Mkutano Mkuu
Kazi ya Hekalu na Historia ya Familia—Kazi Moja na Sawa
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Kazi ya Hekalu na Historia ya Familia—Kazi Moja na Sawa

Kiini cha fokasi ya mpango wa Baba yetu wa Mbinguni ni kuunganisha familia kwa ajili ya maisha haya na milele.

Nina shukrani kwa ujenzi unaoendelea wa mahekalu katika “kipindi hiki cha utimilifu wa nyakati” (Mafundisho na Maagano 128:18). Tangu siku za mwanzo za Urejesho, Watakatifu waaminifu wamefanya dhabihu nyingi ili kupokea ibada na maagano ya hekaluni. Kufuatia mifano yao mikubwa, mnamo 1975, baada ya dhabihu nyingi za kiuchumi za kusafiri kutoka jiji la Mexico, mimi na mke wangu mpendwa, Evelia, tukisindikizwa na wazazi wetu wapendwa, tuliunganishwa kama mume na mke milele katika Hekalu la Mesa Arizona. Siku hiyo, tulipounganishwa kwa mamlaka ya ukuhani ndani ya nyumba ya Bwana, hakika tulipata twasira ndogo ya mbinguni.

Kazi na Lengo la Mahekalu

Uzoefu huo umeniruhusu kuwa na shukrani zaidi kwa jinsi, baada ya miaka mitatu ya kazi ngumu na dhabihu kubwa, Watakatifu wa Kirtland, Ohio, hatimaye walikamilisha hekalu lao la kupendeza katika majira ya kuchipua ya mwaka 1836—la kwanza katika kipindi hiki. Mnamo Machi ya mwaka huo huo, watu zaidi ya elfu moja walikusanyika hekaluni na kwenye malango yake kwa ajili ya shughuli ya uwekaji wakfu. Nabii Joseph Smith alisimama kutoa sala ya kuweka wakfu, ambayo aliipokea kwa ufunuo (ona Mafundisho na Maagano 109). Ndani yake alifafanua baraka nyingi za kipekee ambazo zinatolewa juu ya wale ambao kwa kustahili huingia ndani ya mahekalu ya Bwana. Kisha kwaya iliimba wimbo “Roho wa Mungu” na mkusanyiko ulisimama na kutoa Shangwe za Hosana “kwa [nguvu kubwa kiasi kwamba] zilionekana … kuinua paa kutoka kwenye jengo” (Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith [2007], 307).

Wiki moja baadaye nabii alieleza kutokea kwa Bwana ndani ya hekalu, ambaye alisema:

“Kwani tazama, nimeikubali nyumba hii, na jina langu litakuwa humu; nami nitajionyesha kwa watu wangu kwa rehema katika nyumba hii.

“Na umaarufu wa nyumba hii utaenea hadi nchi za kigeni; na huu ni mwanzo wa baraka ambazo zitamwagwa juu ya vichwa vya watu wangu” (Mafundisho na Maagano 110:7, 10).

Baada ya ono hili na mengine, Eliya nabii, aliyechukuliwa mbinguni bila ya kuonja mauti, alisimama mbele ya Nabii Joseph Smith na Oliver Cowdery na kusema:

“Tazama, wakati umetimia kikamilifu, ambao ulinenwa kwa kinywa cha Malaki—ukishuhudia kwamba yeye [Eliya nabii] lazima atatumwa, kabla ya kuja kwa siku ile iliyo kuu na ya Bwana—

“Kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na ya watoto iwaelekee baba, dunia yote isije ikapigwa kwa laana—

“Kwa hiyo, funguo za kipindi hiki zimekabidhiwa mikononi mwenu; na kwa hili ninyi mpate kujua kwamba siku ile iliyo kuu na ya kutisha ya Bwana ipo karibu, hata milangoni” (Mafundisho na Maagano110:14–16).

Hekalu na Historia ya Familia

Baada ya Bwana kurejesha funguo za kuunganisha kwa Joseph Smith, kazi ya wokovu pande zote mbili za pazia ilianza katika kipindi chetu (ona 1 Wakorintho 15:22, 29; Mafundisho na Maagano 128:8–18)

Mzee Boyd K. Packer alifundisha kwamba “tukio hili la ishara lilipita bila kutiliwa mkazo na ulimwengu, lakini lingeshawishi hatma ya kila nafsi ambayo imewahi kuishi au itakayoishi. Taratibu mambo yalianza kutokea. Kanisa likawa kanisa la kujenga mahekalu.

“Ulimwenguni yalianza hapa na pale, katika njia iliyodhaniwa kuwa ya ghafla, watu na taasisi na jamii zikivutiwa katika kutafuta vizazi. Hii yote imetokea tangu kutokea kwa Eliya ndani ya Hekalu la Kirtland.(The Holy Temple [1980], 141).

“Tangu siku ile, Aprili 3, 1836, mioyo ya watoto ilianza kuwageukia baba zao. Baada ya hapo ibada hazikuwa za muda tu, bali za kudumu. Nguvu ya kuunganisha ilikuwa pamoja nasi. Hakuna mamlaka yanayozidi thamani yake. Nguvu hiyo hutoa kiini na uendelevu wa milele kwa ibada zote zinazofanywa kwa mamlaka sahihi kwa wote walio hai na wafu” (Preparing to Enter the Holy Temple [2002], 28).

Wapendwa akina kaka na akina dada, ujenzi na matumizi sahihi ya mahekalu umekuwa kwa kipindi chochote kile ishara ya kanisa la kweli la Yesu Kristo. Baada ya uwekaji wakfu wa Hekalu la Salt Lake mnamo 1893, Rais Wilford Woodruff aliwahimiza waumini wa kanisa watafute kumbukumbu za mababu zao na kurekodi vizazi vyao kwa kurudi nyuma kadiri walivyoweza ili kuleta majina hekaluni na kufanya ibada za wokovu na kuinuliwa (see Teachings of Presidents of the Church: Wilford Woodruff [2004], 174).

Historia ya Familia na Kazi ya Hekalu—Kazi Moja

Mwaka mmoja baadaye (1894), Rais Woodruff yule yule alisimamia uanzishwaji wa Shirika la Nasaba la Utah. Miaka mia baadaye, mnamo 1994 Mzee Russell M. Nelson, wakati huo akiwa mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alisema, “Matukio ya mwaka huo wa kihistoria yalianzisha utafiti wa historia ya familia na huduma ya hekaluni kama kazi moja katika Kanisa” (“The Spirit of Elijah,” Ensign, Nov. 1994, 85).

Kazi ya Historia ya Familia

Wapendwa akina kaka na akina dada, Bwana anatuhimiza kama waumini wa Kanisa Lake tuhifadhi historia ya familia zetu wenyewe, tujifunze kutoka kwa mababu zetu na tufanye mipangilio muhimu kwa ajili yao kupokea ibada za injili ndani ya mahekalu ili kuwasaidia wapige hatua kwenye njia ya agano, kitu ambacho kitawabariki wao kwa familia ya milele. Hicho ndicho kiini cha fokasi ya mpango wa Baba yetu wa Mbinguni: kuunganisha familia kwa maisha haya na milele.

Kwa wale kati yetu mnaohisi hamwezi kufanya kazi hii, mnapaswa kujua kwamba hamko peke yenu. Sote tunaweza kugeukia nyenzo ambazo Kanisa limeziandaa na ambazo zinapatikana kwenye vituo vya FamilySearch, ambavyo tulivifahamu kama vituo vya historia ya familia. Vituo hivi vya FamilySearch vimesanifiwa ili takribani kila mtu, kwa usaidizi kidogo, aweze kupata taarifa za mababu zao na kuzipanga kwa usahihi ili kwamba waweze kuzipeleka kwenye nyumba ya Bwana. Tafadhali wasiliana na washauri wa historia ya familia katika kata au tawi lako ambao watakuongoza kila hatua unayopiga.

Tunapofuata mwongozo wa manabii na kujifunza jinsi ya kufanya historia yetu ya familia na kufanya ibada za hekaluni kwa ajili ya mababu zetu, tutapata uzoefu wa shangwe kuu kiasi kwamba hatutataka kuacha kuifanya. Roho ataijaza mioyo yetu, ataamsha akili zetu ili kufanya kazi hiyo na kutuongoza pale tunapotafuta majina ya mababu zetu. Lakini acha tukumbuke kwamba historia ya familia ni zaidi tu ya kutafuta majina, tarehe na maeneo. Ni kuunganisha familia na kuhisi shangwe inayokuja kutokana na kuwapa wao ibada za injili.

Ninapenda fundisho lenye uvuvio la nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, ambaye amesema: “Hekalu ni kitovu cha kuimarisha imani yetu na uimara wa kiroho kwa sababu Mwokozi na mafundisho Yake ndiyo kiini hasa cha hekalu. Kila kitu kinachofundishwa ndani ya hekalu, kupitia maelekezo na kupitia Roho, huongeza uelewa wetu wa Yesu Kristo. Ibada Zake muhimu hutuunganisha Kwake kupitia maagano matakatifu ya ukuhani. Kisha, tunapotunza maagano yetu, Yeye hutubariki kwa nguvu Yake ya uponyaji na uimarisho” (“Hekalu na Msingi Wako wa Kiroho,” Liahona, Nov. 2021, 93).

Hakika, kazi ya hekalu na historia ya familia ni kazi moja na sawa katika Kanisa.

Nashuhudia juu ya kweli hizi. Ninajua hili ni Kanisa la Bwana Yesu Kristo, Mwokozi na Mkombozi wetu, ambaye tunamkumbuka na kumtukuza wakati huu wa Pasaka. Ninajua anatupenda na tunapotii maagano yetu na kuweka kujiamini kwetu Kwake, Yeye hutupatia nguvu Yake ya uponyaji na uimarisho. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.