Mlango wa 3
Wanefi wengi wanahamia kwenye nchi iliyopo kaskazini—Wanajenga nyumba za saruji na wanaandika kumbukumbu nyingi—Maelfu wanaongoka na kubatizwa—Neno la Mungu linawaongoza watu kwenye wokovu—Nefi mwana wa Helamani anachukua kiti cha hukumu. Karibia mwaka 49–39 K.K.
1 Na sasa ikawa katika mwaka wa arubaini na tatu wa utawala wa waamuzi, hakukuwa na ubishi miongoni mwa watu wa Nefi isipokuwa kiburi kidogo ambacho kilikuwa kanisani, ambacho kilianzisha mafarakano madogo miongoni mwa watu, mambo ambayo yalirekebishwa mwishoni mwa mwaka wa arubaini na tatu.
2 Na hapakuweko na ubishi miongoni mwa watu katika mwaka wa arubaini na nne; wala hapakuweko ubishi mwingi katika mwaka wa arubaini na tano.
3 Na ikawa katika mwaka wa arubaini na sita, ndiyo, kulikuwa na mafarakano mengi na ugomvi mwingi; hata kwamba kulikuwa na wengi sana ambao waliondoka nchi ya Zarahemla, na kwenda kwenye nchi ya upande wa kaskazini kurithi nchi.
4 Na walisafiri kwa mwendo mrefu sana, mpaka kwamba wakafika kwenye maziwa makubwa na mito mingi.
5 Ndiyo, na hata walitawanyika katika sehemu zote za nchi, katika sehemu zozote ambazo hazikuwa zimefanywa kuwa na ukiwa na bila miti, kwa sababu ya wakazi wengi ambao hapo kabla walikuwa wamerithi nchi ile.
6 Na sasa hakukuwa na sehemu yeyote ya nchi ambayo ilikuwa ya ukiwa, isipokuwa pale pasipokuwa na miti; lakini kwa sababu ya kuangamizwa watu wengi walioishi nchini hapo kabla iliitwa ukiwa.
7 Na kwa vile kulikuwa na miti michache tu nchini, hata hivyo watu walioenda huko walipata kuwa na ujuzi mwingi kwa kutumia saruji; kwa hivyo walijenga nyumba za saruji, ambamo waliishi.
8 Na ikawa kwamba waliongezeka na kutawanyika, na wakasonga mbele kutoka nchi ya upande wa kusini hadi nchi ya upande wa kaskazini, na wakaenea hata kwamba wakaanza kufunika uso wote wa ulimwengu, kutoka bahari ya kusini hadi bahari ya kaskazini, kutoka bahari ya magharibi hadi bahari ya mashariki.
9 Na watu waliokuwa katika nchi ya upande wa kaskazini waliishi kwenye hema, na kwenye nyumba za saruji, na waliachilia mti wa aina yoyote uliomea juu ya ardhi ya nchi kwamba ukue, ili kwa muda ujao wangepata miti ya kujengea nyumba zao, ndiyo, miji yao, na mahekalu yao, na masinagogi yao, na mahali pao patakatifu, na aina yote ya majengo yao.
10 Na ikawa kwa vile miti ilikuwa michache katika nchi ya upande wa kaskazini, walisafirisha mingi kwa kutumia meli.
11 Na hivyo waliwezesha watu waliokuwa kwenye nchi ya upande wa kaskazini kujenga miji mingi, yote ya miti na saruji.
12 Na ikawa kwamba kulikuwa na watu wengi wa watu wa Amoni, ambao walikuwa Walamani kwa kuzaliwa, ambao pia walienda kwenye nchi hii.
13 Na sasa kuna kumbukumbu nyingi juu yao ambazo zimeandikwa za historia ya watu hawa ambazo ni mahsusi na kubwa sana kuwahusu.
14 Lakini tazama, sehemu moja ya mia ya historia ya watu hawa, ndiyo, historia ya Walamani na Wanefi, na vita vyao, na mabishano, na mafarakano, na mahubiri yao, na unabii wao, na meli zao na uundaji wa meli zao, na ujenzi wao wa mahekalu, na ya masinagogi yao na mahali pao patakatifu, na haki yao, na uovu wao, na mauaji yao, na uporaji wao, na unyangʼanyi wao, na aina yote ya machukizo na ukahaba, hauwezi kuwekwa wote kwenye maandishi haya.
15 Lakini tazama, kuna vitabu vingi na maandishi mengi ya kila aina, na ameandikwa zaidi na Wanefi.
16 Na kukabidhiana kutoka kizazi kimoja hadi kingine na Wanefi, hata mpaka wameanza kutenda dhambi na wameuawa, kuporwa, na kuwindwa, na kufukuzwa, na kuuawa, na kutawanywa usoni mwa ulimwengu, na kuchanganywa na Walamani mpaka hawaitwi tena Wanefi, wakiwa waovu, na washenzi, na wakatili, ndiyo, hata kuwa Walamani.
17 Na sasa narudia tena historia yangu; kwa hivyo, yale ambayo nimyaesema yalifanyika baada ya kuweko mabishano makuu, na misukosuko, na vita, na mafarakano, miongoni mwa watu wa Nefi.
18 Mwaka wa arubaini na sita wa utawala wa waamuzi uliisha;
19 Na ikawa kwamba kulikuwa bado na ubishi mkubwa nchini, ndiyo, hata katika mwaka wa arubaini na saba, na pia mwaka wa arubaini na nane.
20 Walakini Helamani alichukua kiti cha hukumu kwa haki na uadilifu; ndiyo, alichunga na kutii sheria na uamuzi, na amri za Mungu; na alifanya kile kilichokuwa cha haki machoni mwa Mungu siku zote; na alikuwa na mwendo sawa na baba yake, mpaka kwamba alifanikiwa nchini.
21 Na ikawa kwamba alikuwa na wana wawili. Alimwita yule mkubwa kwa jina la Nefi, na mdogo, kwa jina la Lehi. Na walianza kukua wakimtii Bwana.
22 Na ikawa kwamba vita na mabishano yalianza kupungua, kidogo, miongoni mwa watu wa Wanefi, katika mwisho wa mwaka wa arubaini na nane wa utawala wa waamuzi juu ya watu wa Nefi.
23 Na ikawa katika mwaka wa arubaini na tisa wa utawala wa waamuzi, kuliimarishwa amani ya kudumu katika nchi, yote isipokuwa makundi maovu ya siri ambayo Gadiantoni mwizi alikuwa ameanzisha katika sehemu za nchi ambazo zilikuwa zimekaliwa kwa wingi, ambazo wakati huo hazikuwa zimejulikana kwa viongozi wa serikali; kwa hivyo hawakuangamizwa kutoka nchini.
24 Na ikawa kwamba katika mwaka huo huo kulikuwa na mafanikio mengi sana katika kanisa, kiasi kwamba kulikuwa na maelfu waliojiunga na kanisa na walibatizwa ubatizo wa toba.
25 Na mafanikio ya kanisa yalikuwa mengi sana, na baraka nyingi zilipokelewa na watu, kwamba hata makuhani wakuu na walimu wenyewe walishangaa kupita kiasi.
26 Na ikawa kwamba kazi ya Bwana ilifanikiwa na watu wengi kubatizwa na kuunganishwa kwa kanisa la Mungu, ndiyo, hata makumi ya maelfu.
27 Hivyo tunaweza kuona kwamba Bwana ana huruma kwa wote ambao, kwa uaminifu wa mioyo yao, wanaolingana kwa jina lake takatifu.
28 Ndiyo, hivyo tunaona kwamba mlango wa mbinguni umefunguliwa kwa wote, hata kwa wale ambao wataamini katika jina la Yesu Kristo, ambaye ni Mwana wa Mungu.
29 Ndiyo, tunaona kwamba yeyote atakaye angelishikilia neno la Mungu, ambalo ni jepesi na lenye nguvu, ambalo litaangamiza ujanja wote na mitego na hila za ibilisi, na kumwongoza mfuasi wa Kristo katika njia iliyosonga na nyembamba mpaka ngʼambo ya shimo la dhiki lisilo na mwisho ambalo limetayarishwa kumeza waovu—
30 Na kuangusha roho zao, ndiyo, roho zao zisizokufa, katika mkono wa kuume wa Mungu katika ufalme wa mbinguni, kuketi chini na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, na babu zetu wote watakatifu, ambako hawataondoka tena milele.
31 Na katika mwaka huu kulikuwa na furaha ya kudumu katika nchi ya Zarahemla, na katika nchi zote zilizokuwa karibu, hata kwenye nchi yote ambayo ilimilikiwa na Wanefi.
32 Na ikawa kwamba kulikuwa na amani na shangwe kubwa katika mwisho wa mwaka wa arubaini na tisa; ndiyo, na pia kulikuwa na amani ya kudumu na shangwe nyingi katika mwaka wa hamsini wa utawala wa waamuzi.
33 Na katika mwaka wa hamsini na moja wa utawala wa waamuzi kulikuwa na amani pia, isipokuwa tu kiburi ambacho kilianza kuingia kanisani—sio katika kanisa la Mungu, lakini katika mioyo ya watu ambao walidai kuwa wa kanisa la Mungu—
34 Na waliinuka kwa kiburi, hata kwenye kudhulumu ndugu zao wengi. Sasa huu ulikuwa uovu mkubwa, ambao ulisababisha sehemu kubwa ya walio wanyenyekevu kuumia udhalimu mkuu, na kuvumilia mateso mengi.
35 Walakini walifunga na kuomba kila wakati, na wakapokea nguvu kwa wingi katika unyenyekevu wao, na wakawa imara zaidi na imara katika imani ya Kristo, hadi nafsi zao jikajazwa na shangwe na faraja, ndiyo, hata kwenye kusafishwa na utakaso wa mioyo yao, utakaso ambao huja kwa sababu ya wao kumtolea Mungu mioyo yao.
36 Na ikawa kwamba mwaka wa hamsini na mbili uliisha kwa amani pia, isipokuwa kiburi kikubwa ambacho kilikuwa kimeingia katika mioyo ya watu; na ilikuwa kwa sababu ya utajiri wao mwingi na kufanikiwa kwao nchini; na kiliendelea kukua ndani yao kutoka siku hadi siku.
37 Na ikawa katika mwaka wa hamsini na tatu wa utawala wa waamuzi, Helamani alifariki, na mwana wake wa kwanza Nefi akaanza kutawala badala yake. Na ikawa kwamba alichukua kiti cha hukumu kwa haki na uadilifu; ndiyo, alitii amri za Mungu, na alienenda katika njia za baba yake.