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


Yenye Kupendeza kwa Urahisi—Yenye Urahisi wa Kupendeza

Na tuifanye injili iwe rahisi tunapojichukulia juu yetu majukumu yetu matakatifu yaliyoainishwa.

Utangulizi

Ninatoa makaribisho ya upendo kwa kila mmoja wenu anayeshiriki katika mkutano huu.

Leo, ninatumaini kelezea vipengele viwili vya injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo, vikifuatiwa na matukio manne ya kusisimua kutoka kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho ulimwenguni kote yakionesha matumizi ya kanuni hizi. Kipengele cha kwanza cha injili iliyorejeshwa—kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa—inafokasi juu ya majukumu matakatifu yaliyoainishwa. Kipengele cha pili kinatukumbusha kwamba injili iko wazi, ina thamani na ni rahisi.

Majukumu Matakatifu Yaliyoainishwa

Ili kupokea uzima wa milele, ni lazima sisi “tuje kwa Kristo, na kukamilishwa ndani Yake.”1 Tunapokuja kwa Kristo na kuwasaidia wengine kufanya vivyo hivyo, tunashiriki katika kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa, ambayo inafokasi juu ya majukumu matakatifu yaliyoainishwa.2 Majukumu haya matakatifu yanafungamana na funguo za ukuhani zilizorejeshwa na Musa, Elia na Eliya, kama ilivyoandikwa katika sehemu ya 110 ya Mafundisho na Maagano,3 na amri kuu ya pili iliyotolewa kwetu na Yesu Kristo ya kuwapenda jirani zetu kama tunavyojipenda wenyewe.4 Yanapatikana katika kurasa mbili za mwanzo za Kitabu cha Mwongozo, kilichofanyiwa maboresho kinachopatikana kwa waumini wote.

Ikiwa kusikia maneno “Kitabu cha Mwongozo” au “majukumu matakatifu yaliyoainishwa” kunakufanya utetemeke kwa hofu ya ugumu, tafadhali isiwe hivyo. Majukumu haya ni rahisi, yenye uvuvio, yenye kuleta ari na yanawezekana kufanyika. Ni haya hapa:

  1. Kuishi Injili ya Yesu Kristo

  2. Kuwajali wale wenye uhitaji

  3. Kuwaalika watu wote waipokee injili

  4. Kuziunganisha familia milele

Unaweza kuyatazama jinsi mimi ninavyoyatazama: kama ramani ya njia ya kurudi kwa Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo.

Picha
Vipengele vya Kazi ya Wokovu na kuinuliwa

Injili Iko Wazi, Ina Thamani na ni Rahisi

Imesemwa kwamba injili ya Yesu Kristo “inapendeza kwa Urahisi na ina urahisi wa kupendeza.”5 Ulimwengu hauko hivyo. Una changamoto, usioeleweka na umejawa dhoruba na migogoro. Tunabarikiwa pale tunapokuwa makini kutoruhusu ugumu, ambao ni wa kawaida ulimwenguni, kuingilia njia ambayo kwayo tunapokea na kufanyia kazi injili.

Rais Dallin H. Oaks alifafanua: “Tunafundishwa vitu vingi vidogo na rahisi katika injili ya Yesu Kristo. Tunahitaji kukumbushwa kwamba kwa ujumla na katika kipindi fulani cha wakati muhimu, vitu hivyo vinavyoonekana vidogo hutenda vitu vikubwa.”6 Yesu Kristo mwenyewe alifafanua kwamba nira Yake ni laini, na mzigo wake ni mwepesi.7 Sote tunapaswa kujitahidi kuifanya injili iwe rahisi—katika maisha yetu, katika familia zetu, katika madarasa na akidi zetu na katika kata na vigingi vyetu.

Mnaposikiliza hadithi zifuatazo nitakazoshiriki nanyi, tambueni kwamba zimechaguliwa kwa umakini ili kutoa msukumo kwa upande mmoja na kutoa ushauri kwa upande mwingine. Matendo ya kila mmoja wa hawa Watakatifu wa Siku za Mwisho ni mfano kwa kila mmoja wetu, katika kutumia injili kwa njia ya wazi, yenye thamani na rahisi wakati tukitimiza moja ya majukumu matakatifu yaliyoainishwa ambayo yametambulishwa punde tu.

Kuishi Injili ya Yesu Kristo

Kwanza, kuishi Injili ya Yesu Kristo. Jens wa Denmark anasali kila siku ili kuishi injili na anatambua misukumo kutoka kwa Roho Mtakatifu. Amejifunza kutenda kwa haraka wakati anapohisi kuongozwa na Roho.

Picha
Jens wa Denmaki

Jens alishiriki yafuatayo:

“Tunaishi kwenye nyumba nzuri ndogo ya mbao yenye paa la majani makavu, katikati ya kijiji kidogo chenye usalama, karibu na bwawa la kijiji.

Picha
Kijiji cha kupendeza
Picha
Bwawa la kijiji

“Kwenye usiku huu wenye hali ya hewa ya joto la kufikirika la Kidenmaki, milango na madirisha vilikuwa wazi na kila kitu kilileta hisia ya amani na utulivu. Kutokana na usiku wetu mrefu wenye ung’aavu wa utukufu na joto, sikuwa na haraka ya kubadili balbu iliyoungua katika chumba chetu cha stoo.

Picha
Mwanga wa chumba cha stoo

“Ghafla nilipata hisia kali kwamba nilipaswa kuibadilisha haraka! Wakati huo huo, nilimsikia mke wangu, Mariann, akituita mimi na watoto tunawe mikono kwa sababu mlo wa usiku ulikuwa tayari!

“Nilikuwa kwenye ndoa kwa muda wa kutosha kujua kwamba huu haukuwa wakati wa kuanza kufanya kitu kingine chochote zaidi ya kunawa mikono, lakini nilijisikia nikimwambia Mariann kwamba ningekimbia mara moja dukani kununua balbu mpya. Nilihisi msukumo mkubwa wa kuondoka mara moja.

“Duka lilikuwa upande wa pili tu wa bwawa. Mara zote tulitembea, lakini leo nilichukua baiskeli yangu. Wakati nikiendesha kuvuka bwawa, pembeni kidogo ya macho yangu, nilimwona mtoto mdogo, takribani miaka miwili, akitembea peke yake, karibu na ukingo wa bwawa, karibu kabisa na maji—ghafla alitumbukia! Dakika moja alikuwepo pale—na dakika iliyofuata hakuwepo!

“Hakuna yeyote aliyeona hili likitokea isipokuwa mimi. Nilidondosha baiskeli yangu ardhini, nikakimbia na kuruka ndani ya bwawa kina cha kiunoni. Upande wa juu wa maji ghafla ulifunikwa na magugu maji, ukifanya isiwezekane kuona ndani ya maji. Kisha nilihisi mjongeo kwenye upande mmoja. Niliweka mkono wangu ndani ya maji, nikaishika fulana na kumvuta nje mtoto. Alianza kutweta, kukohoa na kulia. Punde baadaye mtoto alikuwa pamoja na wazazi wake tena.”

Picha
Jens pamoja na familia

Wakati Kaka Jens anaposali kila asubuhi kwa ajili ya msaada wa kutambua msukumo kutoka kwa Roho Mtakatifu, hata kitu ambacho si cha kawaida kama kubadili balbu haraka, yeye pia husali kwamba aweze kutumiwa kama chombo cha kuwabariki watoto wa Mungu. Jens anaishi injili kwa kutafuta mwongozo mtakatifu kila siku, kujitahidi kuwa mwenye kustahili, kisha kufanya kadiri ya uwezo wake kufuata mwongozo huo wakati unapokuja.

Kuwajali Wale Wenye Uhitaji

Hapa ni mfano wa kuwajali wale wenye uhitaji. Siku moja kiongozi wa kata katika Kigingi cha Cúcuta huko Colombia alikwenda pamoja na rais wa Wasichana wa kigingi kuwatembelea wasichana wawili—pamoja na kaka yao mkubwa—ambao walikuwa wakipitia changamoto za kuhofisha. Hivi karibuni baba yao alikuwa amefariki na mama yao alifariki mwaka mmoja kabla. Ndugu watatu walikuwa sasa wameachwa peke yao katika kibanda chao kidogo na duni. Kuta zilikuwa zimejengwa kwa mbao ghafi zilizofunikwa na mifuko ya plastiki na mabati ya madebe yaliyojikunja yakifunika mahali ambapo walilala tu.

Kufuatia matembezi yao, viongozi hawa walijua vijana walihitaji msaada. Kupitia baraza la kata, mpango wa kuwasaidia ulianza kuibuka. Viongozi wa kata na kigingi—Muungano wa Usaidizi, akidi ya wazee, Wavulana, Wasichana—na familia nyingi wote walijiingiza kwenye jukumu la kubariki familia hii.

Picha
Nyumba ikijengwa
Picha
Nyumba ikijengwa

Taasisi za kata ziliwasiliana na waumini kadhaa wa kata ambao wanafanya kazi ya ujenzi. Baadhi walisaidia kwa usanifu, wengine walijitolea muda na nguvu kazi, wengine walipika chakula na bado wengine walijitolea vifaa vilivyohitajika.

Picha
Nyumba iliyokamilika

Wakati nyumba ndogo ilipokamilika, ilikuwa siku ya furaha kwa wale waliosaidia na kwa waumini watatu vijana wa kata. Watoto hawa yatima walihisi faraja na hakikisho la muunganiko wa familia yao ya kata kujua kwamba hawako peke yao na kwamba Mungu daima yupo kwa ajili yao. Wale waliojitolea walihisi upendo wa Mwokozi kwa familia hii na walitenda kama mikono Yake katika kuwahudumia.

Kuwaalika Wote Kuipokea Injili

Nadhani mtafurahia mfano huu wa kuwaalika wote kuipokea injili. Cleiton mwenye miaka kumi na saba wa Cape Verde hakujua nini kingetokea kama matokeo ya kwenda kwenye darasa lake la kata la seminari siku moja. Lakini maisha yake na maisha ya wengine yangebadilishwa milele kwa sababu alifanya hivyo.

Cleiton, sambamba na mama yake na kaka yake mkubwa, walibatizwa Kanisani wakati fulani kipindi cha nyuma, na bado familia iliacha kuhudhuria. Tendo lake moja la kuhudhuria seminari lingethibitisha kuwa tegemeo lenye ushawishi kwa familia.

Vijana wengine kwenye darasa la seminari walikuwa wakarimu na wenye upendo. Walimfanya Cleiton ahisi nyumbani na walimhimiza ahudhurie shughuli nyingine. Alifanya hivyo, na punde alianza kuhudhuria mikutano yake mingine ya Kanisa. Askofu mwenye hekima aliona uwezekano wa kiroho ndani ya Cleiton na kumwalika kuwa msaidizi wake. “Kutoka wakati ule na kuendelea,” anasema Askofu Cruz, “Cleiton alikuwa mfano na ushawishi kwa vijana wengine.”

Mtu wa kwanza ambaye Cleiton alimwalika kurudi kanisani alikuwa mama yake, kisha kaka yake mkubwa. Kisha alitanua wigo wake kwa marafiki. Mmoja wa marafiki hao alikuwa mvulana wa rika lake, Wilson. Kwenye mkutano wake wa kwanza na wamisionari, Wilson alielezea hamu yake ya kubatizwa. Wamisionari walivutiwa na kushangazwa kwa mengi ambayo Cleiton tayari alikuwa ameshiriki na Wilson.

Picha
Wavulana huko Cape Verde
Picha
Kuwaalika wengine waje kanisani
Picha
Kundi linalokua la vijana wanaoshiriki kikamilifu

Juhudi za Cleiton hazikuishia hapo. Aliwasaidia waumini wengine wasioshiriki kikamilifu kurejea, kama nyongeza kwenye kushiriki injili na marafiki wa imani zingine. Leo kata ina vijana 35 wanaoshiriki kikamilifu, pamoja na programu hai ya seminari, shukrani kwa sehemu kubwa kwa juhudi za Cleiton za kupenda, kushiriki na kualika. Cleiton na kaka yake mkubwa, Cléber, wote wanajiandaa kuhudumu misheni.

Kuziunganisha Familia Milele

Mwisho, acha nishiriki mfano wa kupendeza wa kuziunganisha familia milele. Lydia kutoka Kharkiv, Ukrain, kwa mara ya kwanza alijifunza kuhusu hekalu kutoka kwa wamisionari. Haraka, Lydia alihisi hamu ya dhati ya kuhudhuria hekaluni na baada ya ubatizo wake, alianza maandalizi ya kupokea kibali cha hekaluni.

Lydia alihudhuria Hekalu la Freiberg Ujerumani ili kupokea endaumenti yake na kisha kutumia siku kadhaa kufanya kazi kwa niaba ya wafu huko. Kufuatia kuwekwa wakfu kwa Hekalu la Kyiv Ukrain, Lydia alihudhuria hekaluni mara kwa mara. Yeye pamoja na mume wake, Anatoly, waliunganishwa milele huko na baadaye waliitwa kuhudumu kama wamisionari wa hekaluni. Kwa pamoja wamepata majina zaidi ya 15,000 ya mababu na wamefanya kazi kutoa ibada za hekaluni kwa ajili yao.

Picha
Wanandoa wa Ukrain wakiwa hekaluni

Anapoulizwa kuhusu hisia zake juu ya kazi ya hekalu, Lydia husema, “Ni kitu gani nimepokea hekaluni? Nimefanya maagano mapya na Mungu. Ushuhuda wangu umeimarika. Nimejifunza kupokea ufunuo binafsi. Ninaweza kufanya ibada okozi kwa ajili ya mababu zangu waliofariki. Na ninaweza kuwapenda na kuwatumikia watu wengine.” Alihitimisha na kauli hii ya kweli: “Bwana anataka kutuona hekaluni mara nyingi.”

Hitimisho

Ninavutiwa na wema wa hawa Watakatifu wa Siku za Mwisho, kila mmoja akiwa na historia anuwai na tofauti iliyojikita katika hadithi hizi nne. Mengi yanaweza kuwa funzo kutokana na matokeo ya kimuujiza yaliyoletwa kupitia matumizi rahisi ya kanuni rahisi za injili. Yote waliyofanya yako ndani ya uwezo wetu vilevile.

Na tuifanye injili iwe rahisi wakati tunapojichukulia juu yetu majukumu matakatifu yaliyoainishwa: Ya kuishi Injili ya Yesu Kristo ili tuwe wepesi wa kuhisi misukumo, kama ilivyokuwa kwa Jens huko Denmaki. Ili kuwajali wale wenye uhitaji, kama ilivyooneshwa na waumini wa Kigingi cha Cúcuta huko Colombia katika kutengeneza nyumba kwa waumini yatima wa kata. Ili kuwaalika wote kuipokea injili, katika njia ambayo Cleiton kutoka nchi ya kisiwa cha Afrika cha Cape Verde aliitumia kwa marafiki na familia yake. Hatimaye, kuziunganisha familia milele, kama ilivyooneshwa na Dada Lydia kutoka Ukrain kupitia ibada zake mwenyewe za hekaluni, juhudi za historia ya familia na huduma hekaluni.

Kufanya hivyo hakika kutaleta furaha na amani. Juu ya hili ninaahidi na kushuhudia—na juu ya Yesu Kristo kama Mwokozi na Mkombozi wetu—katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Moroni 10:32.

  2. Ona General Handbook: Serving in The Church of Jesus Christ of Latter-day Saints, 1.2, ChurchofJesusChrist.org.)

  3. Ona Mafundisho na Maagano 110:11–16. Ona pia Dallin H. Oaks, “Ukuhani wa Melkizedeki na Funguo,” Liahona, Mei 2020, 70: “Kufuatia uwekaji wakfu wa hekalu la kwanza la kipindi hiki cha maongozi ya Mungu huko Kirtland, Ohio, manabii watatu—Musa, Elia, na Eliya—walirejesha ‘funguo za kipindi hiki,’ zikiwemo funguo zihusianazo na kukusanya Israeli na kazi ya mahekalu ya Bwana.” Ona pia Quentin L. Cook, “Kujitayarisha Kukutana na Mungu,” Liahona, Mei 2018, 114: “Manabii wa kale walirejesha funguo za ukuhani kwa ajili ya ibada okozi za milele za injili ya Yesu Kristo. … Funguo hizi hutoa ‘nguvu kutoka juu’ [Mafundisho na Maagano 38] kwa ajili ya majukumu ya kiungu yaliyoteuliwa ambayo hujumuisha dhumuni kuu la Kanisa.”

  4. Ona Mathayo 22:36–40.

  5. Katika Matthew Cowley Speaks: Discourses of Elder Matthew Cowley of the Quorum of the Twelve of The Church of Jesus Christ of Latter-day Saints (1954), xii.

  6. Dallin H. Oaks, “Vitu Vidogo na Rahisi, Liahona, Mei 2018, 89.

  7. Ona Mathayo 11:30.