Maandiko
Ushuhuda wa Nabii Joseph Smith


Ushuhuda wa Nabii Joseph Smith

Maneno yenyewe ya Nabii Joseph Smith kuhusu ufunuo wa Kitabu cha Mormoni ni haya:

“Mnamo jioni ya tarehe … ishirini na moja, mwezi wa Septemba [1823] … nilianza sala na maombi kwa Mwenyezi Mungu. …

“Nilipokuwa katika hali ya kumwomba Mungu, niligundua kwamba kulikuwa na mwangaza unaingia chumbani mwangu, ambao uliendelea kuangaza hadi chumba kikangʼaa zaidi ya mwangaza wa adhuhuri, kwa ghafla malaika akatokea kando ya kitanda changu, akasimama hewani, kwani miguu yake haikugusa sakafu.

“Alikuwa amevaa joho jeupe maridadi lenye kupwaya. Lilikuwa jeupe zaidi ya chochote nilichokuwa nimeona duniani; wala siamini kwamba kuna kitu chochote duniani ambacho kinaweza kufanywa kuwa cheupe na kungʼara kama hivyo. Mikono yake ilikuwa wazi, hadi juu kidogo ya kiwiko vivyo hivyo, pia, miguu yake ilikuwa mitupu, hadi juu kidogo vifundoni. Kichwa chake na shingo yake pia vilikuwa wazi. Nikagundua kwamba hakuwa amevaa vazi lolote zaidi ya lile joho, kwa maana lilikuwa wazi, kiasi kwamba niliweza kuona kifua chake.

“Siyo tu joho lake lilikuwa jeupe zaidi, lakini hata kiwiliwili chake kilikuwa na utukufu usioelezeka, na uso wake kwa ukweli ukawa kama umeme. Chumba kilingʼaa kabisa, lakini siyo zaidi ya pale aliposimama huyo mtu. Nilipomtazama mara ya kwanza, niliogopa; lakini hatimaye woga ukanitoka.

“Aliniita kwa jina langu, na kuniambia kwamba alikuwa mjumbe aliyetumwa kwangu kutoka uwepo wa Mungu, na kwamba jina lake lilikuwa Moroni; kwamba Mungu alikuwa na kazi ambayo mimi ningefanya; na kwamba jina langu lingekuwa la mema na maovu miongoni mwa mataifa yote, makabila, na lugha, au lingetajwa kwa wema na kwa uovu miongoni mwa watu wote.

“Akasema kulikuwa na kitabu kimesalimishwa, kimeandikwa kwenye mabamba ya dhahabu, kinaeleza historia ya wenyeji wa kale wa bara hili, na mwanzo ambako walikotokea. Akasema pia kwamba utimilifu wa Injili isiyo na mwisho ulikuwa ndani ya kitabu hicho, kama ilivyotolewa na Mwokozi kwa wenyeji wa kale;

“Pia, kwamba yalikuwa mawe mawili katika pinde za fedha—na mawe haya, yalifungwa kwenye dirii, na hii ndiyo inaitwa Urimu na Thumimu—ikiwa imesalimishwa na yale mabamba; na umiliki na matumizi ya mawe haya vilikuwa kile kilichoanzisha ‘waonaji’ wa kale au zamani; na kwamba Mungu alikuwa ameyatayarisha kwa sababu ya utafsiri wa hiki kitabu. …

“Akaniambia, tena, nikiyapata mabamba hayo ambayo alikuwa ameyazungumzia—kwani wakati wa kuyapokea haukuwa umetimia—Nisiyaonyeshe kwa mtu yeyote; wala ile dirii pamoja na Urimu na Thumimu; isipokuwa tu kwa wale ambao nitaamriwa kuwaonyesha; ikiwa nitazionyeshana nitaangamizwa. Alipokuwa akinizungumzia kuhusu yale mabamba, ono likafunguliwa katika mawazo yangu ili nione mahali ambapo yale mabamba yalisalimishwa, na ilikuwa wazi na dhahiri kwamba ningepajua hapo mahali nikipatembelea tena.

“Baada ya mawasiliano haya, nikaona mwangaza katika chumba ukaanza mara moja kumzingira mtu ambaye alikuwa akizungumza nami, na ukaendelea kufanya hivyo, hadi chumba kikawa tena na giza, isipokuwa tu mahali alipokuwa amesimama, mara, ghafla nikaona, ni kama njia imefunguka hadi mbinguni, na yeye akapanda nayo hadi akatoweka kabisa, na chumba kikaachwa kama vile kilivyokuwa kabla ya mwangaza huu wa mbinguni haujatokea.

“Nikalala nikiwaza kwa upweke kuhusu hilo jambo, na nikashangazwa sana na yale niliyokuwa nimeambiwa na huyu mjumbe mgeni; ambapo, miongoni mwa mawazo yangu, nikagundua kwa ghafla kwamba chumba changu kilianza tena kuangazwa, na ikawa kwamba kwa mara moja, kama ilivyokuwa, mjumbe yule yule wa mbinguni alikuwa tena kando ya kitanda changu.

“Akaanza, na tena kuniambia vitu vile vile alivyofanya hapo awali, bila tofauti yoyote; baada ya kufanya hivyo, akanijulisha kuhusu hukumu kali ambazo zilikuwa zinakuja ulimwenguni, pamoja na ukiwa mkubwa wa njaa, upanga, na tauni; na kwamba hizi hukumu kali zitakuja ulimwenguni katika kizazi hiki. Baada ya kusimulia vitu hivi, akapanda juu tena kama alivyokuwa amefanya hapo awali.

“Kwa wakati huu, mawazo mazito sana yalifanyika akilini mwangu, kwamba usingizi uliniruka machoni mwangu, na nikajilaza nikizimia moyo kwa mshangao kwa yale yote niliyokuwa nimeyaona na kusikia. Lakini ni nini ulikuwa mshangao wangu wakati tena ninamwona mjumbe yule yule kando ya kitanda changu, na nikamsikia tena akirudia mambo yale yale awali; na akaongeza onyo, akaniambia kwamba Shetani angejaribu kunishawishi (akitumia hali ya umaskini wa familia ya baba yangu), kuyachukua mabamba yale kwa kusudi la kupata utajiri. Hili alinikanya, akisema lazima nisiwe na lengo lingine la kuchukua mabamba yale ila tu kwa lengo la kumtukuza Mungu, na kwamba lazima nisishawishiwe na kusudi lingine lolote ila tu la kujenga ufalme wake; kama si hivyo nisingezipata.

“Baada ya ujio huu wa tatu, akapaa tena mbinguni kama hapo mwanzo, na mimi tena nikaachwa nikitafakari juu ya ugeni wa yale ambayo nilikuwa nimeyashuhudia; ambapo punde tu baada ya mjumbe yule wa mbinguni kupaa mara ya tatu, jogoo akawika, na nikafahamu kwamba siku mpya ilikuwa inapambazuka, hivyo basi mahojiano yetu lazima yalikuwa yamechukua huo usiku wote.

“Baada ya muda mfupi nikaamka kutoka kitandani, na kama kawaida, nikaenda kufanya kazi inayonipasa kila siku; lakini nikajaribu kufanya kazi kama nyakati zingine, nikaishiwa na nguvu nikawa mchovu nisijiweze. Baba yangu, ambaye alikuwa anafanya kazi karibu na mimi, akagundua kwamba nilikuwa na kasoro fulani, na akaniambia nirejee nyumbani. Nikaanza nikiwa na kusudi la kurejea nyumbani; lakini nikijaribu kuvuka ua ambao ulikuwa umezingira ule uwanja ambamo tulikuwa, nikaishiwa nikaanguka hoi chini, na kwa muda sikujisikia kabisa.

“Kitu cha kwanza ambacho naweza kukumbuka ni sauti ikinizungumzia, ikiniita kwa jina langu. Nikatazama juu, na nikaona mjumbe yule yule amesimama karibu na kichwa changu, akiwa amezingirwa na mwangaza kama hapo awali. Akanielezea tena yale ambayo alinielezea usiku uliopita, na akaniamuru niende kwa baba yangu na nimwambie kuhusu lile ono na amri ambazo nilipokea.

“Nikatii nikarejea kwa baba yangu huko uwanjani, na nikamwambia vitu vyote. Akanijibu kwamba yalikuwa ni ya Mungu, na akaniambia niende na nitende niliyoamriwa na yule mjumbe. Nikatoka uwanjani, na nikaenda mahali pale yule mjumbe alinielezea kuwa yale mabamba yalizosalimishwa yapo; na kwa sababu ya udhahiri wa lile ono nililoona kuhusu mahali hapo nilipajua mara moja nilipowasili.

“Karibu na kijiji cha Manchester, jimbo la Ontario, New York, kuna mlima mkubwa kiasi na ni mrefu zaidi ya chochote hapo mtaani. Magharibi mwa mlima huu, karibu na kilele, chini ya jiwe la kipimo kikubwa, yale mabamba yalikuwemo, yalifungiwa ndani ya sanduku la jiwe. Jiwe hili lilikuwa nene na upande wa juu katikati lilikuwa kama mviringo, na pande zake zilikuwa nyembamba, kwamba lingeonekana katikati kutoka chini, lakini pande zake zote zilifunikwa na udongo.

“Baada ya kutoa udongo, nikachukua mtaimbo, ambao niliukokomea chini ya upande wa lile jiwe, na kwa bidii kidogo nikaliinua. Nikatazama ndani, na pale kwa kweli nikayaona yale mabamba, Urimu na Thumimu, pamoja na dirii, kama ilivyoelezwa na yule mjumbe. Lile sanduku ambalo zilikuwemo lilikuwa limejengwa kwa saruji na mawe. Chini ya lile sanduku palikuwa na mawe mawili yamepitana, na juu ya mawe haya yalikuwa yamekomelewa yale mabamba pamoja na hivyo vitu vingine.

“Nikajaribu kuzitoa, lakini nikakatazwa na yule mjumbe, nikaambiwa tena wakati wa kuzitoa haukuwa umetimia, wala haungetimia, kabla ya miaka minne kupita tangu ile siku; lakini akaniambia nirudi mahali pale baada ya mwaka moja halisi kutoka siku ile, na kwamba atakutana na mimi pale, na kwamba niendelee kufanya hivyo hadi wakati wa kuyachukua mabamba utimie.

“Kwa hivyo, kama nilivyokuwa nimeamriwa, nilienda kila mwisho wa mwaka, na kila wakati nilimkuta mjumbe yule yule hapo, na nikapokea maelekezo na maarifa kutoka kwake kwa kila mahojiano yetu, kuhusu yale ambayo Bwana atakuja kufanya, na kwa namna na katika utaratibu gani ufalme wake utaendeshwa katika siku za mwisho. …

“Hatimaye wakati ukatimia wa kuyachukua yale mabamba, Urimu na Thumimu, na ile dirii ya kifua. Mnamo tarehe ishirini na mbili mwezi wa Septemba, mwaka wa elfu moja mia nane ishirini na saba, nikiwa nimeenda kama kawaida katika mwisho wa mwaka mwingine mahali pale yalipokuwa yamewekwa, mjumbe yule yule wa mbinguni akayakabidhi kwangu pamoja na agizo: Kwamba ninapaswa kuwajibika; na kwamba kama ningeyaacha yaende kwa uzembe, au kwa sababu ya kutojali kwangu, nitatupiliwa mbali; lakini nikivitunza na kufanya bidii yote ili kuvihifadhi, hadi yeye, mjumbe, ataviitishe, vitalindwa.

“Kwa haraka nikagundua shauri ya kuniagiza kwa ukali kuziweka salama, na ni kwa nini yule mjumbe alisema kuwa nikitimiza yanayohitajika kutoka kwangu, ataziitisha. Kwani kwa haraka ilijulikana kwamba nilikuwa nazo, kuliko juhudi za nguvu zilitumika kuzichukua kutoka kwangu. Kila hila iliyopatikana ilitumika kwa kusudi hilo. Mateso yakawa magumu na kali mno zaidi ya hapo awali, na wengi walikuwa tayari kila mara kuzichukua kutoka kwangu kama ingewezekana. Lakini kwa hekima ya Mungu, zikawa salama mikononi mwangu, hadi nikatimiza nazo kilichohitajika kutoka kwangu. Kulingana na mipango; wakati mjumbe alipoziitisha, nilizikabidhi kwake; na hadi sasa ziko chini ya ulinzi wake, ikiwa tarehe mbili mwezi wa Mei, mwaka wa elfu moja mia nane, thelathini na nane.”

Kwa historia kamili, angalia Joseph Smith—Historia ya katika Lulu ya Thamani Kuu.

Historia hiyo ya kale ilitolewa kwenye ardhi kama sauti ya watu wakizungumza kutoka mavumbini, na ikatafsiriwa kwa lugha ya kisasa kwa karama na uwezo wa Mungu kama ilivyoshuhudiwa na Ushuhuda mtakatifu, ulichapishwa mara ya kwanza ulimwenguni kwa Kiingereza mwaka wa 1830 kama The Book of Mormon.