2010–2019
Tazama Mwanakondoo wa Mungu
Mkutano Mkuu wa Aprili 2019


Tazama Mwanakondoo wa Mungu

Mikutano yetu ya Jumapili iliyopangwa upya ni kutilia mkazo sakramenti ya Chakula cha Bwana kuwa takatifu, inayotambuliwa kama sehemu muhimu ya kuabudu kwetu kila wiki.

Nilikuwa sawa kabisa mpaka pale nilipoona machozi kwenye macho ya wale vijana katika kwaya hii. Machozi hayo ni mahubiri yenye ushawishi zaidi kuliko ninayoweza kutoa.

Akitazama juu kutoka ukingo wa mto, kupita halaiki yenye shauku wakitaka kubatizwa naye, Yohana, aliyeitwa Mbatizaji, alimuona kwa mbali binamu yake, Yesu Mnazareti, akitembea kwa ushupavu kuelekea alipokuwa kufanya ombi kwa ajili ya ibada sawa na hiyo. Kwa heshima kubwa, lakini kwa sauti iliyoweza kusikika na wale waliokuwa karibu, Yohana alitamka sifa ambayo ingali inatuvutia milenia mbili baadaye: “Tazama Mwanakondoo wa Mungu.”1

Ni ya kuelimisha kwamba huyu mtangulizi wa Yesu aliyetabiriwa kwa muda mrefu hakumuita Yeye “Yehova” au “Mwokozi” au “Mkombozi” au hata “Mwana wa Mungu”—yote ambayo yalikuwa majina yanayofaa. La, Yohana alichagua taswira ya kale na pengine inayojulikana zaidi katika desturi ya kidini ya watu wake. Alitumia umbo la mwanakondoo anayetolewa kama dhabihu kwa ajili ya upatanisho wa dhambi na mateso ya dunia iliyoanguka na watu wote walioanguka ndani yake.

Tafadhali mniruhusu nisimulie tena kwa kifupi historia hiyo.

Baada ya kufukuzwa kutoka Bustani ya Edeni, Adamu na Hawa walikabiliwa na wakati ujao wenye uharibifu. Wakiwa wamefungua mlango wa maisha ya mauti na maisha ya muda kwa ajili yetu, walikuwa wamefunga mlango wa maisha bila kifo na uzima wa milele kwa ajili yao. Kwa sababu ya uasi waliokuwa wamechagua kwa hiari kufanya kwa niaba yetu, sasa walikabiliana na kifo cha kimwili na kufukuzwa kiroho, kutengwa kutoka kwenye uwepo wa Mungu milele.2 Ni nini walichohitajika kufanya? Je, kungeweza kuwa na njia ya kuponyoka shida hii? Hatuna uhakika ni kiasi gani hawa wawili walikubaliwa kukumbuka kuhusu mafundisho waliyopokea walipokuwa katika bustani, lakini walikumbuka walihitajika mara kwa mara kutoa dhabihu kwa Mungu mwanakondoo msafi, asiye na dosari, mzaliwa wa kwanza wa kiume katika kundi lao la mifugo.3

Baadaye malaika alikuja kuwaelezea kwamba dhabihu hii ilikuwa mfano, kuonyesha dhabihu ambayo ingefanyika kwa niaba yao na Mwokozi wa ulimwengu ambaye angekuja. “Jambo hili ni mfano wa dhabihu ya Mzaliwa Pekee wa Baba,” malaika alisema. “Kwa hiyo, … nawe utatatubu na kumlingana Mungu katika jina la Mwana milele Yote.”4 Kwa bahati nzuri, kulikuwa na uwezekano wa njia ya kuponyoka na kwenda juu.

Katika mabaraza ya mbinguni kabla ya maisha ya sasa, Mungu alimuahidi Adamu na Hawa (na sisi sote) kwamba msaada ungekuja kutoka kwa Mwana Wake msafi, asiye na dosari, Mzaliwa wa Kwanza, Mwanakondoo wa Mungu “aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia,”5 kama ambavyo Mtume Yohana angezungumza baadaye Kumhusu. Kwa kuwatoa wanakondoo wao wadogo kama ishara katika maisha ya sasa, Adamu na vizazi vyake walikuwa wakionyesha uelewa wao na utegemezi wao juu ya dhabihu ya upatanisho ya Yesu Mpakwa Mafuta.6 Baadaye, maskani ya nyikani yangekuwa maandalizi ya ibada hii na, baada ya hapo, hekalu ambalo Sulemani angejenga.

Kwa bahati mbaya, kama ishara ya toba ya kweli na kuishi kulikojaa imani, utaratibu huu wa kutoa sadaka ya wanakondoo wasio na dosari haukufanya kazi vizuri, kwa kiasi ambacho Agano la Kale linaelezea. Uamuzi adilifu ambao ulifaa kuambatana na dhabihu hizo wakati mwingine haukudumu kwa muda mrefu ili damu iweze kukauka juu ya mawe. Kwa vyovyote vile, haukudumu kwa muda wa kutosha kuzuia uuaji wa kaka, Kaini alipomuua kaka yake Habili katika kizazi cha kwanza.7

Pamoja na majaribu na shida kama hizi zikiendelea kwa karne nyingi, si ajabu kwamba malaika wa mbinguni waliimba kwa shangwe wakati, hatimaye, Yesu alipozaliwa—Masiya Mwenyewe aliyetarajiwa kwa muda mrefu. Kufuatia huduma Yake fupi hapa duniani, huyu kondoo wa Pasaka msafi kuliko wote Aliwatayarisha wanafunzi Wake kwa ajili ya kifo Chake kwa kuanzisha sakramenti ya Chakula cha Bwana, mtindo wa kibinafsi zaidi wa ibada iliyokuwa imeanzishwa nje ya Edeni. Bado kungekuwa na sadaka, bado ingehusisha dhabihu, lakini ingekuwa na ishara ya kina zaidi, ya kujipima zaidi na ya binafsi zaidi kuliko umwagaji wa damu ya mwanakondoo mzaliwa wa kwanza. Kwa Wanefi, baada ya Ufufuko Wake, Mwokozi alisema juu ya hili:

“Na hamtatoa kwangu tena kumwagwa kwa damu. …

“… Mtatoa kwangu dhabihu ya moyo uliopondeka na roho iliyovunjika. Na yeyote atakayekuja kwangu na moyo uliopondeka na roho iliyovunjika, huyo nitambatiza kwa moto na Roho Mtakatifu. …

“… Kwa hivyo, … tubuni, … na muokolewe.”8

Wapendwa kaka na dada zangu, kwa mkazo mpya wa kusisimua kuhusu kuongezeka kwa kujifunza injili nyumbani, ni muhimu kwetu sisi kukumbuka kwamba bado tumeamriwa “utakwenda kwenye nyumba ya sala na kutoa sakramenti zako katika siku yangu takatifu.”9 Kwa kuongezea kwenye kutenga muda kwa ajili ya kufundisha injili kunakolenga-nyumbani, mikutano yetu ya Jumapili iliyorekebishwa upya ina lengo la kupunguza mkanganyiko wa ratiba ya mikutano kwa njia inayotilia mkazo sakramenti ya Chakula cha Bwana kama njia bora takatifu, inayotambuliwa kama sehemu muhimu ya kuabudu kwetu kila wiki. Tunapaswa kukumbuka kwa njia ya kibinafsi iwezekanavyo kwamba Kristo alikufa kutokana na moyo uliopondeka kwa kubeba peke yake dhambi na huzuni ya familia nzima ya wanadamu.

Kadiri ambavyo tumechangia kwenye mzigo huo wa mauti, tukio kama hilo linahitaji heshima yetu. Hivyo, tunahimizwa kuja katika mikutano yetu mapema na kwa heshima kubwa, tukiwa tumevalia inavyofaa kwa ajili ya kushiriki katika ibada takatifu. “Nguo nzuri sana za jumapili” imepoteza kiasi kidogo cha maana yake katika wakati wetu, na kwa ajili ya kumtukuza Yeye ambaye tunakuja katika uwepo wake, tunastahili kurejesha desturi hiyo ya nguo ya Sabato na kuwa nadhifu wakati na mahali tunapoweza.

Kuhusu kuwahi, upitishaji kwa waliochelewa daima utatolewa kwa upendo kwa wale akina mama waliobarikiwa ambao, wakiwa na watoto na asusa na mifuko ya nepi nyuma yao katika mpangilio wa kupendeza wenye vurugu, wana bahati kwamba hatimaye walifika kanisani. Zaidi ya hayo, kutakuwa na baadhi ambao bila kuepukika wanampata ng’ombe wao kwenye matope asubuhi ya Sabato. Hata hivyo, kwa kundi hili la mwisho tunasema kuchelewa mara moja kunaeleweka, lakini ng’ombe akiwa anapatikana kwenye matope kila Jumapili, basi tunakushauri kwa dhati umuuze ng’ombe huyo au ufukie matope hayo.

Katika moyo huo huo, tunatoa ombi la kitume la kupunguzwa kwa kelele katika utakatifu wa majengo yetu. Tunapenda kujuliana hali sisi kwa sisi, na tunapaswa kufanya hivyo—ni mojawapo ya shangwe za kuhudhuria Kanisani—lakini haifai kufanyika kwa sauti ya juu katika mazingira yaliyowekwa wakfu kwa ajili ya kuabudu. Ninaogopa kwamba wageni wasio wa imani yetu wanashangazwa na kile ambacho wakati mwingine chaweza kuwa kelele inayokosa heshima katika mazingira yanayopaswa kuwa na sifa ya sala, ufunuo, na amani. Pengine mbingu kidogo inastaajabishwa pia.

Itaongeza kwenye roho wa mikutano yetu ya sakramenti ikiwa maafisa wasimamizi watakuwa wameketi kwenye jukwaa kabla ya mkutano kuanza, wakisikiliza muziki unaotangulia na kwa heshima kubwa kuonyesha mfano ambao sisi wote tunastahili kuiga. Ikiwa kuna kupayuka payuka kwenye jukwaa, hatufai kustaajabu wakati kuna kupayuka payuka ndani ya mkusanyiko. Tunaupongeza uaskofu unaoondoa matangazo ambayo yanadunisha hisia za kuabudu kwetu. Mimi, siwezi kupata taswira ya kuhani kama Zakaria—pale katika hekalu la kale la Bwana, akiwa karibu kushiriki kwenye fursa moja na ya kipekee ya kikuhani ambayo angeipata katika maisha yake yote—siwezi kupata taswira akiwa amesimama mbele ya madhabahu kutukumbusha kwamba mashindano ya farasi ya pinewood yatafanyika tu baada ya wiki sita na kujiandikisha ni hivi karibuni.

Akina kaka na akina dada, muda huu ulioagizwa na Bwana ni muda mtakatifu zaidi katika wiki yetu. Kwa amri, tunakusanyika kwa ajili ya ibada inayopokewa ulimwenguni kote katika Kanisa. Ni kwa ajili ya ukumbusho wa Yeye aliyeomba ikiwa kikombe Alichokuwa karibu kunywa kingeweza kuondolewa, ila tu aliendelea kwa ujasiri kwa sababu Alijua kwamba kwa ajili yetu hakingeweza kuondolewa. Itakuwa yenye msaada kwetu ikiwa tutakumbuka kwamba ishara ya kikombe hicho taratibu inatembea katika safu kutufikia kwenye mikono ya shemasi wa miaka 11 au 12.

Pale wasaa mtakatifu unapofika wa kuwasilisha zawadi yetu ya dhabihu kwa Bwana, tunazo dhambi zetu na mapungufu tunayohitaji kurekebisha. Lakini tungeweza kufanikiwa zaidi katika moyo huo uliovunjika ikiwa tunaikumbuka mioyo mingine iliyovunjika na roho zenye huzuni zinazotuzunguka . Walioketi karibu nasi ni baadhi ya wale wanaoweza kuwa wamelia—wazi wazi au kwa ndani—muda wote wa wimbo wa sakramenti na wakati wa sala za wale makuhani. Je, tunaweza kimya kimya kutambua hayo na kutoa gamba letu dogo la faraja na kikombe kidogo cha huruma kwao? au kwa ajili ya mshiriki anayelia, anayekabiliana na shida ambaye hayupo katika mkutano na, isipokuwa kwa kitendo fulani cha ukombozi kutoka kwetu, hatakuwepo wiki ijayo pia? au kwa akina kaka na dada zetu ambao si waumini wa Kanisa lakini ni akina kaka na dada zetu? Hakuna upungufu wa mateso humu duniani, ndani na nje ya Kanisa, kwa hivyo tazama upande wowote na utapata mtu ambaye uchungu wake unaonekana mzito kubebeka na huzuni yake inaonekana isiyo na kikomo. Njia moja ya “daima kumkumbuka”10 ni kujiunga na Tabibu Mkuu katika kazi Yake isiyo na kikomo ya kuinua mzigo kutoka kwa wale ambao wamelemewa na kuondoa uchungu wa wale ambao wanahangaika.

Marafiki wapendwa, tunapoungana kote duniani kila wiki katika kile ambacho tunatumaini ni ongezeko zaidi la shukrani takatifu kwa zawadi tukufu ya upatanisho wa Kristo kwa ajili ya wanadamu wote, na tuweze kuleta kwenye madhabahu ya sakramenti machozi zaidi kwa ajili ya masikitiko Yake [na] maumivu zaidi kwa huzuni yake.” Na kisha tunapotafakari, kusali, na kufanya agano upya, na tuweze kuchukua kutoka kwenye muda ule mtakatifu “subira zaidi katika mateso, … sifa zaidi kwa ajili ya msaada.”11 Kwa ajili ya subira na msaada huo, kwa ajili ya utakatifu na tumaini la aina hii, nina sali kwa niaba yetu wote katika jina la Yeye aliyemega mkate wa thamani wa msamaha na kumimina divai takatifu ya ukombozi, hata Yesu Kristo, Mwanakondoo wa Mungu, mkuu na mwenye rehema, amina.

Muhtasari

  1. Yohana 1:29.

  2. Ona 2 Nefi 9:8–9.

  3. Ona Musa 5–8; ona pia Kutoka 12:3–10.

  4. Musa 5:7–8; ona pia Musa 5:9.

  5. Ufunuo 13:8.

  6. Ona Kamusi ya Biblia, “Mpakwa Mafuta”; ona pia Mwongozo kwenye Maandiko, “Mpakwa Mafuta,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org.

  7. Kwa kinaya, Kaini kumuua Habili, kitendo ambacho hatimaye kilielekezwa na Shetani, kinaweza kuhusishwa na hasira ya awali ya Kaini juu ya sadaka yake ya dhabihu kukataliwa na Bwana huku ya Habili ikikubaliwa.

    “Mungu … alitayarisha dhabihu katika zawadi ya Mwana Wake, ambaye alipaswa … kufungua mlango ambao kupitia huo mwanadamu angeweza kuingia katika uwepo wa Bwana. …

    “Kupitia imani katika upatanisho huu au mpango huu wa ukombozi, Habili alimtolea Mungu dhabihu ambayo ilikubaliwa, ambayo ilikuwa ni wazao wa kwanza wa mifugo. Kaini alitoa matunda ya nchi, na hakukubaliwa. … [Dhabihu yake ilipaswa kujumuisha] umwagaji wa damu” (Mafundisho ya Marais wa Kanisa: Joseph Smith [2007], 48; ona pia 107–8)

  8. 3 Nefi 9:19–20, 22.

  9. Mafundisho na Maagano 59:9.

  10. Moroni 4:3; 5:2.

  11. “More Holiness Give Me,” Nyimbo za Kanisa, no. 131.