Miito ya Misheni
Sura ya 11: Wasaidie Watu Waweke na Watimize Ahadi


“Sura ya 11: Wasaidie Watu Waweke na Watimize Ahadi,” Hubiri Injili Yangu: Mwongozo wa Kushiriki Injili ya Yesu Kristo (2023)

“Sura ya 11,” Hubiri Injili Yangu

Picha
Sitapungukiwa na Kitu, na Yongsung Kim

Sura ya 11

Wasaidie Watu Waweke na Watimize Ahadi

Zingatia Hili

  • Ni kwa jinsi gani kutimiza ahadi kunahusiana na uongofu?

  • Ni kwa jinsi gani kutimiza ahadi kunahusiana na kushika maagano?

  • Ni kwa jinsi gani ninaweza kutoa mialiko ili kuwasaidia watu wakue kiroho na waimarishe imani yao katika Yesu Kristo?

  • Kwa nini ni muhimu kushiriki ushuhuda wa dhati?

  • Ni baraka zipi ninazoweza kuahidi?

  • Ni kwa jinsi gani ninaweza kuwasaidia watu watimize ahadi zao?

Toba, Ahadi, na Uongofu

Kama mmisionari na mfuasi wa Yesu Kristo, unatamani wokovu wa nafsi (ona Mosia 28:3). Mwokozi ni “yule aliye mkuu kuokoa” wale ambao wanashika maagano waliyofanya kupitia kupokea ibada muhimu za ukuhani, wakianza na ubatizo (ona 2 Nefi 31:19). Kutoa mialiko na kuwasaidia watu watimize ahadi kutawaandaa wao kwa ajili ya ubatizo.

Watu wanaokolewa kwa sharti la toba (ona Helamani 5:11). Toba ni kumgeukia Yesu Kristo kikamilifu na kwa dhati. Ahadi ni sehemu muhimu ya toba. Unapowaalika watu waweke ahadi kama sehemu ya ufundishaji wako, unawaalika wao watubu.

Ahadi humaanisha kuchagua njia ya kutenda na kufuatilia uchaguzi huo. Kutenda kwa uthabiti juu ya kweli za injili huongoza kwenye uongofu.

Uongofu ni badiliko katika imani ya mtu, moyo, na maisha katika kukubali na kufuata mapenzi ya Mungu. Ni maamuzi ya ufahamu wa kuwa mfuasii wa Kristo. Uongofu hutokea pale watu wanapoonesha imani katika Kristo, kutubu dhambi zao, kubatizwa, kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, na kuvumilia hadi mwisho. Bwana na manabii Wake wanarejelea badiliko hili kama kuzaliwa tena kiroho (ona Yohana 3:3–5; Mosia 27:25–26).

Upatanisho wa Mwokozi hufanya uongofu uwezekane, na Roho Mtakatifu huleta badiliko kuu la moyo (ona Mosia 5:2; Alma 5:12–14).

Uongofu ni mchakato, siyo tukio. Kuwasaidia watu kuwa walioongoka kwa Yesu Kristo ni kiini muhimu kwenye dhumuni lako la umisionari. Kama unavyoongozwa na Roho, waalike watu waweke ahadi ambazo zitawasaidia wakue kiroho na kuhisi ushawishi wa Roho Mtakatifu katika maisha yao. Kisha wasaidie waheshimu ahadi walizoziweka. Unawasaidia wao kutenda kwa imani kuelekea badiliko la kudumu (ona Mosia 6:3).

Watu ambao wanaheshimu ahadi kabla ya ubatizo wana uwezekano mkubwa wa kufanya na kushika maagano matakatifu hapo baadaye. Unapowafundisha watu kushika ahadi, unawafundisha wao kushika maagano. Kufanya na kushika maagano ni sehemu muhimu ya injili ya Yesu Kristo na mpango wa Mungu kwa ajili ya watoto Wake.

Sura hii inajumuisha miongozo kwa ajili ya kutoa mialiko, kuahidi baraka, kushiriki ushuhuda wako, na kuwasaidia watu watimize ahadi zao ili waweze kuja kwa Mwokozi na kuokolewa.

Picha
wamisionari wakimfundisha mwanamke

Toa Mialiko

Kama mwakilishi wa Yesu Kristo, wewe unawaalika watu wamfuate Yeye na wapokee shangwe ya injili Yake. Unatoa mialiko mahususi kwao ya kufanya mambo ambayo yatajenga imani yao katika Kristo. Kisha unawasaidia watimize ahadi zao.

Mialiko na ahadi ni muhimu kwa ajili ya sababu zifuatazo:

  • Inawasaidia watu waishi kanuni wanazojifunza ili wahisi ushahidi wa kuthibitisha wa Roho.

  • Kutimiza ahadi ni njia mojawapo ambayo watu wanadhihirisha toba (ona Mafundisho na Maagano 20:37).

  • Toba husaidia watu wapate uzoefu wa amani na shangwe ya msamaha wa Mungu. Pia watapata ongezeko la msaada kutoka kwa Mungu kwa ajili ya changamoto zao.

  • Kutimiza ahadi huwaandaa watu kufanya na kushika maagano matakatifu.

  • Unaweza kuwaonesha watu upendo wako na imani yako katika ahadi za Mungu kwa kuwasaidia watu watimize ahadi zao.

Waalike kama Unavyongozwa na Roho

Tafuta mwongozo wa Roho kuhusu ni mialiko ipi itatolewa na lini itatolewa kwao. Fikiria ni mafundisho au fundisho lipi, likieleweka vyema, litamsaidia mtu kukubali mwaliko wako. Mwaliko sahihi katika wakati mwafaka unaweza kuwasukuma watu wafanye mambo ambayo yatajenga imani yao. Vitendo hivi vinaweza kuongoza kwenye badiliko kuu la moyo (ona Mosia 5:2; Alma 5:12–14).

Mialiko unayoitoa inaweza kuwa midogo, kama vile kusoma sura ya maandiko au kuja kwenye mkutano wa sakramenti. Au inaweza kuwa muhimu kama vile kubatizwa. Mialiko inapaswa kuwa sahihi kwa ajili ya pale mtu huyu alipo katika safari yake ya kiroho.

Mialiko inayoongozwa na Roho inamjenga kila mmoja ili kusaidia maendeleo ya mtu kiroho (ona 2 Nefi 28:20; Mafundisho na Maagano 93:12–13). Jiulize, “Ni ahadi zipi mtu huyu anazitimiza? Ni kipi kingine anahitaji kukifanya ili asonge mbele?

Wasikilize wale unaozungumza nao au wale unaowafundisha. Kutokana na kile unachosikia na kuhisi, tafuta mwongozo wa Roho kuhusu ni mialiko ipi itamsaidia kila mtu kuendelea kusonga mbele kuelekea kufanya maagano matakatifu.

Kanuni kwa ajili ya Kutoa Mialiko

Kutoa mialiko huhitaji imani katika Kristo. Kuwa na imani kwamba Yeye atawabariki watu pale wanapoikubali na kuifuatilia mialiko yako.

Watu wana uwezekano mkubwa wa kubadilika wakati unapowaalika watende juu ya ukweli wa injili na kuwasaidia waone jinsi badiliko hili litakavyowabariki. Watabadilika kwa kiwango ambacho watamhisi Roho na kupata uzoefu wa shangwe ya kuishi injili ya Yesu Kristo.

Wakati wowote unapochangamana na watu, ana kwa ana au mtandaoni, fikiria ni mwaliko upi ungeweza kuwasaidia waimarishe imani yao katika Kristo na wamhisi Roho. Wakati mwingine hii inaweza kuwa rahisi kama vile kukutana na wewe tena au kuja kwenye shughuli ya Kanisa.

Unapojiandaa kufundisha somo, fikiria mahitaji na maendeleo ya kila mtu. Hakikisha mpango wako wa somo unajumuisha mwaliko mmoja au zaidi ambayo itamsaidia mtu apige hatuaa.

Kuwa makini usitoe mialiko mingi sana kwa wakati mmoja. Mtu anahitaji muda wa kutenda, kukua, na kujifunza kutokana na kila mwaliko.

Kuwa shapavu lakini usizidishe wakati unapowaalika watu waweke ahadi (ona Alma 38:12). Heshimu haki ya watu ya kujiamulia.

Kujifunza Maandiko

Kwa nini ahadi ni muhimu?

Alika kwa Lugha ya Upole na ya Wazi

Mwaliko mara nyingi unakuwa kwenye mfumo wa swali la “je, uta,” ambalo linahitaji jibu la ndiyo au hapana. Fanya mialiko yako iwe ya upole, mahususi, na ya wazi. Inapaswa kuwaalika au kuwaongoza watu waweke ahadi ya kutenda kwa imani katika Yesu Kristo.

Ingawa mialiko yako itakuwa ya kipekee kwa kila mtu, fikiria mifano ifuatayo:

  • Kuhudhuria kanisani hutoa muda na nafasi kwa ajili ya kumwabudu Mungu na kumhisi Roho Wake. Kunaweza pia kukusaidia uwe sehemu ya jamii yenye msaada pale unapofanya mabadiliko ya kuja karibu na Mwokozi. Je, utahudhuria pamoja nasi kwenye mkutano wa sakramenti Jumapili hii?

  • Sasa kwa vile tumejadili umuhimu wa kujifunza maandiko, je, utasoma [kifungu mahususi cha maandiko]? Je, utaandika misukumo yoyote au maswali unayoweza kuwa nayo? Tunaweza kujadili mawazo yako wakati ujao tutapokutana.

  • Tumekuwa tukijadili maisha ya Mwokozi na amri Zake. Je, utafuata mfano Wake kwa kubatizwa katika Kanisa Lake na kuweka ahadi pamoja na Yeye? (Ona “Mwaliko wa Kubatizwa na Kuthibitishwa” katika sura ya 3.)

  • Ulionesha hamu katika kuunganika zaidi na Mungu katika maisha yako. Je, utasali kwa imani katika siku chache zijazo ili uweze kupata uzoefu wa baraka za sala?

  • Tuna video ambayo tunadhani itakuwa na msaada kwako. Je, tunaweza kukuonesha au kukutumia kiungo? Je, utaitazama? Je, tunaweza kukujulia hali kesho ili kuona kile unachofikiria?

Tafuta misukumo ya Roho Mtakatifu wakati unapofikiria njia za asili za kutoa mialiko ya upole, mahususi, na ya wazi.

Kujifunza Binafsi au na Mwenza

Katika shajara yako ya kujifunza, andika mwaliko ambao ni rahisi, wa moja kwa moja, na wa wazi kwa ajili ya kila hadi katika somo. Kama umeshafanya shughuli hii hapo awali, irudie na ulinganishe mialiko yako mipya na ile ya awali.

Ipitie tena mialiko uliyoiandika pamoja na mwenza wako. Kisha jadilini maswali yafuatayo:

  • Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwasaidia watu waelewe baraka za Bwana zilizoahidiwa zinahusiana na mwaliko huu?

  • Kwa nini mwaliko huu ni muhimu kwangu binafsi?

  • Ni kwa jinsi gani ninaweza kuwasaidia watu wahisi upendo wa Mungu kwa ajili yao pale ninapotoa mialiko?

  • Ni kwa jinsi gani ninaweza kujiboresha katika kuwaalika wengine watendee kazi mialiko niliyoitoa?

Fikiria juu ya mtu unayemfundisha. Fanya mazoezi ya kutoa mialiko hii kama vile unazungumza na mtu huyu. Rekebisha mialiko yako kama inavyohitajika.

Waahidi Watu Baraka

Mungu anaahidi kutubariki kama tutazishika amri Zake (ona Mafundisho na Maagano 130: 20–21). Watu ambao wanashika amri na kubakia waaminifu “watabarikiwa katika vitu vyote” na “kukaa na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho” (Mosia 2:41).

Unapowaalika watu waweke ahadi, waahidi baraka za kutimiza ahadi hizo. Unaweza kutambua nyingi kati ya baraka hizi kwa kujifunza maandiko, mafundisho ya manabii wa siku za mwisho, na masomo katika sura ya 3. Fikiria pia baraka katika maisha yako mwenyewe. Kwa sala amua ni baraka zipi za kumwahidi kila mtu wakati unapotoa mialiko.

Unapomualika mtu kuishi amri, fundisha yafuatayo:

  • Kutii amri huonesha upendo wetu kwa Baba wa Mbinguni na Mwanaye, Yesu Kristo (ona Yohana 14:15).

  • Kutii amri humwonesha Mungu kwamba tunamtumainia Yeye (ona Mithali 3:5–6).

  • Baraka za Mungu ni za kiroho na kimwili (ona Mosia 2:41).

  • Baraka kuu ya Mungu ni uzima wa milele (ona Mafundisho na Maagano 14:7).

  • Tunaposali kwa uaminifu na kutenda kwa imani, Mungu atatusaidia tutimize mambo ambayo Yeye anatuamuru tufanye (ona 1 Nefi 3:7).

  • Mungu hutimiza ahadi Zake za kutubariki sisi kulingana na njia Yake na wakati Wake (ona Mafundisho na Maagano 88:68).

Watu kila mara watakabiliwa na upinzani katika kuzishika amri. Wasaidie wale unaowafundisha, na wahakikishie kwamba Mungu atawabariki kadiri wanavyojitahidi kutenda mapenzi Yake. Wasaidie waelewe kwamba upinzani ni fursa za kukua kwa kuchagua kumfuata Kristo hata wakati ni vigumu (ona 2 Nefi 2:11, 13–16).

Mzee Jeffrey R. Holland alifundisha: “Baadhi ya baraka huja mapema, baadhi huchelewa, na baadhi haziji mpaka mbinguni; lakini kwa wale wanaoikumbatia injili ya Yesu Kristo, zinakuja” (“Kuhani Mkuu wa Vitu Vizuri Vijavyo,” Ensign, Nov. 1999,38).

Kujifunza Maandiko

Ni kipi maandiko yafuatayo yanakifundisha kuhusu hamu ya Bwana ya kutubariki sisi?

Kujifunza Binafsi

Soma Mafundisho na Maagano 82:10 na 130:20–21. Kisha jifunze maandiko yafuatayo. Tengeneza safu mbili katika shajara yako ya kujifunzia. Kwenye upande mmoja, andika amri unayoipata katika kila kifungu. Kwenye upande mwingine, andika ahadi kwa kushika amri.

Shiriki Ushuhuda Wako

Shiriki ushuhuda wako wakati wowote unapotoa mwaliko na kuahidi baraka. Sema jinsi gani wewe umebarikiwa wakati ulipoishi kanuni unayoifundisha. Shiriki ushuhuda wako kwamba kanuni hii itabariki maisha ya mtu kama yeye ataiishi.

Ushuhuda wako wa uaminifu utasaidia kujenga mazingira kwa ajili ya watu kumhisi Roho Mtakatifu akithibitisha ukweli. Hii itawatia moyo waikubali mialiko unayoitoa.

Kwa maelezo zaidi, ona “Shiriki Ushuhuda Wako” katika sura ya 10.

Picha
kundi likisali

Wasaidie Watu Waweke na Watimize ahadi

Wakati watu wanapoikubali mialiko yako ya kufanya kitu fulani, fuatilia ili kuwasaidia watimize ahadi zao. Unawasaidia watu wakuze imani katika Kristo. Wajibu wako ni kuwasaidia watu waimarishe imani yao na azimio lao la kuendelea mbele hadi uongofu kamili. Usiwaalike watu kubadilika tu; wasaidie wafanye hivyo.

Watu watapokea ushahidi wa Roho pale wanapoonesha imani iongozayo kwenye toba kwa kutimiza ahadi. Ushahidi huu mara nyingi hauji “mpaka baada ya jaribu la imani [yao]” (Etheri 12:6). Usishangae wakati upinzani unapoibuka. Panga jinsi utakavyowasaidia wavuke majaribu ili waweze kupokea ushahidi wa Roho. Waumini wengine wa Kanisa wanaweza pia kutoa msaada.

Watu mara nyingi wanahisi ushawishi wa Roho wakati unapokuwa pamoja nao. Himiza umuhimu wa kusali, kusoma maandiko, na kufuatilia mialiko yako ili wapate hisia hizi wakati wanapokuwa peke yao.

Kutimiza ahadi huwaandaa watu kwa ajili ya ibada na maagano katika njia ya uongofu wa maisha yote. Juhudi zako zinaweza kuwasaidia wao “wadhihirishwe kwa matendo yao” hamu yao ya kumfuata Yesu Kristo (Mafundisho na Maagano 20:37).

Picha
wanawake wakikumbatiana

Panga Kuwasiliana kwa Muda Mfupi Kila Siku

Kuwasaidia watu washike amri huanza wakati unapowatembelea na kuwafundisha kwa mara ya kwanza. Waombe waandike ahadi yao kwenye simu zao, kalenda, au kitu ambacho unawaachia.

Uliza kama wewe, au muumini ambaye amekuwa akishiriki, mnaweza kufanya mawasiliano mafupi kila siku kati ya matembezi ya ufundishaji. Eleza kwamba lengo la mawasiliano haya ni kuwasaidia, na eleza baadhi ya njia unazoweza kufanya hivyo. Haya mawasiliano ni njia moja ya kutumia kanuni iliyo katika Mafundisho na Maagano 84:106.

Amua mbinu ya mawasiliano ambayo inaweza kufaa zaidi, kama vile matembezi mafupi, simu, ujumbe wa maandishi, au ujumbe wa mitandao ya kijamii. Teknolojia hutoa njia nyingi kwa ajili ya ukumbusho na msaada wa ziada.

Wahimize na Uwasaidie Watu katika Mawasiliano Yako ya Kila Siku

Kwa kila mwaliko unaoutoa, andika muhtasari katika app ya Hubiri Injili Yangu kuhusu jinsi utakavyoufuatilia siku inayofuata. Unapopanga siku inayofuata, tafuta mwongozo wa Roho pale mnapojadili jinsi ya kuwasaidia watu watimize ahadi zao.

Fanya mawasiliano yako ya kila siku na watu yawe chanya na ya kutia moyo. Sali kwa ajili yao. Onesha upendo na uelewa wakati unapowasaidia watimize ahadi zao. Jibu maswali na wasaidie washinde changamoto. Kama kuna muda, someni pamoja kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni. Shiriki vyombo vya habari husika vya Kanisa, ikijumuisha muziki uliozalishwa na Kanisa ambao ungeweza kuwainua. Heshimu muda na matakwa yao.

Watambulishe kwa waumini wengine wa Kanisa. Inapokuwa sahihi, waombe waumini wawasaidie watu watimize ahadi zao (ona sura ya 10).

Wapongeze watu ambao wanafanya bidii kutimiza ahadi zao. Wasaidie waone jinsi gani Bwana anavyopendezwa na juhudi zao. Watu hawa wanabadilisha maisha yao, jambo ambalo huhitaji kazi kubwa sana na subira. Wasaidie watambue baraka wanazozipokea. Onesha imani kwamba wanaweza kufanikiwa.

Pia onesha upendo kama watu hawajatimiza ahadi zao. Jitolee kuwasaidia wakati wa mawasiliano yako ya kila siku. Kwa mfano, kama mtu alikubali mwaliko wa kusoma sura katika Kitabu cha Mormoni lakini bado hajafanya hivyo, jitolee kuisoma pamoja naye. Msaidie mtu agundue kwa uzoefu jinsi gani kutimiza ahadi kunaweza kubariki maisha yake.

Inaweza kuchukua majaribio mengi kwa watu kutimiza ahadi, na wewe unaweza kuhitaji kufanya matembezi kadhaa ili kuwasaidia. Jadili jinsi wanavyoweza kushinda changamoto za kutimiza ahadi. Kuwa na subira na mwenye kusaidia, siyo mwenye kukosoa au kuhukumu.

Kuwa na Ushawishi wa Roho Mtakatifu katika Mawasiliano Yako ya Kila Siku

Wakati unapowafuatilia watu, waombe washiriki uzoefu wao wa kutimiza ahadi. Uliza kile walichojifunza na kuhisi. Hii itawasaidia wagundue ushawishi wa Roho katika maisha yao na wabainishe hatua inayofuata.

Unapowasiliana na watu kila siku, sehemu muhimu ya dhumuni lako ni kualika ushawishi wa Roho Mtakatifu katika maisha yao. Wasaidie wagundue jinsi ya kumhisi Roho wakati wewe haupo. Mawasiliano yako ya kila siku yanapaswa kuimarisha hisia za kiroho walizohisi wakati ulipowafundisha. Wataongoka kadiri wanavyohisi nguvu na ushawishi wa Roho Mtakatifu.

Onesha Upendo

Mchakato wa uongofu ni kiini cha upendo kama wa Kristo (ona 4 Nefi 1:15). Tafuta kipawa cha hisani. Kuonesha upendo kwa uaminifu kunaweza kuwasaidia watu wamhisi Roho katika maisha yao. Dhihirisho lako la upendo linaweza pia kuwasaidia wakubali mialiko na kutimiza ahadi ambazo zinaongoza kwenye uongofu.

Unapowapenda na kuwafundisha wengine, uongofu wako mwenyewe kwa Mwokozi utaongezeka.

Kusaidia uongofu wa mtu mwingine ni kazi takatifu. Utapata shangwe ya kudumu pale unapojitolea katika kazi na kuwatumikia wengine (ona Mathayo 10:39; Mosia 2:17; Alma 27:17–18; Mafundisho na Maagano 18:10–16).

Kujifunza Binafsi au na Mwenza

Andika katika app ya Hubiri Injili Yangu mipango yako ya kila siku ya kuwasiliana na kila mtu unayemfundisha. Panga siku kadhaa kabla kile utakachofanya ili kumfuatilia kila mmoja.

Chagua mwaliko mmoja utakaoutoa wakati unapomfundisha kila mtu. Kisha tambua mashaka tofauti tofauti ambayo yangeweza kumzuia mtu kuikubali ahadi au kuitimiza. Jadili na ufanyie mazoezi jinsi unavyoweza kuwasaidia vyema watu pale wanapofanya bidii kutatua wasiwasi wao.

Bwana Anatamani Watu Waje na Kubakia

Kazi ya umisionari ina athari zake kuu pale watu wanapoweka na kutimiza ahadi ya kuishi injili na kubakia washiriki hai katika Kanisa maisha yao yote. Haitoshi tu wao kuja Kanisani. Bwana anatamani kwamba waje na kubakia (ona Yohana 15:16). Elekeza ufundishaji wako wote na mialiko kuelekea mwisho huo. Ili kupokea baraka zote ambazo Baba wa Mbinguni anazo kwa ajili yao, waumini lazima waendelee kuishi injili kwa kushika amri na maagano waliyofanya wakati wanapokuwa washiriki hai Kanisani.

Nefi alifundisha: “Baada ya kuingia katika njia hii nyembamba na iliyosonga, nitauliza kama yote yamekamilishwa? Tazama, nawaambia, Hapana; … lazima msonge mbele mkiwa na imani imara katika Kristo, … na [ikiwa] mtavumilia hadi mwisho, tazama, hivi ndivyo asema Baba: Mtapokea uzima wa milele” (2 Nefi 31: 19–20).

Toa juhudi zako bora ili kuwasaidia watu wastahili kwa ajili ya“uzima wa milele, kipawa ambacho ni kikuu mno katika vipawa vyote vya Mungu” (Mafundisho na Maagano 14:7).


Mawazo kwa ajili ya Kujifunza na Kutumia

Kujifunza Binafsi

  • Tambua amri kutoka kwenye somo la 4. Tafuta na andika marejeo ya maandiko na nukuu kutoka kwa manabii wa siku za mwisho ambazo zinaelezea baraka zilizoahidiwa zinazohusiana na amri hii. Fikiria baraka ambazo wewe ulizipokea kwa kutii amri hii, na uziandike kwenye shajara yako.

  • Unapowasiliana na familia yako au wengine, waulize jinsi walivyobarikiwa kwa kutii amri mahususi (kwa mfano, kuitakasa siku ya Sabato, kutii sheria ya zaka, au kuishika amri ambayo ni ngumu kwa mtu unayemfundisha).

  • Majibu yafuatayo yanaweza kukusaidia utambue maeneo ambayo unaweza kuboresha wakati unapotoa mialiko. Tengeneza mipango ya kujiboresha.

    • Je, watu wanajua kwamba ninawapenda?

    • Je, mimi nina imani kwamba watabarikiwa kwa kutenda juu ya mialiko yetu?

    • Je, ninatoa muda na usikivu unaofaa kufanya mawasiliano ya kila siku na watu ili kuwasaidia watimize ahadi zao?

    • Je, mipango yetu ya masomo inajumuisha mialiko mahususi ya kutenda?

Kujifunza pamoja na Mwenza na Kubadilishana Mwenza

  • Rejeleeni mialiko katika mojawapo ya masomo ya mmisionari. Kwa kila mwaliko, jibuni maswali yafuatayo:

    • Ni baraka zipi Bwana ameahidi kwa wale wanaotimiza ahadi hii?

    • Ni kwa jinsi gani kutii kanuni hii kutawasaidia watu waongeze imani yao na ushuhuda wao?

    • Ni kwa jinsi gani ahadi hili itawasaidia watu watubu na wawe wasikivu zaidi kwa Roho?

  • Kutoka kwenye zana zako za kufanya mipango, tengeneza orodha ya watu uliowasiliana nao katika siku mbili zilizopita. Jumuisha wale unaowafundisha na waumini.

    • Kwa ajili ya kila mtu, andika mialiko uliyoitoa na ahadi walizoweka.

    • Fikiria ni mialiko ipi mingine ungeweza kuitoa.

    • Jadili ni kwa nini uliweza kufuatilia mialiko hii kutoka kwa baadhi ya watu hawa lakini si kutoka kwa wengine.

    • Je, utafanya nini ili kufuatilia mialiko hii?

Baraza la Wilaya, Mikutano ya Kanda na Baraza la Uongozi la Misheni

  • Jadili mawazo yanayofaa na ya ubunifu kwa ajili ya mawasiliano na watu unaowafundisha. Ni kwa jinsi gani wamisionari walifanya kazi na waumini kwa tija? Ni vyombo gani vya habari vilivyochapishwa au vya kijidigitali vina msaada? Ni kipi unaweza kufanya wakati watu hawako nyumbani au wana shughuli nyingi kiasi cha kutoweza kukuona?

  • Jadili njia ambazo wamisionari kwa ufasaha wamefundisha amri zilizoko katika somo la 4.

Viongozi wa Misheni na Washauri wa Misheni

  • Wakati inapowezekana, andamana na wamisionari wakati wanapofundisha. Wasaidie wafokasi katika kuwasaidia watu waweke na watimize ahadi.

  • Wahimize viongozi wa ukuhani wa kata, viongozi wa makundi, na waumini wafanye mawasiliano ya kila siku na watu wanaofundishwa na wamisionari—kama watu wameyakubali mawasiliano haya.