2025
Kuleta Ulewa wa Maana ya Matukio ya Ono la Kwanza la Joseph Smith
Januari 2024


Njoo, Unifuate

Joseph Smith—Historia ya 1:1-20

Kuleta Uelewa wa Maana ya Matukio ya Ono la Kwanza la Joseph Smith

Ni nini tofauti katika maelezo manne ya Ono la Kwanza la Joseph Smith? Kwa nini yako tofauti? Na yanaweza kutufundisha nini?

Joseph Smith

Je, umewahi kujaribu kumwambia mtu kuhusu uzoefu wa kiroho? Ni maelezo gani uliyajumuisha? Ni maelezo gani uliyaacha? Unafikiri ungesimulia hadithi kwa njia tofauti kama ungekuwa unamwambia rafiki, katika mkutano wa sakramenti, au kwa mtu ambaye si muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho?

Maswali haya ni muhimu wakati wa kufikiria kuhusu jinsi Joseph Smith alivyoelezea ono alilokuwa nalo la Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo huko New York mnamo 1820. Joseph alishiriki uzoefu huu mara kadhaa. Leo tuna maelezo manne ya moja kwa moja ya Joseph:

  1. Historia binafsi Joseph aliiandika majira ya kiangazi ya mwaka 1832. Joseph alielezea kwamba alikwenda msituni ili kusali kwa sababu alikuwa amekanganyikiwa kuhusu mambo ya kiroho. Pia alitaka dhambi zake zisamehewe.

    kijana Joseph Smith
  2. Shajara ya Joseph ya mwaka 1835. Mhubiri aliyeitwa Robert Matthews alikuja Kirtland, Ohio. Alitaka kuzungumza na Joseph kuhusu mambo ya kidini, hivyo Joseph alimwambia kuhusu ono lake. Warren Parrish, ambaye alikuwa akitunza shajara ya Joseph, aliandika kile Joseph alichosema.

    Joseph Smith ameshikilia maandiko
  3. Historia rasmi ya Kanisa ambayo Joseph aliianza mwaka 1838. Alizungumza kuhusu Ono la Kwanza kama sehemu ya jinsi Kanisa lilivyorejeshwa. Maelezo haya yamechapishwa katika Lulu ya Thamani Kuu.

    Maandishi ya Joseph Smith
  4. Barua aliyoandika Joseph mwaka 1842. Mwandishi wa habari aliyeitwa John Wentworth alimwomba Joseph kuelezea jinsi Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho lilivyokuja. Joseph alijibu katika barua na kujumuisha taarifa kuhusu Ono la Kwanza.

    mikono ikiandika

Kila maelezo yalitolewa kwa wakati tofauti kwa ajili ya wasikilizaji tofauti. Joseph alikuwa na malengo tofauti akilini kwa kila mmoja. Lakini tunapoyasoma pamoja, tunapata picha pana zaidi na ya wazi zaidi juu ya tukio la Joseph katika Kijisitu Kitakatifu.

Je, ni kipi kilicho tofauti?

Maelezo haya yote yana maelezo ya kina yaliyo tofauti. Katika maelezo ya mwaka 1832, Joseph analenga hamu yake ya kusamehewa dhambi zake. Yeye hajataja mahususi kutaka kujua ni kanisa lipi lililo la kweli. Anazungumza kuhusu jinsi “Bwana” alivyomtokea—hamwelezei Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo kiutofauti.

Maelezo ya mwaka 1835 na 1838 yanataja nguvu ovu inayojaribu kumzuia Joseph asisali. Maelezo ya Joseph ya mwaka 1835 yanasema alitembelewa na viumbe wawili, vile vile na malaika. Maelezo ya mwaka 1838 na 1842 pia yanataja viumbe wawili, ambapo mmoja hasa hutambuliwa kama Yesu Kristo. Maelezo haya mawili yanasisitiza utafutaji wa Joseph wa kanisa la kweli.

Kwa nini Kuna Tofauti?

Kuna sababu chache za tofauti katika maelezo.

Asili ya Kumbukumbu

Wakati mwingine tunafikiri kumbukumbu zetu daima hubaki zile zile. Lakini hivyo sio jinsi kumbukumbu inavyofanya kazi. Tunakumbuka mambo tofauti tunapozidi kuzeeka. Kitu ambacho kilitokea mapema kinaweza kuchukua maana tofauti kwa sababu ya uzoefu wa ziada wa maisha. Kumbukumbu kuu inabakia, lakini baadhi ya maelezo yanaweza kubadilika. Hiyo haimaanishi kumbukumbu yetu siyo ya kweli au sahihi, ni sehemu tu ambazo zinajitokeza zaidi kwa nyakati tofauti.

Madhumuni Tofauti

Joseph alikuwa na sababu mbalimbali za kusimulia masimulizi yake. Mnamo 1832, alikuwa akielezea maelezo binafsi, hivyo alifokasi zaidi juu ya kile Ono la Kwanza lilichomaanisha kwake binafsi. Mnamo 1838 na 1842, alizungumza kuhusu Ono la Kwanza kama sehemu ya jinsi Kanisa lilivyokuja. Kwa hivyo alisisitiza hamu yake ya kujua ni kanisa gani lilikuwa la kweli.

Wasikilizaji Tofauti

Robert Matthews na John Wentworth hawakuwa waumini wa Kanisa. Joseph alihitaji kuelezea mambo kwa njia tofauti kwao. Alielekeza maelezo ya mwaka 1838 kuelekea zaidi kwa waumini wa Kanisa. Huenda alifikiria maelezo yake ya mwaka 1832 yangesomwa tu na marafiki wa karibu na wanafamilia.

Kipi Kimebakia Kilekile?

Katika maelezo yote manne, maelezo muhimu ni yale yale. Joseph alikanganywa kuhusu wokovu wake mwenyewe na wokovu wa ulimwengu. Alisoma katika Yakobu 1:5–6 kwamba angeweza kupata majibu ya sala zake. Alienda katika msitu na kusali. Viumbe wa Mbinguni walimtokea. Walimwita kwa jina lake. Walisema kwamba makanisa kwa wakati huo hayakuwa yanafundisha mafundisho sahihi.

Ono la Kwanza

Maelezo haya Yananifundisha Nini

Ninapenda kusoma maelezo haya tofauti kwa sababu yananisaidia kuelewa Ono la Kwanza vizuri zaidi. Ninaweza kuona kwa uwazi zaidi kwa nini Joseph alikuwa amekanganywa na alitaka kusali. Ninaweza kumhisi Roho kwa nguvu zaidi ninaposoma kuhusu kile Ono la Kwanza lilichomaanisha kwa Joseph katika nyakati tofauti katika maisha yake. Kwa pamoja, matukio yananisaidia kujua kwamba Joseph alikuwa anasema ukweli. Alimwona Mungu Baba na Yesu Kristo katika Kijisitu Kitakatifu. Hii huongeza matumaini yangu kwamba ninaweza pia kupata majibu ya sala.

Maelezo

Kwa nini Joseph alisema alisali

Ni nani Joseph alisema alitokea

1832

Kwa ajili ya msamaha wa dhambi zake

Bwana

1835

Kujua nani alikuwa sahihi na nani si sahihi katika masuala ya dini

Viumbe wawlili—wa kwanza, akifuatiwa na mwingine—na malaika

1838

Ili kujua ni kanisa lipi lilikuwa Kanisa la kweli la Kristo

Baba na Mwanawe Yesu Kristo

1842

Ili kujua ni kanisa lipi lilikuwa Kanisa la kweli la Kristo

“Viumbe wawili watukufu”