Mkutano Mkuu
Wafuasi wa Mfalme wa Amani
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Wafuasi wa Mfalme wa Amani

Tunapojitahidi kukuza tabia kama za Mwokozi, tunaweza kuwa vyombo vya amani Yake katika ulimwengu.

Katika kutimiza unabii uliotolewa na Zekaria,1 Yesu kwa shangwe aliingia Mji Mtakatifu akiwa juu ya punda, kitu kilichochukuliwa kuwa “alama ya kale ya ufalme wa Kiyahudi,”2 sifa iliyomfaa Mfalme wa wafalme na Mfalme wa Amani.3 Yeye alizungukwa na kusanyiko la wafuasi wenye furaha ambao walitandaza mavazi yao, matawi ya mitende, na majani ya aina nyingine kwenye njia ambayo Yesu alipita. Walimsifu Mungu, wakisema kwa sauti kuu, “Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu.”4 Na tena, “Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni.”5 Tukio hili kuu, tunalolisherehekea katika siku hii ijulikanayo kama Jumapili ya Matawi, ni utangulizi wa shangwe kuelekea matukio ya kutisha ambayo yangetokea katika wiki hiyo yakikamilishwa na dhabibu isiyo ya ubinafsi ya Mwokozi na muujiza mkuu wa kaburi tupu.

Kama wafuasi Wake, tu watu Wake wa kipekee, tulioitwa kutangaza wema Wake,6 wakuzaji wa amani ambayo kwa ukarimu ilitolewa kupitia Yeye pamoja na dhabihu Yake ya kulipia dhambi. Amani hii ni zawadi iliyoahidiwa kwa wote wanaogeuza mioyo yao kuelekea kwa Mwokozi na kuishi kwa haki; amani hiyo hutupatia nguvu ya kushangilia maisha haya na kutusaidia tuvumilie majaribu machungu ya safari yetu.

Mnamo mwaka 1847, Bwana alitoa maelekezo maalumu kwa Watakatifu waanzilishi ambao walihitaji amani ili kubakia watulivu na wamoja walipokuwa wakipitia magumu yasiyotarajiwa katika safari yao kuelekea magharibi. Miongoni mwa vitu vingine, Bwana aliwaamuru Watakatifu “acheni kugombana ninyi kwa ninyi; acheni kuneneana vibaya.”7 Maandiko yanathibitisha kwamba wale wanaotenda matendo ya haki na kujitahidi kutembea katika unyenyekevu wa Roho wa Bwana wanaahidiwa amani wanayoihitaji katika siku za vurugu ambazo tunaishi leo.8

Kama wafuasi wa Mfalme wa Amani, tumeamriwa kuishi “mioyo ikiwa imefumwa pamoja katika umoja na kwa upendo.”9 Nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, amesema hivi karibuni, “Mizozo hukiuka kila kitu ambacho Mwokozi alikisimamia na kufundisha.”10 Nabii wetu pia ametusihi kwamba tufanye yote tuwezayo kumaliza migogoro binafsi ambayo kwa sasa inapamba moto mioyoni mwetu na katika maisha yetu.11

Hebu tutazame kanuni hizi tukirejelea upendo msafi wa Kristo kwa ajili yetu, kwamba kama wafuasi Wake, tunatafuta kuwa nao kwa kila mmoja. Maandiko yanafafanua aina hii ya upendo kama hisani.12 Tunapotafakari juu ya hisani, kawaida akili zetu hugeukia matendo ya ukarimu na matoleo ili kupoza mateso ya wale wanaopitia magumu ya kimwili, umasikini na kihisia. Na bado, hisani haihusiani tu na kitu tunachotoa kwa mtu mwingine, bali ni sifa ya Mwokozi na inaweza kuwa sehemu ya tabia yetu. Si ya kushangaza kwamba Bwana ametuamuru kujivika wenyewe “kwa kifungo cha hisani, … ambacho ni kifungo cha ukamilifu na amani.”13 Bila hisani, sisi si kitu,14 na hatuwezi kurithi mahali ambapo Bwana ameandaa kwa ajili yetu katika makazi ya Baba yetu ya wa Mbinguni.15

Yesu kwa ukamilifu alionyesha kile inachomaanisha kumiliki kifungo hiki cha ukamilifu na amani, hasa wakati wa matukio machungu yaliyotangulia kifo Chake cha kishahidi. Fikiria kwa muda kuhusu kile ambacho Yesu alikihisi wakati kwa unyenyekevu akiiosha miguu ya wanafunzi wake, akijua kwamba mmoja wao atamsaliti usiku huo.16 Au wakati Yesu, masaa kadhaa baadaye, kwa huruma alipoponya sikio la mmoja wa watu walioandamana na Yuda, msaliti Wake, ili wamkamate Yeye.17 Au hata wakati Mwokozi, akiwa amesimama mbele ya Pilato, akishitakiwa pasipo haki na makuhani wakuu na wazee, na hakujibu hata neno moja dhidi ya mashitaka ya uongo dhidi Yake, na akimwacha gavana wa Kirumi akishangaa.18

Kupitia matukio haya matatu, Mwokozi, licha ya huzuni kuu na taabu, alitufundisha kwa mfano Wake kwamba “upendo huvumilia, hufadhili; … hauhusudu; … hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu, [na] hauhesabu mabaya.”19

Jambo jingine la muhimu la kutilia mkazo, na lenye matumizi ya moja kwa moja katika ufuasi wetu na jinsi tunavyokuza amani ya Mwokozi, ni jinsi tunavyojaliana sisi kwa sisi. Wakati wa huduma yake hapa duniani, mafundisho ya Mwokozi yalifokasi—sio tu, lakini hasa—kwenye sifa za upendo, hisani, subira, unyenyekevu na huruma—sifa za msingi kwa wale wanaotaka kuwa karibu Naye na kukuza amani Yake. Sifa hizo ni zawadi kutoka kwa Mungu, na tunapojitahidi kuzikuza, tutaanza kuona tofauti na mapungufu ya jirani yetu kwa huruma zaidi, utayari, heshima na ustahimilivu. Moja ya alama dhahiri kabisa ya kwamba tunasonga karibu na Kristo na kuwa zaidi kama Yeye ni jinsi tunavyowajali wengine kwa upendo, subira na wema, katika hali zozote zile.

Mara nyingi tunawaona watu wanajihusisha na maoni hasi na hata ya dharau kuhusu tabia, udhaifu na mawazo ya wengine, hasa wakati tabia hizo na mawazo zinapotofautiana au kukinzana na jinsi wao wanavyotenda au kuwaza. Ni kawaida kuwaona watu hawa wakisambaza maoni hayo kwa wengine, ambao hurudia kile walichosikia pasipo kwa dhati kujua hali zote zihusianazo na tukio hilo. Kwa bahati mbaya, mitandao ya kijamii huhimiza tabia hii katika jina la ukweli kulingana na mambo yalivyo na uwazi. Pasipo kujizuia, mazungumzo ya kidijitali mara nyingi huwaongoza watu kwenye kushambulia kwa maoni na mizozo mikali, kutengeneza kuvunjika moyo, kujeruhi mioyo na kusambaza uadui mkubwa.

Nefi alitoa unabii kwamba katika siku za mwisho, adui ataghadhibika na kuchochea watu kukasirika dhidi ya kile kilicho chema.20 Maandiko yanafundisha kwamba “kila kitu kinachokaribisha na kushawishi kufanya mema, na kumpenda Mungu, na kumtumikia, ni mwongozo kutoka kwa Mungu.”21 Kwa upande mwingine, “kile kilicho kiovu hutoka kwa ibilisi; kwani ibilisi ni adui wa Mungu, na hupigana dhidi yake siku zote, na hukaribisha na hushawishi kufanya dhambi, na kufanya kile kilicho kiovu siku zote.”22

Ukitafakari fundisho hili la kinabii, haishangazi kwamba moja ya mbinu za adui ni kuchochea uadui na hasira katika mioyo ya watoto wa Mungu. Anashangilia anapowaona watu wakikosoana, kufanyiana dhihaka na kutoleana kashifa. Tabia hiyo inaweza kuangamiza sifa ya mtu, heshima na kujithamini, hasa tunapomhukumu mtu pasipo haki. Ni muhimu kutambua kwamba tunaporuhusu aina hii ya mtazamo katika maisha yetu, tunatengeneza nafasi katika mioyo yetu kwa ajili ya adui kupanda mbegu ya mifarakano miongoni mwetu, kuhatarisha kuangukia katika mtego wake hatarishi.

Kama hatutakuwa makini kwenye fikra zetu, maneno, na matendo yetu, tunaweza kuishia kwenye kukamatwa na njama za ujanja za adui, kuharibu mauhusiano yetu na watu wanaotuzunguka na wapendwa wetu.

Akina kaka na akina dada, kama watu wa kipekee wa Bwana na wadhamini wa amani Yake, hatuwezi kukubali kuruhusu hizi njama za adui kupata nafasi katika mioyo yetu. Sisi hatuwezi kubeba mzigo haribifu ambao huharibu hisia, mahusiano na hata maisha. Injili huwakilisha habari njema ya shangwe kuu.

Bila shaka, hakuna yeyote kati yetu aliye mkamilifu, na hakika, kuna nyakati tunadanganyika na kuingia kwenye aina hii ya tabia. Katika upendo Wake mkamilifu na kwa Yeye kujua yote kuhusu hali zetu za kibinadamu, Mwokozi daima anajaribu kutuonya dhidi ya hatari hizo. Alitufundisha, “Kwani kwa hukumu mnayohukumia, mtahukumiwa nayo; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa tena.”23

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, tunapojitahidi kukuza tabia kama za Mwokozi, tunaweza kuwa vyombo vya amani Yake katika ulimwengu kulingana na mfumo ambao Yeye mwenyewe ameuweka. Ninawaalika kutafakari njia ambazo sisi wenyewe tunaweza kubadilika na kuwa watu wenye kuinua na kusaidia, watu wenye moyo wa kuelewa na kusamehe, watu wanaoangalia mazuri ya wengine, daima tukikumbuka kwamba “kama kuna kitu chochote kilicho chema, chenye kupendeza, au chenye taarifa njema au chenye kustahili sifa, tunayatafuta mambo haya.”24

Ninawaahidi kwamba tunapotafuta na kukuza tabia hizi, tutakuwa wakunjufu zaidi na zaidi na walio tayari kujali mahitaji ya wanadamu wenzetu25 na tutapata shangwe, amani na ukuaji wa kiroho.26 Bila shaka, Bwana atatambua juhudi zetu na kututunukia vipawa tunavyohitaji ili kuwa wenye kustahimili na wenye subira zaidi kwenye mapungufu na madhaifu ya kila mmoja wetu. Zaidi ya hayo, tutakuwa wazuri zaidi kuweza kuhimili hali ya kukosewa au kuwakosea wale wanaotuumiza. Tamanio letu la kusamehe, kama Mwokozi alivyofanya, kwa wale wanaotukosea au kuzungumza baya dhidi yetu hakika itaongezeka na kuwa sehemu ya tabia yetu.

Hivi leo, katika Jumapili hii ya Matawi, tutandaze majoho yetu ya upendo na matawi ya mitende ya hisani, tukitembea katika nyayo za Mfalme wa Amani wakati tunapojiandaa kusherehekea Jumapili hii ijayo, muujiza wa kaburi tupu. Kama akina kaka na akina dada katika Kristo, kwa shangwe tutangaze, “Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni.”27

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo yu hai na kwamba upendo Wake mkamilifu, uliooneshwa kupitia dhabihu Yake ya kulipia dhambi, umetolewa kwa wote wanaohitaji kutembea Naye na kufurahia amani Yake katika ulimwengu huu na ulimwengu ujao. Ninasema mambo haya katika jina takatifu la Mwokozi na Mkombozi, Yesu Kristo, amina.