Misaada ya Kujifunza
TJS, Yohana 1


TJS, Yohana 1:1–34. Linganisha na Yohana 1:1–34

Injili ya Yesu Kristo imekuwa ikihubiriwa kutoka mwanzo. Yohana Mbatizaji ndiye Elia mtayarisha njia kwa ajili ya Kristo, na Yesu Kristo ndiye Elia ambaye hurejesha mambo yote na kupitia yeye wokovu huja.

1 Hapo mwanzo injili ilihubiriwa kupitia kwa Mwana. Na injili ilikuwa ni neno, na neno lilikuwa na Mwana, na Mwana alikuwa pamoja na Mungu, na Mwana alikuwa wa Mungu.

2 Huyo huyo mwanzoni alikuwa kwa Mungu.

3 Vitu vyote vilifanywa naye; na pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika.

4 Ndani yake ndimo ilimokuwa injili, nayo injili ilikuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu;

5 Nayo nuru yangʼara ulimwenguni, wala ulimwengu haukuitambua.

6 Palikuwa na mtu aliyetumwa kutoka kwa Mungu, ambaye jina lake lilikuwa Yohana.

7 Huyo huyo alikuja ulimwenguni kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, ili kutoa ushuhuda wa injili kupitia Mwana, hadi kwa wote, ili kwa njia yake watu wapate kuamini.

8 Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru,

9 Ambayo ilikuwa nuru halisi, ambayo humwangaza kila mtu ajaye katika ulimwengu;

10 Hata Mwana wa Mungu. Yeye aliyekuwako ulimwenguni, nao ulimwengu ulifanywa naye, na ulimwengu haukumtambua.

11 Alikuja kwa walio wake, na walio wake hawakumpokea.

12 Bali kadiri wengi walivyompokea, kwao aliwapa uwezo wa kuwa wana wa Mungu; kwao wale tu walioamini katika jina lake.

13 Yeye alizaliwa, siyo kwa damu, wala siyo kwa mapenzi ya mwili, wala siyo kwa mapenzi ya mtu, bali ya Mungu.

14 Naye huyo neno alifanyika mwili, na akakaa kwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mzaliwa Pekee wa Baba, amejaa neema na kweli.

15 Yohana atoa ushuhuda juu yake, na kulia, akisema, Huyu ndiye yule niliyenena juu yake ya kwamba; Yeye ajaye nyuma yangu, amekuwa mbele yangu; maana yeye alikuweko kabla yangu.

16 Maana hapo mwanzo alikuwako Neno, hata Mwana, ambaye amefanywa mwili, na kuletwa kwetu kwa mapenzi ya Baba. Na kadiri wengi waliaminivyo jina lake wataupokea utimilifu wake. Na katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, hata mwili usio kufa na uzima wa milele, kwa njia ya neema yake.

17 Kwani sheria ilitolewa kwa njia ya Musa, lakini uzima na kweli vilikuja kwa njia ya Yesu Kristo.

18 Maana sheria ilikuwa kwa jinsi ya amri ya kimwili, ambayo huleta mauti; lakini injili ilikuwa kwa jinsi ya uwezo wa uzima usio na mwisho, kwa njia ya Yesu Kristo, Mwana Pekee, aliye kifuani mwa Baba.

19 Na hakuna mtu aliye mwona Mungu wakati wowote, isipokuwa yeye amemshuhudia Mwana; maana hakuna mtu awezaye kuokolewa isipokuwa kwa njia yake.

20 Na huu ndiyo ushuhuda wa Yohana, wakati Wayahudi walipowatuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu, ili wamwulize, Wewe u nani?

21 Naye alikiri, wala hakukana; kwamba yeye alikuwa Elia; bali alikiri, akisema; Mimi siye Kristo.

22 Nao wakamwuliza, wakisema, Ni kwa namna gani basi u Elia? Naye akasema, Mimi siye yule Elia ambaye atarejesha mambo yote. Nao wakamwuliza, wakisema, Wewe u nabii yule? Naye akajibu, La.

23 Basi wakamwambia, U nani wewe? ili tupate kutoa jibu kwa wale waliotutuma. Wanenaje juu ya nafasi yako?

24 Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana, kama asemavyo nabii Isaya.

25 Nao wale waliotumwa walikuwa wametoka kwa Mafarisayo.

26 Na wakamwuliza, na wakimwambia; Kwa nini basi wabatiza, ikiwa wewe siye Kristo, wala Elia ambaye atarejesha mambo yote, wala si yule nabii?

27 Yohana akawajibu, akisema, Mimi nabatiza kwa maji, lakini katikati yenu, amesimama yeye msiyemjua ninyi;

28 Yeye ndiye nimshuhudiaye. Yeye ndiye yule nabii, hata Elia, ambaye yu aja nyuma yangu, amekuwa mbele yangu, ambaye mimi, sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake, au ambaye nafasi yake siwezi kuijaza; maana yeye atabatiza, siyo kwa maji tu, bali kwa moto, na kwa Roho Mtakatifu.

29 Siku iliyofuata Yohana akamwona Yesu akimjia, na akasema; Tazama Mwanakondoo wa Mungu, aondoaye dhambi ya ulimwengu!

30 Naye Yohana alimshududia kwa watu, akisema; Huyu ndiye niliyenena juu yake ya kwamba; Yu aja mtu nyuma yangu ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu, nami nalimjua, na nalijua kwamba yapaswa adhihirishwe kwa Israeli; ndiyo maana mimi nalikuja nikiwabatiza kwa maji.

31 Na Yohana akashuhudia, akisema; Nilipokuwa nikimbatiza, nilimuona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni, naye akakaa juu yake.

32 Nami nalimjua; kwa maana yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo ndiye aliyeniambia; Yeye ambaye utamwona Roho akishuka juu yake, na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu.

33 Nami nimeona, na nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.

34 Mambo haya yalitendeka katika Bethabara, ngʼambo ya Yordani, mahali ambapo Yohana alikuwa akibatiza.

TJS, Yohana 1:42. Linganisha na Yohana 1:42

Kefa maana yake “Mwonaji” au “jiwe.”

42 Naye akampeleka kwa Yesu. Na Yesu alipomtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yona, nawe utaitwa Kefa, ambayo fasiri yake ni mwonaji, au jiwe. Na walikuwa wavuvi. Nao mara wakaacha vyote, na wakamfuata Yesu.