Jiandae kwa ajili ya Nyumba ya Bwana

Fanya uzoefu wako uwe binafsi zaidi na wenye maana zaidi

Jiandae kwa ajili ya Matembezi Yako ya Hekaluni

Ibada za Hekaluni na Njia ya Agano

“Hekalu ni kitovu cha kuimarisha imani yetu na uimara wa kiroho kwa sababu Mwokozi na mafundisho Yake ndiyo kiini hasa cha hekalu. Kila kitu kinachofundishwa ndani ya hekalu, kupitia maelekezo na kupitia Roho, huongeza uelewa wetu wa Yesu Kristo. Ibada Zake muhimu hutuunganisha Kwake kupitia maagano matakatifu ya ukuhani. Kisha, tunapotunza maagano yetu, Yeye hutubariki kwa nguvu Yake ya uponyaji na ya kuimarisha.” (Rais Russell M. Nelson, “Hekalu na Msingi Wako wa Kiroho,” Mkutano Mkuu, Oktoba 2021)

Kupokea endaumenti ya hekaluni na kutunza maagano ni kipengele muhimu cha msimamo wako wa kumfuata Yesu Kristo. Kunakusaidia pia ujiandae ili siku moja urudi na uishi na Yeye na Baba yetu wa Mbinguni. Unaweza kufanya mengi ili kuhakikisha kwamba uko tayari. Kujifunza injili ya Yesu Kristo na kufanyia kazi mafundisho hayo katika maisha yako vinapaswa kujumuishwa. Kutunza maagano ambayo umekwisha kuyafanya ni muhimu kwa utayari wako wa hekaluni.

Yesu alifundisha, “Njia ni nyembamba, iendayo uzimani, nao waipatao ni wachache” (Mathayo 7:14). Lango tunaloingia ni ubatizo na njia tunayoifuata ni injili Yake. Ubatizo ndiyo ibada ya kwanza ya injili na hatua inayohitajika kwenye njia ya agano ya kurejea kwa Mungu.

Ibada zingine pia zitakuongoza njiani. Hizi ziinajumuisha kumpokea Roho Mtakatifu, kutawazwa kwenye Ukuhani wa Melkizedeki (kwa wanaume), kupokea endaumenti ya hekaluni, na kuunganishwa hekaluni. Ibada hizi takatifu za ukuhani huongoza kwenye baraka kuu ambazo Baba yetu wa Mbinguni huwapa watoto Wake—shangwe ya kuishi pamoja Naye na familia zetu baada ya maisha haya ya duniani.

Unaweza kuhisi wasiwasi au hata kuzidiwa wakati unapojiandaa kwa ajili ya hekalu. Kabla hujatembelea kwa mara ya kwanza, ni kawaida kujiuliza ni vipi sherehe za hekaluni zitakuwa. Baadhi ya mambo yatakuwa mapya kwako, lakini mengi ya yale yanayotokea hekaluni yanapaswa kuwa ya kawaida kwa sababu yote yamejikita juu ya injili ya Yesu Kristo.

Huhitaji kujua au kukumbuka kila kitu wakati unapokwenda hekaluni. Wafanyakazi wa hekaluni daima wapo pale kukusaidia. Watu hawa wanaojitolea wana upendo na ni wakarimu. Wako pale kukusaidia ujisikie kukaribishwa na huru ndani ya nyumba ya Bwana.

Kwa sababu umebatizwa, tayari unafahamu baadhi ya mambo kuhusu ibada na maagano. Unafahamu kwamba yana maana kiishara na kiroho. Kwa mfano, ulijifunza kwamba ubatizo ni ishara ya utakaso na kuzaliwa upya. Ulivalia mavazi meupe na kuingia ndani ya maji. Mwenye ukuhani aliinua mkono wake na kuzungumza maneno ya ibada. Kisha ulizikwa (ulizamishwa) ndani ya maji na kuinuka kama mtu mpya. Ulikuwa safi na mtakatifu na tayari kuishi maisha yako kama mfuasi mwaminifu wa Yesu Kristo. Baada ya kubatizwa, ulipokea kipawa cha Roho Mtakatifu wakati mikono ilipowekwa juu ya kichwa chako.

Ulipobatizwa, ulifanya agano na Mungu. Uliahidi kwamba ulikuwa radhi kujichukulia juu yako jina la Yesu Kristo, daima kumkumbuka, kushika amri Zake, na kumtumikia hadi mwisho. Kama muumini wa Kanisa Lake, kwa ishara unafanya upya maagano yako ya ubatizo na maagano mengine yote wakati unapopokea sakramenti.

Ibada za hekaluni zinafuata mpangilio sawa na huo. Utavalia mavazi meupe, utafunzwa kuhusu mpango wa Mungu, na utashiriki kwenye sherehe ambazo ni takatifu na za ishara. Pia utaahidiwa baraka wakati unapoweka agano la kufuata mafundisho na mfano wa Yesu Kristo.

Kumbuka kila kitu hekaluni kinatuelekeza kwa Mwokozi wetu na Baba yetu wa Mbinguni. Kila kitu kimekusudiwa kuinua na kushawishi.

Mikono Safi na Moyo Mweupe

Katika kitabu cha Zaburi, tunaulizwa, “Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana? Au ni nani atakayesimama katika patakatifu pake? Yeye aliye na mikono safi, na moyo mweupe” (Zaburi 24:3–4). Mlima wa Bwana ni hekalu Lake. Sifa mbili zimetajwa za kuingia—mikono safi na moyo mweupe.

Akizungumza kuhusu kifungu hiki, Mzee David A. Bednar alisema: “Acha nipendekeze kwamba mikono inafanywa kuwa safi kupitia mchakato wa kumvua mtu wa asili na kwa kushinda dhambi na ushawishi mwovu katika maisha yetu kupitia Upatanisho wa Mwokozi. Mioyo hufanywa kuwa myeupe tunapopokea nguvu Zake za kuimarisha za kufanya mema na kuwa bora. Matamanio yetu ya haki na kazi njema, kadiri zilivyo muhimu, haziwezi kamwe kutoa mikono safi na moyo mweupe. Ni Upatanisho wa Yesu Kristo ambao unatoa vyote nguvu za kusafisha na kukomboa ambazo zitatusaidia tushinde dhambi na nguvu za kutakasa na kuimarisha ambazo hutusaidia tuwe bora kuliko vile ambavyo tungekuwa tukitegemea nguvu zetu wenyewe. Upatanisho usio na mwisho ni kwa wote mtenda dhambi na mtakatifu katika kila mmoja wetu” (“Mikono Safi na Moyo Mweupe,” Ensign au Liahona, Nov. 2007,82).

Unapojiandaa kwa ajili ya hekalu, utakutana na askofu wako. Pia utakutana na rais wako wa kigingi, ikiwa unapokea endaumenti yako au unaunganishwa. Kila mmoja wao atafanya usaili wa kibali cha hekaluni. Utaweza kushiriki mawazo na hisia zako pamoja nao, na watatoa ushauri wenye uvuvio. Unapojibu maswali yao, pia utathibitisha kwamba una “mikono safi, na moyo mweupe” Kwa maneno mengine, utasema kwamba unastahili na uko radhi kuingia hekaluni, kushiriki katika ibada takatifu, na kutunza maagano yako.

Maagano Matakatifu Ni Binafsi na Yana Nguvu

Unapopiga hatua kwenye njia ya agano ya hekaluni, utaanza kuwa na shukrani kwa baraka za maagano matakatifu katika maisha yako hata zaidi na zaidi. Haya ni baadhi ya mambo ya kuzingatia kuhusu umuhimu wa maagano:

1. Maagano huongeza kina cha uhusiano wako na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.

Agano mara nyingi hufafanuliwa kama ahadi takatifu kati ya Mungu na watoto Wake. Ingawa ufafanuzi huu ni sahihi, hauko kamili. Agano ni zaidi ya mkataba. Ni msimamo binafsi ambao hufafanua na kuongeza kina cha uhusiano wetu na Mungu. Maagano hutengeneza muunganiko mtakatifu kati ya Mungu na watoto Wake. Maagano huzifanya upya roho zetu, hubadili mioyo yetu, na hutusaidia tuwe tuliounganika pamoja Naye. Kadiri unavyokuwa mwaminifu kwenye maagano yako, kujitolea kwako kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo kutaongezeka. Hisia zako za shukrani zitaongezeka. Uwezo wako wa kupenda na kutumikia utaongezeka. Na baraka zilizoahidiwa hekaluni zitatiririka kwenye maisha yako.

2. Maagano yanakusaidia ufokasi kwenye mambo ambayo ni muhimu zaidi.

Wakati wa maisha yako, utakutana na chaguzi ambazo zinahitaji muda wako, nguvu yako, na rasilimali zako. Chaguzi nyingi nzuri zitashindana na zingine zenye thamani. Je, unachaguaje?

Rais Dallin H. Oaks alifundisha: “Kwa sababu tu jambo ni zuri hiyo si sababu ya kutosha kulifanya. … Baadhi ya mambo ni mazuri kiasi zaidi ya mazuri, na haya ndiyo mambo ambayo yanapaswa kudai kipaumbele cha usikivu katika maisha yetu. … Baadhi ya matumizi ya muda binafsi na wa familia ni mazuri kiasi, na mengine ni mazuri zaidi. Hatuna budi kuacha baadhi ya vitu vizuri ili tuchague vingine ambavyo ni bora au bora zaidi kwa sababu vinajenga imani katika Bwana Yesu Kristo na kuimarisha famila zetu” (“Good, Better, Best,” Ensign au Liahona, Nov. 2007, 104, 107).

Kupitia maagano, Mungu hutusaidia tuelewe kanuni, matendo na ahadi ambazo Yeye anajua ni bora zaidi kwetu. Tunaweza kupata umaizi zaidi juu ya vipaumbele na kufanya chaguzi za hekima wakati tunapofokasi kwanza kwenye ahadi zile takatifu tulizofanya na Mungu.

3. Ibada na maagano ya hekaluni yanakubariki wewe pamoja na wengine.

Wakati unapopokea endaumenti yako au unapounganishwa kwa mwenza au familia yako, utaondoka hekaluni ukiwa na ahadi kutoka kwa Bwana zikielekezwa moja kwa moja kwako. Si tu ahadi zilizofanywa kwa baadhi ya manabii au watu wa kale, bali ahadi zilizofanywa kwako. Unapaswa kutafuta kuzielewa na maana yake katika maisha yako.

Baada ya kuwa umepokea ibada kwa ajili yako, unaweza kurejea hekaluni ili kupokea ibada kwa niaba ya wengine ambao wamefariki. Una jukumu maalumu la kuwatafuta mababu zako na kuhakikisha kwamba wanapokea ibada za hekaluni. Huduma yako itabariki maisha yao na kukukumbusha juu ya ahadi na baraka zako binafsi.

Jitahidi Kukumbuka na Kurejea

Unapojiandaa kushiriki katika ibada za hekaluni, kumbuka kwamba Mungu ni Baba yako wa Milele na Yesu Kristo ni Mkombozi wako. Wanakujua wewe binafsi. Wanakupenda kikamilifu. Unapotunza maagano yako, utabarikiwa katika maisha haya na yajayo.

Je unaweza kukumbuka wakati ulipohisi kuwa karibu sana na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo? Hisia hizo zitaongezeka hekaluni. Hekalu limewekwa wakfu dhidi ya viondoa mawazo, mashinikizo, na ushawishi hasi wa maisha. Katika mahala hapa patakatifu, unakumbushwa kwamba wewe na wapendwa wako mko hapa duniani kwa ajili ya lengo kubwa na takatifu. Utapata amani, faraja, mwongozo, na tumaini kubwa.

Pia utapata kwamba baraka za hekaluni zitaingia moyoni mwako na kuinua nafsi yako. Rejea hekaluni mara nyingi kadiri uwezavyo. Unapofanya hivyo, utaelewa zaidi kuhusu upendo ambao Mungu na Yesu Kristo wanao kwa ajili yako na watu wote. Hata unapokuwa umeondoka hekaluni, Roho Mtakatifu ataendelea kukufundisha. Atakukumbusha juu ya kile ulichopitia, kile ulichohisi, na jinsi unavyoweza kuishi kama Mungu anavyotaka.

Unapojiandaa kwa ajili ya hekalu, kumbuka kwamba Mungu anataka uwe karibu Naye. Yeye ametoa hekalu Lake kama mahala maalumu pa kusonga karibu Naye. Shangwe yako ya milele ni shangwe Yake pia. Yeye ametupatia baraka za hekalu ili kutuongoza turudi Kwake. Omba msaada Wake kadiri unavyojiandaa na shiriki Naye safari yako. Yeye atakuongoza. Atakupa msukumo. Na atakusaidia njiani.