Unabii wa Samweli, Mlamani, kwa Wanefi.
Yenye milango ya 13 hadi 15.
Mlango wa 13
Samweli Mlamani anatabiri kuangamizwa kwa Wanefi isipokuwa watubu—Hao na utajiri wao wanalaaniwa—Wanakataa na kuwapiga manabii kwa mawe, wanazingirwa na pepo mbaya, na wanatafuta furaha kwa kutenda uovu. Karibia mwaka 6 K.K.
1 Na ikawa katika mwaka wa themanini na sita, Wanefi walibaki kwenye uovu, ndiyo, katika uovu mwingi, wakati Walamani walitii amri za Mungu, kulingana na sheria ya Musa.
2 Na ikawa kwamba katika mwaka huu kulikuwa na mmoja aliyeitwa Samweli, Mlamani ambaye alikuja kwenye nchi ya Zarahemla, na akaanza kuhuwabiria watu. Na ikawa kwamba alihubiri, siku nyingi, toba kwa watu, na wakamtupa nje, na alikuwa karibu kurudi kwa nchi yake.
3 Lakini tazama, sauti ya Bwana ilimjia, kwamba arejee tena, na kuwatabiria hawa watu vitu vyote vitakavyomjia kwa moyo wake.
4 Na ikawa kwamba hawangemkubalia kwamba aingie kwenye mji; kwa hivyo alienda na kupanda juu ya ukuta wa mji, na kunyosha mkono wake mbele na kupaza sauti, na kutabiria watu vitu vyote ambavyo Bwana aliweka moyoni mwake.
5 Na akawaambia: Tazama, mimi, Samweli, Mlamani, ninaongea maneno ya Bwana ambayo ameweka kwenye moyo wangu; na tazama ameiweka kwenye moyo wangu kuwaambia hawa watu kwamba upanga wa haki unaningʼinia juu ya hawa watu; na miaka mia nne haitapita kabla ya upanga wa haki kuwaangukia hawa watu.
6 Ndiyo, uangamizo mzito unawangojea watu hawa, na kwa kweli utawajia watu hawa, na hakuna kitakachowaokoa watu hawa isipokuwa toba na imani kwa Bwana Yesu Kristo, ambaye kwa kweli atakuja duniani, na atavumilia vitu vingi na atauawa kwa ajili ya watu wake.
7 Na tazama, malaika wa Bwana amenitangazia, na alileta habari njema kwa roho yangu. Na tazama, nilitumwa kwenu niwatangazie pia, ili mpate habari njema; lakini tazama mmekataa kunisikiliza.
8 Kwa hivyo, hivyo ndivyo asemavyo Bwana: Kwa sababu ya ugumu wa mioyo ya watu hawa wa Wanefi, wasipotubu nitachukua ahadi yangu yote kutoka kwao, na nitaondoa Roho yangu kutoka kwao, na sitawavumilia tena, na nitageuza mioyo ya ndugu zao dhidi yao.
9 Na miaka mia nne haitapita kabla ya mimi kusababisha kwamba wauawe; ndiyo, nitawaadhibu kwa upanga na njaa na maradhi ya kuambukiza.
10 Ndiyo, nitawatembelea katika hasira yangu kali, na kutakuwa na wengine wa kizazi cha nne ambao wataishi, baina ya maadui wenu, kuona kuangamizwa kwenu kabisa; na hii kwa kweli itakuja isipokuwa mtubu, Bwana anasema; na wale wa kizazi cha nne watawatembelea kwa maaangamizo.
11 Lakini ikiwa mtatubu na kumrudia Bwana Mungu wenu nitabadilisha hasira yangu, asema Bwana; ndiyo, hivyo ndivyo asemavyo Bwana, wale watakaotubu na kurudi kwangu watabarikiwa, lakini ole kwa yule ambaye hatatubu.
12 Ndiyo, ole kwa huu mji mkuu wa Zarahemla; kwani tazama, ni kwa sababu ya wale wenye haki kwamba umeokolewa; ndiyo, ole kwa mji huu mkuu, kwani ninaona, asema Bwana, kwamba kuna wengi, ndiyo, hata sehemu kubwa ya huu mji mkuu ambao watashupaza mioyo yao dhidi yangu, asema Bwana.
13 Lakini heri wale ambao watatubu, kwani hao ndiyo nitakaowasamehe. Lakini tazama, kama haingekuwa kwa wale wenye haki ambao wako kwenye mji huu mkuu, tazama, ningesababisha kwamba moto uje chini kutoka mbinguni na kuuangamiza.
14 Lakini tazama, ni kwa ajili ya wale wenye haki kwamba umesamehewa. Lakini tazama, wakati unawadia, asema Bwana, kwamba wakati mtatupa walio wenye haki kutoka miongoni mwenu, ndipo mtakapokuwa tayari kwa uangamizo; ndiyo, ole kwa huu mji mkuu, kwa sababu ya uovu na machukizo ambayo yamo ndani yake.
15 Ndiyo, na ole kwa mji wa Gideoni, kwa uovu na machukizo ambayo yamo ndani yake.
16 Ndiyo, na ole kwa miji yote ambayo iko katika nchi karibu na hapa, ambayo imemilikiwa na Wanefi, kwa sababu ya uovu na machukizo ambayo yamo ndani yao.
17 Na tazama, laana itakujia juu ya nchi, asema Bwana wa Majeshi, kwa sababu ya watu ambao wako nchini, ndiyo, kwa sababu ya uovu wao na machukizo yao.
18 Na itakuwa, asema Bwana wa Majeshi, ndiyo, ambaye ni Mungu wetu mkuu na wa kweli, kwamba yeyote ambaye ataficha hazina ardhini hataipata tena, kwa sababu ya laana kuu ya nchi, isipokuwa awe mtu mwenye haki na aifiche kwenye Bwana.
19 Kwani ninawataka, asema Bwana, kwamba wafiche hazina zao kwangu; na laana iwe kwa wale wasioficha hazina zao kwangu; kwani hakuna yeyote ambaye huficha hazina zake kwangu isipokuwa awe mwenye haki; na yule ambaye hafichi hazina zake kwangu, amelaaniwa, na pia ile hazina, na hakuna atakayeikomboa kwa sababu ya laana ya nchi.
20 Na siku itawadia kwamba wataficha hazina zao, kwa sababu wameweka mioyo yao kwenye utajiri; na kwa sababu wameweka mioyo yao kwenye utajiri wao, na wataficha hazina zao wakati watakimbia kutoka kwa maadui wao; kwa sababu hawatazificha kwangu, walaaniwe na pia hazina zao; na katika siku hio ndipo watakapouawa, asema Bwana.
21 Tazama ninyi, watu wa huu mji mkuu, na sikilizeni maneno yangu; ndiyo, sikilizeni maneno ambayo Bwana anasema; kwani tazama, anasema kwamba mmelaaniwa kwa sababu ya utajiri wenu, na pia utajiri wenu umelaaniwa kwa sababu mmeweka mioyo yenu juu yake, na hamjasikiliza maneno ya yule aliyewapatia huo utajiri.
22 Hammkumbuki Bwana Mungu wenu kwa vitu ambavyo amewabariki navyo, lakini kila siku mnakumbuka utajiri wenu, bila kumshukuru Bwana Mungu wenu kwa hivyo vitu; ndiyo, mioyo yenu haimkaribii Bwana, lakini inavimba kwa kiburi kikuu, kwa kujisifu, na kwa uvimbe mkuu, mashindano, ukorofi, uovu, mateso, na mauaji, na kila aina ya uovu.
23 Kwa sababu hii Bwana Mungu amesababisha kwamba laana ije kwa nchi, na pia kwa utajiri wenu, na hii ni kwa sababu ya maovu yenu.
24 Ndiyo, ole kwa watu hawa, kwa sababu ya huu muda ambao umewadia, wakati mnatupa nje manabii, na kuwacheka, na kuwatupia mawe, na kuwaua, na kufanya kila aina ya uovu kwao, hata vile walioishi zamani walivyofanya.
25 Na sasa mkizungumza, mnanena: Ikiwa siku zetu zingekuwa katika siku za babu zetu wa zamani, hatungewaua manabii; hatungewapiga kwa mawe, na kuwatupa nje.
26 Tazama ninyi ni wabaya kuliko hao; kadiri Bwana anavyoishi, ikiwa nabii anaweza kuja miongoni mwenu na kuwatangazia neno la Bwana, ambalo linashuhudia dhambi zenu na uovu, mnamkasirikia, na kumtupa nje na kutafuta njia za namna zote kumwangamiza; ndiyo, mtasema kwamba ni nabii wa uwongo, na kwamba ni mwenye dhambi, na mwenye kutoka kwa ibilisi, kwa sababu anashuhudia kwamba vitendo vyenu ni viovu.
27 Lakini tazama, ikiwa mtu atatokea miongoni mwenu na kusema: Fanya hivi, na hakutakuweko na ubaya; fanya vile na hamtaumia; ndiyo, atasema: Tembeeni katika kiburi cha mioyo yenu yenyewe; ndiyo, tembeeni katika kiburi cha macho yenu, na fanya chochote ambacho moyo wako unapenda—na ikiwa mtu atatokea miongoni mwenu na kusema hivi, hapo mtamkubali, na kusema ni nabii.
28 Ndiyo, mtamheshimu, na mtampatia mali yenu; mtampatia dhahabu yenu, na fedha yenu, na mtamvalisha mavazi ya thamani; na kwa sababu anazungumza maneno ya kusifu ya uongo kwenu, na anasema kwamba yote ni mema, kwa hivyo hamtampata na makosa.
29 Ee ninyi kizazi kilichopotea; ninyi watu wagumu na wenye shingo ngumu, kwa muda gani mnadhani Bwana atawavumilia? Ndiyo, kwa muda gani mtakubali kuongozwa na wapumbavu na vipofu? Ndiyo, kwa muda gani mtachagua giza juu ya mwangaza?
30 Ndiyo, tazama, ghadhabu ya Bwana imewashwa dhidi yenu; tazama, amelaani nchi kwa sababu ya uovu wenu.
31 Na tazama, wakati unawadia kwamba atalaani utajiri wenu, kwamba utateleza, kwamba hamtaweza kuushika; na katika siku za umasikini wenu hamtazishika.
32 Na katika siku za umasikini wenu mtamlilia Bwana; na mtalia bure, kwani ukiwa wenu utakuwa umewajia kitambo, na uharibifu wenu umekamilishwa; na hapo mtatoa machozi na kulia wakati huo, asema Bwana wa Majeshi. Na hapo mtaomboleza, na kusema:
33 Ee kwamba nilikuwa nimetubu, na sikuwaua manabii, na kuwapiga kwa mawe, na kuwatupa nje. Ndiyo, katika siku hiyo mtasema: Ee kwamba tungemkumbuka Bwana Mungu wetu wakati ambapo alitupatia utajiri wetu, na hapo haungeteleza, kwamba tuupoteze; kwani tazama, utajiri wetu umetuwacha.
34 Tazama, tunaweka hapa chombo na kesho yake kimeenda; na tazama, panga zetu zinachukuliwa kutoka kwetu wakati tunapozitafuta kwa vita.
35 Ndiyo, tumeficha hazina zetu na zimeponyokea mbali kutoka kwetu, kwa sababu ya laana ya nchi.
36 Ee kwamba tulitubu wakati ambao neno la Bwana lilitujia; kwani tazama nchi imelaaniwa, na vitu vyote vimekuwa vya kuteleza, na hatuwezi kuvishika.
37 Tazama, tumezingirwa na pepo mbaya, ndiyo, tumezungukwa na malaika wa yule ambaye anataka kuangamiza roho zetu. Tazama, uovu wetu ni mkuu. Ee Bwana, huwezi kugeuza hasira yako kutoka kwetu? Na hii itakuwa lugha yenu wakati huo.
38 Lakini tazama, siku zenu za majaribio zimepita; mmechelewesha siku yenu ya wokovu mpaka imechelewa milele, na maangamizo yenu yamehakikishwa; ndiyo, kwani mmetafuta siku zote za maisha yenu yale ambayo hamwezi kupata; na mmetafuta furaha kwa kufanya uovu, kitu ambacho ni kinyume cha asili ya haki ambayo huja kutoka kwa mkuu na Kiongozi wetu wa Milele.
39 Ee ninyi watu wa nchi, ningetaka kwamba msikilize maneno yangu! Na ninaomba kwamba hasira ya Bwana itolewe kutoka kwenu, na kwamba mtatubu na kukombolewa.