Mkutano Mkuu
Uhusiano Wetu na Mungu
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


Uhusiano Wetu na Mungu

Bila kujali uzoefu wetu duniani unaweza kutaka nini, tunaweza kumtumainia Mungu na kupata shangwe ndani Yake.

Kama Ayubu katika Agano la Kale, katika wakati wa maumivu wengine wanaweza kuhisi kwamba Mungu amewaacha. Kwa sababu tunajua kwamba Mungu anao uwezo wa kuzuia au kuondoa mateso yoyote, tunaweza kujaribiwa kulalamika kama hafanyi hivyo, pengine kujiuliza, “Kama Mungu hatoi msaada ninaouomba, ninawezaje kuwa na imani Kwake?” Wakati mmoja katika majaribu yake makali, Ayubu mwenye haki alisema:

“Jueni basi kuwa Mungu amenipotosha na kunizingira kwa wavu wake.

“Tazama nalia, ‘Udhalimu!’ Lakini sisikiwi; naulilia msaada, wala hapana hukumu.”1

Katika kumjibu Ayubu, Mungu anadai, “Utanitia hatiani mimi ili wewe upate kuwa mwenye haki?”2 Au kwa maneno mengine, “Je, utaniweka mimi kwenye kosa? Utanitia mimi hatiani ili wewe upate kuhesabiwa haki?”3 Yehova kwa nguvu anamkumbusha Ayubu juu ya kuwa Kwake Mwenyezi Mungu na mjua yote, na Ayubu katika unyenyekevu wa kina sana anakubali kuwa yeye hamiliki lolote hata linalokaribia ufahamu, nguvu, na haki ya Mungu na hawezi kusimama katika hukumu ya Mwenyezi:

“Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote,” alisema, “na kwamba hakuna wazo linaloweza kuzuiliwa kutoka kwako.

“… Nimesema maneno nisiyoyafahamu, mambo ya ajabu, nisiyoyajua.

“Kwa sababu hiyo, najichukia nafsi yangu, na kutubu katika mavumbi na majivu.”4

Mwishoni, Ayubu alipata nafasi ya kumwona Bwana, na “Bwana aliubariki mwisho wa Ayubu zaidi kuliko mwanzo wake.”5

Kweli ni upumbavu kwetu sisi kwa kutoona kwetu mbali kibinadamu kudhania kumhukumu Mungu, kufikiri, kwa mfano, “Mimi sina furaha kwa hiyo Mungu lazima atakuwa anafanya kitu kisicho sahihi.” Kwetu sisi, watoto Wake katika mwili wenye kufa tulio katika ulimwengu ulioanguka, ambao tunajua kiasi kidogo sana juu ya yaliyopita, yaliyopo na yajayo, Yeye anasema, “Vitu vyote viko mbele zangu, kwani ninavijua vyote.”6 Yakobo kwa hekima anatutahadharisha: “Msijaribu kumshauri Bwana, lakini mpokee ushauri kutoka mkono wake. Kwani tazama, ninyi wenyewe mnajua kwamba anatoa ushauri juu ya kazi yake yote kwa hekima, na kwa haki, na kwa rehema kuu.”7

Baadhi wanaelewa vibaya ahadi za Mungu kumaanisha kwamba utiifu Kwake huleta matokeo mahususi kwenye ratiba iliyopangwa. Wanaweza kufikiri, “kama nitahudumu misheni kwa bidii, Mungu atanibariki kwa ndoa yenye furaha na watoto,” au “Kama nitaacha kufanya kazi za shule siku ya Sabato, Mungu atanibariki kwa ufaulu mzuri,” au “Kama nitalipa zaka, Mungu atanibariki nipate kazi ile niliyokuwa naitaka.” Kama maisha hayataangukia kwenye njia hii au kulingana na ratiba tarajiwa, wanaweza kuhisi wamesalitiwa na Mungu. Lakini mambo hayako kama utaratibu wa mashine katika uchumi wa kiungu. Hatupaswi kufikiri juu ya mpango wa Mungu kama mashine ya kiulimwengu yenye kujiendesha yenyewe ambapo sisi (i) tunachagua baraka tuitakayo, (ii) tunaingiza jumla ya kiasi kinachotakiwa cha kazi njema, na (iii) oda yetu mara moja inatoka.8

Mungu hakika ataheshimu maagano na ahadi Zake kwa kila mmoja wetu. Hatuhitaji kuwa na hofu kuhusu hilo.9 Nguvu ya Yesu Kristo ya kulipia dhambi—ambaye alishuka chini ya vitu vyote na kisha akapaa juu10 na ambaye ana mamlaka yote mbinguni na duniani11—anahakikisha kwamba Mungu anaweza na atatimiza ahadi Zake. Ni muhimu kwamba tuheshimu na kutii sheria Zake, lakini siyo kila baraka iliyowekwa juu ya utii wa sheria12 imeundwa, kusanifiwa, na kuwekewa muda kulingana na matarajio yetu. Tunafanya kadiri ya uwezo wetu lakini lazima tumwachie Yeye utawala juu ya baraka, zote za muda na za kiroho.

Rais Brigham Young alieleza kwamba imani yake haikujengwa kwenye matokeo au baraka fulani bali kwenye ushahidi wake na uhusiano wake na Yesu Kristo. Alisema: “Imani yangu haipo kwenye Bwana kutenda kazi juu ya visiwa vya bahari, juu ya yeye kuwaleta watu hapa, … wala juu ya upendeleo anaowapa watu hawa au watu wale, wala juu ya ikiwa tumebarikiwa au la, bali imani yangu imewekwa juu ya Yesu Kristo na ufahamu wangu nilioupokea kutoka kwake.”13

Toba na utii wetu, dhabihu zetu, na matendo yetu mema ni muhimu. Tunataka kuwa miongoni mwa wale ambao walielezewa na Etheri kama “daima wakizidi sana kutenda kazi njema.”14 Lakini siyo sana kwa sababu ya hesabu inayotunzwa katika vitabu vya selestia. Mambo haya ni ya muhimu kwa sababu yanatuingiza sisi katika kazi ya Mungu na ndiyo njia ambayo sisi tunashirikiana na Yeye katika kubadilika kwetu sisi wenyewe kutoka kuwa mwanadamu wa tabia ya asili na kuwa mtakatifu.15 Kitu ambacho Baba wa Mbinguni anatupatia sisi ni Yeye Mwenyewe na Mwana Wake, uhusiano wa karibu na wa kudumu pamoja Nao kupitia neema na upatanisho wa Yesu Kristo, Mkombozi wetu.

Sisi ni watoto wa Mungu, tuliosimikwa kwa ajili ya maisha yasiyo na mwisho na uzima wa milele. Hatima yetu sisi ni kuwa warithi Wake, “warithio pamoja na Kristo.”16 Baba yetu yuko tayari kumwongoza kila mmoja wetu kwenye njia ya agano kwa hatua zilizosanifiwa kulingana na mahitaji yetu binafsi na kufumwa kwenye mpango Wake kwa ajili ya kilele cha furaha pamoja na Yeye. Tunaweza kutarajia ongezeko la tumaini na imani katika Baba na Mwana, ongezeko la hisia ya upendo Wao, na faraja na mwongozo endelevu wa Roho Mtakatifu.

Hata hivyo, njia hii haiwezi kuwa rahisi kwa yeyote. Kuna kutakaswa kwingi kunakohitajika ili iwe rahisi. Yesu alisema:

“Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndie mkulima.

“Kila tawi ndani yangu lisilozaa [Baba] huliondoa: na kila tawi lizaalo hulitakasa, ili lizidi kuzaa.”17

Mchakato unaoelekezwa na Mungu wa uondoaji na utakasaji, kwa ulazima, utakuwa wa kuchosha na wakati mwingine wa maumivu. Nikirejelea maelezo ya Paulo, sisi tu warithio pamoja na Kristo; kama ndivyo basi tunateseka pamoja naye, ili tuweze kutukuzwa pamoja naye pia.”18

Kwa hiyo, katikati ya moto huu wa utakasaji, badala ya kumkasirikia Mungu, jisogeze karibu na Mungu. Mlingane Baba katika jina la Mwana. Tembea pamoja na Wao kwa njia ya Roho, siku hadi siku. Waruhusu Wao baada ya muda wadhihirishe uaminifu Wao kwako. Tafuta kwa hakika kuwajua Wao na kwa hakika kujijua wewe mwenyewe.19 Acha Mungu ashinde.20 Mwokozi anatuhakikishia:

“Msikilize yeye aliye mwombezi kwa Baba, anayetetea teto lako mbele zake—

“Akisema: Baba, tazama mateso na kifo chake yeye ambaye hakutenda dhambi, ambaye ulipendezwa naye; tazama damu ya Mwanao iliyomwagika, damu yake yeye ambaye ulimtoa ili upate kutukuzwa;

Kwa hiyo, Baba, wasamehe hawa ndugu zangu [na dada zangu] ambao wanaamini katika jina langu, ili waweze kuja kwangu na kupata uzima wa milele..”21

Zingatia baadhi ya mifano ya wanaume na wanawake waaminifu waliomtumaini Mungu, wakiwa na ujasiri kwamba baraka zake zilizoahidiwa zitakuwa juu yao katika maisha au katika kifo. Imani yao haikuwa juu ya kile ambacho Mungu alifanya au hakufanya katika hali fulani au muda fulani bali katika kumjua Yeye kama Baba yao mwema na Yesu Kristo kama Mkombozi wao mwaminifu.

Wakati Ibrahimu alipokuwa anakaribia kutolewa kama dhabihu na kuhani wa Kimisri wa Elkana, alimlilia Mungu kwa sauti ili amwokoe, na Mungu alimwokoa.22 Ibrahimu aliishi kuwa baba wa waaminifu ambaye kupitia uzao wake familia zote za dunia zingebarikiwa.23 Hapo kabla, juu ya madhabahu haya haya, kuhani huyo huyo wa Elkana alikuwa amewatoa dhabihu wanawali mabikira watatu ambao “kwa sababu ya uadilifu wao … hawangeweza kuisujudia miungu wa mbao au jiwe.”24 Walikufa pale kama mashahidi wa dini.

Yusufu wa kale, aliyeuzwa na kaka zake utumwani akiwa kijana, katika mateso yake alimgeukia Mungu. Hatua kwa hatua, alikuwa maarufu ndani ya nyumba ya bwana wake huko Misri lakini punde maendeleo yake yote yalikatishwa kwa sababu ya tuhuma za uongo za mke wa Potifa. Yusufu angeweza kuwaza, “Kumbe jela ndiyo malipo kwa kutii sheria ya usafi wa kimwili,” lakini badala yake alimgeukia tena Mungu na alistawi hata akiwa gerezani. Yusufu aliteseka kukatishwa tamaa zaidi wakati mfungwa aliyemfanya rafiki, licha ya ahadi yake kwa Yusufu, alisahau yote kuhusu Yusufu baada ya kurejeshwa kwenye nafasi ya uaminifu katika himaya ya Farao. Hatimaye, kama unavyojua, Bwana aliingilia kati kwenye kumweka Yusufu katika nafasi ya juu ya uaminifu na madaraka karibu na Farao, ikimwezesha Yusufu kuwaokoa nyumba ya Israeli na wengine wengi. Hakika Yusufu angeweza kushuhudia “kwamba mambo yote hufanya kazi pamoja kwa wale wampendao Mungu.”25

Abinadi alikuwa amedhamiria kutimiza jukumu lake takatifu. “Namaliza ujumbe wangu,” yeye alisema, “na kisha haijalishi [kile kitakachotokea kwangu], ikiwa kama nitaokolewa.”26 Hakuepushwa kutoka kifo cha kishahidi, lakini kwa uhakika aliokolewa katika ufalme wa Mungu, na mwongofu wake mmoja wa thamani, Alma, akabadilisha mwenendo wa historia ya Wanefi hadi wakati wa ujio wa Kristo.

Alma na Amuleki waliokolewa kutoka gerezani huko Amoniha kama jibu la sala yao na watesi wao wakauawa.27 Mapema, hata hivyo, watesi hawa hawa walikuwa wamewatupa katika moto uwakao wanawake na watoto walioamini. Alma, akishuhudia hali hii ya kutisha kwa uchungu mkubwa alizuiliwa na Roho asitumie nguvu za Mungu ili “kuwaokoa kutokana na ile miale ya moto”28 ili kwamba waweze kupokelewa kwa Mungu katika utukufu.29

Nabii Joseph Smith alinyong’onyea jela huko Liberty, Missouri, akiwa hana nguvu ya kuwasaidia Watakatifu walipokuwa wameporwa na kufukuzwa kutoka majumbani mwao katika majira ya baridi kali. “Ee Mungu, uko wapi?” Joseph alilia. “Ni kwa muda gani mkono wako utazuiliwa?”30 Katika kujibu, Bwana alimwahidi: “Taabu yako na mateso yatakuwa kwa muda mfupi; na kisha kama utavumilia vyema, Mungu atakuinua juu. Wewe bado hujawa kama Ayubu.”31

Mwishoni, Joseph angeweza kutamka pamoja na Ayubu, “Tazama [Mungu] ataniua, lakini nitamtumaini yeye.”32

Mzee Brook P. Hales alisimulia hadithi ya Dada Patricia Parkinson ambaye alizaliwa na uoni wa kawaida lakini katika umri wa miaka 11 akawa kipofu.

Mzee Hales alisimulia: “Nimemjua Pat kwa miaka mingi na hivi karibuni nilimwambia kuwa nilifurahia kwamba yeye daima ana mtazamo chanya na ni mwenye furaha. Alijibu, ‘Sawa, hujawahi kuwa nyumbani pamoja nami, si ndiyo? Huwa nina nyakati zangu. Nimekuwa na mapambano makali ya mfadhaiko, na nimelia sana.’ Hata hivyo, aliongeza, ‘Kuanzia wakati nilipoanza kupoteza uoni wangu, ilikuwa ni ajabu, lakini nilijua kwamba Baba wa Mbinguni na Mwokozi walikuwa pamoja na familia yangu na mimi. Kwa wale wanaoniuliza kama nina hasira kwa sababu ni kipofu, ninawajibu, ‘Ningemkasirikia nani? Baba wa Mbinguni yupo pamoja nami katika hili; siko peke yangu. Yeye yupo pamoja nami wakati wote.’”33

Hatimaye, ni baraka ya uhusiano wa karibu na wa kudumu na Baba na Mwana ndicho tunachotafuta. Inaleta tofauti hii yote na ina thamani ya milele. Tutashuhudia pamoja na Paulo “kwamba mateso ya wakati huu wa sasa [maisha ya duniani] si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.”34 Ninatoa ushahidi kwamba bila kujali uzoefu wetu duniani unaweza kutaka nini, tunaweza kumtumainia Mungu na kupata shangwe ndani Yake.

“Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.

“Katika njia zako zote mkiri Yeye, naye atayanyosha mapito yako.”35

Katika Jina la Yesu Kristo, amina.