Kuhusu Ubatizo na Uthibitisho kwa Uwakilishi

Ubatizo kwa Uwakilishi ni Nini?

Ubatizo na Uthibitisho ni vya Muhimu

Makala ya Nne ya Imani inasema kwamba ibada za kwanza za Injili ya Yesu Kristo ni “ubatizo kwa kuzamishwa kwa ajili ya ondoleo la dhambi” na “kuwekewa mikono kwa ajili ya zawadi ya Roho Mtakatifu.” Yesu alifundisha kwamba ubatizo na uthibitisho huitajika kwa wote ambao wanataka kumfuata Yeye na kurejea kwa Baba yetu wa Mbinguni baada ya maisha haya. Hivyo basi ubatizo ni lango kuelekea njia ya agano ambayo huongoza kwenye kupokea baraka zote ambazo Baba yetu wa Mbinguni anatamani kutupatia. Pia ni lango kuelekea kuwa “wakamilifu katika Kristo” (Moroni 10, 32, 33) wakati kwa utayari wote tukiikumbatia injili Yake.

Mwanzoni mwa huduma yake, Yesu alisafiri kutoka Galilaya hadi mto Yordani huko Yudea. Yohana Mbatizaji alikuwa huko, akiwafundisha watu kutubu na kubatizwa. Yesu alimtaka Yohana ambatize, lakini Yohana alisita kwa sababu alijua kwamba Yesu hakuwa mdhambi. Mwokozi alifafanua kwamba Alihitaji kubatizwa ili “kutimiza haki yote” (Mathayo 3:15) na kuwa mtiifu wa amri za Baba yetu wa Mbinguni. Hivyo Kristo alionyesha mfano kwetu sote wakati Yeye alipoingia katika maji na Yohana kumbatiza (ona 2 Nefi 31:5).Yohana pia alipokea ushahidi binafsi wa uzoefu huo mtakatifu:

“Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake:

“Na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye” (Mathayo 3:16–17).

Yohana Mbatizaji na Yesu Mtoni Yordani.
Yohana Mbatizaji na Yesu Mtoni Yordani

Baadae, mtawala wa kiyahudi aliyeitwa Nikodemo alimjia Yesu usiku. Alitambua kwamba Yesu alikuwa “mwalimu kutoka kwa Mungu” (Yohana 3:2), na alitaka kujifunza zaidi. Yesu alimfundisha kwamba vyote ubatizo na kumpokea Roho Mtakatifu kupitia uthibitisho vilihitajika kwa ajili ya ukombozi:

“Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuingia ufalme wa Mungu.”(Yohana 3:5).

Kuzaliwa kwa maji humaanisha ubatizo. Kuzaliwa kwa Roho humaanisha kupokea zawadi ya Roho Mtakatifu kupitia uthibitisho. Ibada hizi ni takatifu, na tunafanya maagano matakatifu wakati tunapozipokea. Tunaahidi kwamba tuko radhi kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo na siku zote kumkumbuka, na kushika amri za Mungu. Wakati tunapotimiza ahadi hizi, tunaonyesha imani yetu katika Yesu Kristo na utayari wetu wa kumfuata Yeye.

Baada ya Ufufuko Wake, Mwokozi alifundisha tena umuhimu wa ubatizo. Aliwatuma Mitume kwenda kuhubiri injili Yake kwa watu wote, akisema “yule aaminiye na kubatizwa ataokoka” (Marko 16:16).

Wakati Mwokozi aliporejesha Kanisa Lake kupitia Nabii Joseph Smith, Yeye alifundisha tena kwamba ubatizo bado unahitajika (Mafundisho na Maagano 22:4). Pia alifunua njia sahihi ya kufanya ubatizo. Aliweka wazi kwamba ubatizo lazima ufanyike kwa kuzamishwa na kwa mamlaka sahihi ya ukuhani (Mafundisho na Maagano 20:73–74).

Mungu Anawapenda Watoto Wake wote

Kila mtu ni mtoto wa Mungu. Wote ni wa tahamnai Kwake. Anawajua na Huwapenda wote. Alisema, “Kwa maana tazama, hii ndiyo kazi yangu na utukufu wangu—kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu” (Musa 1:39). Ametoa njia kwa watoto Wake wote ya wao kurudi Kwake baada ya maisha haya. Njia hiyo ni injili ya Yesu Kristo.

Watu wengi wana fursa ya kukubali injili na kubatizwa katika maisha haya. Lakini vipi kuhusu wale ambao walikufa bila kubatizwa au hata kujua kuhusu Yesu? Wanawezaje kuokolewa? Mungu hajawasahau!

Kifo si mwisho wa maisha, lakini ni hatua kwenye safari ya kurejea tena kwa Mungu. Wakati tunapokufa, roho zetu huacha miili yetu kwa muda. Tunaingia kwenye ulimwengu wa roho na kuungana na wanafamilia na wengine ambao pia wamefariki. Huko tunajiandaa kwa ajili ya siku ile ya kupendeza wakati tutakapofufuliwa na roho zetu zitaungana na miili iliyokamilishwa. Kisha tutakuwa huru kutoka maradhi, magonjwa na yote yaletayo ulemavu na udhaifu ambayo tunayastahimili kwa sasa. Katika ulimwengu wa roho, wale ambao walifariki bila kuwa na fursa ya kujifunza injili katika maisha haya wanafundishwa kuhusu Mwokozi na mpango wa wokovu (1 Petro 3:18–20; Mafundisho na Maagano 138:16–19).Wanaweza kuchagua kukubali injili na kutubu.Lakini hawawezi kubatizwa wakiwa huko kwasababu hawana miili yao ya kushikika. Baba yetu mkarimu wa Mbinguni ametoa njia nyingine kwa ajili yao ya kupokea ubatizo.

Hekaluni, tunaweza kubatiza na kuthibitisha kwa niaba ya wale ambao wamefariki bila kuwa na fursa hiyo. Kwa maneno mengine, tunaweza kuwawakilisha na kutenda kwa niaba yao. Ibada zifanywazo kwa niaba ya wengine huitwa Ibada kwa uwakilishi (au ibada kwa uwakilishwaji ). Mtume Paulo aliwafundisha Wakorintho kwamba ubatizo kwa niaba ya wafu ulikuwa ukifanyika kwa sababu watu wote watafufuliwa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo (1 Wakorintho 15:29, 55–57).

Fundisho la ibada kwa uwakilishi mara zote limekuwa sehemu ya injili ya Yesu Kristo. Na hakika, Upatanisho Wake ni kitendo kikuu cha uwakilishi kwenye historia ya ulimwengu. Kupitia dhabihu Yake, Alifanya kwa watu wote ambacho hatuwezi kukifanya sisi wenyewe. Kwa sababu Yake, watu wote watafufuliwa. Wote wataisikia injili, na wote watakuwa na nafasi ya kurudi kwa Wazazi wa kimbingu.

Ubatizo hekaluni na uthibitisho uliofanywa kwa niaba ya wale waliofariki ni zawadi zitolewazo kwa upendo. Na kwasababu tunaamini kwamba maisha huendelea baada ya kifo, tunaamini pia kwamba wale waliofariki wanajua kuhusu ibada. Wanaweza kuchagua kuzikubali au kuzikataa.

kisima cha Ubatizo (Hekalu la Ogden Utah)
kisima cha Ubatizo (Hekalu la Ogden Utah)

Unaweza Kuwatumikia Wengine Hekaluni

Kila hekalu ndani lina sehemu ya kubatizia yenye kisima kikubwa cha ubatizo. Kisima kimejengwa juu ya migongo ya sanamu za maksai kumi na wawili ambao wanawakilisha kabila kumi na mbili za Israeli. Hii imefuata tamaduni ya tangu wakati wa hekalu la Sulemani kwenye Agano la Kale (ona 2 Mambo ya Nyakati 4:2–4). Maksai pia wanawakilisha nguvu na uwezo wa injili ya Yesu Kristo.

Waumini wastahiki wa Kanisa wanaweza kupata kibali cha hekaluni ili kufanya ubatizo na uthibitisho kuanzia Januari ya mwaka ambao wanafikisha miaka 12. Ili kupata kibali cha hekaluni, weka miadi ya “usahili wa kibali cha hekaluni” na askofu wako au rais wa tawi. Kisha unaweza kwenda hekaluni na kubatizwa na kuthibitishwa kwa niaba ya wale ambao wamefariki.

Kama ilivyo kwa ubatizo wako, utakuwa na sehemu ya faragha ya uvaaji nguo ambapo utavalia nguo nyeupe ili kufanya ubatizo kwa niaba ya wale waliofariki. Baada ya ubatizo, utarudi kwenye sehemu yako ya kuvalia na kuvaa nguo kavu. Kisha utaenda kwenye chumba kilichotengwa kwa ajili ya uthibitisho kwenye sehemu ya ubatizo. Wenye ukuhani wataweka mikono yao juu ya kichwa chako na kutunuku zawadi ya Roho Mtakatifu kwa niaba ya wale waliofariki. Baada ya ibada hizi kukamilika, wanaweza kuchagua kama wanatamani kuzikubali. Ubatizo na uthibitisho kwa uwakilishi hufanywa hekaluni pekee.

Chumba cha Uthibitisho (Hekalu la Meridian Idaho)
Chumba cha Uthibitisho (Hekalu la Meridian Idaho)

Hekaluni, pia unaweza kuwa na fursa maalum ya kubatizwa kwa niaba ya wanafamilia yako mwenyewe waliofariki. Unapotafuta kujua historia ya familia yako, utapata mababu zako. Kwenda hekaluni na kubatizwa na kuthibitishwa kwa niaba yao inaweza kuwa uzoefu binafsi wa kupendeza.

Unaweza kutoa huduma hii kwa wazazi, mababu, ndugu, mashangazi, wajomba, binamu na wengine. Familia inaweza kuimarishwa kupitia kitendo hiki cha ukarimu. Unaweza kuhisi kwa kina muunganiko kwenye familia yako na ukaribu na Mungu. Aina hii ya hisia za kuwa sehemu ya inaweza kukupa nguvu, mwelekeo na itakubariki katika njia nyingi zisizo hesabika. Unaweza kupata amani na umaizi kwa ajili ya maisha yako mwenyewe wakati ukitafuta na kuwatumikia mababu zako. Utaelewa na kumjua Mwokozi vizuri zaidi wakati pia ukifanya kwa ajili ya wengine kile ambacho hawawezi kukifanya.

Ahadi Maalum kwa ajili Yako

Mzee David A. Bednar alisema: “Ninawahamasisha kujifunza, kutafuta mababu zenu, na kujitayarisha wenyewe ili kufanya ubatizo kwa uwakilishi katika nyumba ya Bwana kwa ajili ya ndugu zenu waliofariki. … Mnapoitikia kwa imani mwaliko huu, mioyo yenu itawageukia mababu. Ahadi alizopewa Ibrahimu, Isaka na Yakobo zitapandwa katika nyoyo zenu. Upendo wenu na shukrani kwa ajili ya mababu zenu utaongeza. Ushuhuda wenu na kuongoka katika Mwokozi kutakuwa kwa kina na imara. Na ninawaahidi mtalindwa dhidi ya ushawishi uliopamba moto wa adui. Mnaposhiriki na kupenda kazi hii takatifu, mtalindwa … katika maisha yenu yote” (“The Hearts of the Children Shall Turn,” Ensign au Liahona, Nov. 2011, 26–27).