Kwenye Hoja
Je, utimilifu wa injili ni nini?
Kristo katika Gethsemane, na Dan Burr
Bwana amesema kwamba utimilifu wa injili ni “agano lisilo na mwisho, ambalo Yeye “amelipeleka kwa watoto wa watu” (Mafundisho na Maagano 66:2). Unajumuisha kila kitu kinachohitajika kwa watoto wa Mungu ili kuingia katika uhusiano wa agano na Yeye na kupokea wokovu na kuinuliwa.
Injili ni “habari njema” kumhusu Yesu Kristo. Ni mpango wa “Mungu wa wokovu, uliowezeshwa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo. Injili inajumuisha kweli za milele au sheria, maagano, na ibada zinazohitajika kwa wanadamu kurudi kwenye uwepo wa Mungu” (Mwongozo wa maandiko, “Injili”). Mengi ya mambo haya yalikuwa yamepotea. Lakini sasa, kupitia ufunuo kwa manabii, kuanzia kwa Joseph Smith, Bwana anarejesha utimilifu wa injili Yake.
Pamoja na Urejesho wa utimilifu wa injili Yake, Yesu Kristo “anatualika sote kuja Kwake na kwenye Kanisa Lake, ili kupokea Roho Mtakatifu, ibada za wokovu, na kupata shangwe ya kudumu” (“Urejesho wa Utimilifu wa Injili ya Yesu Kristo: Tangazo kwa Ulimwengu la Maadhimisho ya Miaka Mia Mbili,” Maktaba ya Injili).