Kuhusu Endaumenti ya Hekaluni

Tunu Yako Binafsi kutoka kwa Mungu

Rais Russell M. Nelson ametukumbusha kwamba “kila shughuli, kila somo, yote tuyafanyayo Kanisani, huelekeza kwa Bwana na nyumba Yake takatifu. Juhudi zetu za kuitangaza injili, kuwakamilisha Watakatifu, na kuwakomboa wafu vyote huongoza hekaluni. Kila hekalu takatifu husimama kama alama ya uumini katika Kanisa, kama ishara ya imani yetu katika maisha baada ya kifo, na kama hatua takatifu kuelekea utukufu wa milele kwa ajili yetu na familia zetu” (“Maandalizi Binafsi kwa ajili ya Baraka za Hekaluni,” Ensign, Mei 2001, 32; Liahona, Julai 2001, 37).

Ni ndani ya hekalu pekee tunaweza kufanya maagano matakatifu ambayo hujumuisha ahadi ya uzima wa milele katika ufalme wa Mungu, ambacho ni “kipawa kikuu katika vipawa vyote vya Mungu.” (Mafundisho na Maagano 14:7). Ibada na maagano ya hekaluni siku zote yamekuwa sehemu ya injili ya Yesu Kristo. Yanaimarisha uhusiano wa kiungu na kutusaidia tufokasi kwa Mwokozi, Upatanisho Wake, na msimamo wetu wa kumfuata Yeye.

Kupokea endaumenti yako ya hekaluni ni uzoefu binafsi. Kujiandaa kwa ajili ya endaumenti huifanya iwe yenye maana zaidi. Waumini wengi wa Kanisa hupokea endaumenti zao kabla ya kwenda misioni au kabla ya ndoa. Wengine wana tamanio kubwa tu la kusonga mbele kwenye njia ya agano. Maaskofu na marais wa matawi wanapaswa kuwahimiza na kushauriana na waumini watu wazima ambao wanatamani kupokea endaumenti yao. Ni muhimu kufahamu kwamba endaumenti yako ni zaidi ya hatua nyingine tu; ni sehemu muhimu na tukufu ya safari yako ya milele.

endaumenti kiuhalisia ni “tunu.” Katika muktadha huu, endaumenti ya hekaluni ni tunu ya baraka za kiungu kutoka kwa Mungu kuja kwa kila mmoja wetu. Endaumenti inaweza kupokelewa katika njia Yake pekee na ndani ya hekalu Lake takatifu. Baadhi ya tunu unazozipokea kupitia endaumenti ya hekaluni hujumuisha:

  1. Ufahamu mkubwa wa madhumuni na mafundisho ya Bwana.

  2. Uwezo wa kufanya yote ambayo Mungu anatutaka tufanye.

  3. Mwongozo wa kiungu na ulinzi kadiri tunavyomtumikia Bwana, familia zetu, na wengine.

  4. Ongezeko la tumaini, faraja na amani.

  5. Baraka zilizoahidiwa sasa na milele.

Waumini wa Kanisa ambao wana angalau umri wa miaka 18 (na wamehitimu shule ya upili au shule ya sekondari) wanaweza kupokea endaumenti yao ya hekaluni ikiwa ni waaminifu na wamejiandaa. Kwa sababu ibada na maagano ya hekaluni ni matakatifu na yana umuhimu wa milele, Bwana ameweka viwango kwa wale wanaotamani kuyapokea. Waumini lazima pia waweze kuelewa majukumu matakatifu watakayoyakubali wakati wanapofanya maagano na Mungu.

Kujiandaa kupokea endaumenti yako kutajumuisha kufuata mafundisho ya Yesu Kristo na kujitahidi kushika maagano uliyoyafanya kwenye ubatizo. Unafanya upya maagano yako kila wakati unapopokea sakramenti. Utapata fursa ya kukutana na askofu wako na kisha rais wako wa kigingi kwa ajili ya usaili wa kibali cha hekaluni. Viwango vya kuingia ndani ya nyumba ya Bwana vitajadiliwa wakati wa usaili. Watakuuliza maswali ambayo yanakuruhusu kushiriki ushuhuda wako wa injili ya Yesu Kristo, manabii Wake walio hai, na Kanisa Lake lililorejeshwa. Majibu yako yatathibitisha kwamba unajitahidi kutii amri za Mungu na kumfuata Yesu Kristo. Rais wako wa kigingi kisha ataweza kukupa kibali cha hekaluni ambacho kitakuruhusu uingie hekaluni na upokee endaumenti yako.

Muhtasari wa Endaumenti

Ulipojiunga na Kanisa, ulipokea ibada mbili—ubatizo na uthibitisho. Vivyo hivyo, endaumenti ya hekaluni pia inapokelewa katika sehemu mbili.

Katika sehemu ya kwanza, kwa faragha na binafsi utapokea kile kinachoitwa ibada za mwanzo. Ibada hizi hujumuisha baraka maalumu zinazohusu urithi wako wa kiungu na uwezekano wako. Kama sehemu ya ibada hizi, pia utaruhusiwa kuvaa gamenti takatifu za hekaluni na kuelekezwa kuzivaa maisha yako yote.

Katika sehemu ya pili, utapokea endaumenti yako iliyobakia katika mpangilio wa kundi. Hii hufanyika kwenye chumba cha maelekezo ukiwa na wengine ambao wanahudhuria hekaluni. Baadhi ya sehemu ya endaumenti huwasilishwa kupitia video na baadhi huwasilishwa na wahudumu wa hekaluni. Wakati wa ibada, matukio ambayo ni sehemu ya mpango wa wokovu huwasilishwa. Yanajumuisha Uumbaji wa ulimwengu, Anguko la Adamu na Hawa, Upatanisho wa Yesu Kristo, Ukengeufu, na Urejesho. Utajifunza pia mengi zaidi kuhusu jinsi watu wote wanavyoweza kurejea kwenye uwepo wa Bwana.

Hekalu la Gilbert Arizona, Chumba cha Endaumenti

Wakati wa ibada ya endaumenti, utaalikwa kufanya maagano mahususi na Mungu. Maagano haya ni:

  • Sheria ya utiifu, ambayo hujumuisha kujitahidi kutii amri za Mungu.

  • Sheria ya dhabihu, ambayo humaanisha kufanya yote tuwezayo kuunga mkono kazi ya Bwana na kutubu kwa moyo uliovunjika na roho iliyopondeka.

  • Sheria ya injili, ambayo ni sheria ya juu ambayo Aliifundisha wakati alipokuwa duniani.

  • Sheria ya usafi wa kimwili, ambayo humaanisha kwamba tunakuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu ambaye tumefunga naye ndoa kisheria na kihalali kulingana na sheria ya Mungu.

  • Sheria ya wakfu, ambayo humaanisha kuweka wakfu muda wetu, vipaji, na kila kitu ambacho Bwana ametubariki nacho ili kulijenga Kanisa la Yesu Kristo dunuani.

Maagano yote yanakusudiwa kuwa ya kuunganisha pamoja. Unapotunza maagano yako na kutubu madhaifu yako, uhusiano wako na Yeye unaimarishwa na Yeye atakubariki kikamilifu zaidi. Uhusiano wako na Mwokozi pia unakuwa wa karibu na wenye maana zaidi. Watunza maagano wanapata kufikia kwa hali ya juu nguvu za Mungu na upendo wa kudumu, amani, faraja, na shangwe. Mungu anaahidi kwamba wale wanaotunza maagano yao watapata fursa ya kurejea kuishi Naye milele.

Rais Russell M. Nelson anafafanua kwamba “Kufanya agano na Mungu hubadilisha uhusiano wetu na Yeye milele. Hutubariki kwa kiasi kikubwa cha upendo na rehema. Huathiri jinsi sisi tulivyo na jinsi ambavyo Mungu atatusaidia tuwe vile tunavyoweza kuwa.” Kwa sababu ya upendo mkarimu wa Mungu kwa wale ambao wamefanya Naye maagano, “Yeye atawapenda. Yeye ataendelea kufanya kazi pamoja nao na kuwapa fursa za kubadilika. Yeye atawasamehe wakati wanapotubu. Na kama watapotoka, Yeye atawasaidia waipate njia yao ya kurudi Kwake” (“Agano la Milele,” Liahona, Oktoba 2022).

Mwisho wa endaumenti, washiriki kwa ishara wanarudi kwenye uwepo kwa Bwana wakati wanapoingia chumba cha selestia. Hapo unaweza kuchukua muda kutafakari, kusali, kusoma maandiko, au kushiriki mawazo yako kimya kimya pamoja na wanafamilia na marafiki. Ni mahala pa amani, ambapo pia unaweza kupata faraja na mwongozo wa kiungu.

Wote wanaoshiriki kwenye endauemnti wanahimizwa kuwa makini kwenye kile kinachofundishwa. Uzoefu wako utakuwa wa kuridhisha zaidi wakati unapokwenda ukiwa na nia ya kufunzwa na Roho Mtakatifu. Usiwe na hofu kuhusu kukumbuka au kuelewa kila kitu kwa mara ya kwanza. Wafanyakazi wa hekaluni daima watakuwepo ili kukusaidia na kukuongoza. Siyo jaribio, bali nafasi ya kuhisi kuwa karibu na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Fokasi kwenye shangwe ya kuwa ndani ya nyumba ya Bwana na misukumo ya kiroho unayoipokea.

Hekalu la Fort Lauderdale Florida, Chumba cha Endaumenti

Songa karibu na Bwana

Endaumenti ya hekaluni ni hatua muhimu kuelekea wokovu na kurejea kwa Baba wa Mbinguni. Pia ni wakati wa kusonga karibu na Yesu Kristo—kumjua vyema na kufuata mfano Wake. Hakika, baraka zote zilizoahidiwa za endaumenti hutegemea uaminifu wetu.

Baada ya kuwa umepokea endaumenti yako binafsi, rejea hekaluni mara nyingi kadiri uwezavyo. Unapofanya hivyo, unaweza kushiriki kwenye ibada za mwanzo na endaumenti kwa niaba ya mababu na wengine ambao wamefariki. Kama ilivyo kwa ibada zingine zote zinazofanywa hekaluni, wale waliofariki wanafahamu juu ya huduma yako na wanaweza kuchagua ikiwa wakubali au wakatae kile kilichofanywa kwa niaba yao.

Ushiriki wako pia unakupa nafasi ya kusikia baraka, maelekezo, na maagano kwa mara nyingine. Unapohudhuria hekaluni, utagundua njia zaidi ambazo kupitia hizo endaumenti inahusiana na mpango wa wokovu na inavyobariki maisha yako. Kile unachojifunza na kuhisi kitakuwa dhahiri zaidi na sahihi zaidi kwako kadiri muda unavyosonga. Unapotembelea hekaluni, utahisi upendo wa Mungu na utakumbushwa juu ya kile kilicho muhimu zaidi.