Maandiko Matakatifu
Maelezo kwa kifupi juu ya Kitabu cha Mormoni


Maelezo Mafupi Kuhusu Kitabu cha Mormoni

Kitabu cha Mormoni ni historia takatifu ya makundi ya watu katika Marekani ya kale, na ilikuwa imechorwa kwenye mabamba ya metali. Vyanzo ambavyo kwavyo kumbukumbu hii ilikusanywa inajumuisha vifuatavyo:

  1. Mabamba ya Nefi, ambayo yalikuwa ya aina mbili: mabamba madogo na mabamba makubwa. Ya kwanza yalikuwa hasa yamekusudiwa zaidi kwa masuala ya kiroho na huduma yake pamoja na mafundisho ya manabii, wakati haya mengine yalikuwa zaidi na historia ya kiulimwengu ya watu husika (1 Nefi 9:2–4). Tangu wakati wa Mosia, hata hivyo, mabamba makubwa pia yalijumuisha mambo yenye umuhimu mkubwa wa kiroho.

  2. Mabamba ya Mormoni, ambayo yalikuwa na ufupisho wa Mormoni kutoka katika yale mabamba makubwa ya Nefi, pamoja na ufafanuzi mwingi. Mabamba haya pia yalikuwa na mwendelezo wa mambo ya kihistoria iliyoandikwa na Mormoni pamoja na nyongeza ya mwanawe Moroni.

  3. Mabamba ya Etheri, ambazo zilikuwa na historia ya Kiyaredi. Historia hii ilifupishwa na Moroni, ambaye aliongeza maneno yake na kuchanganya hayo maandishi katika historia ya jumla ijulikanayo kama “Kitabu cha Etheri.”

  4. Mabamba ya Shaba Nyeupe yaliyoletwa na watu wa Lehi kutoka Yerusalemu mnamo mwaka wa 600 K.K. Haya yalikuwa na “ vitabu vitano vya Musa, … na pia kumbukumbu ya Wayahudi tangu mwanzo, … hadi mwanzoni mwa utawala wa Zedekia, mfalme wa Yuda; na pia unabii wa manabii watakatifu” (1 Nefi 5:11–13). Nukuu nyingi kutoka katika mabamba haya, zikimtaja Isaya na manabii wengine wa kibiblia na manabii wasio wa kibiblia, zinaonekana katika Kitabu cha Mormoni.

Kitabu cha Mormoni kina mgawanyo au sehemu kuu kumi na tano zinazojulikana kama vitabu, isipokuwa kimoja, kwa kawaida vitabu hivi vimetajwa kwa jina la mwandishi wake mkuu. Fungu la kwanza (vitabu sita vya kwanza, cha mwisho kikiwa Omni) ni tafsiri kutoka katika mabamba madogo ya Nefi. Katikati ya vitabu vya Omni na Mosia kuna ingizo linaloitwa Maneno ya Mormoni. Ingizo hili linaunganisha kumbukumbu iliyochorwa juu ya yale mabamba madogo pamoja na ufupisho wa Mormoni wa yale mabamba makubwa.

Sehemu ambayo ni ndefu zaidi, kutoka kitabu cha Mosia hadi Mormoni mlango wa saba, yote pamoja, ni tafsiri ya ufupisho wa Mormoni kutoka katika yale mabamba makubwa ya Nefi. Sehemu ya mwisho, kutoka Mormoni mlango wa nane, hadi mwisho wa kitabu, ilichorwa na mwana wa Mormoni ambaye, ni Moroni, ambaye baada ya kumaliza kuandika kumbukumbu ya maisha ya baba yake, alifupisha kumbukumbu ya Wayaredi (kama kitabu cha Etheri) na baadaye akaongeza sehemu zijulikanazo kama kitabu cha Moroni.

Katika au karibia mwaka wa 421 B.K., Moroni, wa mwisho katika manabii-wanahistoria wa Kinefi, alifunga kumbukumbu ile takatifu na kuificha katika Bwana, ili itolewe katika siku za baadaye, kama vile ilivyotabiriwa na sauti ya Mungu kupitia manabii Wake wa kale. Katika mwaka wa 1823 B.K., huyo huyo Moroni, akiwa mtu aliyefufuliwa, alimtokea Nabii Joseph Smith na hatimaye akamkabidhi yale mabamba yaliyochongwa maandishi.

Juu ya toleo hili; Ukurasa asili wa kwanza wenye jina la kitabu, ulio kabla tu ya ukurasa wa yaliyomo, umetolewa kutoka kwenye mabamba na ni sehemu ya maandishi matakatifu. Utangulizi katika maneno yasiyo ya kiitaliki, kama vile yalivyo katika 1 Nefi na kabla tu Mosia mlango wa 9, nayo ni sehemu ya maandishi matakatifu. Utangulizi ulio katika kiitaliki, kama vile katika vichwa vya milango, siyo maandiko ya asili hayakuwepo mwanzoni lakini ni msaada katika kujifunza yamejumuishwa ili kurahisisha katika usomaji.

Baadhi ya makosa madogo madogo katika maandishi yameendelezwa katika matoleo yaliyopita ya Kitabu cha Mormoni kilichochapishwa kwa Kiingereza. Toleo hili lina masahihisho ambayo yameonakana yanafaa katika kuileta taarifa iliyotumika katika maandiko haya katika ulinganifu na miswada iliyokuwepo kabla ya kuchapishwa na matoleo ya mwanzoni yaliyo sahihishwa na Nabii Joseph Smith.