Maandiko
Utangulizi


Utangulizi

Kitabu cha Mormoni ni juzuu ya maandiko matakatifu sawa sawa na Biblia. Ni kumbukumbu ya matendo ya Mungu kwa kikundi cha wakazi wa kale wa bara la Marekani na inayo utimilifu wa injili isiyo na mwisho.

Kitabu hiki kiliandikwa na manabii wengi wa kale kwa roho ya unabii na ufunuo. Maneno yao, yaliyoandikwa kwenye mabamba ya dhahabu, yalinukuliwa na kufupishwa na mwanahistoria nabii aliyeitwa Mormoni. Kumbukumbu hii inaelezea kuhusu historia ya mataifa mawili makubwa. Moja lilitoka Yerusalemu katika mwaka wa 600 K.K. na baadaye kugawanyika kuwa mataifa mawili, ambayo yalijulikana kama Wanefi na Walamani. Lingine lilikuja mapema zaidi wakati Bwana alipovuruga lugha katika Mnara wa Babeli. Kikundi hiki kinajulikana kama Wayaredi. Baada ya maelfu ya miaka, wote waliangamizwa isipokuwa Walamani, na hawa ni miongoni mwa mababu wakuu wa Wahindi wa Kiamerika.

Tukio kuu lililoandikwa katika Kitabu cha Mormoni ni huduma binafsi ya Bwana Yesu Kristo miongoni mwa Wanefi mara baada ya ufufuko Wake. Kinaeleza mafundisho ya injili, kinafafanua juu ya mpango wa wokovu, na kuwaambia binadamu mambo wanayopaswa kuyafanya ili wapate amani katika maisha haya na wokovu wa milele katika maisha yanayokuja.

Baada ya Mormoni kukamilisha maandishi yake, akamkabidhi mwanawe Moroni historia hiyo, ambaye naye akaongeza maneno yake machache na kuficha mabamba hayo katika Kilima Kumora. Mnamo 21 Septemba 1823, Moroni huyo huyo, sasa akiwa ametukuzwa, kiumbe mfufuka, akamtokea Nabii Joseph Smith na kumpa maelekezo kuhusu kumbukumbu hiyo ya kale na hatima ya tafsiri yake katika lugha ya Kiingereza.

Wakati ulipofika mabamba hayo yalitolewa kwa Joseph Smith, ambaye aliyatafsiri kwa karama na uwezo wa Mungu. Kumbukumbu hii sasa imechapishwa katika lugha nyingi kama ushuhuda mpya na wa nyongeza kuwa Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu aliye hai na kwamba wote ambao watakuja Kwake na kutii sheria na ibada za injili Yake wataokolewa.

Kuhusu maandishi haya Nabii Joseph Smith Nabii alisema: “Niliwaambia ndugu kwamba Kitabu cha Mormoni ndicho kitabu sahihi duniani, na ndicho jiwe la katikati la teo la dini yetu, na kuwa mwanadamu angemkaribia Mungu zaidi kwa kufuata mafundisho yake, zaidi ya kitabu kingine.”

Pamoja na Joseph Smith, Bwana aliwachagua wengine kumi na moja kujionea mabamba yale ya dhahabu na kuwa mashahidi maalum wa ukweli na utakatifu wa kitabu cha Mormoni. Ushuhuda wao wameuandika na umechapishwa hapa na kujulikana kama “Ushuhuda wa Mashahidi Watatu” na “Ushuhuda wa Mashahidi Wanane.”

Tunawakaribisha watu wote kutoka kila mahali kusoma Kitabu cha Mormoni, kutafakari mioyoni mwao ujumbe wake, na kisha kumuuliza Mungu, Baba wa Milele, katika jina la Kristo kama hiki kitabu ni cha kweli. Wale ambao watafuata njia hii na kuuliza kwa imani watapata ushuhuda wa ukweli na utakatifu wake kwa nguvu za Roho Mtakatifu. (Soma Moroni 10:3–5.)

Wale ambao wanapata ushuhuda huu mtakatifu kutoka kwa Roho Mtakatifu watakuja pia kujua kwa uwezo huo huo kwamba Yesu Kristo ndiye Mwokozi wa ulimwengu, na kwamba Joseph Smith ndiye mfunuzi na nabii Wake katika siku hizi za mwisho, na kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni ufalme wa Bwana ambao kwa mara nyingine tena umekuja duniani kwa ajili ya matayarisho ya Ujio wa Pili wa Masiya.