Vitabu vya Maelekezo na Miito
3. Kanuni za Ukuhani


“3. Kanuni za Ukuhani,” Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho (2020)

“3. Kanuni za Ukuhani,” Kitabu cha Maelezo ya Jumla.

Picha
kijana akipokea baraka za ukuhani

3.

Kanuni za Ukuhani

3.0

Utangulizi

Ukuhani ni mamlaka na nguvu za Mungu. Daima umekuwepo na utaendelea kuwepo bila mwisho (ona Alma 13:7–8; Mafundisho na Maagano 84:17–18). Kupitia ukuhani, Baba wa Mbinguni anatimiza kazi Yake “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu” (Musa 1:39). Mungu anatoa mamlaka na nguvu kwa wana na mabinti Zake duniani ili wasaidie kutekeleza kazi hii (ona sura ya 1).

3.1

Urejesho wa Ukuhani

Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni taasisi pekee duniani yenye mamlaka ya ukuhani. Nabii Joseph Smith alipokea Ukuhani wa Haruni na funguo zake kutoka kwa Yohana Mbatizaji (ona Mafundisho na Maagano 13:1). Alipokea Ukuhani wa Melkizedeki na funguo zake kutoka kwa Mitume Petro, Yakobo, na Yohana (ona Mafundisho na Maagano 27:12–13).

Katika Hekalu la Kirtland, Musa, Elia, na Eliya walimtokea Joseph Smith na kumkabidhi mamlaka zaidi muhimu ili kutimiza kazi ya Mungu katika siku za mwisho (ona Mafundisho na Maagano 110:11–16)).

  • Musa alikabidhi funguo za kukusanyika kwa Israeli (ona Mwongozo wa Maandiko “Israeli”).

  • Elia alikabidhi kipindi cha injili ya Ibrahimu. Hii inajumuisha urejesho wa agano la Ibrahimu (ona Ibrahimu 2:9–11; Mwongozo wa Maandiko, “Agano la Ibrahimu”).

  • Eliya alikabidhi funguo za nguvu ya kuunganisha (ona Mwongozo wa Maandiko, “Unganisha, Kuunganisha”). Funguo hizi zinatoa mamlaka ambayo yanaruhusu ibada zinazofanywa duniani ziwe na nguvu katika maisha yajayo (ona Mafundisho na Maagano 128:9–10).

Kila mshiriki wa Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili anashikilia funguo hizi zote za ukuhani leo. Ni Rais wa Kanisa tu, ambaye ni Mtume mwandamizi, aliye na mamlaka ya kuzitumia funguo hizi zote. Viongozi hawa wanawaita na kuwapa mamlaka waumini wengine wa Kanisa kutumia mamlaka na nguvu ya ukuhani wa Mungu ili kusaidia katika kazi ya wokovu na kuinuliwa.

Kwa maelezo kuhusu funguo za ukuhani, ona 3.4.1

3.2

Baraka za Ukuhani

Kupitia maagano na ibada za ukuhani, Mungu anafanya baraka kubwa zipatikane kwa watoto Wake wote. Baraka hizi zinajumuisha:

  • Ubatizo na uumini katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

  • Kipawa cha Roho Mtakatifu.

  • Kushiriki sakramenti.

  • Mamlaka na nguvu ya kuhudumu katika miito na majukumu ya Kanisa.

  • Kupokea baraka za kipatriaki na baraka nyingine za ukuhani za uponyaji, faraja, na mwongozo.

  • Kupewa endaumenti ya nguvu za Mungu hekaluni.

  • Kuunganishwa na wanafamilia milele.

  • Ahadi ya uzima wa milele.

Watoto wa Mungu wanaweza kupokea baraka hizi za ukuhani na kupokea shangwe kuu wakati wanapoishi injili ya Yesu Kristo.

3.3

Ukuhani wa Melkizedeki na Ukuhani wa Haruni

Katika Kanisa, ukuhani una sehemu mbili: Ukuhani wa Melkizedeki na Ukuhani wa Haruni (ona Mafundisho na Maagano 107:1).

3.3.1

Ukuhani wa Melkizedeki

Ukuhani wa Melkizedeki ni “Ukuhani Mtakatifu, kwa mfano wa Mwana wa Mungu” (Mafundisho na Maagano 107:3). Ni nguvu ambayo kwayo wana na mabinti wa Mungu wanaweza kuwa kama Yeye alivyo (ona Mafundisho na Maagano 84:19–21; 132:19–20).

“Ukuhani wa Melkizedeki unashikilia haki ya urais.” Unayo “nguvu na mamlaka juu ya ofisi zote katika Kanisa katika zama zote za ulimwengu, ili kusimamia katika mambo ya kiroho” (Mafundisho na Maagano 107:8). Kupitia mamlaka haya, viongozi wa Kanisa wanaelekeza na kusimamia kazi zote za kiroho za Kanisa (ona Mafundisho na Maagano 107:18). “Mamlaka mengine yote au ofisi zote katika kanisa ni viambatisho kwenye ukuhani huu” (Mafundisho na Maagano 107:5).

Rais wa Kanisa ni kuhani mkuu kiongozi juu ya Ukuhani wa Melkizedeki (ona Mafundisho na Maagano 107:65–67). Rais wa kigingi ni kuhani mkuu kiongozi katika kigingi (ona Mafundisho na Maagano 107:8, 10; ona pia sura ya 5 katika kitabu hiki). Askofu ni kuhani mkuu kiongozi katika kata (ona Mafundisho na Maagano 107:17; ona pia sura ya 7 katika kitabu hiki cha maelezo ya jumla).

Kwa ajili ya taarifa kuhusu ofisi na wajibu wa Ukuhani wa Melkizedeki, ona 8.1.

3.3.2

Ukuhani wa Haruni

Ukuhani wa Haruni ni “kiambatisho kwa … Ukuhani wa Melkizedeki” (Mafundisho na Maagano 107:14). Unajumuisha funguo za:

  • Kuhudumu kwa malaika.

  • Injili ya toba.

  • Kusimamia ibada za nje, ikijumuisha ubatizo kwa ajili ya ondoleo la dhambi.

(Ona Mafundisho na Maagano 13:1; 84:26–27; 107:20.)

Askofu ni rais wa Ukuhani wa Haruni katika kata (ona Mafundisho na Maagano 107:15).

Kwa ajili ya maelezo kuhusu ofisi na wajibu wa Ukuhani wa Haruni, ona 10.1.3.

3.4

Mamlaka ya Ukuhani

Mamlaka ya Ukuhani ni kibali cha kumwakilisha Mungu na kutenda katika jina Lake. Katika Kanisa, mamlaka yote ya ukuhani yanatumika chini ya maelekezo ya wale ambao wanashikilia funguo za ukuhani.

Waumini wanaume wa Kanisa wanaostahili wanapokea mamlaka ya ukuhani kupitia utunukiwaji wa ukuhani na kutawazwa kwenye ofisi za ukuhani. Waumini wote wa Kanisa wanaweza kutumia mamlaka yaliyonaibishwa wanaposimikwa au kupangiwa kazi ya kusaidia katika kutimiza kazi ya Mungu. Waumini wanawajibika kwa Mungu na kwa wale ambao Yeye amewateua kuongoza kwa jinsi wanavyotumia mamlaka Yake (ona 3.4.4).

3.4.1

Funguo za Ukuhani

Funguo za Ukuhani ni mamlaka ya kuelekeza matumizi ya ukuhani kwa niaba ya watoto wa Mungu. Matumizi ya mamlaka yote ya ukuhani katika Kanisa yanaelekezwa na wale wanaoshikilia funguo za ukuhani (ona Mafundisho na Maagano 65:2).

3.4.1.1

Wale Wanaoshikilia Funguo za Ukuhani

Yesu Kristo anashikilia funguo zote za ukuhani. Chini ya maelekezo Yake, funguo za ukuhani zinatolewa kwa wanaume ili zitumike katika miito maalumu kwa ajili ya kutimiza kazi ya Mungu, kama ilivyoelezwa hapa chini.

Bwana ametunukia juu ya kila mmoja wa Mitume Wake funguo zote ambazo zinahusiana na ufalme wa Mungu duniani. Mtume mwandamizi aliye hai, ambaye ni Rais wa Kanisa, ndiye mtu pekee duniani aliyeruhusiwa kutumia funguo hizo zote za ukuhani (ona Mafundisho na Maagano 81:1–2; 107:64–67, 91–92; 132:7).

Chini ya maelekezo ya Rais wa Kanisa, viongozi wa ukuhani wanapewa funguo ili waweze kuongoza katika maeneo yao ya majukumu. Viongozi hawa ni pamoja na:

  • Marais wa vigingi na wilaya.

  • Maaskofu na marais wa matawi.

  • Marais wa akidi za Ukuhani wa Melkidezeki na Haruni.

  • Marais wa mahekalu.

  • Marais wa misheni na marais wa vituo vya mafunzo ya umisionari.

  • Marais wa maeneo ya kihistoria ya Kanisa.

Viongozi hawa wanapokea funguo za ukuhani wakati wanaposimikwa kwenye miito yao.

Funguo za Ukuhani hazitolewi kwa wengine, ikijumuisha washauri kwa viongozi wa ukuhani wa maeneo husika au marais wa vikundi vya Kanisa. Bali, viongozi hawa wanapewa mamlaka yaliyonaibishwa wakati wanaposimikwa na wakati wanapopangiwa majukumu chini ya maelekezo ya hao wanaoshikilia funguo za ukuhani. Marais wa vikundi vya Kanisa wanaongoza chini ya maelekezo ya hao wanaoshikilia funguo za Ukuhani (ona Mafundisho na Maagano 4.2.4).

Picha
Mkutano wa baraza la kata

3.4.1.2

Utaratibu kwenye Kazi ya Bwana

Funguo za ukuhani zinahakikisha kwamba kazi ya wokovu na kuinuliwa inatimizwa kwa njia ya utaratibu (ona Mafundisho na Maagano 42:11; 132:8). Wale ambao wanashikilia funguo za ukuhani wanaelekeza kazi ya Bwana ndani ya maeneo yao ya uwajibikaji. Wanafanya hivyo kwa upendo na haki. Mamlaka haya ya uongozi yana uhalali tu kwenye majukumu maalumu ya wito wa kiongozi. Wakati viongozi wa ukuhani wanapopumzishwa kutoka kwenye miito yao, hawashikilii tena funguo hizi.

Wote wanaohudumu katika Kanisa wanasimikwa au kupangiwa majukumu chini ya maelekezo ya mtu anayeshikilia funguo za ukuhani. Wakati waumini wanaposimikwa au kupangiwa majukumu, wanakuwa wamepewa mamlaka na Mungu ya kuhudumu katika kazi Yake.

3.4.2

Kutunukiwa na kutawazwa katika Ukuhani

Chini ya maelekezo ya wale wanaoshikilia funguo za ukuhani, Ukuhani wa Haruni na Ukuhani wa Melkizedeki hutunukiwa juu ya waumini wanaume wa Kanisa wenye kustahili (ona Mafundisho na Maagano 84:14–17). Baada ya ukuhani sahihi kuwa umetunukiwa, mtu huyo anatawazwa kwenye ofisi katika ukuhani ule, kama vile shemasi au mzee. Mwenye kushikilia ukuhani anatumia ukuhani kulingana na haki na majukumu ya ofisi hiyo (ona Mafundisho na Maagano 107:99).

Kila mwanamume katika Kanisa la Yesu Kristo anapaswa kujitahidi kuwa mwenye kustahili ili kupokea na kutumia Ukuhani wa Melkizedeki ili awahudumie wengine. Wakati mwanamume anapopokea ukuhani huu, anafanya agano kuwa kwa uaminifu atatimiza wajibu wake wa ukuhani. Pia yeye hupokea kiapo kutoka kwa Mungu, au ahadi, ya baraka za milele (ona Mafundisho na Maagano 84:33–44); ona pia Mwongozo wa Maandiko, “Kiapo na Agano la Ukuhani”).

Kwa maelezo zaidi kuhusu kutunukiwa na kutawazwa katika ukuhani, ona 8.1.1, 10.6, 18.10, na 38.2.5.

3.4.3

Unaibishaji wa Mamlaka ya Ukuhani ili Kuhudumu katika Kanisa

Mamlaka ya ukuhani ya kuhudumu ndani ya Kanisa yananaibishwa katika njia zifuatazo:

  • Kwa kusimikwa kwenye wito wa Kanisa

  • Kwa kupangiwa jukumu kutoka kwa viongozi wa Kanisa

3.4.3.1

Kusimikwa

Wakati wanaume na wanawake wanaposimikwa chini ya maelekezo ya wale wanaoshikilia funguo za ukuhani, wanapewa mamlaka kutoka kwa Mungu ili kutenda kazi katika wito huo. Wakati wanapopumzishwa wito huo, wanakuwa hawana tena mamlaka yanayohusishwa na wito huo.

Baadhi ya miito inahusiana na ofisi na akidi za ukuhani. Kwa mfano, mwanamume anayeshikilia Ukuhani wa Melkizedeki anaweza kuitwa kama rais wa akidi ya wazee. Wakati anaposimikwa na rais wa kigingi, anapewa funguo za ukuhani, mamlaka, na wajibu wa kuelekeza kazi ya akidi ya wazee (ona 3.4.1).

Miito mingine mingi ya Kanisa haihusiani na ofisi na akidi za ukuhani. Lakini waumini wote wa Kanisa wanaosimikwa kutumikia wanapewa mamlaka na wajibu wa kiungu ili kutenda kazi katika miito yao. Kwa mfano:

  • Mwanamke ambaye ameitwa na kusimikwa na askofu kama rais wa Muungano wa Usaidizi katika kata anapewa mamlaka ya kuelekeza kazi ya Muugano wa Usaidizi katika kata.

  • Mwanamume au mwanamke ambaye ameitwa na kusimikwa na mshiriki wa uaskofu kama mwalimu wa Watoto anapewa mamlaka ya kufundisha Watoto katika kata.

Wale wote wanaoitwa na kusimikwa wanahudumu chini ya maelekezo ya hao wanaoongoza juu yao (ona 3.4.1.2).

Kwa maelezo zaidi kuhusu kusimikwa kwa waumini kwa ajili ya miito ya Kanisa, ona 18.11.

3.4.3.2

Majukumu

Viongozi wa Kanisa wanaweza kunaibisha mamlaka kwa kuwapangia wengine majukumu. Wakati wanaume na wanawake wanapopokea majukumu haya, wanapewa mamlaka ya kutenda kutoka kwa Mungu. Kwa mfano:

  • Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili wananaibisha mamlaka kwa Sabini wanaopangiwa kutumikia maeneo na kusimamia katika mikutano ya kigingi.

  • Marais wa misheni wananaibisha mamlaka kwa wamisionari wa kiume na wa kike ambao wanapangiwa kuongoza na kuwafundisha wamisionari wengine.

  • Mamlaka yananaibishwa kwa waumini wa Kanisa ili kuhudumu kama akina kaka na akina dada wahudumiaji. Hii inatokea wakati wanapokuwa wamepangiwa kufanya hivyo na rais wa akidi ya wazee au rais wa Muungano wa Usaidizi chini ya maelekezo ya askofu.

Mamlaka ambayo yamenaibishwa kwa kupangiwa jukumu yana ukomo kwenye majukumu na muda wa kazi hiyo.

Kwa maelezo zaidi kuhusu jukumu kupitia unaibishaji, ona 4.2.5.

3.4.4

Kutumia Mamlaka ya Ukuhani kwa Haki

Viongozi wa Kanisa na waumini wanatumia mamlaka ya ukuhani wa kutunukiwa au kunaibisha ili kubariki maisha ya watu wengine.

Mamlaka haya yanaweza kutumika tu kwa haki (ona Mafundisho na Maagano 121:36). Yanatumika kwa ushawishi, ustahimilivu, upole, unyenyekevu, upendo na ukarimu (ona Mafundisho na Maagano 121:41–42). Viongozi wanashauriana na wengine katika roho ya umoja na kutafuta mapenzi ya Bwana kupitia ufunuo (ona Mafundisho na Maagano 41:2). Kwa maelezo kuhusu kushauriana na wengine, ona 4.4.3.

Wale wanaotumia mamlaka ya ukuhani hawalazimishi mapenzi yao kwa wengine. Hawayatumii kwa ajili ya malengo yenye ubinafsi. Kama mtu anayatumia isivyo haki, “mbingu hujitoa zenyewe [na] Roho wa Bwana husikitika” (Mafundisho na Maagano 121:37).

Baadhi ya miito ya Kanisa hujumuisha wajibu wa kuongoza. Kwa maelezo kuhusu kuongoza katika Kanisa, ona 4.2.4.

Picha
Wanaume wawili na mwanamke wakizungumza

3.5

Nguvu ya Ukuhani

Nguvu ya Ukuhani ni nguvu ambayo kwayo Mungu anawabariki watoto Wake. Nguvu ya Mungu ya ukuhani inatiririka kwa waumini wote wa Kanisa—wanawake na wanaume—wakati wanaposhika maangano waliyofanya na Yeye. Waumini wanafanya maagano haya pale wanapopokea ibada za ukuhani. (Ona Mafundisho na Maagano 84:19–20.)

Baraka za nguvu ya ukuhani ambazo waumini wanaweza kupokea zinajumuisha:

  • Mwongozo kwa ajili ya maisha yao.

  • Mwongozo wa kiungu ili kujua jinsi ya kuwahudumia wanafamilia na watu wengine.

  • Nguvu ya kuvumilia na kushinda changamoto.

  • Vipawa vya Roho ili kukuza uwezo wao.

  • Ufunuo wa kujua jinsi ya kutimiza kazi ambayo kwayo wametawazwa, kusimikwa, au kupangiwa kufanya.

  • Msaada na nguvu ya kuwa zaidi kama Yesu Kristo na Baba wa Mbinguni.

3.5.1

Maagano

Agano ni ahadi takatifu kati ya Mungu na watoto Wake. Mungu hutoa masharti kwa ajili ya agano, na watoto Wake wanakubali kutii masharti hayo. Mungu anaahidi kuwabariki watoto Wake pale wanapotimiza agano.

Waumini wanafanya maagano na Mungu wakati wanapopokea ibada za wokovu na kuinuliwa (ona 18.1). Wote wanaovumilia mpaka mwisho katika kushika maagano yao watapokea uzima wa milele (ona 2 Nefi 31:17–20; Mafundisho na Maagano 14:7). Kuvumilia mpaka mwisho kunajumuisha kuonyesha imani kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo na kutubu kila siku.

Wazazi, viongozi wa Kanisa, na wengine wanawasaidia watu binafsi kujiandaa kufanya maagano pale wanapopokea ibada za injili. Wanahakikisha kwamba mtu anaelewa maagano atakayoyafanya. Baada ya mtu kufanya agano, wanamsaidia alishike. (Ona Mosia 18:8–11, 23–26.)

3.5.2

Ibada

Ibada ni tendo takatifu linalofanywa kwa mamlaka ya ukuhani. Ibada siku zote zimekuwa sehemu ya injili ya Yesu Kristo. Ibada za kwanza duniani zilifanywa katika siku za Adamu na Hawa (ona Mwanzo 1:28; Musa 6:64–65).

Katika ibada nyingi, watu binafsi wanafanya maagano na Mungu. Mifano inajumuisha ubatizo, sakramenti, endaumenti, na ibada ya kuunganishwa katika ndoa. Katika ibada zingine kama vile baraka za kipatriaki au baraka kwa wagonjwa, watu hawafanyi maagano, bali hupokea mwongozo na nguvu ya kutunza maagano.

Ibada zina maana ya kiishara ambayo humwelekeza mtu kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Katika ibada ambazo zinajumuisha maagano, ishara humsaidia mtu binafsi kuelewa ahadi wanazoziweka na baraka wanazopokea kupitia uaminifu wao.

Kila ibada inamruhusu mtu kupokea baraka nyingi za kiroho. Bwana alifunua, “Katika ibada [za ukuhani], nguvu za uchamungu hujidhihirisha” (Mafundisho na Maagano 84:20). Ibada za wokovu na kuinuliwa ni muhimu kwa ajili ya uzima wa milele. Kwa maelezo zaidi, ona 18.1.

Watu walio hai wanapokea ibada za wokovu na kuinuliwa kwa ajili yao wenyewe. Inapowezekana, wanarudi hekaluni kufanya ibada hizi kwa niaba ya wale walioaga dunia. Kwa maelezo zaidi kuhusu kufanya ibada kwa ajili ya wafu, ona sura ya 28.

3.6

Ukuhani na Nyumbani

Waumini wote wa Kanisa ambao wanatunza maagano yao—wanawake, wanaume, na watoto—wanabarikiwa kwa nguvu ya ukuhani wa Mungu katika nyumba zao ili kujiimarisha wao wenyewe na familia zao (ona 3.5). Nguvu hii itawasaidia waumini katika kufanya kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa katika maisha yao binafsi na ya familia (ona 2.2).

Wanaume wanaoshikilia Ukuhani wa Melkizedeki wanaweza kutoa baraka za ukuhani kwa wanafamilia ili kutoa mwongozo, uponyaji, na faraja. Inapohitajika, waumini wa Kanisa wanaweza pia kutafuta baraka hizi kutoka kwa wanafamilia, akina kaka wahudumiaji, au viongozi wa Kanisa wa eneo husika. Kwa maelezo zaidi kuhusu baraka za ukuhani, ona 18.13 na 18.14.

Kwa maelezo kuhusu kuongoza katika familia, ona 2.1.3.

Picha
mwanamke akipokea baraka ya ukuhani